[wanabidii] Uchambuzi: Watangaza Nia Na Sanaa Ya Kuhutubia.. ( 2)

Wednesday, June 03, 2015



Ndugu zangu,

Naomba nianze na tungo hii fupi...

" SINA sauti nzuri ya kuimba, siwezi kucheza muziki watu wakanistaajabia. 
Najua siwezi kuchora. Najua siwezi kuandika kitabu kikapata tuzo.
Maneno yangu si ya kurembesha sana, yanatoka moyoni.
Kipaji nilichojaaliwa si kikubwa na wala si cha upekee duniani.
Lakini, wote waliojaaliwa vipaji si sharti wang'ae wakaonekana."

Basi, ukiachilia mbali itikadi, siasa inahusu pia sanaa ya mawasiliano. Kwa mwanasiasa, kama huiwezi sanaa ya kuwasiliana na wananchi, basi, ni sawa na mtu anayejiita fundi mekanika , lakini hawezi kushika spana.

Watanzania tunashuhudia sasa wagombea watarajiwa wa nafasi mbali mbali za uongozi wa kisiasa wakitangaza nia zao. Wanafanya hivyo hadharani, ama kwenye viwanja vya michezo, kumbi za mikutano au sebule za nyumba zao. Kubwa, hawafanyi kwa siri.

Na huu ndio msimu wake haswa. Lakini, kwa baadhi yetu tuliopata bahati ya kusoma vitabuni na hata kuishi na kushuhudia kampeni za chaguzi mbali mbali za ndani na nje ya mipaka yetu, kuna mapungufu tunayoyaona. Mapungufu ambayo, yumkini wengine walio ndani ya vuguvugu la kisiasa kwa sasa hawayaoni. Ni hao wagombea watarajiwa wenyewe.

Hapa nitajikita kwenye eneo la mawasiliano ya mwanasiasa kwa wapiga kura. Kuna watakaokubaliana nami, kwamba kuwa mwanasiasa ni jambo moja, na kuwa na uwezo wa kuwasiliana na wapiga kura ni jambo jingine kabisa.

Hadi ninapoandika makala haya, na kwa uzoefu wangu mdogo kwenye sanaa ya mawasiliano na hususan sanaa ya kuongea mbele ya hadhara, naliona tatizo kubwa kwa baadhi ya watangaza nia kwenye eneo hili.

Kwamba, bila wao wenyewe kujua, ukweli kuna wanaotumia fedha nyingi na kupata mavuno haba kwa makosa ya kiufundi kwenye kujipanga kwenye eneo hili la sanaa ya mawasiliano kwa umma. Nimesema jana, kuwa ningeweza kabisa kutoa ushauri wa bure, kwa ninayoyafahamu, ili kuwasaidia wanasiasa hawa, iwe wa kutoka chama tawala au upinzani, ili, kama Watanzania wenzangu, waweze kufanya vema zaidi kwenye kufikisha ujumbe wao kwa Watanzania, jambo ambalo, kwa masikitiko makubwa, nimeshuhudia watangaza nia wenye ' kupotea' jukwaani bila kujua kuwa wameshapotea. Nafurahi, kuwa tayari jana ile ile, kuna walionitafuta niwasaidie.

Na anayepotea jukwaani yawezekana akawa amenunua hata muda wa televisheni wa saa zaidi ya mbili na kwa gharama kubwa. Alichoshindwa ni kupata wa kumshauri vema namna ambavyo, angeweza kutumia dakika 45 tu za kuwa ' Live' kwenye runinga na kutoa hotuba ya kutangaza nia ambayo ingewaacha watu wengine wakipiga kuta kwa ngumi wakitamani uchaguzi uwe juma lijalo ili wamalize kazi.

Hiyo ndio sanaa ya mawasiliano. Imekuwepo tangu enzi za Wayunani, wakiita ' Retorik'. Na hakika, ni ushauri wa bure kutoka kwangu, kuwa kwa mtangaza nia yeyote, atenge bajeti ya kununua muda wa kuwa ' live' kwenye runinga na redio japo kwa saa moja. Na kwamba asilifanye tukio la yeye kuongea likazidi saa nzima. Hapo kutakuwa na dalili zote za mtangaza nia ' kupotea' na pengine ' kujizamisha' mwenyewe kwenye bahari ya taarifa nyingi na zenye kumchanganya msikilizaji. Msikilizaji hapaswi kumsikiliza mtangaza nia na akafikia kufikiria mambo mengine nje ya yale anayozungumza mtangaza nia. Hivyo, kuna haja ya mzungumzaji mkuu kuwa na mbinu za kumbakisha msikilizaji wake kutoka sekunde ya kwanza mpaka anapomaliza kuzungumza.

Ni kwa namna gani?

Mzungumzaji mkuu anapaswa kujua mbinu za kuingia ' uwanjani' na kuwafanya mashabiki washangilie. Kujua anawezaje kubaki mchezoni huku akihakikisha mara kwa mara anajua wapi atazipiga ' kanzu' na kutuliza mpira huku akiwaacha washabiki wakilipuka kwa furaha. Hii ina maana ya uwezo wa mzungumzaji kujua namna ya kuingia kwenye mazungumzo yake na wanaomsikiliza. Ajue, kuwa maneno yanapashwa moto pia, tena taratibu. Hupaswi kuanza na moto mkali. Mzungumaji hapaswi kuanza na kulalamika! Ajue pia namna ya kupangilia hoja zake na wapi pa kuweka kituo kupisha wasikilizaji wake washangilie. Na ukiona pale ambapo walipaswa kushangilia hawakushangilia, basi, mzungumzaji ujue kuwa kuna hesabu kwenye mtiririko wako wa hoja haziko sawa, au , umeshindwa kujua uongee nini kwenye hadhira gani.

Na kuzungumza ni kama kupiga muziki. Kuna midundo ndani ya hotuba. Ndio maana, unaweza kuona mzungumzaji anaongea na watu wakitingisha vichwa. Ni kama wanacheza ndani ya hotuba.

Mzungumzaji anapaswa kuzitambua rasilimali zinazomzunguka wakati akitoa hotuba yake. Unapopewa jukwaa uongee ni fursa kubwa. Na unapokuwa na fursa ya kuwafikia Watanzania kwa mamilioni ni jambo adimu sana. Bahati mbaya, wengi hushindwa kuzitumia fursa hizo na huku wakiwa wamezigharamia kwa mamilioni ya shilingi. Ni mahali hapa, wenye kuzipata fursa hizo walipaswa kuomba hata ushauri. Mathalan, mzungumzaji anashindwa hata kutambua kuwa viungo vya mwili wake ni moja ya rasilimali hizo. Kujua namna nzuri ya kutumia lugha ya mwili. Unamwona mzungumzaji akiwa amesimama jukwaani mahali pamoja wakati hajawa hata Rais au Mbunge, hilo ni tatizo. Huo ndio wakati wa kushika kipaza sauti na kutembea jukwaani ukiongea na hata kushuka chini kwa wanaokusikiliza kutengeneza ukaribu nao.

Mzungumzaji, kama ni mtangaza nia na unataka kuomba kura kwa Watanzania wanachama wa chama chako na wasio wanachama wa chama chako. Basi, ukweli hapo ni kuwa, unaotaka kuwafikia walio wengi si wanachama wa chama chako. Hivyo, kosa kubwa la kwanza utakalolifanya ni kutanguliza maslahi ya chama chako badala ya nchi yako. Hapo chama chako ni tiketi tu, na kwamba sera zake ama ilani yake ya uchaguzi ndio unayoamini kuwa itawasaidia walio wengi wasio wanachama wa chama chako. Hivyo, kwenye shughuli ya kutangaza nia kumruhusu DJ kucheza nyimbo za chama chako ni sawa na kuamua kwa makusudi kupunguza idadi ya wasio na vyama ambao wangeweza kukuunga mkono katika harakati zako. Lengo la kwanza la mtangaza nia liwe ni kuwafikia wasio wanachama wa chama chake, na mara nyingi, wasio wanachama wa vyama vya siasa.

Hakika, ili eneo la sanaa ya mawasiliano ni pana mno. Nitaendelea na chambuzi hizi. Na anayetaka ushauri wa bure awasiliane nami;

0754 678 252, mjengwamaggid@gmail.com
NB: Hii ni sehemu pia ya makala yangu Raia Mwema.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments