[wanabidii] Kukionea aibu Kiswahili ni kujidharau wenyewe

Saturday, February 16, 2013
MWALIMU  Julius Nyerere aliwahi kueleza Taifa lisilojivunia lugha yake halina uhai, lakini pia Wachina wakaenda mbali kidogo kwa kusema nchi isiyotumia lugha yake kujiletea maendeleo makubwa, kwanza ya wananchi wake na baadaye ya wengine, ni sawa na maji yaliyooshewa maiti.

Kwamba maji yakioshewa maiti yanakosa faida kubwa inayoweza kuelezwa. Yakitumika, basi yametumika.

Wachina kama ilivyo kwa Mwalimu Nyerere (sasa marehemu) wote wana maana kubwa katika dunia ya sasa inayohitaji mwenye nguvu au anayetumia ubunifu zaidi kuhakikisha maendeleo makubwa na ya haraka ya familia na taifa kwa jumla yake yanapatikana.

Kwa kiasi kikubwa, dhana ya Mwalimu Nyerere imejikita mno Tanzania na watu wake wameielewa na wameendelea kujivunia lugha ya Kiswahili. Lugha hiyo, mbali na kuwaunganisha wananchi wetu kupigania uhuru wao na baadaye maendeleo yao kidogo yanayoonekana sasa, bado haijaweza kumea na haina mizizi ya kuhakikisha inakuwa  rasilimali nyingine kubwa ya kuingiza fedha katika Hazina ya Tanzania.

Hali hiyo ya kushindwa kukisambaza Kiswahili na kukifanya mtaji wa kuleta fedha nyingi kutoka nje ya nchini, kunatufanya tusiwe mbali sana na falsafa ya Kichina kwamba lugha yetu, mbali na faida kidogo inayopatikana,  inaonekana kuwa baada ya kazi ya kutuunganisha na kuendelea kutuweka sawa katika mawasiliano na kuleta maendeleo kidogo, hakuna anayeipigania ili iwe mtaji.

Kila mmoja wetu; iwe serikali yenyewe, taasisi zake, mashirika, watu binafsi na hasa wasomi, anajipiga kifua tu ndani ya maeneo ya nchi yetu mbele ya umati akipiga 'kelele' za kuhimiza ukuzaji wa Kiswahili.

Wapo waliopanda majukwaani, tena wakizungumza na povu likiwatoka midomoni mwao; kwamba Kiswahili lazima kipiganiwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha kinapasua anga na kuwafikia watu wengi zaidi nje ya nchi.

Hao walifanya hivyo kwa nia njema kabisa, lakini nguvu zao zikakatishwa na Waswahili wenzao, tena ajabu Watanzania wakidai lugha hiyo haina lolote na wala siyo chochote nje ya mipaka ya Tanzania. Hawa baadhi yao ni wasomi, waandishi wa habari na hata viongozi wa siasa.

Kukatishwa kwao tamaa na ndugu zao kukawavunja moyo na wakaamua kuacha na kuendelea na shughuli zao. Ingawa hivi karibuni baadhi ya wasomi wa lugha hiyo adhimu wameanza kukipigania Kiswahili kwa nguvu, kwa maelezo ya kuwa ni mtaji mkubwa na rasilimali yenye mwanga wa kuleta fedha nyingi kutoka nje.

Jitihada za wataalamu hao zinaonesha jinsi wanavyopenda, kuona Kiswahili kinakuwa chanzo kingine kikubwa, siyo cha mtaji tu, bali ajira kwa Watanzania, ambao dunia inaamini ni walimu wazuri wa lugha hiyo kuliko eneo jingine lolote.

Ikiwa jitihada hizo zitafanikiwa, kwa kuweka mikakati ambayo itahakikisha mafanikio yanapatikana, uhakika ni kuwepo kwa madarasa na taasisi za ukuzaji wa lugha hiyo katika nchi nyingi duniani.

Wenzetu Wakenya, ambao historia inawataja kuwa 'wanafunzi' wetu katika lugha, wao wanaonekana kuwa walimu zaidi katika taasisi na vyuo vya nje, tena wakiwa na 'spidi' kubwa ya kuhimiza ufundishwaji wa lugha hiyo adhimu ya Afrika.

Kama ilivyo katika utalii, Wakenya ndiyo wanaotangaza kuwa magwiji wa Kiswahili na kwamba ni lugha inayokua na kuzungumzwa na idadi kubwa ya Waafrika. Katika matangazo yao wanasema; -unataka kufanya kazi au biashara Afrika, basi jua kuzungumza lugha ya Afrika- Kiswahili.

Sisi inavyoonekana jitihada zetu zimo ndani ya nchi tu.Tumelala. Tunaonekana mno katika vipindi vya televisheni tukikizungumza na kukichambua Kiswahili, lakini nguvu ya kukitangaza na kukipeleka nje haionekani.

Haitoshi tu kuwaona wataalamu wakikichambua Kiswahili kwenye televisheni wakieleza tu kwamba ni lugha inayoweza kuwa mtaji, bila kuitaja mikakati thabiti ya kukikuza na kukitangaza nje ili kupata wanafunzi wengi zaidi na hivyo fedha zaidi.

Mara nyingine nimekuwa nikisita kuamini usemi huu; Muua nchi ni mwananchi mwenyewe, lakini linapokuja suala la Kiswahili ninaamini – Muua Kiswahili ni Mswahili mwenyewe, tena Mtanzania.

Wenyewe kwa wenyewe tumeshindwa kabisa kukubali Kiswahili kinaweza kuwa lugha ya kufundishia hata elimu ya juu, kwa maelezo ya kizandiki- kuwa tutakuwa mbali na dunia ya sasa ya utandawazi au hatutaweza kuwa na hatua kubwa za maendeleo. Ebo!

Ni sisi wenyewe hadi leo, pamoja na kuwa mimba zetu zinatungwa kwa Kiswahili, zinalelewa kwa Kiswahili, watoto wanazaliwa wakilia kwa Kiswahili na wanalelewa na kukua kwa Kiswahili, lakini  'kinapondwa' na kuoneshwa dhalili dhidi ya lugha nyingine.

Eti hadi leo sheria zetu zinatungwa na kupitishwa na waheshimiwa sana wabunge kwa Kiingereza. Taratibu nyingi  za kuendesha vikao hata vya Waswahili wenyewe kwa wenyewe zinafanywa kwa Kiingereza. Sisi hatuna maneno stahiki ya sheria, sayansi na kada zingine, hadi tuweke lugha za kukopa kwa wengine. Makubwa haya!

Mbona Wachina, Wajerumani na wengine wanatumia lugha zao, tena wakikiona Kiingereza au lugha zingine kuwa za 'kitumwa' na wana maendeleo makubwa kuliko sisi tunaojifaragua? Ni nani katuroga katika hili? Hata tunalala usingizi wa pono bila kushtuka kwa kuiponda lugha yetu wenyewe!


Wajerumani, Wafaransa na sasa Wachina, kwa kutambua lugha ni mtaji, wamekuwa na taasisi ama vyuo nje ya nchi zao, wakifundisha lugha zao za taifa na kuwa chanzo kikubwa cha mapato na ajira kwa vijana wao. Sisi wenyewe lugha yetu, tunajifanya hatuwaoni. Tumelala fofofo na kuendelea kudai Kiswahili ni lugha adhimu. Adhimu ya nini endapo hakisaidii ajira wala kipato kwa idadi kubwa ya Watanzania wanaokifahamu na wanaokizungumza!

Kweli Kiswahili hakina mwenyewe. Hata wanaokipigania na hawapati kuungwa mkono, wanaonekana ni abiria tu, tena waliosimama ndani ya basi lisilokuwa na dereva wa kutufikisha salama.

Kila la heri Kiswahili na inawezekana kukilea na kukigeuza rasilimali.

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

Share this :

Related Posts

0 Comments