Privatus Karugendo
KURA za maoni zilizotolewa kuonyesha Dk. John Magufuli anaongoza, zilikataliwa na washabiki wa Edward Lowassa. Wanasema ni za kupikwa. Wengine wanasema idadi ya watu walioulizwa ni ndogo. Tanzania tunakimbilia idadi ya watu milioni 45, kuuliza watu elfu moja na kufikiri umepata maoni ya Watanzania, wanasema si sawa.
Kura hizi za maoni zinazoonyesha Magufuli, kuongoza, zilionyesha tofauti kubwa kati ya Lowassa na Magufuli, ndiyo maana washabiki wanazikataa. Wanaamini kwamba wawili hawa wanazidiana kidogo tu.
Lakini pia zile zilizoonyesha Lowassa, anaongoza, ingawa hazikuwa na tofauti kubwa, lakini washabiki wa Magufuli walizikataa. Wanasema zilitengenezwa na watafiti ambao ni makada wa Ukawa. Hivyo hadi sasa hivi hakuna mwenye imani na kura za maoni. Kila mtu anataka kura za moni ziegemee matumaini yake. Zionyeshe anayeongoza ni mtu ambaye yeye anamuunga mkono.
Sikuwa na lengo la kuandika kuhusu kura za maoni. Imejitokeza kwa bahati tu. Nilipokuwa nikiandika makala na kuonyesha kumkubali Magufuli na kumkataa Lowassa, nilipokea sms za matusi. Lakini pia kulikuwa na nyingine za kuniunga mkono na pongezi. Wale waliotuma sms za matusi, walisisitiza kwamba hawatakaa wasome makala zangu tena. La kushangaza watu wale wale waliendelea kunitumia sms za matusi kila nikiandika, kumaanisha kwamba bado wanaendelea kusoma makala zangu. Kwa vile mimi ni mtafiti pia, nikaamua kufanya kazi.
Jinsi tunavyosogea kwenye tarehe ya uchaguzi, na jinsi tunavyoendelea kuchambua wagombea na kuonyesha ni yupi anatufaa zaidi ya mwingine, na hasa baada ya makala yangu ya Jumatano iliyopita kwenye safu hii inayosema " Nabii hakubaliki nyumbani", asilimia ya matusi inapungua. Matusi yalikuwa na asilimia 60, na wanaoniunga mkono walichukua asilimia 40. Hii ni kutokana na sms nilizokuwa nikipokea kila nikiandika. Leo hii ninapoandika makala hii, asilimia ya matusi ni 30 na wanaoniunga mkono ni asilimia 70.
Je, hii ina maana kwa sasa, kama tungepiga kura leo hii, Lowassa, angeshinda kwa asilimia 30 na Magufuli asilimia 70? Nauliza tu kutokana na utafiki wangu wa sms na wala hapa hakuna kuchakachua au kuhongwa. Sikupanga kufanya utafiti, huu. Mimi nimeandika, watu wamesoma na kutoa maoni yao, wengine wakatukana na wengine wakaunga mkono. Matokeo yake ni kwamba wanaotukana wanapungua siku hadi siku na wanaounga mkono wanaongezeka siku hadi siku.
Hata hivyo bado si wakati wa kushangilia kwa wale wanaomuunga mkono Magufuli, maana kuna tatizo kubwa linalojitokeza nalo ni dalili za watu kukata tamaa. Pamoja na asilimia ya matusi kupungua, bado kuna asilimia kubwa ya watu ambao wanasema hata kama ni jiwe watalipigia kura. Kwa kujieleza, wanasema wanajua na kutambua ubora wa Magufuli, sifa zake zote wanazijua na kuzikubali, lakini wanasema bahati mbaya yuko CCM. Wao hawaipendi CCM, na wangependa kuona CCM, inaondoka madarakani.Hivyo wako tayari kupigia kura jiwe, lakini si Magufuli wa CCM.
Tofauti na ilivyo kwa Lowassa, kuna wanaosema kama ingetokea Magufuli, akabinuka na kuiingia Ukawa, basi ushindi ungekuwa ni asubuhi. Lakini kwa vile amebaki CCM, basi watapigia kura jiwe. Huku ni kukata tamaa na hizi si dalili nzuri.
Kukata tamaa ni dhambi. Mara nyingi watu wanaokata tamaa wanatenda matendo mabaya kama vile kujinyonga na kutoa uhai wao au uhai wa watu wengine. Tunasikia habari za watu huko Amerika wanaochukua bunduki na kuwauwa watu na mwishowe kujiua wao wenyewe. Hawa ni watu ambao wanakuwa wamekata tamaa. Kama watu wana imani na Magufuli, kama wanazitambua sifa za Magufuli na kuzikubali, kwa nini wasiamini Magufuli, huyu huyu, anaweza kubadilisha hiyo CCM. Kwa nini wafanye kulichagua jiwe kitu ambacho hakina uhai na hakitaleta tija kwa taifa letu?
Hatuwezi kukata tamaa kama taifa, itakuwa ni dhambi kubwa. Hatuwezi kupiga kura kwa kukata tamaa na kumchagua yeyote yule, tutakuwa tunalitendea vibaya taifa letu na vizazi vijavyo. Tutakuwa tunaliangamiza taifa letu bila ya huruma. Hapa ndipo tunawahitaji manabii na msaada mkubwa wa viongozi wa kidini. Ni muhimu roho zetu zikaongozwa na kuelekezwa njia iliyo sahihi.
Bahati mbaya, hata baadhi ya viongozi wa kidini wanasema " hata kama ni jiwe…". Nimekutana na maaskofu, mapadri na baadhi ya viongozi wa kiislamu ambao nao pia wamekata tamaa. Hii ni hatari kubwa.
Bado tuna siku za kuwasikiliza wagombea wetu. Bado tuna muda wa kutosha kuangalia ni nani anafaa zaidi ya mwingine. Tunapojikuta njia panda, ni muhimu kushikamana kama taifa na kufanya uamuzi mgumu. Uamuzi mgumu ni pamoja na kushinda "udhaifu" huu wa kukata tamaa. Tuwaweke wagombea wetu kiti moto, tuwaulize maswali magumu, ili na wao watoe majibu. Tusikubali kufanye uamuzi wa kijinga au uamuzi wa kishabiki. Tuiangalie Tanzania ya leo, kesho, keshokutwa na vizazi vijavyo.
Tusiangalie ahadi za wagombea, maana ni nyingi kiasi cha kutilia shaka. Tusiangalie vyama vya wagombea, maana kinachotangulia ni "Utanzania" wetu. Tuangalie na kupima uwezo, uzalendo na nia ya mgombea. Kuna wagombea wengine ambao nia yao kubwa ni kutimiza ndoto za maisha yao, kuhakikisha wanaingia Ikulu. Mfano, mbwa daima akiona gari linapita, analifukuza.
Gari hilo likisimama, mbwa hafanyi kitu kingine zaidi ya kulikojolea gari hilo na kuondoka zake. Hamu yake, gari likisimama inakuwa imekwisha. Aina ya watu hawa haitufai kabisa. Kama mtu amejaribu kugombea zaidi ya mara mbili inashindikana, kwa nini yeye mwenyewe asijipime na kuchukua hatua? Au anakuwa na nia kama ya mbwa? Akiingia Ikulu, basi hamu yake imekwisha?
Kuna wagombea, ambao kwa mwonekano wao, kwa mawazo yao, kwa matendo yao wanaonyesha nia ya kutaka kuingia Ikulu, kuliongoza taifa letu kupiga hatua ya maendeleo. Wanaonyesha nia ya kutaka si kutumikia tu chama chao cha siasa bali ni kutaka kulitumikia taifa zima. Miongoni mwa wanaogombea nafasi ya urais tunao watu wa aina hii. Kwa nini tusiwachague watu hawa na badala yake tunaleweshwa na "udhaifu" wa kutaka kulichagua jiwe.
Hapo ndipo tunasimama na kusema: "Kwa ajili ya ndugu zangu na jumuiya yangu, sitanyamaza, sitatulia… nitapiga kelele na kuzitangaza sifa za kiongozi tumtakaye."
Kiongozi asiyenunua kura kuingia Ikulu, kiongozi ambaye anatambua kwamba Tanzania ni nchi ya kidemokrasia yenye kuheshimu usawa wa binadamu. Kiongozi mzalendo anayeguswa na maisha ya kila siku ya wananchi, kiongozi mwenye nguvu kimwili na kiroho, kiongozi mwenye hekima na busara. Kiongozi anayetambua uwepo na uwezo wa watu wengine.
Mtu anayefikiri bila yeye, hakuna wengine wenye uwezo wa kuliongoza taifa letu, mtu anayefikiri yeye ndiye mwenye uwezo wa kuwatengeneza viongozi wa taifa letu, hatufai kabisa. Hakuna haja ya kukata tamaa na kuamua kuchagua jiwe, watu wenye uwezo wa kuliongoza taifa letu tunao. Tuwasikilize kwa makini, tuwapime kwa utendaji kazi wao. Kazi ni uhai, na yule anayesisitiza kazi, maana yake ni mtetezi wa uhai wetu. Hivyo tusifanye makosa ya kulichagua jiwe, wakati tunaye mtetezi wa uhai wa taifa letu la Tanzania.
Rai Mwema
Related Posts
- [wanabidii] Africa: State Department Assisting Family of Ebola Patient
- [wanabidii] AFISA WA CHADEMA MKOA WA DAR ES SALAAM AJIUNGA ACT - TANZANIA
- [wanabidii] US and China's climate diplomacy, plus...
- [wanabidii] New content updates
- [wanabidii] Record za utendaji wa Edward Lowassa zinashangaza sana
- [Mabadiliko] AFISA CHADEMA DAR AJIUNGA ACT.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Comments