[wanabidii] Kwa nini jina la Apson Mwang’onda?

Friday, August 07, 2015
Kwa nini jina la Apson Mwang'onda?

Godfrey Dilunga

JULAI, mwaka 2012, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Tanzania, Apson Mwang'onda, alinukuliwa na Gazeti la Nipashe, akimjibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, baada ya waziri huyo kuelekeza tuhuma zake za masuala ya siasa kwa mkurugenzi mkuu huyo.

Majibu ya Mzee Apson yalikuwa yakikabili kile kilichoandikwa na Profesa Mwandosya kupitia kitabu chake; "Sauti ya Umma ni Sauti ya Demokrasia" ambamo alikuwa akionyesha namna Apson alivyoshiriki kumchezea rafu za kisiasa.
Mwandosya katika kitabu chake hicho alidai kwamba alihujumiwa na Apson katika mbio za kuwania urais mwaka 2005 na vile vile aliendelea kumhujumu katika harakati za kuwania nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Mkoa wa Mbeya, mwaka 2007.

Angalau katika majibu yake, Apson aligusia suala la maadili ya kazi yake. Kwamba kuhusu kumsaidia Mwandoysa kuusaka urais mwaka 2005, ilikuwa ni vigumu, kwa kuwa; "maadili ya kazi yake hayamruhusu."

Alisema; "Mimi siwezi kuwa mkuu wa Idara, eti nimuunge mkono kwenye uchaguzi wa urais, maadili ya kazi zangu hayaniruhusu hivyo."

Leo hii, kuelekea Uchaguzi Mkuu hapo Oktoba, 2015, jina la Apson Mwang'onda linaibuka tena katika mijadala ya siasa za ushindani wa kuisaka Ikulu.

Jina hili lilianza kuhusishwa na mbio binafsi za Lowassa akiwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na sasa, kwa namna fulani linaendelea kuhusishwa na Lowassa huyo huyo akiwa ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Apson kwa sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa mstaafu, mwenye kuendelea kula matunda ya kazi yake hiyo ambayo bila shaka, aliifanya kwa umahiri mkubwa na anastahili pongezi.

Kazi ambayo kwa nukuu yake hapo awali, aliifanya kwa kuzingatia maadili na vile vile kwa sasa, anastahili kuendeleza maadili, nidhamu na unyenyekevu wake huo katika wakati huu wa maisha yake ya kustaafu.

Naam, katika maisha yake ya kustaafu kama mmoja wa wakuu wa masuala ya ujasusi nchini bado, kwa sababu za maana na muhimu, anapaswa kuendelea kuheshimu kiapo chake cha kudumu.

Kiapo ambacho anapaswa kukiheshimu kwa kadiri ya maisha yake.
Hata hivyo, kutokana na jina lake kuendelea kuhusishwa na mikakati ya binafsi ya kusaka urais ya mmoja wa wasaka madaraka hayo makubwa zaidi nchini, heshima yake kwa kiapo chake hicho katika maisha yake ya kustaafu inatia shaka.

Kutajwa mara kwa mara kwa Mzee Apson katika mapambano binafsi ya kisiasa miongoni mwa makundi ya wanasiasa kunafifisha nidhamu ya kiapo chake hicho na kwa kweli hatua hiyo inapandikiza nakisi kubwa mno katika muktadha wa kutii mamlaka ya juu.

Ni sawa na kusema, baada ya kustaafu, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa anaweza kuishi maisha kwa kadiri anavyotaka, ikiwamo hata kuthubutu kupuuza mamlaka ya juu zaidi, kwa wakati husika.

Hebu tafakari, hali inakuwaje pale Mkurugenzi Mkuu mstaafu (A) wa Idara ya Usalama wa Taifa anapoamua kutumia uzoefu wake wa kijasusi kumpigania mwanasiasa binafsi (A) na vile vile, Mkurugenzi Mkuu mstaafu (B) naye anaamua kutumia uzoefu wake wa kijasusi kumpigania kufa au kupona mwanasiasa (B)? Hali itakuwaje Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (A) aamue kutumia uzoefu wake kumpigania kufa au kupona mwanasiasa (A) katika kuisaka Ikulu na kisha Mkuu (mstaafu) wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (B) aamue kumpigania mwanasiasa (B)?

Katika muktadha huo, najiuliza kwa nini jina la Mzee Apson linatajwa?
Na kwa kweli, wakati najiuliza hivyo, natambua kwamba wapo viongozi wakuu wa kitaifa wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini ambao maisha yao ya kustaafu ni mfano bora kwa wenzao waliochukua nafasi zao.

Kwa mfano, hakuna shaka yoyote kwamba Jenerali Mirisho Sarakikya, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (mstaafu) amekuwa mmoja wa wakuu wa kupigiwa mfano wa namna ya kuishi kwa nidhamu ya kuheshimu kiapo katika maisha ya kustaafu.

Nina uhakika, pengine siku moja akiwa amekwishakwea Mlima Kilimanjaro kwa mapenzi yake mwenyewe, na akiwa huko akasikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anapita jirani na anga la mlima huo, atapiga saluti ya utii.
Kwa maana nyingine, atakuwa anaendeleza nidhamu ya kijeshi katika maisha yake ya kustaafu.

Hakuna mgombea urais ambaye mbio zake zimehusishwa na Sarakikya. Hakuna mgombea urais ambaye mbio zake za kuisaka Ikulu zimehusishwa na Jenerali (mstaafu) George Waitara.

Wanatii viapo vyao, hawataki kutumia uzoefu wao kufaidisha kundi binafsi la msaka madaraka kwa gharama za ustawi wa nchi. Wanaweza kutumia uzoefu wao kutoa ushauri katika mamlaka husika na si kwa genge binafsi la kusaka madaraka.

Wanatambua wakifanya hivyo watakuwa wameweka rekodi (precedent) mbaya- tena mbaya kabisa- kwa vizazi vijavyo vitakavyokuwa na majukumu waliyowahi kuyashika nchini.

Nawasifu hao na wengine wengi nchini, kwa kuwa sikusikia majina yao yakitajwa, nimeshangaa kusikia jina la Mzee Apson likitajwa mara kwa mara kwenye michuano binafsi ya kisiasa miongoni mwa wanasiasa. Najiuliza kwa nini? Kuna lengo gani?

Kwa kiongozi wa ngazi ya juu mfano wa Apson, maisha yake ya kustaafu yanapaswa kubeba deni kwa taifa. Ni deni kwa taifa kwa sababu alitumia nguvu, akili, na kila mbinu kulitumikia kwa heshima kubwa taifa lake na kwa hiyo, baada ya kustaafu, taifa nalo ni lazima lilipe deni hilo na deni husika linaweza kulipwa kwa njia nyingi ikiwamo kuhakikisha anapata, bila vikwazo, stahiki (privileges) zake kama bosi mstaafu.

Hata hivyo, inawezekana vipi kuvumilia kutoa stahiki husika kwa mhusika ambaye tayari sehemu ya jamii inabeba tafsiri tofauti dhidi yake – tafsiri inayofanana na mtu anayekusudia kuukata mkono unaomlisha.

Katika maisha yake ya kustaafu yeye bado ni alama ya idara aliyowahi kuitumikia.
Ndivyo ilivyo, kwamba ingawa amestaafu lakini bado anaendelea kuwa alama ya taasisi hiyo katika maisha yake hayo ya kustaafu.

Bado swali liko pale pale; kwa nini Apson? Kwa nini sio wengine? Kwa nini siyo Waitara au Sarakikya ingawa wao walikuwa wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama?

Hakika, nadhani ni wakati sasa kwa mamlaka husika kuchukua uamuzi wa kubadili mwelekeo wa mashua ili kufika katika kituo stahili.
Kubadili mwelekeo wa mashua inawezekana kuliko kubadili mwelekeo wa upepo unaovuma baharini au ziwani.

Aliwahi kusema Jimmy Ray Dean, mwanamuziki, mfanyabiashara na mtangazaji wa televisheni kwamba; "I can't change the direction of the wind, but I can adjust my sails to always reach my destination."

Raia Mwema
Toleo la 417
5 Aug 2015

Share this :

Previous
Next Post »
1 Comments
avatar

Mungu fundi
Hakuna bingwa Dunia utamchukia mtu Kwa hili unataka hata afe.pengina hata ukamdhuru
Je unauhakikika utaishi milele baada yakuondoka yeye

Unamkataba na Mungu
Siasa tuu ndio tumjengee mtu chuki chuki
Kwanini huyu Yuko na flan hayuko namimi 😂

REPLY