Dk. Slaa: Mjenzi makini wa taifa
Na Maureen Urio - Imechapwa 13 October 2011
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimepata msaidizi mpya katika kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwezi huu.
Msaidizi huyo ni kitabu kinachoitwa Dkt. Slaa, mjenzi makini wa taifa, ambacho kilizinduliwa Jumamosi iliyopita, kwenye Maktaba ya taifa, jijini Dar es Salaam.
Dk. Willibrod Slaa ni mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA anayemtikisa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete. Amekuwa mbunge wa Karatu kwa miaka 15.
Kwa wale ambao walikuwa hawajui historia ya mwanasiasa huyu, kitabu hiki kitakuwa cha msaada mkubwa kwao kwani kimesheheni maelezo juu ya maisha yake kutoka utotoni hadi sasa.
Kitabu hiki cha kurasa 55, kinamwelezea Dk. Slaa kuwa ni kiongozi mwenye sifa zote za kuwa kiongozi bora kutokana na moyo wake wa kupambana dhidi ya rushwa, kwa kauli na vitendo.
Kuhusu kazi yake ya miaka 15, kitabu kinasifia “mahudhurio mazuri†ya Dk. Slaa bungeni; uwezo wake mkubwa wa kufanya utafiti wa kina na moyo wake wa kushirikiana na wabunge wenzake.
Aidha, kitabu kinamtambua mwanasiasa huyu kwa umahiri wa kujenga hoja ndani na nje ya bunge, kusimamia hoja zake na kuendelea kuwa mtetezi wa wananchi.
Dk. Slaa ndiye alitoa hadharani, orodha ya majina 11 ya wale alioita mafisadi wanaokamua uchumi wa nchi. Miongoni mwa aliowataja ni rais anayemaliza muda wake, Jakaya Kikwete, rais mstaafu Benjamin Mkapa, mawaziri na viongozi wengine wa CCM na serikali.
Hiyo ilikuwa kwenye mkutano wa hadhara wa chama chake, eneo la Mwembeyanga, Temeke jijini Dar es Salaam mwaka 2007.
Akiongea na waandishi wa habari kabla ya kuzindua kitabu chake, Henry Muhanika alisema ameandika kitabu hicho kusaidia Watanzania kumfahamu vizuri kiongozi anayegombea urais.
Muhanika, pamoja na kutaka wananchi wamfahamu, alisema alitaka kuvunja mazoea ya kuandika juu ya viongozi baada ya kuondoka madarakani na kwamba ni vema kuwaenzi viongozi wangali hai.
Aliwahimiza waandishi wa habari kujikita katika uandishi wa vitabu, akisema “kazi hii siyo ngumu kama inavyofikiriwa,†akisisitiza kuwa uandishi wa vitabu vya aina hiyo huchochea moyo wa uzalendo.
Uandishi wa vitabu vya aina hii, alisema Mhanika, ni njia nzuri ya kutia moyo wananchi, kwamba hata katika “mfumo mbovu wa uongozi uliopo†katika taifa hili, bado kuna viongozi wachache wenye upendo na uchungu kwa taifa lao.
Miongoni mwa waliohudhuria hafla ya kuzindua kitabu hicho, ni Profesa Mwesiga Baregu, Mwenyekiti wa kampenzi za urais CHADEMA na kaimu katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika.
Mwandishi wa kitabu hiki ni Katibu Mtendaji wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), mhadhiri katika idara ya uandishi wa habari ya chuo kikuu cha kiislamu Morogoro na mshauri katika taaluma hiyo.
Aliwahi kuwa mhariri mkuu Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA) na baadaye akawa mhariri mkuu wa gazeti la The East African - Tanzania.
Muhanika ni mtunzi wa vitabu vingine vikiwemo, Utenzi wa vita vya Kagera na anguko la Idd Amin, Njia panda, My dear bachelor na Killer drink and other stories.
Dk. Slaa, mjenzi makini wa taifa, kimeanza kuuzwa wiki hii katika maduka ya vitabu na vituo vya kuuzia magazeti. Nakala moja inauzwa kwa Sh. 5,000/-.
chanzo Mwanahalisi
0 Comments