[wanabidii] huyu ndiye pinda anayeutaka urais wa Tanzania

Friday, June 12, 2015
Mizengo Pinda alizaliwa Agosti 12, 1948 mkoani Rukwa (atafikisha miaka 67 Agosti mwaka huu). Pinda ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 2008.Wazazi wa Mizengo Pinda wote walikuwa wakulima kwa hiyo kijana pia alifuata nyayo hizo huku akifanya jitihada kubwa kwenye masomo yake na kufanikiwa kuhitimu shule ya msingi na sekondari, akifaulu vizuri kila alikopita.

Baada ya masomo yake ya sekondari, Pinda alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea Shahada ya Sheria (LLB) mwaka 1971 hadi 1974. Baada ya kuhitimu, alijiunga katika utumishi kwenye Wizara ya Sheria akiwa Mwanasheria wa Serikali na alikaa katika utumishi huo tangu mwaka 1974 hadi 1978.Mwaka 1978, alifanya kazi akiwa "Ofisa Usalama wa Taifa" akiwa Ikulu hadi mwaka 1982,

Rais wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere alipomteua kuwa katibu wake binafsi (Katibu wa Rais) nafasi aliyoishikilia hadi mwaka 1985.
Baada ya Mwalimu Nyerere kung'atuka na kuikabidhi nchi kwa Ali Hassan Mwinyi, Pinda alitakiwa kubaki kuendelea kumsaidia Mzee Mwinyi na alikubali wito huo. Akaendelea kuitumikia Ikulu chini ya utawala wa Mwinyi hadi mwaka 1992.

Mnamo mwaka 1995, Pinda alijaribu kugombea ubunge katika Jimbo la Mpanda Mashariki lakini alishindwa katika hatua ya kura za maoni na ikampasa kurejea kwenye kazi yake ya awali Ikulu.
Baada ya Mkapa kuteuliwa kurithi Ikulu mwaka 1995, alimteua Pinda kuwa karani wa Baraza la Mawaziri. Wadhifa alioushikilia kuanzia mwaka 1996 hadi 2000. Pinda amemuoa Tunu na wamepata watoto wanne; Janet, Jenifer, Hardwick na Narusi.

MBIO ZA UBUNGE
Mwaka 2000, Pinda aliachana na utumishi ndani ya Serikali na Ikulu akajitupa jimboni Katavi kusaka ubunge kwa mara nyingine, safari hii alipita ndani ya kura za maoni za CCM akafanikiwa kuwashinda wapinzani na kuwa mbunge. Nyota ya Pinda ilizidi kung'ara mwaka 2001, pale Rais Mkapa alipomteua kuwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) akifanya kazi chini ya waziri wake, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi, hadi mwaka 2005. Mwaka 2005, Pinda aliwashinda Sebastian Bedastus wa TLP na Albert Damian wa CUF na kuchaguliwa kwa mara ya pili kuwa Mbunge wa Katavi na aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa waziri kamili wa Tamisemi.

Bahati ya Pinda kisiasa iliruka angani wakati wa "ajali ya kisiasa" ya Edward Lowassa iliyoacha nafasi ya uwaziri mkuu wazi kutokana na kashfa ya Richmond, Rais Kikwete alimteua Pinda kuwa Waziri Mkuu. Jimboni Katavi mwaka 2010, Mizengo Pinda alishinda uchaguzi kwa "kupita bila kupingwa" na aliteuliwa tena na Rais Kikwete kushika wadhifa wa Waziri Mkuu hadi sasa.

MBIO ZA URAIS
Pinda ni mwanasiasa aliyeamua kwa dhati kuachana na mambo ya ubunge na kujitosa miguu miwili kwenye kinyang'anyiro cha urais. Wanasiasa wengi hujaribu kugombea urais huku wakiwa wanautaka ubunge, hutupa ndoano kwenye urais lakini wanapiga hesabu za ubunge ikiwa watakosa ridhaa ya uteuzi, hawa ni aina ya watu ambao huamini kuwa wanapaswa kusalia madarakani kwa njia yoyote ile, Pinda si mmoja wao.

Hivi ninapoandika, Pinda amekwishawaaga wana Katavi tangu mwaka jana na amekuwa akijiweka hadharani na kuendelea na mikakati ya chini kwa chini ya kuingia Ikulu.
Hata hivyo, kutangaza nia kwake kumekuwa na maoni tofauti kutoka kwa wananchi hasa ikizingatiwa kuwa wengi wanamfahamu vizuri kwa uimara na udhaifu wake na kila mmoja ana sababu yake.
Oktoba, 2014 akiwa nchini Uingereza alieleza kuwa amejitokeza kugombea urais ili pamoja na wenzake walioanza harakati, Watanzania wapate muda wa kuwapima.

Mwandishi wa BBC alipomhoji kama na yeye ni miongoni mwa watu wanaotaka kuvaa viatu vya Kikwete alisema, "… umesikia kama nimo? … basi tukubali hilo na yeye Waziri Mkuu yumo. Hao wote waliojitokeza pamoja na Waziri Mkuu aliyejitokeza ni katika jitihada za kusema hebu Watanzania nitazameni je, mnaona nafaa au hapana?"

NGUVU YAKE
Pinda ana nguvu ya asili, ni kiongozi mtulivu na msikivu. Mawaziri wakuu wengi waliopita hapa nchini si watu wa 'chapchap', Pinda yuko tofauti, ukimpigia simu muda wowote ambao yuko karibu nayo atapokea na atakusikiliza nini unasema, atakushauri hatua zipi zichukuliwe au atakuomba muda afuatilie suala husika kwa mawaziri wake. Mara nyingi husikiliza zaidi kuliko kuongea, hii ni sifa muhimu mno kwa kiongozi yeyote yule anayehitaji madaraka makubwa.

Jambo la pili linalompa nguvu ni kutojikweza. Pinda si mtu wa makuu wala mbwembwe, ni mtu asiyejikweza na kila mara anaishi maisha ya kawaida tofauti na mawaziri wakuu wengi duniani na hata baadhi ya waliopita hapa Tanzania. Yeye mwenyewe hujiita "mtoto wa mkulima" na aina ya maisha anayoishi yanafanana na "ukulima".

Jambo la tatu ni "usafi wa kisiasa". Ukiondoa kashfa ya Escrow ambayo almanusura imuondoe katika wadhifa alionao hivi sasa, Pinda hakuwahi kutuhumiwa kuhusika na ubadhirifu wowote ule serikalini. Hata Escrow kwa kiasi kikubwa tuhuma zilimwendea kwa sababu tu ya nafasi yake ya Waziri Mkuu lakini si kwa sababu alishiriki kukwapua fedha hizo.
Pinda ana nguvu ya asili ndani ya CCM, kwa sababu ni waziri mkuu anayemaliza muda wake, siyo jambo la ajabu kuwa ana watu wengi wanaomuunga mkono ndani ya chama hicho.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments