[wanabidii] Tutafakari kwa makini tuhuma za Slaa dhidi ya Chadema na Lowassa

Wednesday, September 02, 2015
Ningependa kuwatahadhari wachangiaji wenzangu kutohamaki ktk kuuunga mkono au vinginevyo madai ya Dk. Slaa juu ya Chadema na Lowassa kwa sababu zifuatazo:-

1. Siku zote ukisikiliza upande mmoja utashawishika kuwa upande  huo unasema ukweli mtupu; mpaka hapo utakaposikia na upande wa pili; Hii ni kanuni inayotumika popote; na ndiyo maana hata  vyombo vya kutoa haki  kama mahakama hufanya hivyo kabla ya kutoa hukumu. Husikiliza kwanza pande zote.
2. Tuhuma za Dr. Slaa kwa kiasi kikubwa zinatokana na nyaraka mbalimbali  alizonazo ambazo ni mawasiliano ya kiofisi kati ya pande mbili katika mgogoro huu. Ni nyaraka ambazo siyo za siri, bali ni mawasiliano ya kawaida katika suala lilikuwepo wakati huo. Kwa habari ya nyaraka kama zile alizokuwa anazitumia Slaa kujengea hoja zake, tatizo hapo ni moja tu, nalo ni namna mtu anavyotafsiri maudhui yaliyopo katika nyaraka hizo ( how you interpret the contents of a particular document).
Kwa hiyo siyo busara kutoa hukumu kwa upande unaotuhumiwa kabla ya kuwapa nafasi nao kuja na tafsiri ya maudhui ya nyaraka hizo hizo. Na tukumbe nyaraka mara nyingi huwa ni ufupisho tu wa kile ambacho pande mbili zinazowasiliana wanajua kuliko upande wa tatu utakaotumia nyaraka hizo.
3. Ikumbukwe kuwa madai ya Dr. Slaa ya kutaka kuhongwa millioni mia tano mwaka 2008 ili kupotosha ripoti ya Richmond ni madai mapya ambayo kwa kumbukumbu zangu  hakuwahi kuyasema popote. Ingekuwa vema kama madai hayo ya rushwa angeyatoa Bungeni wakati huo, kwa sababu bungeni unaweza kusema lolote na sheria inakulinda. Kutoa madai kama haya sasa inatia shaka ukweli wake.
4. Ikumbukwe kuwa ripoti ya Richmond/Downas iliyowasilishwa na Dr. Mwakyembe Bungeni akiwa m/kiti wa kamati teule ya Bunge ilipingana na ile ya TAKUKURU juu ya suala lile lile. Isitoshe, hata yale maazimio ya Bunge juu ya suala hilo la Richmond hayakutekelezwa na Serikali; maana Bunge liliazimia kuwa mamlaka ya utezi iwaajibishe aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali wakati huo na pia Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ambaye yupo kazini mpaka leo. Tujiulize kwa nini serikali ilikataa kuwajibisha wakuu hao? Mbali na Lowassa kujiuzulu pamoja na mawaziri kama Dr. Msabaha, serikali ilikaa kimya mpaka leo kuhusu utekelezaji wa maazimio hayo na hatujasikia bunge likipiga kelele juu ya ukimya huo wa serikali. Hii inatia shaka ukweli wa ripoti ya Mwakyembe kama kweli haikuegemea kwenye mlengo wa kisiasa; ripoti ambayo kwa sehemu kubwa anaitumia Slaa leo pamoja na viongozi wa CCM walioko kwenye kampeni sasa.
5. Tunavyo vyombo vya dola ambavyo vina mamlaka kamili kushughulikia tuhuma kama hizi za Slaa. Takukuru na Baraza la maadili wana uwezo kuchunguza au kumtaka mtuhumiwa kama Lowassa athibitishe juu ya uhalali wa utajiri wake. Lowassa ni mtumishi wa umma kwa miaka yote hiyo,na hata baada ya kujiuzulu uwaziri mkuu bado ubunge ni utumishi wa umma; kwa nini aendelee kutuhumiwa na mamlaka hizo bila kujua  hatua za kisheria kama vilivyofanya kwa Daniel Yona na Basili Mramba?  Katika hili, hata Rais pamoja na chama chake nao wanatushangaza pale wanapokuwa wanaungana na wananchi kama Dr. Slaa kulalamikia hadharani utajiri wa Lowassa wakati wana mamlaka ya kumshughulikia kisheria. Kwa nini wangoje wakati huu wa uchaguzi? Je, huo si unafiki wa kisiasa?

6. Katiba na sheria ya maadili ya umma zinakataza, na kusema ukweli ni kosa kumtuhumu mtu bila ushahidi. Ambacho kwa muda mrefu Dr, Slaa pamoja na wengine wote wanaomtuhumu Lowassa walipaswa kufanya, ilikuwa ni kuwakilisha ushahidi walio nao kwenye TAKUKURU na Secretariat ya maadili ya watumishi wa umma ili wayafanyie kazi madai hayo na kutoa taarifa kwa umma. Na kama tatizo ni taasisi zetu kushindwa kuwajibika hapo tunamlaumu vipi mtuhumiwa?
7. Nimalizie kwa kusema tu kwamba, mpaka sasa ni vigumu na haifai kumhukumu  Lowassa au Chadema  na watu wengine wanaotuhumiwa kama yeye katika sakata hili. Tusubiri nao wajibu mapigo, kisha tupime na pia tuzitake mamlaka za dola kuingilia katika mtafaruku huu na kutoa mwelekeo. Kwa nini tulumbane bila mwisho, utadhani tunaishi katika nchi ambayo hakuna utawala wa sheria?
Nawakilisha,
Mwassa Jingi.

Share this :

Related Posts

0 Comments