[wanabidii] huyu ndiye rais tunayemuhitaji watanzania

Tuesday, June 16, 2015

Kabla hata ya kuanisha vigezo inabidi wananchi na wapiga kura tutambue kwamba kazi ya urais ni kazi ngumu! Ni kazi ngumu kwa sababu Rais ndiye jicho la nchi yeyote ile duniani. Kwa sababu hii Rais akifanya vizuri nchi inakuwa imefanya vizuri na akivurunda sote tunakuwa tumevurunda.

Heshima yetu kama nchi kwa kiasi kikubwa itatokana na heshima ya Rais wetu. Ndiyo kusema Rais akijiheshimu na akaheshimiwa na sisi pia tunapata heshima. Vivyo hivyo ikitokea Rais akawa haheshimiwi nje ya mipaka yetu sisi pia tunakosa heshima kama nchi. Akiwa makini tutaonekana makini kama nchi. Akiwa mropokaji tutaonekana waropokaji kama nchi. Akiwa mlevi tutaonekana walevi kama nchi. Akiwa mwizi tutaonekana ni majambazi kama nchi. Akiwa malaya na mzinzi tutaonekana wazinzi na malaya kama nchi.

Kwa hiyo urais ni taswira ya Taifa na unabeba dhamana nzito. Ni lazima basi tumtathimini mtu yeyote anayetaka kuwa Rais wetu kwa jicho kali na macho mapana katika kila hali aliyo nayo: maneno yake, matendo yake, haiba yake, akili yake, afya yake, n.k. Ili aweze kukidhi haja ya kiti cha urais sawasawa na sawia, Rais tunayemchagua lazima asiwe mtu wa kawaida. Ni lazima awe ni mtu bora kuliko sisi wote. Tutafanya makosa makubwa kuchagua mtu wa kawaida, anayefanana na sisi, mwenye tabia kama zetu na mwenye maono kama sisi.

Kwa kuwa Rais si mtu wa kawaida na hapaswi kuwa mtu wa kawaida, ni watu wachache sana wanaoweza kuchukua dhamana ya urais katika nchi yeyote ile duniani. Kwa sababu hii ni muhimu tuwe makini sana tunapochagua mgombea urais kwa vyama vyote ili tushindanishe watu ambao ni bora kabisa katika nchi yetu.Tukikosea tukachagua mtu wa kawaida huyu ataendesha mambo kikawaida sana. Kwa hiyo kama wananchi walio wengi wamezoea ubabaishaji, uhuni, rushwa, wizi, n.k., tutapata Rais ambaye ni mbabaishaji, mhuni, na mpenda rushwa kama sisi na hatutasogea.

Ninajadili vigezo vya mtu anayefaa kuwa Rais wetu wa tano. Vigezo hivi nimevigawa katika makundi makubwa mawili. Kundi la kwanza linabeba sifa za kihaiba na kundi la pili ni la sifa za kikazi. Leo ninabainisha sifa za kihaiba. Kwa maoni yangu, mgombea urais anapaswa kuwa na vigezo angalau sita vinavyoangukia katika kundi la sifa za kihaiba.

Kigezo cha kwanza ni uaminifu. Ili Rais aweze kukamilisha ajenda yake, ni lazima aaminike kwa watu anaowaongoza. Bila watu kumuamini hakuna atakachofanya na watu wakakikubali. Kama watu hamwamini Rais itasababisha wabunge na vyombo vingine vya dola kuanza kumtilia shaka katika utendaji wake na hii itasababisha programu zake nyingi zikwame kwa sababu ufanisi wake unategemea kuungwa mkono na vyombo vingine vya dola likiwamo Bunge.

Tukumbuke pia kwamba Rais wa nchi ndiye msuluhishi mkuu wa migogoro katika nchi. Ili aweze kufanya kazi hii kwa ufanisi ni lazima aaminike. Ili Rais aweze kuaminika yampasa kuwa na historia ya kusema ukweli. Kwa hiyo kwa kutumia kigezo hiki, tutadadisi kila mgombea ni kwa kiasi gani amekuwa mkweli katika maisha yake binafsi na ya umma na kama amewahi kudanganya katika kazi nyingine ambazo amewahi kufanya.

Kigezo cha pili katika sifa ya haiba ni uvumilivu. Urais ni kazi ya shutuma. Ni kazi ambayo muda mwingi utapingwa, kuchekwa, kukejeliwa, kutukanwa na hata kuzomewa. Kwa hivyo, Rais lazima awe na uwezo wa kukabili hasira na awe na uwezo wa kusikiliza kila aina ya mtu na hasa wale watu ambao wanampinga.

Hii inamaanisha pia kwamba Rais lazima mara zote awe na moyo wa kusamehe. Mtu aliyezoea kusifiwa tu hafai kuwa Rais na hawezi kufanya kazi ya urais ama sivyo atalazimika kuwa mbabe na dikteta. Rais mbabe hatufai kwa sababu kazi yenyewe ya urais inampa mtu maguvu ya kutisha kikatiba na kisheria. Katika kupima wagombea wetu kwa kigezo hiki, tutadodosa maisha yao huko nyuma walipofanya kazi ili kujaribu kupima kiwango chao cha uvumilivu walipokuwa wanapambana na watu ambao walitofautiana nao kimtazamo na kimaono.

Kigezo cha tatu ni haki. Rais lazima awe na uwezo wa kutoa haki bila upendeleo. Hii inaanzia kwenye uteuzi wa watendaji mbalimbali na katika utendaji wa kazi zake kwa ujumla. Rais mtenda haki katika eneo hili ni yule anayezingatia sifa na vigezo vya weledi, uchapa kazi na umakini katika uteuzi wake badala ya kuangalia uswahiba na watu waliomsaidia katika kampeni.

Uteuzi na utendaji wa Rais mtendahaki pia haupaswi kuzingatia vigezo vya kinasaba na kidemografia kama vile kabila, jinsia, umri, n.k. Rais wa nchi ana kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba kila mtu anastahili haki na heshima katika maisha yake. Kigezo cha nne ni utii wa sheria. Kazi mojawapo kubwa ya Rais ni kuhakikisha kwamba anajenga jamii ya watu wanaoheshimu utawala wa sheria. Kigezo cha awali kabisa cha mgombea anayeheshimu utawala wa sheria ni kuangalia kiwango ambacho yeye mwenyewe huheshimu sheria.

Kwa hiyo katika kudodosa hili tutaangalia historia ya mgombea katika utiifu wa sheria katika kazi ambazo amewahi kuzifanya huko nyuma. Hapa pia tutaangalia uwezo wake wa kuheshimu sheria katika mambo ya kawaida ya maisha ya kila siku kama vile kuwa na leseni ya gari, kulipa kodi zote zinamhusu, kukaa katika barabara kuu wakati wa foleni kubwa badala ya kuchepuka pembeni, ustahimilivu wa kupanga mstari wakati wa kupata huduma, n.k.

Kigezo cha tano ni uwazi. Katika mfumo wa demokrasia uwazi ni kigezo na sifa muhimu kwa kiongozi. Tungependa Rais wetu awe muwazi katika mambo ya nchi na atakayehakikisha kwamba wananchi wanapata taarifa muhimu kuhusu mambo ya nchi na yanayohusu maisha yao. Kwa hivyo, katika kigezo hiki, tutadadisi ni kwa kiasi gani mgombea amekuwa muwazi katika utendaji wake wa kazi za umma, na anaamini nini kuhusu uhuru na haki ya wananchi kupata na kutoa habari kuhusu umma na jamii.

Aidha, Rais lazima awe muwazi katika maisha yake binafsi. Kwa mfano, kiwango na chanzo cha utajiri, aina ya familia yake-ana watoto wangapi na amewalea vipi, amewahi kuwa na wake au waume wangapi, anafanya nini wakati wa ziada, n.k. Kigezo cha sita cha sifa haiba ni uadilifu. Katika mazingira ambayo wananchi wamepoteza imani na serikali na vyama vya siasa katika kupambana na rushwa, uadilifu ni sifa mama kwa mgombea yeyote wa urais. Bahati mbaya kwamba wananchi walio wengi (70%) hawaamini pia kwamba hata vyama vya upinzani vina uwezo wa kupambana na rushwa vikiingia madarakani.

Hii inamaanisha kwamba rushwa imeshakuwa sehemu ya utamaduni wetu. Tunahitaji mgombea ambaye kwa haiba yake ataweza kuaminika kwamba ana uwezo wa kuvunja utamaduni wa rushwa katika nchi yetu. Nyenzo ya kuvunja utamaduni huu ni uadilifu.

Mgombea yeyote lazima awe na kiwango cha uadilifu kisichotiliwa shaka. Ndiyo maana nimesema mapema kwamba tunahitaji mtu ambaye si wa kawaida kuwa Rais wetu ajaye. Tukichagua mtu wa kawaida ambaye amezoea rushwa kama jambo la kawaida hatatusaidia kuvunja utamaduni wa rushwa. Hizi ni baadhi ya sifa haiba za msingi ambazo ninaamini tunahitaji kwa mtu anayetakiwa kuwa Rais wetu katika awamu ijayo.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments