Ni Jumatatu nyingine tena imewadia na ambayo inaanzisha au pengine kumaliza au hata kuzidisha machungu kwa Watanzania walio wengi, isipokuwa kwa wachache kati yetu hasa wale waliojaliwa kuukata.
Leo hii, wabunge wetu kule mjini Dodoma wanaanza kujadili hotuba ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2013/14 ambayo iliwasilishwa Alhamisi na Waziri wa Fedha, Dk William Augustao Mgimwa.
Binafsi, ninajiuliza, je, ni kitu gani zaidi Watanzania walio wengi mijini na vijijini wakitegemee katika mijadala hii ambayo ninasema haina mantiki.
Ninaiona kuwa haina mantiki kwani tayari wengi wao wametangaziwa maumivu makali kwa miezi 12 ijayo.
Hakuna nafuu yoyote, ila kwa wateule wachache wakiwamo wabunge, mawaziri ,wakurugenzi , maofisa watendaji wakuu wa idara zinazojitegemea au mashirika, ambao ninaweza kusema ndiyo pekee wameukata kwani wanaweza kuwa wanaishi peponi kwa posho, marupurupu mengi ambayo hayakatwi kodi.
Ni makali haya ya maisha ambayo kama mimi ningekuwa na nafasi serikalini, ningeona aibu kujitangaza mbele ya watu kwamba ninawatumika wananchi.
Ni ajabu kwamba kuwa mtumishi wa umma, wengine hawafikirii tena kuhusu mishahara yao midogo na duni, wanawekeza akili zao zote katika kusaka mbinu za kuiba, kuchota chochote ili kuziba pengo linalojitokeza kila mwezi.
Kwa jumla, kama ambavyo wameeleza wachambuzi wengi, bajeti hii imejaa machungu zaidi ambayo ni vigumu kuyaeleza na hata kueleweka.
Hata hivyo, mimi kama mwanajamii sina budi kusema kwamba Serikali yetu haina budi kujitathmini upya hasa wakati huu ambao vilio vya ugumu wa maisha vinasikika kila kona ya nchi, kuangalia vyanzo vipya vya kodi, kuzikusanya.
Ni ajabu kuona kwamba serikali yetu imeamua kwa makusudi kuwatosa au kuwakaanga kwa mafuta yao wananchi wake walio wengi mijini na vijijini.
Sioni Serikali yetu pendwa imeandaa mbinu gani za muda mfupi, wa kati au mrefu katika kuwaondolea mateso makali wananchi.
Ziko wapi mbinu mbadala ambazo imeziandaa katika kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki katika mipango au juhudi za kuleta maendeleo, hasa wanapokamuliwa hadi tone la mwisho la damu.
Wakulima na hata wafanyakazi, hawaoni mwanga katika handaki la maisha yao ya kila siku.
Matokeo yake, wanalia na hata kuomboleza, wamepoteza matumaini, hata leo wabunge wanapoanza kujadili bajeti, mitazamo ya wengi ni ya kukata tamaa.
Kwa nini wamekata tamaa? Ni kwa sababu kama ambavyo imekuwa kwa miaka nenda rudi, ushuru wa petroli, dizeli unapanda, sigara, bia, soda zinaongezewa kodi, hakuna anayejali.
Siku chache baada ya Julai Mosi, subiri baa na grosari zitapandisha bei, Watanzania wanaumia, lakini kama chawa anayefia kidoleni, wapo kimya!
Kupanda kwa bei ya petroli na dizeli, hakuna shaka ni mwanzo wa kupanda kwa nauli za magari ya aina zote mijini na vijijini licha ya ukweli kwamba miezi michache iliyopita nauli hizo zimepanda.
Mazingira ya Watanzania walio wengi kujiendeleza yanazidi kuonekana kuwa finyu, kutokana na vikwazo vingi ambavyo vinawekwa kupitia bajeti ya mwaka huu ambayo inajadiliwa asubuhi hii kule Dodoma. Sioni ni kwa kiasi gani serikali yetu ambayo imekuwa ikidai kuwa inawajali watu wake inavyoweza kudhihirisha kuwa bado ni kipenzi cha wengi.
Mtazamo wa wachambuzi wengi, wachumi, wanasiasa unaonyesha kuwa Serikali inawabeba zaidi watu wachache na kuwasahau wengi.
Nilisema wiki mbili zilizopita kwa mfano, kwamba mazingira ya kutoza au kulipa kodi katika nchi yetu hayako sawa, hayalingani.
Kwa mfano mdogo, wakazi wengi wa mijini ni wapangaji katika nyumba ambazo wanalipa kodi ya pango inayotofautiana kuanzia Sh10,000 kule uswahilini, bila umeme au maji, wakilipa hadi Sh1,000,000 hasa kwenye maeneo ya wazito, wenye uwezo.
Je, wenye nyumba hizi wanaingiza kipato kikubwa, mamlaka zetu kama TRA au hata Hazina (Wizara ya Fedha) au Ardhi zinatambua kwamba fedha hizi hazikatwi au kutozwa kodi?
Inawezekana kusema kuwa wenye nyumba hizi kama zilivyo nyingine za kulala wageni wanalipa kodi ya ardhi, je, hiyo inatosha au inalingana na biashara hizi ambazo wengi wanaifanya?
Je, biashara hii inachangia kwenye pato la taifa kulingana na kiasi hicho cha fedha zinazopatikana kwa siku, wiki au mwezi?
Huu ni mfano mdogo wa vyanzo vya mapato kama ambavyo wafanyabiashara baadhi wanakadiriwa kwa mwaka kwamba mapato yake kwa mwaka ni wastani wa Shilingi 0 mpaka 4,000,000, hawatozwi kodi.
Kwa nini iwe kwa mtumishi ambaye anakatwa kodi kila mwezi, kadirio lisiwe kwa kipato chake kwa mwaka?
Inaweza vipi Serikali itangaze bajeti, lakini isizungumzie suala hili gumu la ongezeko la mishahara kwa watumishi wake, licha ya ahadi ambazo zilitolewa awali?
Ninakubali kuwa mishahara ni siri baina ya mtumishi na mwajiri, lakini uamuzi wa Dk Mgimwa kutosema lolote kuhusu ahadi ya mwenzake wa Utumishi, Celina Kombani au hata bosi wao, Rais Jakaya Kikwete Mei Mosi mwaka huu kule Mbeya kuwa mishahara itaangaliwa upya pia kuboreshwa, ni jambo ambalo linashangaza.
Hata hivyo, hata mishahara imepanda kwa watumishi wa umma, lakini kama nilivyoeleza wiki mbili zilizopita mdudu huyu, Lipa Kwa Kadiri Unavyopata, 'Pay As You Earn(PAYE)' kuachiwa ang'ate apendavyo, kwani kushushwa kutoka asilimia 14 hadi 13, hii ni dhihaka kwa watumishi.
Kisheria, PAYE ambayo ni kodi ya zuio inatozwa na mwajiri kutoka kwenye kipato cha mwajiriwa wake kila mwisho wa mwezi na chini ya mfumo huo, mwajiri hutoza kodi kutoka kwenye mshahara au kipato kingine kinachostahili.
Kwa maana hiyo, je, tujiulize, posho za vikao vya wabunge wetu na hata marupurupu yao mengine mengi, mazuri yanatozwa kiasi gani kama kodi? Dk Mgimwa inafaa utuambie!
(Source: Gazeti la Mwananchi 17/06/2013)
0 Comments