[wanabidii] KUFUNGULIWA RASMI KWA KITUO CHA MAENDELEO CHA KANDA YA KUSINI MASHARIKI MWA TANZANIA

Sunday, October 12, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

YAH: KUFUNGULIWA RASMI KWA KITUO CHA MAENDELEO CHA KANDA YA KUSINI MASHARIKI MWA TANZANIA.

1.0 UTANGULIZI.
Ndugu Wanahabari, kwa niaba ya bodi ya Utawala wa Shirika la Kusaidia Jamii Tanzania ambalo kwa kiingereza linaitwa "Tanzania Social Support Foundation" ninayo heshima kubwa mbele yenu kwanza kumshukuru Mwenyenzi Mungu aliyetujaalia uzima na nguvu za kuweza kufika hapa tulipo, pamoja na afya njema, vitu ambavyo vimetufanya leo hii tuweze kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi, kila mmoja kwa nafasi yake katika jamii. Pia Shirika linawashukuru sana kwa kuwa mmekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa mnaihabarisha jamii na hivyo kuutekeleza wajibu wenu vyema na kwa ufanisi Mkubwa.
2.0 KITUO CHA MAENDELEO CHA KANDA YA KUSINI MASHARIKI MWA TANZANIA.
Kituo Cha Maendeleo Cha Kanda ya Kusini Mashariki Mwa Tanzania (Centre for Development in South – Eastern Tanzania [CDSET]) ni Taasisi ya Shirika la Kusaidia Jamii Tanzania ambayo imeanzishwa kwa ajili ya kuwaandaa wananchi wa Mkoa wa Mtwara, Lindi, na Ruvuma ili waweze kuzitumia vyema fursa za kiuchumi ambazo zinapatikana katika mikoa ya Lindi, Mtwara, na Ruvuma.
Mtakumbuka kwamba mnamo Desemba 2012 mpaka sasa kumekuwepo na sintofahamu mbalimbali kati ya Wananchi wa Kanda ya Kusini Mashariki mwa Tanzania (hasa mikoa ya Lindi na Mtwara) na Serikali kuhusiana na namna ambavyo wananchi watanufaika na rasilimali za gesi na mafuta ambazo zilivumbuliwa hivi karibuni. Serikali kwa upande wake imekuwa ikitoa nyaraka mbalimbali za kuonyesha kuwa ni kwa namna gani wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara watavyonufaika na rasilimali zilizovumbuliwa hivi karibuni lakini kwa bahati mbaya sana hakuna hatua muhimu na za haraka ambazo zimechukuliwa ili kuwawezesha wananchi katika kujiandaa vyema ili hatimaye waweze kunufaika na hizo rasilimali.
Ni kwa sababu hiyo sasa Shirika la Kusaidia Jamii Tanzania (Tanzania Social Support Foundation) limefungua Kituo Cha Maendeleo Cha Kanda ya Kusini Mashariki mwa Tanzania ambacho makao yake makuu yapo katika Ofisi za makao makuu ya Shirika la Kusaidia Jamii Tanzania (Tanzania Social Support Foundation) ambapo ofisi za Shirika zipo katika Ploti Na. 164 Block "H", Barabara ya TANU, Karibu na Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mtaa wa Rahaleo Chini, Kata ya Rahaleo, Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mkoani Mtwara.
Kituo Cha Maendeleo Cha Kanda ya Kusini Mashariki Mwa Tanzania kitahudumia mikoa ya Lindi, Mtwara, na Ruvuma na kitakuwa na Majukumu yafuatayo;-
(i) Kuwawezesha wananchi kwa kuwapa elimu itakayowajengea uwezo wa kutambua, kubaini, kuanzisha na kuendeleza fursa za uzalishaji ili kuweza kujipatia kipato na hivyo kujikwamua kiuchumi. Katika hilo ni vyema wananchi wakafahamu kwamba, ujasiriamali siyo kufungua biashara ndogondogo tu bali ujasirimali ni zaidi ya kufanya biashara. Katika jambo hili, Kituo kitawafundisha wananchi katika vikundi vidogo vidogo kuhusiana na namna ya kupanga mipango pamoja na kuendesha shughuli mbalimbali za uzalishaji.
(ii) Kituo Kitatoa elimu kwa wananchi kuhusiana na namna ya kuanzisha vikundi vidogo vidogo vya ujasiriamali, kuboresha vikundi vilivyopo kama vile VICOBA, SACCOS, na asasi za kiraia sanjari na kutoa elimu ya kutatua migogoro katika vikundi na asasi za kiraia ili ziweze kuwa endelevu. Mtakuwa mshahidi wa TSSF kwamba, vikundi vingi vya uzalishaji mali na kukuza kipato ni vya akina mama na kwamba, vikundi hivi vimekuwa vikisambaratika kwa sababu ya migogoro na kutokuelewa hatua stahiki za kuchukuliwa pindi sintofahamu zinapokuwa zimejitokeza katika vikundi husika. Hii ndiyo sababu kubwa inayofanya Kituo hiki kijishughulishe na utoaji wa mafunzo kama ilivyoelezwa hapo juu.
(iii) Kituo kimeandaa mpango maalum wa kurasimisha asasi za kiraia, mtu mmoja mmoja ambaye yupo katika sekta isiyo rasmi, na vikundi vidogo vidogo vya uzalishaji mali au ujasiriamali ambavyo vipo katika sekta isiyo rasmi, ili kwamba makundi yaliyotajwa hapo juu yaweze kutambulika kisheria na kupata fursa ambazo zitawawezesha kujikwamua kiuchumi. Fursa hizi ni kama vile mikopo, na huduma nyingine za kifedha ambazo zitachangia kuongezeka kwa kiwango cha uwekezaji katika shughuli za kiuchumi na hivyo kuongeza kipato cha mwanachi mmoja mmoja na jamii nzima kwa ujumla.
(iv) Katika hoja nzima ya kupambana na changamoto ya upatikanaji wa ajira kwa vijana, Kituo kimejipanga kutoa elimu kwa vijana kuhusiana na stadi za maisha, na pia kituo kimeanzisha kanzi data (Database) maalum ambayo inarekodi taarifa za msingi za waombaji wa ajira na hivyo kuwaunganisha na waajiri ambao wanakuwa wametangaza nafasi za kazi pale inapotokea. Zaidi ya hayo, Kituo kinatoa mafunzo rasmi ya elimu ya kujitegemea jambo litakalosababisha vijana kubuni na kuanzisha shughuli mbalimbali ambazo zitawafanya wajiajiri wenyewe na hivyo kutengeneza ajira kwa wao wenyewe na vijana wenzao kuliko kukaa na kuendelea kusubiri kuajiriwa kama ilivyozoeleka hivi sasa.
(v) Kituo kinatoa huduma za ushauri katika ufanyaji na uandishi wa tafiti mbalimbali, ushauri katika uandishi wa miradi ya maendeleo ya kijamii inayoleta tija kwa wananchi, ushauri katika uandishi wa wazo la kuanzisha biashara, ushauri katika kuanzisha taasisi mbalimbali kama vile, Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali, Vyama vya Kijamii, SACCOS, VICOBA, Makampuni na vikundi vidogo vidogo vya kijasiriamali, kwa mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu wanaotaka kuanzisha moja ya taasisi tajwa hapo juu.
(vi) Elimu ya Uraia na kujitambua ni sehemu ya mafunzo yanayotolewa na Kituo Cha Maendeleo Cha Kanda ya Kusini Mashariki Mwa Tanzania kwa Wananchi.
(vii) Katika kuandaa kizazi cha sasa na vijavyo, Kituo kimeanza kutekeleza mkakati wa kuboresha elimu katika shule za msingi na sekondari zilizopo katika kanda ya kusini mashariki mwa Tanzania ili kuhakikisha kwamba, elimu inayotolewa inakuwa na tija kwa wanafunzi pindi wanapohitimu masomo. Mtakumbuka kwamba, elimu siyo kuongeza ufaulu kwamba, mwanafunzi huyu alikuwa na alama "F" katika matokeo ya mitihani yake ya wakati uliopita sasa ana alama "A". Bali ni kumfanya mwanafunzi aweze kuyatawala mazingira yake baada ya kuhitimu masomo yake na siyo kutawaliwa na mazingira. Hilo ndilo jambo kubwa linaloshughulisha kituo chetu katika muktadha wa elimu.
(viii) Hakuna maendeleo yanayopatikana bila ya kufanya tafiti zenye tija, zinazoandaliwa katika mrengo wa kati, na zenye manufaa kwa walengwa. Kwa kulitambua hilo, Shirika la TSSF linajishughulisha katika kufanya tafiti ambapo tunda la kwanza la kufanya tafiti ambalo limekuwa ni faida kwa wananchi ni kuanzishwa kwa kituo hiki baada ya kubaini changamoto za kijami zinazoikabili mikoa ya kanda ya kusini mashariki mwa Tanzania kwa sasa.
3.0 Wito wa Shirika la TSSF na Kituo Cha CDSET Kwa Wananchi.
Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi ili wanufaike na huduma hizi ambazo zimeletwa karibu na wao na ikumbukwe kwamba, si busara kulalamika na kukumbatia matatizo wakati njia ya kuweza kupata suluhu ya matatizo ipo. Pia haiwezekani kufanikiwa katika maisha bila ya kujishughulisha. Hivyo basi naomba kwa umoja wetu kama jamii tuwajibike na baada ya kutimiza wajibu wetu, tutaweza kutembea kifua mbele katika kuidai haki yetu.
Nawatakia siku njema na utendaji mwema na asanteni kwa kunisikiliza.

Wenu

Ndg. Donati Salla
Mkurugenzi Mkuu wa TSSF.


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments