[wanabidii] Umma walaani Polisi kuua ovyo - NIPASHE

Tuesday, September 04, 2012
 

Umma walaani Polisi kuua ovyo

Na Mwandishi wetu

4th September 2012

B-pepe

Chapa

Maoni

Aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi

Wadau wamelaani vikali kitendo cha polisi kuua Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, na kutaka uchunguzi huru ufanyike kubainisha hasa chanzo cha kadhia hiyo.

Wakati sauti hizo zikipazwa, Jukwaa la Wahariri limepingana taarifa za Jeshi la Polisi kuhusu mauaji ya Mwangosi, kwa kile kinachoonekana ni kama njama za kuficha ukweli wa tukio hilo.

Hayo yakitokea, Mkuu wa Jeshi hilo, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, pamoja na maofisa wengine waandamizi wa jeshi hilo, wamekutana na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuzungumzia hali ya baadaye baada ya kutokea kwa mauaji hayo.

Habari za uhakika zilizolifikia NIPASHE jana jioni zilieleza kuwa mkutano huo ulioitishwa na IGP Mwema, ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Iringa, maofisa wengine waandamizi wa jeshi hilo pamoja na Rais wa Vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Keneth Simbaya.

Chadema katika mkutano huo, iliwakilishwa na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, aliyefuatana na viongozi wengine wa chama hicho.

Kwa mujibu wa habari hizo, mazungumzo hayo yalichukua zaidi ya saa mbili kabla ya IGP Mwema kwenda wilayani Mufindi kujionea mwenyewe eneo la tukio hilo katika kijiji cha Nyololo.

Habari hizo zinasema katika mazungumzo hayo, viongozi wa Chadema walimshutumu Kamanda Kamuhanda wakisema ndiye aliyesababisha vurugu.

Walisema kabla ya hapo Chadema walifanya mkutano wao wa kwanza uliohudhuriwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) bila vurugu kabla ya Kamanda Kamuhanda kufika na kuamuru watu kukaa chini na baadaye kuruhusu watu kupigwa mabomu.

"Ni sheria gani inayoruhusu mtu, ambaye amekaa chini na wengine kukaa ndani ya ofisi kumpiga mabomu? Ndani ya ofisi hiyo yalipigwa mabomu zaidi ya 50. Kitu hicho ni cha kushangaza wakati watu walitii amri na sisi hatukufanya mikutano ya hadhara, bali ni mkutano wa ndani. Ni vigumu kuwaweka ndani watu zaidi ya 100 katika chumba kimoja. Na ndiyo maana watu walikaa nje," habari hizo zimemnukuu Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed, akisema kwenye mkutano huo.

IGP Mwema alisema pamoja na yote yaliyotokea, kikubwa ni jinsi gani mazungumzo yanavyoweza kuleta mwafaka na siyo kila mtu kuchukua maamuzi yake.

Alitaka busara zitumike zaidi ili kufikia maelewano na kukiri kuwa baadhi ya mambo mengine yalikiukwa katika utekelezaji wa tukio hilo ambapo alisema kwa sasa tayari tume imeundwa kushughulikia tatizo hilo ili kubaini ukweli.

Kwa upande wake, Kamishna Manumba alisema ni kitu cha busara kila mtu akaangalia tumetoka wapi na tunakwenda wapi na kila mmoja ni lazima akiri upungufu wake kama binadamu.

Alisema amani ya nchi haitajengwa kwa kutumia nguvu ya risasi, mabomu ama kupinga sheria kwa aina yoyote ile bali pia viongozi wa vyama vya siasa wanao wajibu mkubwa wa kuwazuia wafuasi wao ili kuleta amani nchini.

Dk. Slaa alimtaka IGP Mwema kuwaambia ni kwani nini wamekuwa wakizuia mikutano ya Chadema peke yake wakati vyama vingine vikiendelea kufanya mikutano bila kupigwa mabomu na kumkumbusha kuwa walisitisha operesheni Sangara kupisha zoezi la sensa kwa siku tano, lakini iweje leo waambiwe wao kuwa ndio wakorofi?

Habari za ndani ya kikao hicho zinasema kuwa jeshi hilo lilikubaliana kuwa taratibu zote zifuatwe ili kuhakikisha kuwa watu waliokamatwa katika tukio lile wanapata huduma na taratibu za kisheria zifuatwe na kuunda timu mbili za Polisi na Chadema ili watu walioshuhudia tukio hilo watoe maoni yao katika tume ya usuluhishi.

Baadhi ya viongozi wa Chadema waliokuwapo kwenye tukio hilo watatoa maoni yao walivyoona tukio hilo na kwa upande wa polisi, timu hiyo itaongozwa na Kamishna Manumba.

Katika mkutano huo, polisi na Chadema walikubaliana chama hicho kiendelee na mikutano yake ya ndani kama kawaida na isifanye mikutano yoyote ya hadhara na maandamano mpaka siku zilizoongezwa za sensa zitakapoisha.

Pia walikubaliana kujenga kuaminiana na kuondoa uhasama kati ya viongozi wa Chadema na polisi.

 

 

Share this :

Related Posts

0 Comments