[wanabidii] Kwenye ITV; Wanawake Goma Wanalilia Amani, Sisi Tumechoka Kuihubiri...!

Monday, October 19, 2015


Ndugu zangu,

Kwenye habari za ITV usiku huu, tumeonyeshwa wanawake wa Goma, DRC waliotembea kilomita 15 kwa miguu kuomba pande zinazogombana kuacha vita. Wametembea kuomba amani; wanasema wanawake ndio wanaoathirika zaidi na hali za vurugu na vita. Ni pamoja na kubakwa.

Ndugu zangu, 
Katika jamii yeyote ile, uwepo wa amani na utulivu ni msingi mzuri katika kutafuta haki na usawa, kwa njia ya majadiliano.

Na habari ile ya wanawake wa Goma imenikumbusha nilichokiandika Mei 23, 2013. Asubuhi ya tarehe hiyo, kwenye televisheni ya Aljazeera tulioneshwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon akiwa Goma, DRC. Pale Uwanja wa Ndege wa Goma wameonekana akina mama wakiwa na mabango. Walikuwa wakimlilia Ban Ki Moon awasaidie kurejesha amani na utulivu katika Goma na DRC. Kwamba wamechoka na 
vita.

Kwenye mitaa ya Goma wakaonekana pia vijana wakiwa na mabango wakifikisha ujumbe wa kulilia amani kwenye msafara wa magari ya Umoja wa Mataifa. Vijana wengine wakaonekana wakiyagonga kwa mikono madirisha ya magari yaliyowabeba maofisa wa Umoja wa Mataifa. Wanataka amani. Wamechoka na vita.

Hapa nyumbani, wakati tukielekea kwenye Uchaguzi Mkuu, tumeanza kuwasikia baadhi ya wanasiasa wasiowajibika kwa kauli zao wakiwahamasisha wafuasi wao wakaidi sheria na taratibu zilizowekwa na mamlaka husika kuhakikisha kuwa Uchaguzi wetu unakuwa wa amani.

Hawa ni wanasiasa, ambao kwa kauli zao zisizotanguliwa na hekima na busara, wanaweza kuiingiza nchi yetu kwenye machafuko, hivyo, uvunjifu wa amani.

Mara nyingi, kwenye hali ya vita na hata vurugu, ni akina mama na watoto wenye kuteseka sana. Maana, kuna hata wenye kudhalilika kwa kubakwa. Ndio maana ya Wanawake wa Goma, DRC kuwa mstari wa mbele katika kuiomba amani irudi.

Na siku zote, kuwasha moto ni jambo jepesi sana, lakini, kazi kubwa ni kwenye kuuzima moto. Hivyo, kuanzisha vurugu katika jamii ni jambo jepesi, lakini, kurudisha amani na utulivu ni jambo gumu sana.

Ndugu zangu,

Nchi yetu bado ni ya amani na utulivu. Tusifanye yale yatakayopelekea kuitumbukiza nchi yetu kwenye dhahma ya vurugu na machafuko. Na kwa viongozi wetu, watangulize busara na hekima katika kushughulikia kadhia zinazojitokeza.

Na media yetu pia ifanye kazi yake katika kutoa taarifa sahihi zisizo za kishabiki. Maana, pamoja na umuhimu wa kuripoti matukio ya vurugu, hakuna faida ya kuripoti kwa namna ya kushabikia hata pale zinapotokea huku tukiacha kutoa elimu juu ya kuitunza amani iliyopo.

Na hakika, tusipoyapa mazungumzo nafasi yake stahiki katika kutatua kadhia zinazojitokeza, basi, hatari iliyo mbele yetu ni kuhatarisha amani yetu ambayo wengine hata usiku huu kwenye ITV, tumewashuhudia kule Goma, DRC, wakiililia. Nasi tunaonekana kuwa tumechoka kuihubiri!

Maggid Mjengwa,

Iringa.


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments