Ezekiel Kamwaga
NIMESOMA kwa makini maelezo ya mwandishi Ben Saanane kwenye matoleo yaliyopita ya gazeti hili. Ni maelezo marefu na ukisoma unapata picha kwamba anapiga vita kitendo cha mgombea urais wa CCM, John Magufuli, kupiga push ups (pushapu) majukwaani kwenye wakati huu wa kampeni.
Nina imani kwamba sababu ya kwanza, na pengine kubwa kulizo zote, ya Saanane kuandika makala ile ni ukweli kwamba anafahamu nini ambacho Magufuli anawaambia wapiga kura na Watanzania kwa ujumla kupitia kitendo kile cha sekunde chache.
Kitu anachofanya Magufuli sasa (cha kupiga pushapu) ni jambo lililoelezwa vizuri kwenye medani za siasa kwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Kwa waliowahi kumsoma mwanafalsafa wa Kiyunani, Quintus Tullius Cicero, kwenye andishi lake la "How To Win An Election" lililotolewa miaka 64 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, watajua kwamba alichokifanya mgombea huyo ni jambo la kawaida kisiasa.
Kuna mambo makubwa matatu ambayo Cicero aliandika wakati huo ambayo wanasiasa kote duniani wanayafanya hadi sasa. Jambo la kwanza ni kuahidi wakati wa kampeni. Kwamba wakati wa kampeni ni wakati wa kuahidi.
Mgombea yeyote makini, atatoa ahadi za kueleza nini anataka kufanya endapo wapiga kura watamchagua. Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, John Magufuli na wagombea wa vyama vingine wote wametoa ahadi kwa wapiga kura.
Jambo la pili ambalo Cicero aliandika wakati huo ni kwamba wagombea wanatakiwa kuonekana wako jirani na wananchi masikini.
Kwenye kampeni hizi, Magufuli ameonyesha alivyo mtetezi wa wanyonge. Wapo wagombea waliopanda daladala "kujifunza kuhusu adha za watu masikini". Yote haya yameandikwa na Cicero miaka 64 kabla Yesu hajazaliwa.
La tatu, na hili ndilo hasa Magufuli analolieleza kwa kupiga pushapu majukwaani, lilielezwa na Cicero kwamba mwanasiasa anatakiwa kushambulia udhaifu wa mpinzani wake.
Kwamba, kama unashindana na mtu ambaye ni mla rushwa, itakuwa makosa kama hutaikemea rushwa kwenye kampeni zako. Kama mshindani wako ni mzinzi, ni lazima utumie kipindi cha kampeni kukemea uzinzi. Hii ndiyo siasa ya kushinda uchaguzi.
Kwenye uchaguzi huu, kuna maswali kuhusu afya ya mgombea urais wa Ukawa. John Magufuli angeweza kutumia dakika tatu kutoa lugha isiyo ya kistaarabu kuhusu afya ya mshindani wake lakini ameamua kutumia njia ya kiungwana.
Wakati akifukuzia urais wa Russia, Vladmir Vladmirovic Putin alitumia muda mrefu zaidi kueleza kuhusu utimamu wa afya yake. Baada ya kubaini kuwa Warusi wamechoshwa na ulevi na uchovu wa Boris Yeltsin, yeye aliamua kuandaa mapambano ya Judo ambayo yeye alishiriki kuonyesha namna alivyo timamu.
Kuna wakati Putin alikuwa akienda Siberia na wapiga picha za televisheni na magazeti ili apigwe picha akiwa anaendesha farasi kwenye jua kali na akiwa kifua wazi. Alijua anachowaonyesha Warusi.
Barack Obama aliposhindana na Seneta John McCain, hakutaka kuwaambia Wamarekani kwamba mshindani wake huyo alikuwa na afya mbovu. Alichofanya Obama ni kuandaa mechi za kirafiki za mchezo wa mpira wa kikapu na akina Magic Johnson, Kobe Bryant na Shaq O'neill. Yeye mwenye alicheza na Wamarekani wakajua alikuwa anawaonyesha nini.
Kama tunakubali kwamba wanasiasa wanatakiwa kuahidi wakati huu wa kampeni, wanaruhusiwa kula kwa mama ntilie au kupanda daladala –tukubali kwamba wanatakiwa pia kupiga pushapu.
Kimsingi, tukio ambalo Magufuli amelifanya lilichukua takribani sekunde kumi tu. Kama angekuwa Obama au Putin, angetumia dakika 40 au saa nzima kuonyesha wananchi namna alivyo fiti kulinganisha na mpinzani wake. Na hili liko kwenye vitabu vilivyoandikwa miaka zaidi ya 2000 iliyopita.
Pushapu za nini?
Nchini Marekani, hivi sasa kuna kampeni maarufu iliyopewa jina (hashtag) mitandaoni la #PushUpsEverywhere. Kampeni hii imeanzishwa na taasisi ijulikanyo kwa jina la Health Fitness Revolution. Lengo la kampeni hii ni kutaka kuigeuza Marekani kuwa Taifa la watu walio timamu (fit) kimwili.
Kinachofanyika kwenye kampeni hiyo ni kwa mtu kupiga pushapu kumi kila unapoamka na kujirekodi halafu unaituma kwenye mitandao kama Facebook, Twitter au Youtube, huku ukiwataka rafiki zako wawili nao kukujibu kwa kufanya hivyo.
Na kila anayekujibu naye anafanya hivyo kwa kuwataka rafiki zake wengine nao kujiunga. Hivi sasa kampeni hiyo imepata umaarufu mkubwa Marekani. Watu wanapiga pushapu kama hawana akili vizuri! Watu wazima, vijana, wanawake na wazee wote wanashiriki.
Badala ya kumponda Magufuli kwa kupiga pushapu, Ben Saanane anatakiwa kumsifu Magufuli kwa kitendo chake kile. Kama Watanzania wote wakiamua kupiga pushapu kila siku –wakiiga mfano wa kiongozi wao huyo, maisha yatakuwa tofauti sana.
Takwimu mbalimbali za kiafya zilizowahi kutolewa zinaonyesha kwamba zaidi ya nusu ya magonjwa yanayowasumbua watu yanatokana na watu kutokuwa fiti. Maana yake ni kwamba, asilimia 50 ya fedha zinazotumika kutibu watu, zinaweza kuokolewa kwa watu kufanya mazoezi tu.
Miongoni mwa watu mazoezi mepesi kufanywa na watu wa kada zote ni pushapu. Hili ndilo zoezi pekee ambalo mtu yeyote, kuondoa walemavu wa mikono, anaweza kulifanya. Unaweza kulifanya popote ulipo, saa yoyote na wakati wowote.
Kama wewe ni mwajiriwa wa ofisini, unaweza ukalifanya ukiwa kazini, kama wewe ni mfugaji unaweza kufanya ukiwa malishoni, kama wewe ni mwendesha bodaboda, unaweza kufanya kwenye kituo chako. Ni zoezi rahisi kwa watu wote.
Halihitaji mtu kuwa na bwawa la kuogelea nyumbani kwake au kwenda Gym. Pushapu ni zoezi la kila mtu. Hoja hapa ni kwamba, kama kila Mtanzania akiwa anapiga pushapu 20 tu kwa siku, bajeti ya afya itapungua na fedha kupelekwa kwingine.
Kuna hoja nyingine kuhusu Taifa la watu wenye afya njema. Watu wakiwa na afya njema maana yake wanakuwa wachapa kazi zaidi. Wakiwa wachapa kazi maana yake ni kuwa tija inaongezeka kwa kila mmoja wao. Tija ikiwa kubwa, faida inakuwa kubwa na matokeo yake uchumi unakua.
Taifa la watu goigoi haliwezi kwenda kokote. Angalia Wachina namna walivyopiga hatua kubwa kiuchumi. Ukweli usiosemwa ni kwamba hawa jamaa wanachapa kazi kwelikweli. Wanachapa kazi kwa vile wako fiti. Wako fiti kwa sababu wanafanya mazoezi. Wanapiga pushapu.
Ni ajabu kwamba watu wanampinga Magufuli anayetaka kujenga Taifa la watu walio timamu kimwili. Tutake tusitake, tunatakiwa kuwa na afya njema ili kuipeleka Tanzania yetu kwenye Mabadiliko tunayoyataka.
Jambo moja ambalo akina Ben Saanane wanaliruka wakati wanapozungumzia pushapu za Magufuli ni kwamba hawataki kusema kuwa pushapu si sifa pekee inayomfanya mgombea huyo wa CCM awe kipenzi cha wapiga kura.
Ben Saanane, anaepuka kusema kwamba tafiti zinaonyesha Watanzania wanamwamini Magufuli kuliko mwanasiasa yeyote wa Tanzania wakati linapokuja suala la kutimiza ahadi. Kwamba John Joseph Pombe Magufuli akisema nitafanya hili maana yake ni kuwa atafanya.
Saanane anazungumzia pushapu kana kwamba Watanzania hawajui sifa nyingine za Magufuli. Kwamba katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, amejitokeza kama waziri mwenye kiwango cha juu cha uchapakazi na maamuzi ya kizalendo kuliko mwanasiasa mwingine yeyote hapa nchini.
Wanaojadili pushapu za Magufuli wanafanya hivyo bila ya kusema kwamba hadi sasa ndiye mgombea aliyekutana na wapiga kura wengi zaidi, aliyesikika kwa wapiga kura wengi zaidi na ambaye umaarufu wake umeongezeka zaidi wakati huu wa kampeni kuliko mwingine yeyote.
Wanaokosoa pushapu wanakosoa utadhani Magufuli ni mtu asiyejulikana ambaye anakwenda kwenye mikutano kupiga pushapu na halafu anaondoka.
Ben Saanane, atake asitake, nchi yetu inahitaji Rais mchapakazi, mwadilifu, mzalendo, mwenye maamuzi na asiye na simile na rushwa. Inataka Rais ambaye ana uchungu na umasikini wetu na anataka kututoa hapa tulipo.
Na kwa sababu tuna changamoto nyingi za kutatua, tunahitaji Rais ambaye watu wakimwona katika siku ya kwanza, wanajua kwamba yu tayari kimwili na kiakili kuweza kukabiliana na changamoto hizo.
Watanzania wanataka Rais atakayeweza kuzungumza nao na kuwaeleza kuhusu utatuzi wa kero zao uso kwa uso na si Rais wa kuwaambia wakasome kwenye tovuti kuhusu majibu ya kero zao hizo.
Ifike wakati tuwe wakweli kwa nafsi zetu na kwa nchi yetu. Sote sasa na tufanye mazoezi ili kujenga Taifa letu.
Nadhani sasa naweza kuendelea na zoezi langu la kupiga pushapu. Leo nataka kupiga pushapu 50 kwa siku nzima
Rai Mwema
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments