[wanabidii] TOROKA UJE NA TOROKA URUDI: NANI ANASHANGAA?

Saturday, July 15, 2017
Kumeanza uhamiaji (migration) ya wanachama wa CHADEMA kuhamia CCM na nashangaa kuona watu wanashangaa na kusema mengi. Mbaya zaidi kati ya wanaoshangaa na kulaumu ni wahamiaji kutoka CCM waliohamia CHADEMA ambao ama walihama kutafuta kichaka cha kujificha wasishughulikiwe kwa waliyoyatenda ama kwa sababu tusizozijua bado maana siamini kwamba walikwenda kuimarisha upinzani. Wangekuwa walienda kuuimarisha basi watu wangeendelea kutoroka kuhamia huko.
 
Mimi nimegundua kuwa kumbe sasa watanzania wanaongozwa na HOJA kuliko T shirts; pilau na kanga, kama zamani.
 
Turudi nyuma. Nyuma kabisa. Sogea mpaka 2007. Hapo ndipo kulianza mchezo huo. Lilikuwa Bunge la bajeti kama nakumbuka vizuri. Kukatoka hoja ya  Mkataba wa madini wa Buzwagi uliosainiwa na waziri hotelini Uingereza; na ile hoja ya "List of shame". Uchache wa wabunge wa upinzani ulifanya hoja hizi za msingi zipuuzwe mpaka Zitto akatimuliwa Bungeni na Dr. Slaa akaamua hoja kuitoa Bungeni na kuirudisha kwa wananchi.
Baada ya bunge kuahirishwa na wawakilishi wetu kutoka nje ya Mjengo uchache wa wabunge wa upinzani ukapotea na wingi wa wabunge wa CCM ukapotea pia. Wabunge wa CCM wakazomewa majimboni. Kuanzia hapo moto wa watu kukihama chama cha mapinduzi kukashamiri. Ni wale waliokuwa na maslahi binafsi au wachache wanaoongozwa na itikadi ndio tulibaki CCM. Wengi walitoroka. Lakini hata tuliobaki haikuwa kazi ndogo. Ufisadi na ukumbatiaji rushwa wa viongozi wa CCM ulikipiromosha chama cha mapinduzi mpaka 'kikanuka' badala ya kunukia. Nikumbushe mwana-CCM mmoja aliyekatisha Kariakoo amevaa nguo za CCM. Nani anakumbuka kilichompata? Kuelekea 2014 mpaka 15 ilikuwa ni aibu kuwa mwanachama wa CCM. Siku moja nilivaa tracksuit ya CCM na kukatisha mjini Bukoba nikazomewa sana kabla vijana hawajajua ni mimi, (maana msimamo wangu katika eneo hilo unafahamika kuwa mimi ni MwanaCCM anayetumia chama kuendeleza utanzania.
 
Hoja za Upinzani zilitikisa dunia ya Tanzania. Kama CCM si kuwa nyuma ya dola huenda kingesambaratika zaidi. Hata waliojilazomisha kubaki tulikuwa na makundi mawili: Moja liliamini hakitafufuka kwa hiyo likaanzisha chama cha CCJ, na wengine tulifikiri hakitaweja kujirekebisha kikiwa madarakani kwa hiyo tuungane na upinzani kuking'oa kikae pembeni, manyang'au wakikimbia wanachama halali tukibaki tutakirekebisha.
Watanzania wote tunaamini kuwa ni juhudi hizi za HOJA za upinzani zilizosaidia sana kukirekebisha Chama cha mapinduzi mpaka kufikia kuteua watu wasiotarajiwa kugombea nafasi muhimu ikiwemo ya Urais. Ninaandika makala inakuja kujadili "Nani alimpa mwingine Urais 2015: CCM ilimpa Magufuli au ni Magufuli aliipa CCM?" Ukweli baada ya Magufuli kupitishwa kugombea urais nilijua watafungana na mgombea wa CHADEMA yaani Dr. Slaa. Mpaka Slaa "anatoroka" CHADEMA, nilikuwa sijaamua nani atapata kura zangu (ninazo nyingi!) kati ya wawili hao.
 
Sera za upinzani wakati ule ziliwagusa wananchi kwa sababu ya chama hicho kujikita kuongelea maswala yanayotatiza wananchi. CCM iliandaa ilani yake kuyashughulikia lakini hakuna aliyeamini kuwa yatafanyiwa kazi maana siku zote Ilani za CCM nzuri tu. Shida ilikuwa utekelezaji wa Ilani. Ilikuwa rahisi kukosa pesa za dawa lakini si za vikao vya madiwani. Kukosa fedha za madawati na madarasa lakini si za rais kwenda kutumbua nje.
 
Msingi wa kinachotokea sasa cha wanaCHADEMA Kutoroka kurudi walikotoka uliwekwa kuanzia chama hicho kilipolazimika kutelekeza HOJA zake ili kuruhuzu 'watoto" kutoka CCM. CHADEMA ilitelekeza hoja zake tena bila kuwa na hoja mbadala yenye mashiko kwa wananchi. Tulisema hatukusikika. Tulitahadhalisha na kuandika makala bila kusikiwa. Mfano wa Sangara kutoishi akihama bwawa ulikuwa mfano hai. Lakini sikio la kufa bwana!!
 
Ni dhahili kuwa vyama vya upinzani vimekosa hoja vikakosa mtetezi. Hakuna mtu angeweza kutoa amri ya kuzuia hata mikutano ya chama cha upinzani ikatekelezeka kati ya 2014 na 15. Neno NGUVU YA UMMA lilikuwa moto wa kuotea mbali. Nakumbuka wakati Fulani Halima mdee alikwenda kufanya ziara Kyerwa Mkoani kagera. Nikawasikia Askari polisi wakiwaambia viongozi wa CHADEMA kuwa "tumetumwa kuwatawanya". Hii ilikuwa kawaida askari kuwatonya CHADEMA. Na kuwatawanya hakukufanikiwa. Watu walikusanyika kusikia hoja. Sasa ni rahisi kuionea CHADEMA. Na Kweli inaonewa. Unyanyasaji wa wabunge Bungeni ulitokea 2007. Kilichotokea baadaye kilifanya "Mzee wa Viwango" awe wa viwango kweli. Aligundua kuwa pasipo kusikiliza hoja za Upinzani chama chake kinapoteza dola.
 
Hivi wakati ule wa hoja moto moto nani angethubutu kuondoa bunge Live? Hajipendi? Lakini sasa ilifikia hatua watu wanafunga TV wakisimama wabunge waporomosha matusi. Kuliondoa bunge Live ikawa neema. Kisa Chama KIKUU cha upinzani kupoteza UKUBWA. Kikabaki kikuu lakini sio KIKUBWA.
 
Tunakoelekea Nchi hii inageuka ya Chama kimoja kama Botswana. Bila mikakati maalum haitaepukika.
 
Dawa ni moja: Wapinzani tulia kwanza. Jiangalie mweleka huu ulianzia wapi? Bada ya hapo sera ya 'VUA GAMBA VAA GWANDA itekelezeke ndani ya CHADEMA. Hakuna cha kuogoba cha "tutamuanzaje kumwambia wewe ndiyo tatizo".
Baada ya matengenezo ya ndani, wekeni mifumo na ifuateni. Kama uchaguzi ni hivi hakuna kuwa hivyo. Onyesheni demokrasia ya kweli kwanza kwenye chama.
Huku hayo yakifanyika yaangalie kisayansi mazingira ya kisiasa tuliyomo. Haiwezekani Serikali ikawa kamilifu. Ili uaminiwe anza kwa kuyaongelea mafanikio. Tukiwa pamoja katika hilo ndipo ukosoaji uje. Uwe ukosoaji wa hoja. Lengeni maisha ya watanzania sio uchaguzi. Muda utapita lakini CHADEMA itarudi kwenye nafasi yake. Mkifikia hapo hakuna atakayeweza kusema mikutano ya siasa basi. Ataogopa nguvu ya Umma. Hataogoba ukuu wa chama cha upinzani bali UKUBWA wake.
Kinyume chake watatoroka sana. Watabaki watu mbumbumbu wasio na elimu (hata kama wana ma-degree).
CHADEMA mmesikia???
 
Elisa Muhingo
0767 187 507
 
--


Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.


Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments