*Ametajwa kuwa dalali uchotwaji fedha za Escrow
*Chini ya utawala wake, deni la Tanesco limepaa maradufu kufikia bil. 456/-
*Umeme bado hautabiriki, unakatika kila uchao
* Mikataba ya madini haijapitiwa kama alivyoahidi
Waziri wa Nishati na Madini,Profesa Sospeter Muhongo.
Jitihada za kumtetea Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa kudai kuwa amefanya mambo makubwa katika kipindi kifupi alichokaa na hivyo hastahili kuondoshwa licha ya kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bili. 300 za akaunti ya Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zimepingwa vikali kwa maelezo kuwa mengi aliyofanya waziri huyo ni kinyume cha matarajio ya Watanzania.
Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki, baadhi ya wabunge walisema tangu aanze kuiongoza wizara hiyo Mei mwaka 2012, kutoka kwa mtangulizi wake (William Ngeleja), Muhongo hajaweza kutimiza mambo mengi yaliyotarajiwa na kwamba maeneo mengi yaliyo chini ya usimamizi wake yameendelea kukabiliwa na changamoto nyingi zinazokwaza maendeleo ya nchi.
Aidha, imeelezwa kuwa miongoni mwa masuala ambayo watetezi wa Muhongo wanatakiwa kuyatolea ufafanuzi ni pamoja na ahadi kadhaa alizowahi kutoa waziri huyo bila kuzitekeleza hadi sasa; hivyo kudhihirisha kwamba siyo kweli (Muhongo) amefanya mambo makubwa na kuwa mkombozi wa dhati wa matatizo yanayolikabili taifa katika nidhati na madini kiasi cha kustahili kuachwa kwenye nafasi hiyo.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde, alisema utendeji wa Wizara ya Nishati na Madini hasa katika uongozi wa Waziri Muhongo umekuwa ni wa kukatisha tamaa na mfano mmojawapo ni kuendelea kuwapo kwa wachimbaji wa madini wanaozidi kutorosha madini kwa nia ya kukwepa kodi.
Bila kufafanua kiundani, Silinde alisema jambo linaloiangusha serikali katika kutimiza mipango yake mingi ni pale watu wanaoteuliwa kushika nafasi za juu kugeuza nafasi zao kama sehemu ya kufanya ujasiriamali (binafsi) badala ya kuutumikia umma.
"Wananchi wanakosa imani na sisi viongozi kwa sababu tumesahau wajibu wetu... kwamba tunapaswa kuitumikia hii nchi kwa kuweka mbele uzalendo na uwajibikaji. Hilo ndilo linalokosekana kwa viongozi wengi," alisema.
Kuhusu kupatikana kwa umeme, Silinde alisema: "Hata hapa ninapoongea na wewe umeme huku Mbozi umekatika na unajua umeme umekuwa ukikatika kila mara, tena bila taarifa zozote."
Akizungumzia ahadi ya Muhongo aliyosema kwamba chini ya uongozi wake, serikali ingeipitia mikataba ya madini ili taifa linufaike zaidi, Silinde alisema jambo hilo bado halijafanyika.
Silinde ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, alisema: "Kamati haijawahi kupitia mikataba yoyote. Sana sana labda kuwe na matatizo madogo madogo tu wanaleta sehemu ndogo lakini hawaji na mkataba mzima."
Aliongeza kuwa: "Wanaleta vimikataba vidogo vidogo vilivyo ndani ya mkataba mkubwa mfano Mererani kwa hiyo wanaleta kisehemu kidogo tu pindi linapotokea tatizo. Ahadi ya Muhongo kwamba Wizara ingepitia (review), mikataba ilikuwa ni siasa tu."
"Viongozi ni lazima tutambue kwamba tunawajibika katika hii nchi na kwamba tunapaswa kutimiza ahadi tunazotoa."
Kuhusu utoroshwaji wa madini, hasa ya Tanzanite, Silinde alisema urasimu uliopo katika biashara hiyo ndani ya nchi unachangia tatizo hilo.
Alisema jambo jingine ni wizi na ubadhirifu wa fedha za umma unaoshusha morali ya watu kukwepa kodi kwa kuwa fedha ambazo zingepaswa kuboresha huduma muhimu za elimu, afya na miundombinu zinawanufaisha wachache kama ilivyotokea kwenye kashfa ya Escrow.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, alisema deni la Tanesco linapanda sana na sababu mojawapo ni serikali kununua umeme kwa dola senti 55 na kuuza kwa dola senti 12.
Alisema ili kuondokana na tatizo hilo, ni muhimu nchi ikawa na mitambo yake ili kuondoa tozo za 'capacity charge.'
Kuhusu mikataba, alisema kwa sasa mbunge anaruhusiwa kumwandikia Katibu wa Bunge barua ya kuomba mkataba wowote ambao ataletewa na kuusoma.
Aidha, alisema Kamati yake pia imeletewa mikataba kadhaa ambayo serikali inataka kuipitia kwa nia ya kuifanyia marekebisho.
Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage, alisema deni la Tanesco limeongezeka zaidi pale serikali ilipoamua kuwasha mitambo ya IPTL ambayo kwa mwezi inalipwa Sh. 4.6 bilioni kama 'capacity charge'.
Kuhusu utoroshaji wa Tanzanite, Mwijage alisema mwarobaini wa kumaliza tatizo hilo ni kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ili wachimbaji hasa wadogo wauze madini hayo hapa nchini.
Mbali na kupitia mikataba ili inufaishe taifa, ahadi nyingine maarufu ya Muhongo nilikuwa ni kutoingia mikataba mipya ya gesi kabla ya sera na sheria mpya, kupunguza gharama za kuunganisha umeme na kupeleka umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), ambao ulianzishwa kitambo na yeye kuukuta tu na kuendeleza mazuri yake .
Februari Mosi mwaka huu, Prof. Muhongo alitangaza kupunguza gharama za kuunganisha umeme kutoka Sh177,000 za awali hadi Sh. 27,000 vijijini.
Awali, punguzo hilo lilitolewa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, ambako bomba la kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam limeanzia, lakini sasa gharama hizo zitakuwa kwa vijiji vyote nchi nzima. Hata hivyo, punguzo hilo na kwa mwaka mmoja tu kuanzia Machi, 2014 na kumalizika Juni, 2015.
Kwenye eneo la mapato ya Tanzanite, katika uongozi wa Prof. Muhongo Taifa limeendelea kuumia chini ya utawala wake kwa kuwa takwimu za mwaka 2013 zinaonesha kuwa Tanzania ilisafirisha nje ya nchi madini ya kiasi cha dola za Marekani milioni 38 tu, lakini Kenya waliingiza mapato yatokanayo na madini ya Tanzanite ya dola za Marekani milioni 100 na India waliingiza madini ya Tanzanite yenye thamani ya dola za Marekani milioni 300; hivyo inakadiriwa kuwa katika kiasi cha madini ya Tanzanite yanayosafirishwa nje ya nchi ni asilimia 20 tu ya madini hayo ndiyo yanayoingia kwenye rekodi za serikali na asilimia 80 yanasafirishwa kinyemela.
Jambo hilo ni kinyume cha Sera ya Madini ya mwaka 2009 ambayo inaelekeza kuwa Tanzania itakuwa kitovu cha madini ya vito barani Afrika.
Kuhusu kupunguza gharama za umeme, ahadi hiyo ni kinyume chake kwani mwaka mmoja baada ya Prof. Muhongo kuingia madarakani, Tanesco iliomba kupandisha gharama za umeme ambazo zilianza kutumika Januari Mosi, mwaka huu.
Baada ya kupitia maombi ya Tanesco ya Oktoba 11, mwaka jana, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), iliidhinisha ongezeko la umeme kutoka Sh. 221 kwa uniti moja hadi Sh. 306; hii ni kwa watumiaji wa majumbani na biashara ndogo ndogo.
Ongezeko lingine ni kwa watumiaji wa wadogo wa majumbani, hasa vijijini, ambao hutumia wastani usiozidi wa uniti 75 kwa mwezi; ambao uniti moja ilipanda hadi Sh. 100 kutoka Sh. 40.
Wateja wanaotumia zaidi ya uniti 7,500 kwa mwezi, umeme ulipanda hadi Sh. 205 kutoka Sh. 132. Ongezeko hilo kwa wenye viwanda vikubwa, lilipanda kwa Sh. 45 kutoka Sh. 121 hadi Sh. 166 kwa uniti moja.
VITALU VYA GESI
Kuhusu ahadi kwamba serikali isingetoa vibali vya gesi na mafuta hadi sheria na sera ikamilike, Prof. Muhongo alitenda kinyume chake baada ya kusema Tanzania haiwezi kusubiri miaka 100 bila kuchimba rasilimali hizo kwa kigezo cha kusubiri wazalendo wapate mitaji ya kuwekeza kwenye vitalu vya gesi na mafuta.
Akiwa kwenye ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam Oktoba mwaka jana, Prof. Muhongo alisem: "Muda wa mjadala umekwisha, serikali haiwezi kuongea na watu (Watanzania), wasiojua masuala ya gesi, hawana uwezo kuingia kwenye miradi ya gesi na Tanzania haiwezi kusubiri miaka 100 kufaidika na gesi yake."
Waziri Muhongo alisema wao ushauri waliopewa na wadau mbalimbali hawatautekeleza kwani siyo wa kitaalamu.
Alisema utafutaji na uendelezaji wa mafuta siyo biashara ndogo, bali yenye kuhitaji mitaji mikubwa na teknolojia ya hali ya juu.
Waziri Muhongo alisema hoja kuhusu sheria, ipo ya mwaka 1980 na sera ipo ya nishati ya mwaka 2003, ambayo ingeboreshwa.
Alisema serikali haiwezi kuendelea kupoteza muda kwa kupiga porojo, badala yake wanasonga mbele kwa kutazama mambo ambayo tayari yanaonyesha kuna kufaidika.
Katika kutetea hoja yake, alisema Tanzania kwa sasa iko katika mchuano mkali, kwani tayari jirani zao, Msumbiji, Kenya, Ushelisheli na hata Somalia wameanza kutafuta gesi na kuwa kuendelea kubweteka ni kupoteza muda na kufanya ushindani kuwa mkubwa zaidi.
Awali, wadau walitoa mapendekezo yake kwa serikali na kuomba isitishe mpango wake wa ugawaji wa leseni za vitalu vya gesi hadi hapo itakapopatikana sheria na sera ya gesi itakayofafanua na kuonyesha namna mwananchi atakavyonufaika nayo na hata kutoa fursa kwa Watanzania kumiliki vitalu hivyo.
DENI LA TANESCO LAPAA
Taarifa za Tanesco zinaonyesha kuwa chini ya utawala wa Muhongo, shirika hilo limeendelea kupata hasara maradufu, ambayo imeongezeka kutoka Sh. bilioni 47.3 katika mwaka 2010 na kufikia Sh. bilioni 223.4 mwishoni mwa mwaka 2012 na hadi mwishoni mwa mwaka 2013, ilikuwa na deni hilo lililofikia Sh. bilioni 456.8.
Kutokana na kukua kwa deni hilo, Ewura inaeleza kuwa 'inatishia uendelevu wa huduma ya umeme hapa nchini.'
Wakati wa kuidhinisha nyongeza hiyo, Ewura pia iliiagiza Tanesco kuzalisha umeme kwa kutumia mitambo yenye gharama nafuu na kuwasilisha ripoti kwa Mamlaka katika kila mwezi ikionyesha uzalishaji halisi na mpango wa uzalishaji.
Pia ilitakiwa kuhakikisha inapunguza kiwango cha upotevu wa umeme katika mtandao wa usambazaji kutoka asilimia 19 ya mwaka 2012 hadi asilimia 15.1, ifikapo mwisho wa mwaka 2015.
KAULI YAKE YAZUA VURUGU MTWARA
Akiwasilisha makadirio ya bajeti yake bungeni Mei mwaka jana, hotuba ya Prof. Muhongo ilisababisha vurugu kubwa katika mikoa ya Mtwara, ambazo ziligharimu maisha ya watu, majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali.
Chanzo cha vurugu hizo ni pale Prof. Muhongo alipolitangazia Taifa kwamba gesi itasafirishwa kwa bomba kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, wakati Serikali iliahidi mitambo ya kusafisha gesi ingejengwa katika mikoa hiyo ili kuiinua kiuchumi.
Katika vurugu hizo, serikali ilisema hasara iliyosababishwa na vurugu hizo ni zaidi ya Sh. bilioni nne.
WANANCHI WANENA
Mhadhiri mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo, alisema ahadi za Prof. Muhongo kutotekelezwa ni mwendelezo wa viongozi kutoa ahadi hewa zisizotekelezeka.
"Suala la umeme kukatika, hili labda nijibu kama mtu tu wa kawaida wala halihitaji msomi. Hii ni ahadi ambayo isingeweza kutekelezwa kwa mazingira yetu haya ambayo hatuna vyanzo vya uhakika vya umeme ndio maana hali imeendelea kuwa hivyo (umeme kukatika). Ilikuwa ni uongo tu," alisema.
Alisema wananchi wanayo silaha muhimu ambayo ni kura na kwamba wanatakiwa waitumie kuwaondoa viongozi wanaotoa ahadi za uongo kwenye uchaguzi kuanzia wa serikali za mitaa hadi Uchaguzi Mkuu ujao.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na NIPASHE kutoka sehemu mbalimbali nchini, walisema umeme umekuwa sio jambo la kutegemea na kwamba ahadi ya Waziri Muhongo ilikuwa 'danganya toto.'
"Kama hapa Kariakoo unavyoona ni majenereta tu tunatumia karibu wiki hii yote, kwa hiyo ukikuta umeme ni sawa ukikosa ni sawa, tumeamua kuzoea hali hii," alisema Prosper Mushi, ambaye ni mfanyabiashara katika eneo hilo.
Malalamiko hayo yametolewa pia na wananchi wa Sinza, Kibamba, Tegeta, Kawe, Dodoma, Kilimanjaro na Tanga.
EZEKIEL MAIGE: NCHI ITASONGA MBELE
Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige, amesema jimbo lake ni miongoni mwa majimbo yaliyo vijijini na kwa sehemu linapakana na mgodi wa Kahama lakini halina umeme.
Aidha, amesema Prof. Muhongo hawezi kutamba kwamba amesambaza umeme vijijini kupitia Rea kwa sababu wazo la kuanzisha wakala huyo liliasisiwa na Ngeleja mwaka 2011 ikiwa ni njia ya kukomesha uchakachuaji kwenye dizeli na petroli.
Kuhusu usambazaji wa umeme Maige ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema: "Suala la REA (Wakala wa Nishati ya Vijijini) jamani lilianzishwa na Ngeleja. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.
Ngeleja alianzisha Rea akilenga kupambana na uchakachuaji wa mafuta kwa hiyo akaweka kodi kwenye mafuta ya taa na wananchi walivyolalamika akasema fedha itakayopatikana kwenye kodi hiyo itaingizwa kwenye mfuko maalum unaoitwa Rea."
"Na alisema Rea itapeleka umeme vijijini ili wananchi waliokuwa wanatumia mafuta ya taa wapate umeme. Utakumbuka pia kwamba Ngeleja ndiye aliyeanzisha uagizaji wa mafuta kwa pamoja (Bulk Procurement). Prof. Muhongo akiondoka nchi haitasimama, itaendelea."
DALALI FEDHA ZA ESCROW
Akiwasilisha mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deo Filikunjombe, alisema Kamati imethibitisha kuwa Prof. Muhongo, ndiye alikuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Harbinder Singh Sethi na James Rugemalira, tena katika ofisi ya umma.
"Waziri wa Nishati na Madini alifanya udalali huo akijua dhahiri kuwa Sethi hana uhalali wa kisheria kufanya biashara kwa jina la IPTL," alisema Filikunjombe.
Alisema iwapo Waziri wa Nishati na Madini angetimiza wajibu wake ipasavyo, Fedha za Tegeta Escrow zisingelipwa kwa watu wasiohusika, na nchi ingeweza kuokoa mabilioni yaliyopotea kama kodi za VAT, Capital Gain Tax na Ushuru wa Stempu ambazo ni takribani Sh. bilioni 30.
Ripoti ya kashfa ya IPTL kuhusu uchotwaji wa zaidi ya Sh. 306 bilioni katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliwasilishwa bungeni mwezi uliopita na Muhongo ni miongoni mwa mawaziri ambao bunge limependekeza waondoshwe, mwingine akiwa ni Waziri wa Ardhim, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka.
Wengine waliotakiwa kuondolewa kwenye nafasi zao ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema na Katibu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/CACChgVQCYgHTN3mJdLcwMTAfFpGTFyiMEZ4E7tyB7kQ53AXJEQ%40mail.gmail.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments