[wanabidii] MAAZIMIO YA KAMATI KUU YA ACT - TANZANIA - JAN 2015

Wednesday, January 07, 2015

Alliance for Change and Transparency

(ACT-Tanzania)

___________________________________

 

Msingi wa Mtafaruku uliosababishwa na Mwenyekiti wa Muda wa Taifa Ndugu Kadawi Lucas Limbu

________________________________________________________________

1.                  Ndugu wanahabari, katika siku za hivi karibuni kumetokea mtafaruku ndani ya Chama cha ACT-Tanzania kufuatia aliyekuwa Mwenyekiti wa Muda wa Taifa Ndugu Kadawi Lucas Limbu kutangaza kwa umma kuwafukuza uongozi na kuwafuta uanachama baadhi ya viongozi na wanachama wetu. Kama alivyokwishaeleza waziwazi mwanasheria wa chama, maamuzi aliyoyafanya ndugu Limbu hayana uhalali wa kisiasa, kikatiba na kisheria na yalilenga kuwasaidia baadhi ya mahasimu wa kisiasa wa ACT-Tanzania kuonyesha kwamba Mimi na wenzangu tuliofukuzwa CHADEMA ni watu wakorofi na kwamba ilikuwa sahihi kwa CHADEMA kuchukua hatua walizochukua na kwamba malalamiko yetu ya kudai uchaguzi wa haki, uwazi, huru na amani katika chama yalikuwa hayana msingi.

2.                  Kupitia waraka huu, napenda nieleze kuwa kinachoendelea ndani ya ACT-Tanzania ni mwendelezo wa mapambano ya kupanua demokrasia ndani ya vyama. Bado tunaendelea kupigania tulichokuwa tunapigania huko nyuma, ambacho ni vyama vya siasa kukubali kufuata misingi ya demokrasia ikiwemo kukubali kufanya chaguzi za ndani zenye ushindani wa kisiasa na zinazofuata misingi ya haki, uwazi, uhuru na amani.

3.                  Msingi wa hasira za Ndugu  Limbuni uchaguzi ndani ya Chama. Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa Tanzania, Chama kikishapata usajili wa kudumu, pamoja na mambo mengine, viongozi wanapewa jukumu la kuandaa uchaguzi wa ndani ya chama ndani ya mwaka mmoja tangu kilipopata usajili. Chama chetu kilipata usajili wa kudumu tarehe 5 Mei 2014 na kinapaswa kuwa kimekamlisha uchaguzi kabla ya tarehe 5 Mei 2015. Hata hivyo Ndugu Limbu alikuwa hataki uchaguzi ufanyike kwa sababu ana hofu kwamba tukienda kwenye uchaguzi atapoteza nafasi yake. Hofu yake hiyo ameitamka waziwazi ndani ya vikao akisema kwamba angalau aachiwe miaka miwili tu kuwa mwenyekiti inatosha na atampisha mwingine. Hata hivyo, wajumbe wa vikao mbalimbali wamekuwa wakimsihi kwamba ni lazima aruhusu uchaguzi ufanyike kwa sababu hakuna namna ya kukwepa kwa sababu ni swala la kisheria na kidemokrasia. Mara ya mwisho kutumia mbinu ya kushawashawishi wajumbe wa vikao vya chama kukubaliana naye kutofanya uchaguzi ni katika kikao cha Kamati Kuu cha Oktoba 25 mwaka jana kilichofanyika Vina Hotel Dar es salaam. Katika kikao hicho aliwashangaza wajumbe alipoeleza kwamba tayari amefanya mazungumzo na Msajili wa Vyama vya siasa na eti kumwomba chama chetu kisifanye uchaguzi hadi baada ya 2016 na kwamba eti msajili amemkubalia. Wajumbe wakamhoji amepata wapi mamlaka ya yeye mtu mmoja bila kikao chochote kufanya uamuzi mzito kama huo wa kuomba msajili amkubalie kuvunja sheria ya vyama namba 5 ya mwaka 1992 na Kanuni za kudumu za uendeshaji chama cha ACT-Tanzania ambazo katika ibara ya 6 zinasema, "Uongozi wa muda utabaki na uhalali wake kwa muda usiozidi miezi kumi na mbili (12) tangu kupata usajili wa kudumu kama inavyoelezwa na sheria ya vyama vya siasa". Jibu lake lilikuwa la ajabu Zaidi pale aliposema eti hakuna chama kinachoweza kuongozwa kwa kufuata sheria asilimia mia.Baada ya Kamati kuu kumkatalia na kuitaka sekretariet ya chama kuandaa kanuni za uchaguzi na mfumo wa uchaguzi ndani ya chama na kuleta mapendekezo kwenye kikao kinachofuata cha Kamati kuu, katika kipindi cha kuanzia baada tu ya kikao hicho cha Oktoba 25 hadi leo, Ndugu Limbu amefanya yafuatayo:

a.       Tarehe 27 Oktoba 2014 Kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu bara, na bila viongozi wengine kujua akiwemo Katibu mkuu ambaye kisheria ndiye anapaswa kuwasiliana na ofisi ya msajili, aliandika barua kwenda msajili akiomba Msajili akiruhusu chama kisifanye uchaguzi hadi mwaka 2016. Hata hivyo Novemba 4, 2015 Msajili wa Vyama vya Siasa alimwandikia barua Katibu Mkuu akikataa maombi hayo na kusisitiza kwamba chama lazima kifanye uchaguzi kwa mujibu wa Sheria na Katiba yake. Sisi wengine tulikuja kujua kwamba kuna barua ya namna hiyo iliandikwa baada ya kupokea majibu kutoka kwa msajili. Tulipomuuliza Mwenyekiti akasema aliona afanye hivyo ili kukiokoa chama.

b.      Baada ya kufahamu kwamba msajili ameyakataa kisheria maombi yake ya kuahirisha uchaguzi na vikao vya chama navyo vilishamkatalia, Ndugu Limbu aliwatuma wajumbe wawili ambao pia hawataki uchaguzi Ndugu Grayson Nyakarungu na Leopold Mahona wafanye mkutano na waandishi wa Habari na watangaze kwamba wamekirudisha chama mikononi mwa waasisi na kwamba wamemfukuza Katibu Mkuu na Mwekahazina wa chama. Wajumbe hawa walifanya mkutano huo wa waandishi wa Habari tarehe 10 Novemba 2014 na kutangaza kumfukuza Katibu Mkuu na kuwapa makaripio baadhi ya viongozi na wanachama wetu. Aidha waliwasilisha barua kwa Msajili wa Vyama vya Siasa wakimpa taarifa ya maamuzi yao ya kukirudisha chama mikononi mwa waasisi na kuwachukulia hatua za kinidhamu baadhi ya viongozi na wanachama kama nilivyoeleza hapo juu. Tulipomuuliza Limbu kuhusu udhia huu, alicheka na kusema kwamba hawa vijana wanahitaji kusikilizwa na kudai eti hiyo ni sauti ya mnyonge. Kwa kuwa tunaamini kwamba uvumilivu, ikiwa ni pamoja na kuvumilia ujinga, ni sehemu muhimu ya kujenga demokrasia na maelewano hasa katika taasisi changa, tulijikaza na tukakubali kukutana na vijana wake hao na tukajadili kwa kina msingi wa tamko lao. Msisitizo wa wote watatu (Limbu, Nyakarungu na Mahona) ukawa ni kwamba lazima wahakikishiwe usalama wao ndani ya chama kwamba uchaguzi utakapofanyika watabaki na nafasi walizonazo. Sisi majibu yetu yameendelea kuwa usalama wa kiongozi na mwanachama katika chama upo kwa mujibu wa katiba na wanachama wenyewe. Hata hivyo tulikubaliana kuwa watu wote ambao tulianzisha chama katika hatua ya awali tuwe tunawasiliana kwa karibu na kujizuia kutumia vyombo vya habari katika kutoa madukuduku yetu. Mazungumzo yetu yakahitimishwa kwenye ofisi ya msajili wa vyama ambapo alitolea ufafanuzi wa mambo mbalimbali na hatimaye kuwataka waliojiita waasisi kuandika barua ya kufuta ile waliyokuwa wamemwandikia msajili kwa kuwa tulikuwa tumemaliza jambo hilo kwa maridhiano. Lakini msajili aliwaambia wasipofanya hivyo ndani ya wiki moja, itabidi aijibu barua yao. Hawakutii maelekezo ya msajili na hivyo msajili akawajibu barua yao kwa barua ya tarehe 17 Desemba 2014 ambapo pia aliwaeleza waziwazi kwamba maamuzi yao ni batili kwa sababu hayana msingi wa kisheria na katiba ya ACT-Tanzania.

4.                  Baadaya hapo Ndugu Limbu akaibua hoja nyingine na kudai kwamba Kamati Kuu na Halmashauri kuu ya chama havina mamlaka kisheria kuongoza chama katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa uongozi wa muda akadai eti orodha ya watu 11 viongozi wa kitaifa iliyowasilishwa kwa msajili na watu wawili waliojaza fomu ya kuanzisha chama eti ndiyo kamati kuu inayotamabuliwa na msajili na hao ndio wanapaswa kuongoza chama hadi uchaguzi ufanyike. Baadhi yetu tulipigwa butwaa tukishangaa kwamba inawezekanaje Msajili asitambue uwepo wa vyombo ambavyo vimeundwa na wanachama wenyewe kwa kuzingatia Katiba ya chama. Mimi nikashauriana na Mwenyekiti kuhusu umuhimu wa kuomba ufafanuzi wa maandishi toka kwa  Msajili kuhusu jambo hili. Akakubali kwa shingo upande baada ya kushindwa kunishawishi nimwamini yeye kwa uzoefu wake. Hivyo tarehe 11 Desemba 2014nilimwandikia Msajili wa Vyama vya Siasa kuomba ufafanuzi kuhusu vyombo vya maamuzi vya chama. wa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu. Msajili alitujibu na kuweka wazi kwamba baada ya usajili Chama kinaendeshwa kwa mujibu wa Katiba na vyombo vyote vya maamuzi vilivyoundwa na viongozi na wanachama ni halali na vinapaswa kufanya kazi kamili kama ilivyo katika Katiba ya chama.

5.                  Baada ya ufafanuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Sekretariati ya Chama ilikutana tarehe 23 Desemba 2014 kupanga tarehe na ajenda za mkutano wa Kamati Kuu ya Chama. Sekretariati ilipanga Mkutano wa Kikao cha Kamati Kuu ufanyike tarehe 5 Januari 2015. Pamoja na ajenda zingine, Sekretariati ilipanga ajenda ya ratiba za shughuli za chama ikiwemo ratiba ya uchaguzi ndani ya chama. Baada ya kikao mwenyekiti alipewa taarifa ya tarehe ya kikao cha Kamati Kuu na hakuwa na pingamizi. Hivyo Katibu Mkuu akapeleka mwaliko kwa wajumbe akiambatanisha na ajenda. Baaada ya Mwenyekiti kutaarifiwa na 'vijana' wake kwamba ndani ya agenda ya ratiba ya shughuli za chama kutakuwepo na kupanga ratiba ya uchaguzi alitaharuki na kuanza kufoka huku akisema kuwa kikao hicho kifutwe mara moja. Baada ya kuona kwamba hakuna aliyemkubalia kufuta kikao, akatamka kwa baadhi ya wajumbe kwamba na mimi nitaitisha Kamati Kuu yangu na kwamba sitokubali, bora chama kife kulikoni mimi kwenda 'kufia' kwenye uchaguzi. Baada ya hapo alikata mawasiliano na viongozi wengine wote ndani ya chama isipokuwa wale wajumbe ambao wanakubaliana katika kukataa uwepo wa uchaguzi. Yaliyotokea baada ya hapo ndio hiyo ya kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kutoa matamko aliyoyatoa ya kuwavua uongozi na kuwafuta uanachama baadhi ya viongozi wenzake na wanachama katika mtindo wa kampuni binafsi.

6.                  Tunasisitiza kwamba tumeanzisha chama cha kidemokrasia na hakuna namna ya kudhihirisha demokrasia zaidi ya kuruhusu uchaguzi huru, wazi, wa haki, na wa kidemokrasia. Haya ni mambo ambayo tumeyapigania kwa muda mrefu na tutaendelea kuyapigania. Tutashinda kwa kuwa tuko sahihi kisiasa na kisheria.Tupo sahihi kisiasa kwa sababu maelfu ya wanachama wetu wanapenda uchaguzi ufanyike na chama kiendeshwe ka mujibu wa katiba. Tuko sahihi kisheria kwa sababu tunasimamia sharia ya vyama vya siasa, Katiba ya ACT-Tanzania na Kanuni zake. Tunamshauri Ndugu Kadawi Lucas Limbu asiogope uchaguzi, ajiandae kupambana katika mchakato wa uchaguzi na awape fursa wanachama kuamua viongozi wanaowataka.

 

 

Pamoja na salamu za uzalendo za ACT-Tanzania

 

 

 

Katibu Mkuu, ACT-Tanzania


 







Alliance for Change and Transparency

                                       
(ACT-Tanzania)

___________________________________

 

Maazimio ya Kinidhamu ya Kamati Kuu ya ACT-Tanzania kufuatia Mkutano wake wa Tatu Uliofanyika Tarehe 5 Januari 2015 katika Hoteli ya Popex, Jijini Dar es Salaam

________________________________________________________________

Sisi Wajumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Tanzania tuliokutana katika Mkutano wa tatu wa kawaida siku ya Jumatatu tarehe 5 Januari 2015 katika Hoteli ya Popex Jijini Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine, tumepokea na kujadili kwa kina taarifa ya hali ya siasa ndani ya chama chetu. Kwa upekee kabisa tumejadili mwenendo wa kiuongozi wa Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Tanzania, Ndugu Kadawi Lucas Limbu, na kuzingatia yafuatayo:

 

1.      Mwenyekiti wa Taifa wa Muda Ndugu Kadawi Lucas Limbu amekuwa na tabia ya kufanya maamuzi peke yake bila kushirikisha vikao na katika namna inayovunja Katiba ya ACT-Tanzania na Sheria za Nchi. Kwa mfano, tarehe 31 Desemba 2014 Mwenyekiti wa Muda wa ACT-Tanzania alitangaza kuwafukuza katika uongozi na uanachama Makamu Mwenyekiti Bara (Shaban Mambo), Katibu Mkuu (Samson Mwigamba) na Katibu wa Ngome ya Wazee (Wilson Mushumbusi) na kuwafuta uanachama baadhi ya wanachama wa ACT-Tanzania.  Mwenyekiti alidai maamuzi hayo yalifanywa na Kikao cha Kamati Kuu kilichoketi siku hiyo hiyo kikishirikisha wajumbe wengine watano wafuatao: Ndugu Ramadhan Sulemani Ramadhan (Makamu Mwenyekiti Zanzibar), Ndugu Leopold Mahona (Naibu Katibu Mkuu Bara), Msellem Masrur Msellem (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar), Dotto Wangwe na Grayson Nyakarungu. Ukweli ni kwamba:

                                                  i.      Hakuna Kamati Kuu iliyokaa katika tarehe iliyotajwa na Ndugu Limbu

                                                ii.      Wajumbe wa Kamati Kuu wa ACT-Tanzania wapo 21 na kwa mujibu wa Katiba ya ACT-Tanzania, ili kikao kiwe halali akidi ya mkutano ni asilimia 50 (wajumbe 11) na lazima kikao husika kiitishwe na Katibu Mkuu.

                                              iii.      Ndugu Msellem Masrur Msellem anayetajwa kuhudhuria kikao hakuwepo nchini katika tarehe hiyo kwani yupo safarini nchini Uingereza akimuuguza ndugu yake tangu mwaka jana.

b.      Mwenyekiti amevunja makufuli ya ofisi ya Makao Makuu ya chama cha ACT-Tanzania yaliyopo Kijitonyama na kuweka makufuli aliyonunua yeye. Katika hili Ndugu Limbu ametenda kosa la jinai na amevunja Katiba ya ACT-Tanzania kwa kujitwalia madaraka yasiyo yake kwa sababu mdhibiti mkuu wa mali za Chama na mwenye mamlaka ya ulinzi na usalama wa mali za chama ni Katibu Mkuu (Katiba ya ACT-Tanzania, Ibara ya 37 (y[vi & vii]).

2.      Kamati Kuu imezingatia pia kuwa:

a.       Mwenyekiti wa ACT-Tanzania hana mamlaka ya kikatiba kuitisha kikao chochote ndani ya Chama. Kwa mujibu wa Katiba ACT-Tanzania (Ibara ya 37y(v)), mwenye mamlaka ya kikatiba ya kuandaa na kuitisha mikutano yote ya vikao vya chama vya taifa ni Katibu Mkuu wa chama. Kipengele husika kinasomeka hivi: Katibu Mkuu, pamoja na kazi zingine, "atakuwa na wajibu wa kuandaa na kuitisha mikutano yote ya vikao vya Chama vya Mkutano Mkuu wa chama Taifa, Halmashauri Kuu ya Chama ya Taifa na Kamati Kuu, na kuchukua hatua za utekelezaji wa maamuzi ya Chama".

b.      Mamlaka ya Nidhamu ya Viongozi wa Kitaifa yamewekwa mikononi wa Halmashauri Kuu ya Taifa kama ilivyoanishwa katika Ibaya ya 27 (a) ya Katiba ya ACT-Tanzania.

3.      Mamuzi yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Muda wa Taifa wa ACT-Tanzania Ndugu Kadawi Lucas Limbu tarehe 31 Desemba 2014 na baadaye kusambazwa kwa kasi katika vyombo vya habari na Ndugu Grayson Nyakarungu ni BATILIkwa kuwa hayana msingi wa kikatiba, sheria na kiutaratibu.

4.      Katika siku za hivi karibuni Ndugu Grayson Nyakarungu amekuwa akijitambulisha kwa cheo cha Katibu Itikadi na Uenezi na kuachana na cheo chake cha Mwenyekiti wa Muda wa Ngome ya Vijana ambacho aliteuliwa na Halmashauri Kuu katika Mkutano wake wa kwanza uliofanyika tarehe 25-26 Julai 2014 Mjini Singida. Tunapenda kuutarifu umma kuwa Ndugu Grayson Nyakarungu sio Katibu wa Itikadi na Uenezi wa ACT-Tanzania. Katibu wa Itikadi na Uenezi ametajwa waziwazi katika Fomu ya Viongozi wa ACT-Tanzania na katika Barua ya Msajili wa Vyama vya siasa,ambaye ni Ndugu Mohammed Massaga.

5.      Kutokana na mwenendo wa kiungozi wa Mwenyekiti wa Taifa Ndugu Kadawi Lucas Limbu pamoja baadhi ya viongozi wa ACT-Tanzania aliyoshirikiana nao kuyafanya yote yaliyoanishwa hapo juu, sisi wajumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Tanzania tumechukua hatua zifuatazo:

a.       Kutokana na kutokuridhishwa na mwenendo wa kiungozi wa Mwenyekiti wa Muda, Kamati Kuu imejiridhisha kuwa Mwenyekiti wa Muda wa Taifa wa ACT-Tanzania Ndugu Kadawi Lucas Limbu amepoteza sifa za msingi za kuendelea kukiongoza chama. Aidha, mwenendo wa Mwenyekiti ni hatari kwa taswira ya kisiasa ya chama na kwamba mwenendo huo unatishia uhalali wa kisheria wa chama cha ACT-Tanzania. Kwa kuzingatia hili, Sisi Wajumbe 13 waKamati Kuu ya ACT-Tanzania ambao tumehudhuria mkutano wa leo tarehe 5 Januari 2015 na ambao majina yetu na saini zetu zimeameambatanishwa hapa chini tumepiga kura ya kutokuwa na imani na Mwenyekiti wa Muda wa Taifa Ndugu Kadawi Lucas Limbu. Hivyo basi:Kwa kuwa Kamati Kuu sio mamlaka ya Nidhamu kwa ngazi ya Mwenyekiti wa Taifa, tumependekeza kwa mamlaka yake ya nidhamu ambayo ni Halmashauri Kuu ya Taifa kuchukua hatua stahiki.

6.      Kwa kuzingatia mamlaka yake ya Kikatiba (Ibara ya 27(c)), Kamati Kuu imemsimamisha Ndugu Leopold Mahona katika nafasi yake ya Naibu Katibu Mkuu (Bara) na hatua dhidi yake zitasubiri uamuzi wa Halmashauri Kuu ambayo ndiyo mamlaka ya uteuzi wake.

7.       Kwa kuzingatia mamlaka yake ya Kikatiba (Ibara ya 37(n[xxii]), Kamati Kuu imwemwachisha Ndugu Grayson Nyakarungu nafasi yake ya Mwenyekiti wa Muda wa Ngome ya Vijana kwa kuwa ameikataa kuitumikia nafasi yake alivyoteuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa.

8.      Kamati Kuu imeunda Kamati Maalumu ya Nidhamu kwa ajili ya kushughulika tuhuma mbalimbali kwa Ndugu Grayson Nyakarungu, Leopold Mahona na Kadawi Lucas Limbu na imeagizwa kukamilisha kazi yao ndani ya siku saba tangu walipokabidhiwa jukumu hili tayari kuwasilisha mapendekezo kwa Kikao cha Halmashauri Kuu. Hati za mashtaka zimeshatumwa kwa wahusika wote.

 



Alliance for Change and Transparency

(ACT-Tanzania)

___________________________________

 

Maazimio ya Kikazi na Kiutendaji ya Kamati Kuu ya ACT-Tanzania kufuatia Mkutano wake wa Tatu Uliofanyika Tarehe 5 Januari 2015 katika Hoteli ya Popex, Jijini Dar es Salaam

________________________________________________________________

Kamati Kuu ya ACT-Tanzania ilifanya Mkutano wake wa tatu wa kawaida siku ya Jumatatu tarehe 5 Januari 2015 katika Hoteli ya Popex Jijini Dar es Salaam. Kamati Kuu ilipokea na kujadili taarifa mbalimbali na kutoa maamuzi na maazimio kadhaa. Katika mkutano huu na waandishi wa habari tunawaletea maazimio katika maeneo makubwa mawili, ambayo ni maazimio ya kikazi na kiutendaji na maazimio ya kinidhamu. Mimi nitaeleza maazimio ya kikazi na kiutendaji, na Katibu Mkuu na Mwanasheria wataeleza maazimio ya kinidhamu. Aidha, Katibu Mkuu ataeleza kwa kina kidogo kuhusu msingi wa mtafaruku uliokikumba chama katika siku za karibuni. Ninaanza na maazimio ya Kikazi na Kiutendaji.

1.      Kamati Kuu ilipokea na kujadili matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa katika ngazi mbalimbali kwa chama cha ACT-Tanzania na kutoa maazimio yafuatayo:

a.       Kamati Kuu imewapongeza viongozi wa muda wa mikoa na majimbo kwa kufanikisha uchaguzi wa serikali za mitaa na kupata mafanikio makubwa kwa kuzingatia kuwa chama kilishiriki uchaguzi huu kwa mara ya kwanza na miezi saba (7) tu tangu kuanzishwa kwake. Sisi tunaamini kwamba baadhi ya mahasimu wetu kisiasa hawakufurahishwa na mafanikio haya ya haraka kwa chama chetu na sasa wanajaribu kututoa kwenye reli. Tunawaambia kwamba hatutoki katika reli na tunasonga mbele katika safari yetu ya kujenga chama cha kidemokrasia.

 

Matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa Chama cha ACT-Tanzania ni kama ifuatavyo:

                                                  i.      Wenyeviti wa Mitaa 13

                                                ii.      Wenyeviti wa Vijiji 13

                                              iii.      Wenyeviti wa Vitongoji 45

                                              iv.      Wajumbe 193

Jumla: 264

b.      Kamati Kuu iliwapongeza kwa kipekee viongozi na wanachama wa Mikoa ya Dodoma, Kagera, Katavi, Kigoma, Mara, Mbeya, Mwanza, Shinyanga, Simiyu,Tabora na Tanga kwa kufanikisha chama kupata wenyeviti wa mitaa, wenyeviti wa vijiji, wenyeviti wa vitongoji na wajumbe katika mikoa yao.

2.      Kamati Kuu ilipokea, kujadili na kupendekeza kwa Halmashauri Kuu ya Chama Mwongozo na Kanuni za Uchaguzi ndani ya Chama cha ACT-Tanzania unaopaswa kufanyika kabla ya tarehe 5 Mei 2015. Kamati Kuu imependekeza uchaguzi ndani ya chama ufanyike kama ifuatavyo:

i.        Shina: 19-24 Januari 2015

ii.      Tawi: 25-31 Januari 2015

iii.    Kata/Wadi: 01-10 Februari 2015

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments