Johnson Mbwambo
NIANZE kwa kuwashukuru mamia ya wasomaji wangu ambao nikiwa huku kijijini kwangu wamekuwa wakiendelea kunitumia sms za kunisihi niendelee kuandika katika safu hii kuwakumbusha Watanzania mgombea urais yupi anastahili kupigiwa kura Oktoba 25 – Jumapili ijayo.
Baadhi yao walifikia hatua ya kutaka kunitumia fedha ili niweke mtu wa kuangalia shughuli zangu za kilimo huku kijijini, na kisha nirejee Dar kuendelea kuandika makala za kuwaamsha Watanzania wasimpigie kura mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Nawashukuru wote kwa imani kubwa waliyoionyesha kwangu. Hata hivyo, nilikataa ombi hilo kwa sababu si sahihi kurubuniwa kwa fedha kufanya jambo fulani unaloliamini moyoni, na pia kwa sababu siko huku kijijini kwa ajili tu ya shughuli za kilimo. Nipo pia kijijini kwa ajili ya kumuuguza mama yangu mzazi anayesumbuliwa na maradhi ya utu uzima.
Nilisema katika makala yangu ya mwisho kuwa sitaandika tena katika safu hii hadi Desemba nitakaporejea Dar. Hata hivyo, baada ya kupata fursa huku kijijini ya kuhudhuria mikutano ya kampeni ya wagombea urais – Edward Lowassa wa Chadema na John Magufuli wa CCM, nimeamua kubadili uamuzi huo, na hivyo kuandika makala hii ya mwisho kabla ya Oktoba 25 – siku ya upigaji kura.
Kilichonifanya nibadili uamuzi huo ni baada ya kuhudhuria mkutano wa Lowassa na kujiridhisha kuwa kile kinachozungumzwa kwa kunong'ona kwamba afya yake ina utata kina ukweli ndani yake. Baada ya kumuona mwenyewe akizungumza, nimejiaminisha kuwa hali yake ya afya ni ya utata.
Kabla ya kurejea hapa kijijini Ndungu, Same Mashariki, niliisikia minong'ono ya utata wa hali ya afya ya Lowassa nikiwa Dar. Ni kwa sababu ya minong'ono hiyo nilikuwa nikiangalia kwa makini kwenye luninga hotuba zake za kampeni ili kutafuta ishara zozote zitakazonithibitishia ukweli wa madai hayo ya utata wa afya yake. Hata hivyo, hotuba zake za luninga hazikunitosha kunifanya niamini pasi shaka yoyote ukweli wa minong'ono hiyo.
Lakini nimeamini sasa ukweli wa minong'ono hiyo baada ya kumshuhudia mwenyewe akihutubia hapa kijijini. Kabla ya ujio wake hapa kijijini, gumzo kubwa kati ya wafuasi wa Chadema na CCM lilikuwa kuhusu hali ya afya ya mgombea urais huyo.
Wafuasi wa CCM walikuwa wakidai ya kuwa hali ya afya ya Lowassa ni tete; huku wafuasi wa Chadema wakijibu mapigo kuwa hali yake ya afya inatiwa chumvi mno na CCM kwa sababu ya kumhofia kuwa anaweza kushinda uchaguzi na kuingia Ikulu.
Naamini malumbano kama hayo yametanda hivi sasa nchi nzima.
Kwa hiyo, mamia ya watu waliofurika katika mkutano wake hapa kijijini (wakiwemo wa kutoka vijiji vya jirani), kusema kweli, hawakwenda kusikiliza sera zake au kuangalia chopa yake; bali walikwenda kutafuta jibu la suala lililokuwa likiwatatiza la ukweli kuhusu hali yake ya afya.
Niseme ya kwamba kama Lowassa na timu yake ya kampeni wangelijua hilo mapema, bila shaka wangelimwandaa mgombea wao (kama inawezekana) asionyeshe dalili zozote ambazo zingewathibitishia wanavijiji hao kuwa ni mgonjwa, na kwamba hastahili kubebeshwa 'suluba' za kuiongoza nchi.
Na kwa sababu hawakumwandaa Lowassa, bila kujitambua akawapatia 'jibu' wanavijiji wale kuwa kweli hali yake ya afya si nzuri sana. Nasema hivyo kwa sababu kwa muda mfupi tu aliokaa hapo kijijini aliwaonyesha wanavijiji dalili zile zile za udhaifu wa afya yake walizokuwa wakibishania – yaani kutembea kwa shida, kuzungumza kwa shida, kushindwa kuhutubia kwa zaidi ya dakika 10, kushindwa kutumia mikono kusisitiza hoja zake, na mbaya zaidi kwenda msalani mara mbili katika kipindi kifupi tu alichokaa jukwaani!
Kwa hakika, haikunishangaza kwamba baada ya kumaliza mkutano wake huo wa kampeni na kuondoka, gumzo liliendelea kupamba moto huku nyuma kuhusu utata wa hali yake ya afya; huku baadhi ya wafuasi wa Chadema wakinywea na kukubali kwamba kweli mgombea urais wao hana afya nzuri ya kuhimili 'suluba' za Ikulu.
Baada ya Mh. Lowassa kuondoka, baadhi ya wanakijiji, kwa kutambua kuwa mimi ni mwandishi wa habari na waandishi wa habari wanapaswa kujua mambo mengi, walinifuata na kuniomba niwaeleze ni tatizo gani hasa la kiafya linalomkabili Lowassa. Sikuwaeleza lolote kwa sababu hata mimi sijui nini hasa kinamsibu; japo nilijiridhisha kwenye mkutano huo kuwa kweli ni mgonjwa.
Nieleze hapa pia kwamba siku tatu baadaye Magufuli naye aliingia kijijini kwetu na kufanya mkutano wa kampeni kama alioufanya Lowassa. Kwa waliohudhuria mikutano yote miwili ilikuwa ni rahisi kwao kuelewa ni nani akiingia Ikulu anaweza kuwa rais mkakamavu na mchapakazi kati ya Magufuli na Lowassa.
Hicho – ndugu zangu – ndicho kilichonifanya niandike makala hii ya mwisho kwa sababu katika makala zote nilizoandika kuhusu ugombea urais wa Lowassa nilijadili kwa kina suala la tuhuma za ufisadi zinazomwandama kwa miaka 20 sasa (na si Richmond tu ya majuzi) lakini si hilo la utata wa afya yake.
Nimeamua katika makala hii ya mwisho kabla ya uchaguzi nilizungumzie kidogo hilo suala la utata wa afya yake ambalo waandishi wetu wanaogopa kuligusa hata kwa kuomba tu ufafanuzi kutoka kwa Lowassa mwenyewe au kwa Team Lowassa.
Kwa hakika, binafsi sielewi mpaka sasa ni kwa nini Team Lowassa wanapuuza kulizungumzia (kulifafanua) suala hilo; ilhali limekuwa ndiyo gumzo kubwa nchi nzima katika kampeni za safari hii.
Mgombea urais (Lowassa) anatumia chopa kukampeni badala ya gari linalopita kwenye vijiji vingi. Wananchi wanahoji iweje kwenye kampeni mgombea urais atumie chopa tu? Je, akiingia Ikulu atazuru vijiji vya Tanzania kwa chopa?
Lakini Team Lowassa haijibu swali hilo, na hivyo wananchi wanajitafutia wenyewe jibu lao; nalo ni kwamba ni mgonjwa na hivyo hawezi kusafiri kwa gari vijijini kama afanyavyo Magufuli!
Mgombea urais (Lowassa) anasubiriwa kwa zaidi ya saa nne, anafika kwenye mkutano anazungumza kwa dakika 10 tu, na kisha anawaachia kina Mbowe, Sumaye na sasa Kingunge wazungumze kwa muda mrefu kana kwamba wao ndiyo wanaogombea urais!
Wananchi wanahoji kulikoni? Team Lowassa inaendelea kukaa kimya, na hivyo wananchi wanajitafutia jibu lao. Na jibu lao ni hili; ni mgonjwa hawezi kusimama jukwaani na kuzungumza kwa muda mrefu.
Mgombea urais (Lowassa) akiwa jukwaani hazungumzi kwa sauti kubwa inayosikika vizuri uwanja mzima unakofanyika mkutano wa kampeni, na wala hawezi kutumia mikono kusisitiza hoja zake.
Hata pale anapowachagiza wafuasi wake wa Chadema kwa kauli mbiu yao maarufu ya peoples' power hawezi kuinua mkono wake juu kabisa kama inavyopaswa au kama wafanyavyo wengine. Wananchi wanahoji kulikoni lakini Team Lowassa inakaa kimya – haina jibu.
Kukosa kwao jibu kunawafanya wananchi watafute jibu lao wenyewe. Na jibu lao ni kwamba Lowassa anaumwa, na hivyo hawezi kunyanyua juu mikono yake au kuitumia kusisitiza hoja zake kama ilivyo kawaida kwa mzungumzaji yeyote jukwaani.
Wako pia wanaohoji kutoka kwake jukwaani na kwenda msalani zaidi ya mara moja katika kipindi kifupi tu (kama ilivyotokea kijijini kwangu) lakini Team Lowassa imekaa kimya bila kufafanua hilo. Haitaki kulizungumzia hilo, na hivyo jibu la wananchi linabaki lile lile – ni mgonjwa!
Chukulia mfano mwingine wa majuzi huko Tunduma. Umati ulifurika lakini mgombea huyo akashindwa kuzungumza nao bila kipaza sauti hata kwa hizo dakika 10 tu. Lakini Mbowe yeye aliweza kuzungumza kwa sauti kubwa iliyosikiwa na wote. Kwa nini Mbowe aweze Lowassa ashindwe?
Team Lowassa haitaki kujibu swali hilo, lakini jibu la wananchi ni kwamba hali yake ya afya si nzuri na hivyo hawezi kuzungumza bila kipaza sauti umati ukamsikia.
Kwa sababu ya ukosefu wa ufafanuzi kuhusu kasoro hizo za Lowassa, minong'ono kuhusu suala hilo la utata wa afya yake inaendelea; huku wananchi wengi (nikiwemo mimi) sasa wakiamini kwamba ni kweli afya ya mgombea urais huyo ina walakini.
Ukweli ni kwamba minong'ono hiyo ilianza muda mrefu uliopita. Naamini ni kwa sababu ya minong'ono hiyo Lowassa alipata kuandaa mjini Dodoma apigwe picha akifanya mazoezi, na picha hizo zikatumwa na kuchapwa katika magazeti mengi nchini. Naamini lengo la hatua hiyo ilikuwa ni kufifisha minong'ono hiyo kuhusu afya yake.
Hata hivyo, minong'ono hiyo ilipamba moto wakati gazeti ndugu na hili la Raia Tanzania liliporipoti, mwanzoni mwa mwaka huu, kwamba Lowassa alishindwa kubeba tofali wakati akiweka jiwe la msingi kwenye mradi mmoja mkoani Arusha!
Badala ya kufafanua jambo hilo, Lowassa alikasirishwa mno na habari za gazeti hilo kiasi kwamba baadaye alimpiga marufuku mhariri wa Raia Mwema kuhudhuria mkutano wa wahariri wa vyombo vya habari nchini aliowaita Dodoma Julai mwaka huu.
Mhariri wetu alizuiliwa mlangoni, lakini Team Lowassa ilipong'amua baadaye kuwa imefanya kosa kubwa kumzuia mhariri huyo, Lowassa akalazimika kumpigia simu usiku kumwomba radhi na kumwita usiku huo huo ili ampe taarifa ya kilichojiri kwenye mkutano huo aliozuiliwa kuhudhuria.
Kwa mtazamo wangu, kikao kile cha wahariri cha mjini Dodoma kilikuwa ni fursa maridhawa kwake kufafanua kuhusu suala hilo la utata wa afya yake, lakini naambiwa yeye Lowassa alikataa kabisa kuzungumzia suala hilo. Na ndo maana minong'ono imeendelea mpaka leo.
Hata mkewe – Regina Lowassa – hakutoa ufafanuzi wa kina kuhusu suala hilo wakati ule alipozungumza na wanawake wa Chadema jijini Dar hivi karibuni. Aliishia tu kusema ya kuwa suala la afya ya mumewe Lowassa aulizwe yeye Regina!
Je, kauli kama hiyo inatosha peke yake kumaliza minong'ono hiyo ya muda mrefu? Jibu ni hapana, na ndo maana suala la utata wa afya yake limeendelea kuwa gumzo kubwa nchini mpaka sasa tunapoelekea Jumapili ya Oktoba 25 – siku ya kupiga kura.
Ndugu zangu, bila hata kuelezwa lolote na Lowassa mwenyewe au na mkewe Regina au na Team Lowassa, mtu yeyote yule aliyebahatika kumwona jukwaani Edward Lowassa akihutubia mkutano wa kampeni katika hizo dakika 10 zake, atakubaliana nami ya kwamba Lowassa huyu si yule Lowassa wa mwaka 2005. Lowassa huyu wa sasa ana matatizo ya afya; japo yeye mwenyewe na timu yake ya kampeni hawataki kukiri hilo.
Sina haja ya kusisitiza sana hapa umuhimu wa kuchagua rais mwenye afya njema kwa sababu mhariri wa gazeti hili, Ezekiel Kamwaga, alilifafanua vyema suala hili katika makala yake ya wiki iliyopita iliyobeba kichwa kinachosomeka: Watanzania wote tukipiga push ups uchumi utapaa.
Hata hivyo, nikumbushe tu hapa kwamba itakuwa ni usanii tu kama mgombea urais atawaahidi wapiga kura 'mchakamchaka' wa maendeleo; ilhali yeye mwenyewe hawezi hata kunyanyua mikono yake juu au hata kuzungumza jukwaani kwa zaidi ya dakika 30!
'Mchakamchaka' upi huo wa maendeleo unaoweza kusimamiwa na rais mgonjwa asiyeweza kuzungumza jukwaani hata kwa dakika 30 tu? Rais wa namna hiyo anawezaje kuendesha kikao marathon cha baraza la mawaziri au mkutano wa zaidi ya saa tatu bila mapumziko?
Ndo maana kwa wenzetu Ulaya na Marekani suala la afya ya rais ni suala muhimu mno. Marekani au Ulaya huwezi kuwa ni mgombea urais mwenye afya yenye utata, na kisha wakakachagua kuwa rais wao.
Ndo maana Wamarekani walimkataa mgonjwa John McCain (Republican) na kumchagua mkakamavu Barack Obama (Democrat). Ndo maana pia Warusi walimkataa mgonjwa Boris Yelsin na kumchagua mkakamavu Vladimir Putin. Mifano iko mingi kote duniani. Hakuna watu wanaopenda kutawaliwa na rais mgonjwa popote pale duniani. Huo ndiyo ukweli.
Kwa hiyo, Watanzania tunapoelekea Jumapili ya Oktoba 25 – siku ya uchaguzi, ni wakati muafaka kwetu sote kufanya tafakuri jadidi na kujiuliza iwapo kuna busara yoyote kumchagua urais mgonjwa Edward Lowassa na kumwacha mchapakazi John Magufuli kwa sababu tu mmoja ni Chadema na mwingine ni CCM.
Au kwa sababu tu tunataka mabadiliko. Kufanya hivyo itakuwa ni uendawazimu wa kihalaiki.Tukifanya hivyo, basi, pengine sisi ni mazuzu tusiofahamu athari za kumwingiza Ikulu rais ambaye ni mgonjwa. Hapana ndugu zangu, tunahitaji rais mkakamavu na mwenye afya nzuri anayeweza kuchapakazi hadi hata saa 6 usiku, na siku inayofuata akawa wa kwanza kuingia ofisini asubuhi!
Na hii inanikumbusha Rais Paul Kagame wa Rwanda. Huyu ni rais mkakamavu anayepiga mzigo Ikulu hadi saa 6 au saa 7 usiku! Mwaka 2006 wahariri kadhaa wa Tanzania tulibahatika kualikwa na Serikali ya Rwanda kutembelea nchi hiyo.
Tulipoomba kukutana na Rais Kagame tukapangiwa miadi ya kumuona saa 12 jioni.
Tulipofika Ikulu tukamkuta yumo mkutanoni. Tukalazimika kusubiri hadi saa 4 usiku ndipo alipotoka nje kuzungumza nasi. Yaani ni milolongo ya mikutano ya kufuatilia utendaji wa serikali yake hadi saa 7 usiku!
Kama leo tunakubali ya kwamba Rwanda imepiga haraka hatua kubwa kimaendeleo kutuzidi sisi Tanzania, ni kwa sababu ina rais mchapakazi. Lakini zaidi ya yote ni kwa sababu ina rais aliye mkakamavu na mwenye afya nzuri.
Nakumbuka pia kwamba waziri mkuu wetu wa zamani, marehemu Edward Moringe Sokoine, naye alikuwa kama Kagame – yaani alikuwa anachapa kazi hadi saa 6 au saa 7 usiku! Ilikuwa ni kawaida kwake kuwapigia simu mawaziri wake usiku kuwauliza hili na lile au hata kuwaita usiku huo huo ofisini kwake!
Je, hayo yaweza pia kusemwa hivyo hivyo kwa mgombea urais wetu kupitia tiketi ya Chadema, Edward Lowassa? Je, Lowassa huyu tunayemwona kwenye mikutano ya kampeni akipata shida kuzungumza au kunyanyua mikono yake anaweza kweli kuchapa kazi Ikulu hadi saa 6 au 7 usiku? Labda kama tunataka kumuua kwa kuzorotesha zaidi afya yake.
Kwa Magufuli sina shaka hiyo, lakini kwa Lowassa nasita kutoa jibu la 'ndiyo'. Kwa Magufuli sina shaka yoyote kwamba atakuwa kama Kagame kwa uchapakazi wa hadi saa 6 usiku. Sina shaka kwa sababu ameshathibitisha hivyo kwa uchapakazi aliouonyesha kwenye wizara alizozisimamia ikiwemo ya Ujenzi.
Ndugu zangu, nihitimishe kwa kusema hivi: Nimelijadili suala hili la utata wa afya ya Edward Lowassa nikitambua kuwa suala la afya ya mtu ni jambo nyeti na siri. Natambua pia kwamba si ubinadamu au uungwana kujadili suala la afya ya mtu gazetini.
Lakini ndugu zangu, kazi ya urais ni kazi nyeti duniani kushinda kazi nyingine zote, na hivyo tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania kama tutaendelea kuifanya hali ya afya ya mgombea urais wao kuwa siri.
Ndo maana kipindi kile Rais Kikwete alipoenda Martekani kwa matibabu na kulazwa hospitalini kwa muda mrefu ilikuwa ni lazima umma wa Watanzania uelezwe nini hasa ugonjwa wa rais wao. Ndipo sote tulipojua ya kwamba kumbe alikuwa akisumbuliwa na tezi dume. Nirudie tena afya ya rais wa nchi haiwezi kufanywa jambo la siri.
Ni hivyo hivyo kwa wagombea urais wetu. Itakuaje kama tutampigia kura mgombea dhaifu kiafya, na kisha akiingia Ikulu hali ya afya yake ikazidi kuwa mbaya? Ni heri watu wajue mapema wafanye maamuzi wenyewe wakiwa na taarifa sahihi kuliko kuwaficha. Urais si jambo la kupeana kura za huruma!
Najua wako watakaonilaumu na pengine kunitukana sana na kunitishia maisha kwa kuchokonoa suala hili la afya ya Lowassa. Najua pia wapo watakaosema kwamba sijawahi kuugua, na ndiyo maana nakosa huruma na kuanika hadharani mapungufu ya kiafya ya mtu mwingine anayeugua.
Napenda niwajibu mapema wote hao ya kwamba hata mimi najua kuugua ni nini. Si tu niliwahi kulazwa ICU pale TMJ kwa zaidi ya siku mbili, lakini pia nilipelekwa hadi Appolo India kutibiwa. Kwa hiyo najua kuugua ni nini, na najua pia kwamba kifo kinaweza kutokea kwangu muda wowote Mungu atakaponiita.
Lakini pamoja na kutambua yote hayo, si dhambi wala kukosa heshima au uungwana kuhoji afya ya mgombea urais wetu. Na sihoji kwa sababu labda binafsi namchukia Lowassa.
Nimeshasema tena na tena kwamba sina sababu yoyote binafsi ya kumchukia Lowassa. Nampenda Lowassa kama ninavyowapenda binadamu wengine ila tofauti inakuja tu kwenye suala la yeye kuutaka urais kwa udi na uvumba; ilhali ni mtuhumiwa wa ufisadi na ni mgonjwa.
Kwenye suala hilo bado nitashikilia msimamo wangu wa muda mrefu kuwa Lowassa hafai kuwa rais wa nchi yetu. Kama si kwa sababu ya kuhusishwa na tuhuma za ufisadi kwa miaka 20, basi angalau kwa sababu ya utata wa afya yake.
Kwa mtazamo wangu, moja kati ya kasoro hizo mbili inatosha kuliweka pembeni jina lake Oktoba 25, na badala yake kumchagua mchapakazi John Pombe Magufuli.
Kama huamini kuwa Lowassa ni mtuhumiwa wa miaka mingi wa ufisadi; je pia huamini ya kuwa afya yake ina utata?
Je, uko tayari kumuingiza Ikulu mtu mwenye utata wa afya wa kiasi hicho kikubwa kinachompunguzia uwezo wa utendaji wake?Tuambizane ukweli - Lowassa anaumwa. Tumwonee huruma kwa kumuepusha na 'suluba' za kazi ngumu za urais Ikulu - leo mgomo wa madaktari, kesho mgomo wa waalimu, keshokutwa ukata serikalini, mtondogoo tatizo la umeme nk!
Je, kweli rais mgonjwa atazimudu 'suluba' za kushughulikia matatizo kama hayo au ndo tunataka 'kumuua' mapema kwa presha za mara kwa mara Ikulu? Hapana ndugu zangu, tumwokoe Lowassa na suluba za sampuli hiyo za Ikulu. Tumchague mgombea mwenye afya imara ambaye ni Magufuli.
Na kwa kufanya hivyo maana yake si kwamba hatumpendi Lowassa. La hasha. Lowassa tunampenda, na tutaendelea kumpenda lakini (kama Brutus alivyomwambia Julius Kaizari kwenye igizo la Shakespeare – nakupenda Kaizari lakini naipenda Roma zaidi yako) nami niseme; tunaipenda Tanzania yetu kuliko tunavyompenda Edward Ngoyai Lowassa. Tafakari.
Raia Mwema
0 Comments