[wanabidii] Mawaziri kuchunguzwa

Wednesday, October 14, 2015

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, atatumia muda mrefu kutangaza baraza lake la mawaziri endapo atashinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ili kujiridhisha kwamba watakaopita kwenye chujio ni wale wasio na kashfa, Raia Mwema, limeambiwa.

Taarifa hizi mpya zimekuja katika wakati ambapo tayari ametangaza kuunda jopo la wataalamu wazalendo wa masuala mbalimbali watakaomsaidia kufanya uchambuzi wa masuala muhimu anayoweza kuyatatua haraka mara atakapoanza urais.

Vyanzo vya gazeti hili vilivyo karibu na Magufuli vimeeleza kwamba mgombea huyo anataka kutumia staili iliyotumiwa na Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari, ambaye ametangaza baraza lake la mawaziri takribani miezi sita baada ya kushinda uchaguzi.

"Magufuli ameamua kwamba atachagua mawaziri ambao wataendana na kasi yake, wasio na kashfa na ambao wataweza kumudu changamoto za utawala wake. Ndiyo maana itabidi ajiridhishe kwa mengi.

"Kama ikibidi, kuna uwezekano wa watu wanaotakiwa kupewa uwaziri kuchunguzwa kwanza na vyombo vya usalama kuhusu historia zao za huko nyuma na sasa. Wanahusiana na nani? Ni wasafi? Hawataichafua serikali yake? Yote hayo yatasababisha wapekuliwe kwenye maisha yao," kilisema chanzo hicho ambacho ni sehemu ya timu ya kampeni ya CCM.

Mjumbe huyo ambaye ni miongoni mwa wale wanaozunguka naye kwenye mikoa mbalimbali, alisema Magufuli amedhamiria kuunda serikali ambayo wananchi watakuwa na imani nayo kuanzia siku yake ya kwanza madarakani.

Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Tanzania zinazoendelea hivi sasa, Magufuli amekuwa akisema kwamba anachukia rushwa na kwamba amedhamiria kuunda Mahakama Maalumu itakayokuwa ikishughulika na rushwa kubwa ambayo amekuwa akiita "Mahakama ya Majizi".

Raia Mwema ambalo ndilo pekee lililoweza kumhoji Magufuli tangu alipojitosa kwenye kinyang'anyiro hicho, linafahamu kwamba mgombea huyo tayari amejiwekea utaratibu wa kampeni ambao unamuepusha kukutana na watu ambao wana historia zenye utata.

Gazeti hili linafahamu kuwa Magufuli, ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, hakutani na watu asiowafahamu au wenye kashfa za kifisadi kabla au baada ya mikutano yake ya kampeni inayoendelea hapa nchini.

Mawaziri hao wapya watakaoteuliwa endapo Magufuli atashinda katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, watatakiwa kutekeleza mapendekezo mbalimbali ya kitaalamu ambayo jopo hilo la Magufuli litakuwa limeyafanyia uchambuzi.

Jopo hilo na hadidu zake za rejea ilizopewa lilitangazwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Makamba alizitaja hadidu hizo kumi za rejea kwa jopo hilo kuwa ni "Kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo serikali itabana matumizi, ikiwemo manunuzi ya umma, posho za vikao na matumizi ya magari, ili atoe maamuzi kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa;

"Kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo serikali itaongeza mapato mara moja bila hatua za kibajeti kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa. Kuchunguza na kupendekeza maboresho makubwa katika mfumo wa utendaji na utumishi na ufanisi katika Serikali;

"Kupitia kodi na ushuru wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wa ngazi zote, wakulima, wafugaji na wavuvi iwapo unaweza kurekebishwa bila kuathiri bajeti ya serikali inayotekelezwa sasa," alisema Makamba.

Katika maeneo hayo ya awali, Magufuli inaonekana anataka kuongeza mapato ya serikali ili iweze kutoa huduma zaidi kwa wananchi na pia kupunguza matumizi ya serikali yasiyo ya lazima ili kutunisha mfuko wa serikali.

Masuala mengine ambayo jopo hilo la wataalamu litayaangalia kwa kina ni; "Kupitia sheria zote za nchi na kuorodhesha sheria ambazo zinapaswa kubadilishwa haraka ili kuharakisha mabadiliko ya kweli na ya haraka ambayo ameyaahidi kwa Watanzania;

"Kupitia na kuorodhesha masuala yote na kero zote zinazosubiri maamuzi ya Serikali ili atoe uamuzi kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa.

"Kupendekeza miundo na idadi ya Wizara na kutengeneza rasimu za mikataba ya kazi kwa Mawaziri, Makatibu Wakuu na watendaji wengine wakuu atakaowateua mara baada ya kuapishwa.

"Kupendekeza njia za haraka za kumaliza kero za watumishi wa umma, hasa walimu, askari, madaktari na wauguzi, ili aanze nao kazi wakiwa na ari na morali ya kusukuma mabadiliko ya kweli.

"Kutengeneza rasimu ya mpango-kazi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM na ahadi alizozitoa kwenye kampeni, hasa upatikanaji wa ajira kwa haraka na umeme wa uhakika.

"Kupendekeza muundo wa kitaasisi na utaratibu muafaka wa kutekeleza ahadi ya kutoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na mtaa nchini," alisema Makamba.

Kwa kutazama hadidu hizo za rejea kwa jopo alilounda Magufuli, inaonekana kuwa mgombea huyo wa CCM ana lengo la kupunguza ukubwa wa baraza lake la mawaziri kama anavyoahidi katika wakati huu wa kampeni.

Hadidu hizo za rejea kwa jopo zinaonyesha kuwa Magufuli pia anataka kuwa na suluhisho la kudumu la matatizo ya ajira nchini pamoja na suala la matatizo ya umeme yanayogubika taifa hivi sasa.

Katika historia ya siasa za Tanzania, Magufuli atakuwa mgombea wa kwanza wa nafasi ya urais ambaye ataingia madarakani wakati tayari akiwa na picha ya nini anatakiwa kufanya kuibadilisha nchi kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu wa ndani.

Baadhi ya wasomi kama Profesa Issa Shivji wamekuwa wakilaumu kwamba baadhi ya mipango ya kuikwamua Tanzania kutoka ilipo imekuwa haifanikiwi kwa sababu imekuwa ikiandaliwa na wataalamu kutoka nje ya nchi ambao hawajui maslahi ya taifa letu wala mazingira yake.

Raia Mwema

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments