hospitali nilipata taarifa kuwa Imam wa msikiti wa Masjid Haq (ulioko
jirani na Afisi Kuu ya CUF na ambapo nasali sala ya Ijumaa nikiwa
Afisi Kuu) na watu wengine watatu akiwemo Sheikh Ramadhan S. Sanze
(ambaye namfahamu kwa muda mrefu). Sadik Gogo na Mzee Abdillah
wamekamatwa na wamefikishwa kituo cha polisi cha kati (Central Police
Station). Nilistushwa na kamata kamata hii na nikahofia kuwa inaweza
kuongeza jazba miongoni mwa waumini wa Kiislam. Baada ya shangazi
kupata tiba katika hospitali ya Muhimbili nilimrudisha nyumbani na
nikampigia simu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na mahusiano ya umma,
Abdul Kambaya, tukutane kituo cha polisi cha kati kuulizia sababu za
kukamatwa Imam wa Masjid Haq na wenzake watatu na kama tunaweza
kuwawekea dhamana.
Tulipofika kituo cha polisi tulibaini kuwa Imam wa Msikiti wa Masjid
Haq hajakamatwa bali kuna muumini mwingine kwa jina la Mkadam Swalehe
ndiye aliyekamatwa. Tulizungumza na RPC Kova na RCO Msangi kuhusu
kuachiliwa kwa wale waliokamatwa. Tukafahamishwa kuwa itabidi
wafanyiwe mahojiano na baadaye wataachiliwa isipokuwa Mkadam Swalehe
ambaye ana faili jingine pale polisi linaloendelea kufanyiwa
upelelezi. Tulifahamishwa kuwa nitume mtu saa 10:30 jioni ili aweze
kufuatilia utaratibu wa kuachiliwa watuhumiwa watatu akiwemo Sheikh
Ramadhan Sanze, Sadik Gogo na Mzee Abdillah.
Nilishauriana na Wakurugenzi wa CUF walioko Dar es Salaam na Naibu
Katibu Mkuu, Julius Mtatiro hatua za kuchukua. Taarifa za kukamatwa
Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake zilikuwa zinaenea na kupandisha jazba
ya Waislam wengi. Tulipata wasiwasi kuwa jazba hii inaweza kupelekea
Waislam wengi kuandamana baada ya sala ya Ijumaa. Ikiwa Sheikh
Ramadhan Sanze na wenzake wataachiwa na Waislam wakapata taarifa hiyo
inaweza kusaidia kupunguza jazba na watu wasishiriki maandamano baada
ya sala ya Ijumaa.
Nilimpa jukum Abdul Kambaya afuatilie Central PoliceStation, suala la
kuachiliwa Sheikh Sanze na wenzake. Niliwasiliana naye kwa simu na
kuzungumza na RCO na nikaamini kuwa Sheikh Ramadhan Sanze, Sadik Gogo
na Mzee Abdillah wataachiwa baada ya kukamilisha mahojiano. Ilikuwa
inakaribia saa 12 jioni. Muda wa kuitisha Press Conference haukuwepo.
Tukakubaliana Naibu Katibu Mkuu awasiliane na wahariri wa habari wa
vituo vya televisheni Channel 10, TBC1, Star TV, Mlimani TV na ITV ili
niweze kutoa taarifa ya kuwasihi Waislam warudi majumbani na kwenye
shughuli zao baada ya sala ya Ijumaa.
Niliweza kufanya mahojiano na Channel 10, TBC1, na ITV. Kwa bahati
mbaya Camera person wa Star TV alikuwa kwenye shughuli nyingine na kwa
hiyo sikuweza kufanya mahojiano na Star TV. Vilevile wapiga picha wa
Mlimani TV hawakuwepo kwenye studio. Pia nilipata bahati ya kuzungumza
na Radio Iman inayosikilizwa na Waislam wengi na kueleza maoni yangu
kuwa Waislam wasiandamane baada ya sala ya Ijumaa.
Baada ya kutoa taarifa kwenye vituo vitatu vya televisheni na Radio
Iman kuwa Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake wataachiliwa na kuwasihi
Waislam wasishiriki maandamano baada ya sala ya Ijumaa nilimpigia simu
Abdul Kambaya kuulizia kama naweza kuzungumza na Sheikh Ramadhan
Sanze. Kambaya akanieleza mambo yamebadilika na hawajaachiwa.
Niliwasiliana na RCO na nikabaini kuwa suala hilo haliko tena chini ya
uamuzi wake na litakamilishwa siku ijayo.
Usiku wa alhamisi kuamkia Ijumaa nilijaribu kuwasiliana na Rais
Kikwete kupitia wasaidizi wake ili nimfahamishe mantiki na sababu ya
hatua nilizochukua na atumie uwezo wake alionao Sheikh Ramadhan Sanze
na wenzake waachiliwe. Kwa bahati msaidizi mmoja alipata ujumbe wangu
wa simu na akanipigia simu saa 6:50 usiku na kunifahamisha atajitahidi
kuufikisha ujumbe wangu kwa Mhe. Rais ili nipate kuongea naye kuhusu
jamaa wanaoshikiliwa na polisi waachiwe ili kupunguza jazba na
kuepusha shari. Niliyezungumza naye alikuwa Dodoma na Rais alikuwa
Arusha na ratiba yake ilikuwa imebana sana na kwa hiyo hakuweza kupata
fursa ya kunipigia simu siku hiyo ya Ijumaa.
Siku ya Ijumaa Abdul Kambaya aliendelea kufuatilia kuachiwa kwa Sheikh
Ramadhan Sanze na wenzake Central Police Station. Nami katika
kuhangaika ili waliokamatwa waachiliwe nilipata fursa ya kuzungumza na
IGP na kumfahamisha sababu ya juhudi nilizochukua na mategemeo yangu
kuwa Sheikh Sanze na wenzake wangeachiwa. Ninakiri kuwa katika
mazungumzo ya simu, IGP Mwema alikuwa msikivu na mkarimu sana katika
kauli yake. Alinishukuru kwa kauli niliyoitoa katika vituo vya
televisheni na kuwa atafuatilia suala nililomueleza. Hatimaye Sheikh
Ramadhan Sanze na wenzake waliachiwa.
Naamini kama Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake wangeachiwa ingesaidia
sana kupunguza jazba. Hata hivyo Waislam wengi na wananchi wengine kwa
ujumla walipokea vizuri wito wangu na hawakushiriki katika maandamano.
Baadhi wamenikosoa na kushauri kuwa ilifaa nisubiri mpaka baada ya
maandamano kufanyika na kama patatokea majeruhi na vifo ndipo nitoe
tamko la kulaani vitendo vya polisi na serikali.
Katika mitandao ya kijamii wengine wamekejeli juhudi zangu. Nilikubali
kushiriki katika kipindi cha Makutano show kinachoendeshwa na Bi. Fina
ambapo hupata maswali toka Jamii Forum. Moja ya swali lililotolewa ni
"Muulize very very solid, kuna agenda gani kati ya Cuf na uislam?
mtaani leo wanasema kauli ya Lipumba ya jana kusitisha maandamano
wameitii, na ukiangalia mikutano yake pale jangwani utafikiri kuna
mawaidha ni balaghashia na baibui." Fina hakupata muda wa kuniuliza
swali hili. Jibu lake ni la wazi.
CUF inasimamia Haki Sawa kwa Wananchi Wote. Kuna Watanzania wengi
ambao ni Waislam na wao pia wanastahiki kutendewa haki katika nchi
yao. Kuhusu balaghashia na baibui ni vyema vijana wakatazama picha za
umati wa watu uliokuwa unahutubiwa na Mwalimu Nyerere wakati wa
kupigania uhuru wa nchi hii. Picha hizo pia zinaonyesha waliokuwa
wakipigania uhuru wengi walivaa balaghashia na baibui hata Mwalimu
Nyerere alipewa zawadi nyingi za balaghashia na akaamua kuzivaa.
Kushamiri kwa demokrasia ya kweli msingi wake mkubwa ni amani na
utulivu. Amani ya kweli haipatikani bila kuwepo haki. Kesi ya Sheikh
Ponda msingi wake na madai ya kiwanja. Ki msingi kesi ya madai ya
kusuluhishwa na Mahakama ya ardhi. Sheikh Ponda ana haki ya msingi ya
kupewa dhamana hata kama kauli zake haziifurahishi serikali.
Nasikitika sana katika kipindi hiki tete, viongozi wa serikali
wameshindwa kuchukua juhudi za makusudi kuzungumza na Maimam wa
misikiti na viongozi wa asasi za Kiislam kupunguza jazba. Badala yake
wameachia kauli za vitisho vya Kamanda Kova ndiyo viwe mawasiliano
kati ya serikali na Waislam. Ni vyema serikali ikatumia busara na
kuwasiliana na Maimamu wa misikiti na viongozi wa asasi za Kiislam
kuelewa hoja na malalamiko yao.
Hatimaye nimepata fursa ya kuzungumza na Mheshimiwa Rais leo asubuhi
na nikamueleza juhudi nilizozichukua kuweza kupunguza jazba na
kuwaomba Waislam wasishiriki kwenye maandamano baada ya sala ya
Ijumaa. Ni wazi hali hii ya mtafaruku ndani ya jamii inamsononesha
sana Mheshimiwa Rais na ninaamini atajitahidi kwa uwezo wake wote
kutafuta suluhisho.
Katika kutafuta suluhu ya mtafaruku huu nitaendelea na jitihada za
kutafuta fursa niweze kubadilishana mawazo na Rais Kikwete.
Nitazungumza na viongozi wa asasi za Kiislam. Nitazungumza na viongozi
wa Makanisa ya Kikristo. Madhumuni ya mazungumzo yangu ni
kuwafahamisha mantiki ya juhudi nilizofanya na kushauriana misingi
muhimu ya Waumini wote kuheshimiana na kuvumiliana ili tujenge
Tanzania yenye haki sawa kwa wote.
--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
0 Comments