KILICHOFANYIKA TAREHE 06-07/07/2013 KATIKA HOTEL YA BLUE PEARL, DAR ES
SALAAM.
Kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo ilikutana katika Kikao
cha dharura kuanzia tarehe 06-07/07/2013 katika Hotel ya Blue Pearl
Dar es salaam kujadili pamoja na mambo mengine Rasimu ya Katiba mpya
na hali ya Siasa nchini.
Kamati kuu imejadili na kuyatolea maamuzi mambo mbalimbali kama ifuatavyo:
1:0. Hali ya Siasa Nchini.
Kamati kuu imepokea taarifa ya hali ya siasa nchini na kuzingatia
mambo yafuatayo:
a) Shambulio la Bomu Arusha.
Kamati Kuu imesikitishwa na kulaani kwa nguvu zote tukio la Bomu
Arusha lililosababisha watu wanne kuuwawa na zaidi ya watu 70 wengine
kujeruhiwa vibaya.
Kamati Kuu imeridhika kwamba shambulio hilo lililenga kuwaua
viongozi wakuu wa CHADEMA akiwamo Mwenyekiti wa Taifa Mheshimiwa
Freeman A. Mbowe na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini na Mjumbe wa
Kamati Kuu, Mheshimiwa Godbless J. Lema na viongozi na wanachama
wengine wa CHADEMA waliohudhuria Mkutano wa kufunga kampeni za udiwani
katika Jiji la Arusha pamoja na kuvuruga Uchaguzi huo na kuinyima
CHADEMA ushindi mkubwa;
Kamati Kuu imeridhika kwamba ushahidi uliopo wa vielelezo na wa
mashuhuda wa shambulio unaonyesha ushiriki wa moja kwa moja wa Jeshi
la Polisi katika shambulio hilo;
Kamati Kuu imefadhaishwa na kauli ya Serikali bungeni iliyolenga
kulikosha Jeshi la Polisi kwa kuhusika kwake na shambulio hilo dhidi
ya CHADEMA na wananchi wa Jiji la Arusha na kuilaumu CHADEMA wakati
CHADEMA ndio mhanga wa shambulio hilo;
Kamati Kuu imeshangazwa na kitendo cha Serikali kupuuza maafa
yaliyowafika wananchi wa Arusha kwa kushindwa kushiriki katika mazishi
ya wahanga wa mauaji ya Soweto na kuwashambulia kwa mabomu ya machozi,
vipigo na maji ya sumu waombolezaji waliokusanyika kuwaaga marehemu
waliouawa kwenye shambulio;
Kamati Kuu imesikitishwa na Rais Kikwete kuendelea kukaa kimya juu
ya shambulio la Arusha na kushindwa kwake kuunda Tume huru ya
Kimahakama kuchunguza kwa uwazi shambulio hilo. Aidha, Kamati Kuu
inaamini kwamba ukimya huu wa Rais Kikwete na kushindwa kwake hata
kuwatembelea wafiwa na wahanga wengine wa shambulio hilo ni ushahidi
mwingine wa kuhusika kwa vyombo vya ulinzi na usalama vya Serikali
katika kupanga na kutekeleza shambulio la Arusha;
Kamati Kuu imefadhaishwa na kitendo cha Bunge la Jamhuri ya Muungano
kuendelea na vikao vya Bunge kama kawaida; kukataa kutoa mchango
wowote kwa wahanga na kushindwa kupeleka ujumbe wa Bunge kuwatembelea
na kuwafariji wahanga na waathirika wa shambulio kinyume na utaratibu
uliozoeleka wa Bunge kutambua na kushiriki katika majanga na misiba ya
aina hii.
Kamati Kuu inautaka uongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano uwaeleze
Watanzania kama maafa ya shambulio la Arusha yalikuwa na tofauti
yoyote na maafa ya shambulio la bomu la Olasiti, au na maafa ya mabomu
ya Gongo la Mboto, ajali ya MV Skargit au maafa mengine
yaliyosababisha Bunge la Jamhuri kuahirisha shughuli zake, kutoa
michango kwa waathirika pamoja na kupeleka ujumbe wa Bunge kuwafariji
wafiwa na wahanga wa matukio hayo;
Kutokana na maelezo hayo hapo juu Kamati kuu imeazimia kuwa:
• Iwapo Rais ataendeleza msimamo wa kutokuunda tume huru ya
kimahakama, Ushahidi uliopo juu ya tukio la kurushwa Bomu Arusha
utawekwa wazi muda utakapofika kwa wananchi wa Tanzania; vyama na
mashirika ya kiraia ya haki za binadamu hapa nchini na ya nje ya nchi;
ofisi za kibalozi za mataifa rafiki na Tanzania pamoja na jumuiya ya
kimataifa ili yaishinikize Serikali kuunda Tume huru ya Kimahakama
kuchunguza shambulio hilo na matukio mengine ya mauaji yenye sura ya
kisiasa ambayo yamehusishwa na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya
usalama vya Serikali au vya Chama cha Mapinduzi;
2:0. Hali ya Wananchi wa Mtwara.
Kamati kuu imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa juu ya unyanyasaji,
utesaji, ubakaji na uonevu wanaofanyiwa wananchi wa Mtwara hivi sasa
na vyombo vya dola huku serikali ikikaa kimya juu ya jambo hili bila
kukemea. Kamati kuu imejadili kwa kina namna wananchi wa Mtwara
wanavyofanyiwa na vyombo vya dola na kufikia maazimio yafuatayo;
Vyombo vya dola vitimize wajibu wake wa kulinda amani na mali ya
raia na siyo kuwatesa na kuwapiga wananchi kwa kuwasababishia vifo
kinyume na Haki za Binadamu.
Serikali iwasikilize wananchi wa Mtwara na siyo kutumia ubabe,
unyanyasaji, uonevu na mateso kama mbinu za kuhalalisha kukubalika
kwake kwa wananchi.
Rais Kikwete alitangazie taifa "hali ya hatari" kwa mkoa wa Mtwara
kama anaona kuwa Mtwara ni hatari kwa kiasi hicho cha kulitumia JWTZ
kuzunguka mitaani na silaha za kijeshi ili taifa liweze kujua,Aidha
kama jeshi la polisi limeshindwa kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa
sheria atangaze kulivunja jeshi hilo mara moja.
Serikali iunde tume huru ya kuchunguza matukio ya
mauaji,ubakaji,utesaji na ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyofanywa
na vyombo vya dola na waathirika wote waweze kufidiwa kwa mujibu wa
sheria.
3:0. Kauli ya Waziri Mkuu.
Kamati Kuu imejadili kwa kina kauli ya Waziri Mkuu Bungeni kwamba ni
sahihi kwa Jeshi la Polisi nchini kuwapiga Wananchi wote wanaotumia
haki zao za Kikatiba kupinga sera au maamuzi ya Serikali. Kamati Kuu
imeazimia kuwa:
Kauli ya Waziri Mkuu imekiuka Katiba na sheria za nchi yetu
zinazokataza Jeshi la Polisi kutumia nguvu dhidi ya raia wasiokuwa na
silaha na ambao wanatumia haki zao za kikatiba kufanya maandamano;
Kamati Kuu inaamini kwamba kauli ya Waziri Mkuu inatoa Baraka kwa
Jeshi la Polisi kuendeleza vitendo vya ukatili na mauaji dhidi ya
wananchi ambayo yamelifanya Jeshi la Polisi la Tanzania kutangazwa
kuwa moja ya majeshi katili ya polisi katika Afrika Mashariki;
Kamati Kuu inaungana na wananchi, taasisi na mashirika ya kitaifa na
kimataifa ambayo yamelaani vikali kauli hiyo ya Waziri Mkuu na
inawataka wananchi, taasisi na mashirika hayo kuendelea kumlaani
vikali Waziri Mkuu kwa kauli hiyo;
Kamati Kuu inaamini kwamba Waziri Mkuu amepoteza sifa za kuendelea
kuwa Waziri Mkuu na inaungana na wananchi na taasisi ambazo zimedai
Waziri Mkuu awajibike au awajibishwe kutokana na kauli yake hiyo.
Aidha, Kamati Kuu inawaelekeza Wabunge wote wa CHADEMA washirikiane na
Wabunge wengine wote wenye mapenzi mema na nchi hii na ambao wanaamini
katika utawala wa sheria waanzishe mchakato wa kumpigia kura ya
kutokuwa na Imani Waziri Mkuu kupitia Bunge;
Kamati Kuu imewataka Jeshi la Polisi kama sehemu ya jamii ya
watanzania kupuuza kauli ya Waziri Mkuu katika utekelezaji wa kazi zao
kwa kuwa kauli hiyo ni ya uvunjifu wa Katiba na Sheria na inachochea
uvunjifu wa amani.
4:0. Uchaguzi wa Madiwani.
Kamati Kuu imepokea taarifa kuhusu ushiriki wa CHADEMA katika Uchaguzi
wa Madiwani uliofanyika tarehe 16/06/2013 katika kata 22.
Kamati Kuu imeipongeza Sekretarieti na uongozi wa Kanda mbalimbali
za CHADEMA kwa maandalizi mazuri katika Uchagzuzi huo uliosababisha
CHADEMA kuwapokonya CCM ushindi katika kata 4 ilizokuwa imeshinda
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Kamati Kuu imewapongeza wananchi
kwa kuipatia CHADEMA kura asilimia (47.7%) dhidi ya CCM (49%) na
(3.3%) za CUF.
Kamati kuu imesikitishwa na vitendo vya fujo walivyofanyiwa
viongozi, wagombea pamoja na Wanachama mbalimbali katika sehemu
mbalimbali palipo fanyika Uchaguzi. Kamati Kuu imesikitshwa na kulaani
vitendo hivyo vikiwemo vya watu kukatwa mapanga , kuchomwa visu na
kubakwa kwa akina Mama na vijana wahuni walioandaliwa na Chama cha
Mapinduzi.
Kamati Kuu imelaani vitendo hivyo vya kinyama vilivyofanywa mbele ya
jeshi la polisi na Wakuu wa Wilaya.
Ili kukabiliana na vitendo vya fujo vinavyofanywa na vijana wa CCM
dhidi ya wagombea, Wanachama na viongozi wa CHADEMA, Kamati Kuu
imeagiza kwamba kitengo cha ulinzi cha Chama "Red Brigade" kiimarishwe
zaidi kwa kuhakikisha kuwa vijana wote wa Red Brigade Nchi nzima
wanapewa mafunzo maalum ya UKAKAMAVU yatakayoandaliwa katika Makambi
maalum katika mikoa yote.
Kamati Kuu imejadili maandalizi ya Uchaguzi wa madiwani katika kata
nne (4) katika Jiji la Arusha. Kamati Kuu imepokea kwa masikitiko
taarifa juu mipango inayofanywa na jeshi la polisi kwa kushirikiana na
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo na viongozi wengine wa CCM
mkoani Arusha katika kuhujumu zoezi la Uchaguzi kwa kuwatisha wapiga
kura kwa kutumia polisi na vijana wa Green Guard siku ya uchaguzi.
Kamati Kuu inamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kuchukua hatua
stahiki kuzuia harakati za polisi na CCM za kuvuruga Uchaguzi na
kutaka kujipatia ushindi kwa njia za hila. Aidha Kamati kuu imelitaka
jeshi la polisi kuheshimu maadili ya uchaguzi yaliyosainiwa na
Serikali, Tume ya uchaguzi na vyama vya siasa.
Kamati Kuu imesikitishwa na Tume ya Uchaguzi kushindwa kuwazuia CCM
kuendelea na kampeni za Uchaguzi huku wakiwa wamezuia kampeni hizo kwa
vyama vingine.
Kamati Kuu imeendelea kuwapa pole wananchi wa Arusha kwa matukio
mabaya wanaofanyiwa na serikali ya CCM mkoani humo, na imewapongeza
kwa kusimama kidete katika kulinda haki na ukweli.
Kamati Kuu imewaomba wananchi wa Arusha wajitokeze kwa wingi siku ya
kupiga kura tarehe 14 Julai 2013, na imewataka wabunge wote washiriki
katika kusimamia zoezi la upigaji kura na uhesabuji kura siku ya
Uchaguzi na wananchi wajitokeze kwa wingi kulinda kura bila hofu.
5:0. Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Kamati Kuu imejadili kwa kina sana maudhui yaliyomo katika Rasimu ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyotolewa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba;
• Kamati Kuu imetambua kazi kubwa iliyofanywa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba katika kukusanya na kuchambua maoni ya wananchi na kuandaa
Rasimu ya Katiba Mpya;
• Hata hivyo, Kamati Kuu imetambua na kuainisha mapendekezo mengine ya
msingi ambayo yanastahili kuboreshwa zaidi katika Rasimu hiyo;
• Msimamo na maazimio ya Kamati Kuu juu ya Rasimu ya Katiba Mpya
yameainishwa na kuchapishwa katika kijitabu maalumu ambacho
kitazinduliwa katika Mkutano wa hadhara utakaofanyika siku, tarehe na
mahali patakapo tangazwa hapo baadaye.
Imetolewa na:
……………………….
Freeman A. Mbowe, (MP)
Mwenyekiti Taifa
--
"Tukosoane, Turekebishane, Tuwajibishane, ndipo Tusameheane". Regia Mtema.
--
Mobile: +255 (0) 713 24 67 64
Alternative: +255 (0) 784 24 67 64
Skype: Mohamedi.Mtoi
Twitter: @mohamedimtoi
Facebook: http://www.facebook.com/mouddymtoi
--
--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
0 Comments