[wanabidii] LILETENI FAILI LA LOWASSA TULICHAMBUE

Sunday, September 06, 2015
LILETENI FAILI LA LOWASSA TULICHAMBUE HARAKA

Na Daniel Mbega
MASHAIRI ya sasa ya siasa hayana mizani wala vina, tena hayana urari! Hata ngonjera na tenzi vyote huwa na beti, mizani na vina.
Tanzania imegubikwa na tufani ya Ukawa, hususan Edward Lowassa. Wimbi kubwa la wanaohemka ni la vijana, wengi wao wakiwa waliozaliwa katika miaka ya 1980, ambao kwa hakika ndio viongozi wa sasa wanaotakiwa kuleta mabadiliko. Vijana siyo taifa la kesho tena, ni la leo.
Naam. Wale wazee na vijana hirimu yangu wanaogelea katika wimbi la mageuzi hayo ambapo wapiga kasia ni vijana. Wengi wanafurahia upepo unakoelekea na wanaomba usije ukabadilisha mwelekeo – pepo za Kusi na Kaskazi huwa hazitabiriki wakati mwingine na zinaweza kuleta madhara.
Wanasiasa wakongwe wanaona huu ndio wakati muafaka wa kupata neema nyingine. Ndiyo. Wapo waliokuwa wabunge kwa miaka mingi, wapo waliokuwa wanaongoza vyama vya siasa kwa miaka mingi. Wengi kati ya hawa wamechokwa na wananchi waliokuwa wanawaongoza. Wametemwa na vyama vyao na sasa wameona kimbilio pekee ni kudandia mashua inayopelekeshwa na upepo wa mabadiliko – ya vijana!
Japokuwa tayari mashua imempata nahodha, ambaye ni Lowassa, lakini kwa kiasi kikubwa vijana ndio wanaoisukuma, tena kwa kasi ya ajabu kiasi kwamba kama litatokea wimbi kubwa linaweza kukipaisha chombo na wote wakazama. Ni mtazamo wangu tu miye ambaye niko ng'ambo naangalia.
Lowassa ametoka katika Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya chama hicho kumbwaga akiwa ndiyo kwanza anataka kuianza safari yake ya matumaini. Amekaa akatafakari wee akaona hapana, safari ya matumaini inaweza kuendelea, hata kwa kutumia ngalawa.
Akapokelewa kwa huba na mahaba huko Chadema na hata Ukawa kiasi kwamba ndani ya siku mbili tu, tayari akawa amekabidhiwa mikoba ya kuwania urais. Mikoba ambayo kabla ya kuelekea huko wapinzani hao walikuwa wameafikiana kwamba aibebe yule Paroko mstaafu, Dakta Wilbrod Peter Slaa.
Na mara tu Lowassa alipotua Ukawa, Dk. Slaa akaingia mitini, kukaa kidogo, Profesa Ibrahim Lipumba naye akatimua. Wale waliokuwa nguzo ya upinzani wameondoka kabla chombo hakijang'oa nanga.
Yanaendelea kusemwa mengi kutokana na kuondoka kwa wanasiasa hao wawili ndani ya Ukawa. Wanatuhumiwa kwamba wamelambishwa sukari guru, ndiyo maana wameondoka ili wakidhoofishe chombo hicho na kukwamisha safari ya matumaini ya Lowassa pamoja na ndoto za Chadema za kukaa pale Magogoni kwa mara ya kwanza!
Kuvuja kwa pakacha, nafuu kwa mchukuzi, maana mzigo utakuwa mwepesi. Ukawa inabidi wafurahie kuondoka kwao. Unadhani wakichukua nchi si watakuwa na nafasi mbili za Paroko na Profesa ambazo lazima wangepewa hao kama wangekuwepo?
Leo hii wanaozisubiri nafasi hizo ni wengi mno – Ukawa kuna orodha ndefu, halafu Lowassa kama taasisi ameondoka CCM pamoja na 'watu wake' ambao alikuwa nao kitambo na wengi walikwishaahidiwa nyadhifa nyeti kama wakifanikisha safari ya matumaini. Uongozi mzuri bwana, asikwambie mtu, na hasa unapopigiwa mizinga 21!
Lakini tayari Profesa Lipumba amekwishasema kwamba ameondoka Ukawa na CUF – alikoachia nyadhifa zake zote – kwa sababu dhamira yake inamsuta. Yawezekana anayajua mengi yaliyo nyuma ya pazia kuhusu mchakato wa kuingia kwa Lowassa.
Dk. Slaa kwa upande wake ndiye amemwaga sumu Septemba Mosi, 2015 wakati alipoeleza bayana kwamba mchakato uliyumbishwa na viongozi wenzake ndani ya Chadema na Ukawa kwa ujumla, kiasi kwamba hata barua yake ya kujiuzulu ilichanwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari.
Unaweza kusoma zaidi makala haya hapa: http://www.brotherdanny.com/2015/09/lileteni-faili-la-lowassa-tulichambue.html


--
DANIEL MBEGA
INVESTIGATIVE JOURNALIST, BLOGGER, RESEARCHER & PUBLISHER
CELL: +255 767 939 319/ +255 715 070 109
WHAT'S APP: +255 656 331 974
BLOGS: www.kilimohai.wordpress.com
               www.brotherdanny5.blogspot.com

"Kama hawatuwekei mgombea mzuri, kwanini watutawale?" Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Dar es Salaam, 1995

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments