[wanabidii] Lowassa na Magufuli, nabii hakubaliki nyumbani

Wednesday, October 14, 2015
Privatus Karugendo

UKIONA nabii anakubalika nyumbani, anasifiwa na kupongezwa, ujue huyo hafanyi kazi zake za kinabii. Hata ukiangalia kwenye misaafu, daima nabii alionekana kama adui wa umma. Maana aliwaambia watu yale wasiyotaka kusikia. Nabii akiona mawingu, atasema mvua itanyesha. Hata kama jamii husika, haina haja ya mvua, au mvua inaleta maafa, ni kazi ya nabii kusema mvua sasa inakuja.

Waandishi wa habari na wachambuzi wa masuala ya kijamii, kisiasa, kidini na kiuchumi, tunafanya kazi ya unabii. Na mwandishi au mchambuzi mzuri hawezi kusifiwa au kupongezwa mara zote, maana kama anafanya kazi yake vizuri, ni lazima atagusa yale ambayo watu hawataki kusikia. Ukiyagusa hayo, ni lazima utukanwe na kuchukiwa na wale wasiopenda kusikia ukweli. Katika hali ya kawaida, ukweli ni mchungu pamoja na tujuavyo kwaba ukweli utatufanya huru.

Nabii wa kweli hawezi kulipwa ili aifanye kazi yake. Huwezi kulipwa ili uwaambie watu yale wasiyotaka kusikia. Maana matokeo yake si mazuri, ni matusi na labda kifo. Hivyo nabii wa kweli, anafanya kazi yake kwa kusukumwa na dhamira yake ndani ya moyo wake. Kinyume na hapo atakuwa nabii bandia.

Matusi na vitisho ninavyopokea, ninapoandika juu ya Lowassa, ni ishara ya wazi kwamba ninafanya kazi yangu ya unabii vizuri. Ni kuona mawingu na kusema sasa mvua itanyesha. Wale wasioipenda mvua, wanachukia na kutukana.

Wanaonitukana, wanasema hawatasoma tena makala zangu, lakini la kushangaza kila Jumatano, matusi yanaongezeka na nikiangalia namba za simu ni wale wale. Kumbe bado wanasoma? Ni wazi si mimi peke yangu ninayesema kwa sasa, Magufuli, anafaa zaidi ya Lowassa. Wako wengi wamesema hivyo. Kuwahonga wote hao na kuwanunua, ni lazima mtu awe na kiwanda cha kutengeneza fedha. Sina uhakika kama kiwanda hicho kipo hapa Tanzania.

Tunaposema kwamba Lowassa, hapana kwa sasa, hatuna maana mtu huyu ni mbaya, au mdhambi. Tunajua Lowassa, ametenda mengi, mema na mabaya. Yeye ni binadamu, hivyo hawezi kuwa na mabaya tu au mazuri tu, ni lazima awe na mazuri mabaya. Tunajua aliyatoa maji Ziwa Victoria na kuyafikisha Kahama, tunajua jitihada zake za kuanzisha sekondari za kata, tunajua alivyo mtu wa kutoa misaada na kuwapenda watu, tunajua kabisa huyu ni mtu wa watu, tunajua jitihada zake za kutaka kuleta wataalamu wa kutengeneza mvua na mengine mengi.

Tunayajua yote hayo, lakini mabadiliko tunayoyataka sasa hivi yanahitaji mtu mwingine.Tanzania ina watu wengi na si Lowassa peke yake. Urais ni utumishi na si kitu cha kufa na kupona. Mtu, akitaka kuwa mtumishi mnataka msitake, ni lazima shaka iwepo. Hivyo si kumchukia Lowassa, bali ni kutilia shaka nia yake ya kutaka kuwa rais iwe na isiwe. Kwa vile yeye anataka tuamini ni yeye peke yake, tunasema hapana!

Na tunaposema anayetufaa kwa sasa ni Magufuli, hatuna maana kwamba mtu huyu ni mtakatifu. Yeye pia ni bainadamu, ana mazuri yake na mabaya yake. Tukipima mazuri na mabaya yake, mazuri yanakuwa uzito zaidi. Tunaangalia mtu ambaye anaweza kulitumikia taifa hili na kuliongoza kutoka njia panda.
Kuna mama mmoja wa Tabata Dar-es-salaam, baada ya kusoma maoni yangu juu ya Lowassa na Magufuli, alinipigia simu si kunitukana wala kunipongeza, bali alikuwa na ombi.

Alipiga simu akilia na kusema; "Mwandishi, kwa nini umemwandika vibaya Lowassa? Mimi nina imani huyu ndiye atapita na kuwa rais wa Tanzania, sasa ukimwandika vibaya, watu wataacha kumchagua. Ninakuomba sana, andika hata neno moja zuri juu ya Lowassa".

Mama huyu, alikuwa tofauti kabisa na washabiki wengine wanaotuma ujumbe wa matusi na kupiga simu kutukana. Ningependa kumjibu mama huyu kupitia kwenye makala hii kwamba sijamuandika vibaya Lowassa, bali ninafanya kazi yangu ya unabii. Ninaona mawingu na kusema sasa mvua itanyesha.

Kwa vile na mimi ninaishi Tanzania, ninajua fika kwamba kuna ambao hawaitaki mvua hii ya masika, wanataka jua, lakini ukweli ni kwamba mvua itanyesha. Nitakuwa kichaa, nitakuwa sifanyi kazi yangu nikiona mawingu, tena mazito nikasema kuna jua! Ni mvua kwa wote, wanaokubali na wanaokataa! Kinyume na hapo, Lowassa ni mtu mwema, mchapakazi na ni mwerevu. Hakuna shaka kwamba Lowassa, ana uwezo mkubwa wa kuongoza. Mtu huyu ana sifa nyingi ndani na nje ya nchi. Lakini kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu ameteleza, ndiyo maana tunasimama na kusema hapana.

Nchi inaongozwa kwa sera, ilani ya vyama na itikani. Kwa kuteleza Lowassa, ataiongoza nchi kwa sera ipi na itikadi ipi? Kama atafuata yale ya CCM, awaachie wenyewe! Upinzani, yeye ni mwanafunzi. Kuna watu wanaufahamu upinzani, wamezaliwa humo na kukulia humo. Msimamo wa Lowassa juu ya Katiba mpya haujulikani, maana wakati wa mchakato wa kuandika Katiba mpya, alikaa kimya kana kwamba hakujua kilichokuwa kinaendelea.

Leo hii mtuambie huyu ndiye anafaa kuiongoza Tanzania? Wenye mapenzi na nchi yao, tuliwaona wakati wa mchakato wa kuandika katiba. Walijitokeza na kusema msimamo wao bila kuogopa. Lakini Lowassa, alibaki kimya, kwa kuogopa asiseme, ili asikatwe wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea wa urais kupitia CCM. Mtu, anayeogopa kuonyesha msimamo wake wazi wazi, tena msimamo unaohusu uhai wa taifa lake, mtu huyo hafai kabisa kuwa kiongozi wa nchi.

Ninafanya kazi ya unabii. Inawezekana Lowassa, akachaguliwa kuwa rais, maana anayechagua si mimi ni wananchi. Ikitokea hivyo, maandishi hayafutiki, tukianza kunyosheana vidole, mambo yakienda ndivyo sivyo. Maandishi yatakuwepo kutukumbusha. Na nitaendelea kuandika, maana akichaguliwa na kuvurunda, nitaandika bila kuogopa. Nilianika wakati wa Mkapa, nikaandika wakati wa Kikwete, na nitaendelea kuandia awe Lowassa au Magufuli.

Aina maana kwa vile leo hii ninasema Magufuli, anatosha, akiingia madarakani na kutupa ahadi zake nyuma na kutenda mengine kinyume na matakwa ya watanzania, nitakaa kimya kwa kuogopa au kwa kuhongwa. Nitaendelea kufanya kazi yangu ya unabii.

Binafsi sina chuki na Lowassa, hata yeye anafahamu. Labda niazime msemo wake wa "Watanzania wanajua na dunia nzima inajua!". Lowassa anajua na ndugu na marafiki wa karibu wanajua kwamba huyu ni mjomba wangu. Lowassa anajua na ndugu na marafiki wa karibu wanajua kwamba sina chuki na mjomba wangu. Lowassa anajua na ndugu na marafiki wa karibu wanajua kwamba ninachokifanya ni unabii na yale ninayoaandika naweza kuyazungumza na Lowassa macho kwa macho.

Mzee Kinguge, ametangaza kujitoa CCM, anasema katiba haikufuatwa. Lakini akasema hayuko tayari kujiunga na chama kingine. Tunavyomfahamu Kingunge, tunaweza kuelewa ni kwa nini hapendi kujiunga na chama kingine. Kwa busara zake, anaamini hata asipofanya siasa yeye kuna Watanzania wengine wengi watafanya siasa. Hawezi kusema bila Kingunge, hakuna siasa au hakuna CCM.

Tofauti na mjomba Lowassa, ambaye anafikiri CCM imekiuka katiba na haikumtendea haki. Badala ya kufuata msimamo kama wa Mzee Kingunge, yeye anafikiri bila yeye hakuna siasa, bila yeye hakuna rais wa Tanzania. Ndiyo maana akaamuua kujiunga na upinzani ili awaonyeshe watanzania kwamba bila Lowassa, hakuna siasa na bila Lowassa hakuna CCM, hakuna rais. Anataka aweza rais, tunataka hatutaki!

Ndiyo maa sisi manabii, tunajitokeza kueleza hali hii, kwamba si ya kawaida na wala haina faida kwa taifa letu. Mtu anayetaka kuwa rais kwa kulazimisha, ni lazima atakuwa na mipango yake, ambayo si mipango ya taifa. Atakuwa na mipango yake na watu wake. Mungu, isaidie Tanzania kupata kiongozi bora.

Chanzo Raia Mwema

Share this :

Related Posts

0 Comments