> Msimu wa Vichaa?
> (Dkt.Muhammed Seif Khatib)
> Ukichaa ni ugonjwa.Ugonjwa unaomfanya muwele kuacha kujitambua kwa
> matendo au maneno ayasemayo.Ugonjwa huu hauna mtu maalum kuugua.Hugua mwanamume ama mwanamke. Huweza kumpata mtoto au mtu mzima.Haubagui dini,
> kabila ama tajiri waama masikini.Hugua wenye vyeo na mali na makabwela.Huwashika
> wasomi na mazuzu.Almradi,ukichaa haukimbiliki mtu ukimwandama. Wapo wanaoamini
> ukichaa na daraja na viwango.Wale ealiokubuhu kwa matendo, tabia na kauli hutambulika
> haraka sana.Si kawaida kwa mtu kutembea nusu uchi, miguu chini,nywele timutimu na kuongea ovyo pekee yake ukakaidi kama huyo kichaa chake hakikufurutu ada! Umwonapo
> mtu barabarani ana mawe hata kama anacheka lakini yumo kuwavurumishia wapita njia
> ukaridhika kuwa yumzima!Ama mwengine kavaa vizuri na kuonekana mtanashati lakini
> anapita akicharaza watu bakora nawe ukaamini kuwa zake ni timamu! Watu kama hawa
> hawawezi kuchukuliwa kuwa akili zao zinawatosha. Ni wehu.Yakitoea kwa watu kama hawa
> hulazimika kuondosha katika jamii.Ama hupelekwa katika hospitl maalum kwaajili ya
> kuhifadhiwa na kupewa tiba.Ingawa Waswahili huwa na usemao kuwa, ' Mwenye kichaa
> Haponi'.Wapo wagonjwa wanaoweza kuvumilika na kuachwa kuwepo katika jamii hasa
> kwa vile ukichaa wao hauhatarishi usalama wa wengine. Mgonjwa wa akili anayeokota
> makopo, chupa au kubeba makaratasi na maboxi hana madhara kwa wapita njia.Mwenye
> kuongea pakee yake au anayehubiri kwa kelele na sauti chini ya mti au juu ya jiwe hana
> mashaka yeyote.Anayeyazuru majaa na kula mabaki ya vyakula hawezi kudhuru watu
> wengine wenye akili timamu.Kwa muktadha huu siyo kila kichaa au mwendazimu hufungiwa
> ndani ya nyumba au kupelekwa hospital.Jamii yetu katika mitaa tupo wenyeakili timamu
> na tupo akili zilizotupungua lakini sote tunapishana barabarani na kusalimiana buheri wa hamsa ishirini.Wakati mwengine usipoambiwa au kuoneshwa utadhani watu uwaonao barabarani na mitaani akili zao zinawatosha na timamu.
> Kama ilivyo kwa mazao, kila msimu unao wakati wake kuwepo kwa wingi au kuadimika.Yapo mazao yenye kuonekana katika majira ya joto na kiangazi.Mengine
> huadimika wakati wa Kiangazi lakini huwa chekwa na vururu wakati wa Kipupwe.Yapo
> yanayovunwa wakati wa Masika na kadhalika.Hivi tunatambua kuwa hata vichaa hawa
> wasiodhuru watu nao wana msimu wao? Hawa hawahitaji kufungwa kamba au kupelekwa
> hospital ya vichaa kwa utabibu. Utawaona majiani,mitaani na vijijini wameshughulika bila kuwadhuru watu.Huu sasa msimu umeanza.Hutokea kila baada ya miaka mitano kati ya
> mwezi wa April na Oktoba.Mara ya mwisho ilitokea mwaka 2010. Mwaka huo watu
> waliheuka na kuchagawaa.Kadiri mwezi wa Oktoba unapokaribia uchakaramu huzidi.
> Msimu wa vichaa wa wanasiasa umeanza.Tunapigana vikumbo nao mitaani na vijijini. Hukusikia watu wakichagua majimbo na kujitangazia maeneo yao? Wazamani husema
> hawatoe majimbo yao kama vile wana hati miliki yao.Wapya huteua majimbo kama vile
> wameyaumba wao na wapiga kura wana ahadi nao kuwajazia kura zote siku ikifika.Hivi
> hudhani kuwa huo wazimu wa kiwango chake?Wapo wanaoomba wabunge na wawakilishi
> wafe ili watoe nafasi ya wagombea kujiandaa kwa uchaguzi.Baada ya vifo kuwa misiba
> na simanzi, wapo wanaofurahia kimoyomoyo vinapotokea.Wale wale wanaobeba jeneza
> la mheshimiwa na kusoma risala ya masikitiko haifiki arubaini, yeye ni wa kwanza kuanza
> kupitapita kuotangaza nia.Na wanasiasa wanawake wale wanaolia na kugaragara kwa
> kwikwi na kilio cha kite, ni wao baada ya kukunjwa tanga tu wanawania nafasi.Utu uko
> wapi? Hawasubiri tanga kukunjwa.Hawasubiri kufika arubaini ya maiti.Hawasubiri hata
> maiti kuoza sandukuni au katika mwanawandani wa kaburi.Hiki hakiwezi kuitwa kichaa?
> Hata misiba mengine ya watu mashuhuri katika miji,vijiji,mitaa ikitokea waombolezajj
> wakubwa na kundi la wanasiasa hawa walioathirika.Wataonesha ukarimu wa kuhudumia
> maiti na msiba wote.Wataleta vipolo vya mchele, viteweo na gari la kubebea maiti.Yukama
> yupo kijijjini atachanja kuni,atateka maji na kuongoza kuchimba kaburi.Hiki hakiwezi kuitwa kichaa ?Huko makanisani Jumapili haiwapiti.Sadaka huongoza kwa kutoa.Misikitini hawabanduki.Maulid yakisomwa ni wao watatoa chakula na kusimamia
> visomo vifanikiwe. Hakuna Harusi ifungwayo watu hawa wasijipitishe na kushiriki hata
> kama hakualikwa.Huo siyo ugonjwa?Wale watiwao wavulan wao jando,wanasiasa
> hutoa chochote kunogesha ngoma.Wale watiao wari wao unyagoni, wanasiasa hao
> hata bila kuambiwa hufanikisha msondo. Matatizo haya ya wagonjwa wa akili yapo
> kila jimbo la uchaguzi.Ni msimu wa vichaa.Msimu hauanuki mpaka Disemba 31 mwaka huu
> 2015.Tuombe wazimu usuwazidi ikabidi tuwafunge kamba au tuwapeleke Hospital za
> Wendawazimu!
>
>
> Sent from my iPad
--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments