[wanabidii] WATUMISHI WA UMMA CHAGUENI MOJA,SIASA AU KAZI - IKULU

Saturday, March 28, 2015

WATUMISHI WA UMMA CHAGUENI MOJA,SIASA AU KAZI-IKULU

Ikulu imetoa waraka mpya kwa watumishi wa umma wenye nia ya kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa, ikiwamo urais, ubunge na udiwani katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba Mwaka huu.

Kwa mujibu wa waraka huo, mtumishi wa umma anayetaka kuwania moja ya nafasi hizo za kisiasa, atalazimika kuacha kazi na kulipwa mafao yake, endapo jina lake litateuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kama mgombea, tofauti na hapo awali ambapo alikuwa akiruhusiwa kuomba likizo.

Waraka huo wenye Kumbukumbu CAB 157/547/01/47 ukiwa na kichwa cha habari 'Kuhusu utaratibu kwa watumishi wa umma wanaogombea nyadhifa za kisiasa nchini', umetolewa hivi karibuni na kusainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.

Pamoja na mambo mengine, utaratibu huo umelenga kuondoa upendeleo katika utoaji huduma kwa wananchi na matumizi mabaya ya ofisi kunakofanywa na baadhi ya watumishi wa umma wenye nafasi za kisiasa.

"Baadhi ya watumishi wa umma wenye nafasi za uongozi wa kisiasa wamekuwa wakitoa huduma kwa upendeleo, hususani pale anayehudumiwa akiwa mpigakura wake au anatoka katika chama chake cha siasa," unasema waraka huo..

Waraka huo uneongeza kuwa baadhi ya watumishi hao wa umma wenye nafasi za kisiasa, wamekuwa wakitumia nafasi walizanazo katika ofisi zao kushawishi watumishi wenzao kupigia kura chama fulani au mgombea fulani.

Aidha unasema upo uwezekano wa kuwapo mgongano wa kimasilahi baina ya siasa na utumishi wa umma, ambao unaweza kusababisha baadhi ya watumishi wasio waadilifu kutoa siri za Serikali kwa masilahi ya kisiasa.

"Katika baadhi ya kazi imekuwapo migongano baina ya watumishi ambao ni viongozi wa kisiasa na menejimenti, hasa katika masuala ya kinidhamu, hali ambayo inaathiri ufanisi wa kazi.

"Kutokana na kasoro hizo na ili kuhakikisha kazi za kiutendaji haziingiliani na kuathiriwa na shughuli za kisiasa, Serikali imeamua kutoa mwongozo mpya kwa lengo la kurekebisha kasoro zilizojitokeza.

"Kwa msingi huo, Serikali imetoa utaratibu utakaozingatiwa na watumishi wote wa umma watakaogombea nafasi za uongozi wa kisiasa katika ngazi mbalimbali," ilisema sehemu ya waraka huo.

Waraka huo unasema madhumuni yake ni kuweka mipaka ya nafasi ya mtumishi wa umma anapoamua kushiriki kwenye shughuli za kisiasa bila kuathiri utendaji wa shughuli za Serikali.

Maelekezo ya Serikali:
"Mtumishi wa umma atakayeamua kugombea ubunge wa viti maalumu aruhusiwe kufanya hivyo na baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kumtangaza kuwa mbunge, utumishi wake ukome na alipwe mafao yake," ilisema sehemu ya waraka huo.

Waraka huo unasema mtumishi atakayeamua kugombea ubunge katika Bunge la Afrika Mashariki, Bunge la Jamhuri ya Muunguno na udiwani watalazimika kuacha kazi na kulipwa mafao yao.

"Mtumishi wa umma anayeteuliwa na waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuwa diwani, atakuwa na hiari ya kuchukua likizo bila malipo kwa kipindi chote cha wadhifa huo."

Pia waraka huo umesema endapo mtumishi atashindwa katika uchaguzi na anataka kurudi kwenye utumishi wa umma, hana budi kuomba upya ajira kwa mamlaka zinazohusika.

Aidha waraka huo umeonya kuwa mtumishi atakayekiuka maelekezo hayo atachukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu katika chombo anachokisimamia.

Waraka huo umetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 8 (1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 na kuanza kutumika Desemba Mosi, 2014.

Masharti hayo ni tofauti na utaratibu uliokuwapo awali ambao unaruhusu mtumishi wa umma kugombea nafasi za kisiasa kwa kuomba likizo bila malipo, huku akitambuliwa bado ni mtumishi aliyepo kazini


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments