Kulikoni Wanaharakati katika jukwaa la uandishi wa habari?
Na Siyovelwa hussein
Kauli na matamko mbalimbali yametolewa na taasisi mbalimbali juu ya kadhia iliyojitokeza hivi karibuni ya waandishi wa habari kushambuliwa na askari wa jeshi la polisi katika makao makuu ya jeshi la polisi jijini Dar es salaam.
Katika kauli hizo taasisi hizo zimelilaumu jeshi la polisi na serikali kwa ujumla wake kushindwa kuheshimu tasnia ya habari na mara kwa mara kuwafanyia waandishi wa habari vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji ikiwemo kuwapiga na kuwanyang'anya vitendea kazi vyao.
Bila shaka hizi ni kauli zenye maana kubwa si tu kwa ustawi wa tasnia ya habari hapa nchini lakini zaidi kwa dhana ya uhuru wa habari ambao kila mmoja ni mdau wake. Ni kweli kwamba baadhi ya askari wasio waadilifu wakati mwingine wamekuwa wakitumia mabavu kupambana na waandishi wa habari bila kujali kwamba nao wana jukumu kubwa na halali la kufikisha taarifa za matukio katika jamii.
Ni lazima polisi na serikali kwa ujumla ielewe kwamba uwepo wa waandishi wa habari katika tukio lolote si suala la ridhaa au hisani ya jeshi la polisi isipokuwa haki ya msingi ya kikatiba nak isheria. Waandishi wa habari ni kiungo muhimu cha mawasiliano baina ya wananchi na mihimili mingine yote ya uongozi wa nchi.
Haieleweki ni vipi wakuu wa jeshi la polisi mara kwa mara wameshidwa kuwaelewesha askari wao juu ya umuhimu na ulazima wa waandishi wa habari katika operesheni zao ilhali wao wenyewe wamekuwa maswahiba wakubwa wa waandishi pale wanapotaka taarifa zao ziifikie jamii kwa ukamilifu na usahihi.
Kwa vyovyote jeshi la polisi na serikali kwa ujumla lina wajibu wa kutunza nidhamu ya ushirikiano uliopo baina ya waandishi wa habari na vyombo vingine vya dola kwani ndio njia pekee ya kuthibitisha uwazi na uadilifu wa serikali sio tu mbele ya wananchi isipokuwa mbele ya ulimwengu kwa ujumla wake.
Na hili mara nyingi hata rais wa nchi, mheshimiwa Jakaya Kikwete amekuwa akilirudia kila alipopata nafasi. Uadilifu wa jumla wa serikali yenyewe au taasisi au idara yake yoyote utaonekana na kupimwa kirahisi kupitia vyombo vya habari.
Hata hivyo liko jambo moja la muhimu sana wakati tunapovikumbusha vyombo vya dola, likiwemo jeshi la polisi, juu ya ulazima na umuhimu wa uwepo na ushiriki wa waandishi wa habari na vyombo vyao katika operesheni zao. Jambo hili si lingine isipokuwa uhalali wa waandishi wa habari wenyewe.
Kwamba ili huo upimaji wa uadilifu wa serikali na vyombo vyake upimwe kupitia vyombo vya habari ni lazima pia na vyombo vyenyewe viwe na uadilifu wa kutosha. Na tunapoongelea uadilifu wa vyombo vya habari ni lazima tuangalie nyanja zake zote, ikiwa ni pamoja na sera za vyombo hivyo, weledi wa waandishi wake katika taaluma ya uandishi, pamoja na uadilifu wa vyombo na waandishi wake kujiepusha na ushabiki katika utendaji wao. Kutokana na kadhia ya juzi binafsi kama mwandishi wa habari nimelazimika kujiuliza maswali kadhaa ambayo bila shaka na wengine pia wamewahi kujiuliza.
Mfano, Je ni kweli kwamba wanaojiita waandishi wa habari katika operesheni mbalimbali zinazohusisha matumizi ya jeshi la polisi ni waandishi wa habari na sio wanaharakati waliojificha katika mgongo wa waandishi wa habari? Je polisi watatumia jinsi gani kuwatofautisha waandishi wa habari na wanaharakati wengine, ikiwa wote wamebeba vijitabu na kalamu au vipaza sauti na kamera?
Kwa vyovyote haya ni maswali ya msingi sana kuyatafakari pale tunapotazama uhalali wa Waandishi katika operesheni mbalimbali za kipolisi na ubatili wa polisi katika kuwashambulia waandishi wa habari.
Kwa kadiri itakavyokuwa hakuna mwandishi wa habari asiyejuwa kwamba tasnia yake imevamiwa na watu wa kila aina. Kutokana na ukosefu wa njia za utambuzi wa nani ni mwandishi na nani siyo, uandishi wa habari sasa umegeuzwa chaka la kila mwenye dhamira yake kujifichia.
Wakati katika masuala ya kutafuta pesa tunawaita wavamizi hawa makanjanja bado hatujapa jina zuri kwa wale ambao wanajichanganya katika kundi la waandishi wa habari kwa sababu nyingine tofauti na ile ya kutafuta pesa.
Ukweli ni kwamba hakuna utambulisho makini wanaoutumia waandishi wa Tanzania pale wanapokuwa katika shughuli zao hususani zile zinazohusisha utendaji wa taasisi au vyombo vingine kama ya dola. Utambulisho pekee walionao waandishi wetu wanapokuwa katika shughuli zao ni vitendea kazi vyao pamoja na vitambulisho vya ajira pale inapobidi kuvitoa. Hata Press Card wengi hawana kwa sababu ama hawakidhi sifa za kupewa vitambulisho hivyo au wamekuwa wakidharau kuvichukua.
Hata hivyo ni lazima kuelewa kwamba vitambulisho ni vitu vinavyokuja baada ya watu kukutana ana kwa ana. Katika mazingira ya vurugu ni vigumu kwa mwandishi kujitambulisha kwa kitambulisho ili aweze kutofautishwa na watu wengine wenye dhamira tofauti.
Tulipokuwa tukishuhudia matukio ya pale makao makuu ya jeshi la polisi ni kweli tuliona baadhi ya watu wakitimuliwa ovyo na polisi. Bila shaka ni kweli kwamba wengine walikuwa ni waandishi wa habari. Hata hivyo tulijaribu pia kuwatambua baadhi ya watu waliokuwa wakipiga kelele zaidi kulalamika kwamba wao kama waandishi wa habari wamedhalilishwa na jeshi la polisi.
Ukweli ni kwamba miongoni mwao wengi hatukuweza kuwatambua. Mtu anapiga kelele kwamba waandishi katika Tanzania tunanyanyaswa na jeshi la polisi. Unapojaribu kumtambua wewe kama mwandishi mwenzake huoni dalili yoyote kwamba siku moja huyu uliwahi kukutana naye mahala popote katika shughuli za kiuandishi. Lazima unapigwa na butwaa huyu mwandishi mwenzetu anaandikia gazeti gani au anatangazia chombo gani. Iweje sisi wenziwe wote tusimjue?
Kwa vyovyote hii ni changamoto mpya lakini yenye hatari kubwa katika tasnia ya habari. Haiwezekani kamwe uandishi wako wewe usijulikane unajihusisha na chombo gani. Ikiwa unaonekana siku za shughuli za chama au kundi fulani tu Siku nyingine huwa unafanya kazi gani?
Ieleweke kwamba si dhamira ya makala hii kujipa mamlaka ya kuwatambua waandishi wote katika nchi. Kadhalika ieleweke pia kwamba tunajua wako waandishi wapya wanaoingia katika fani kila siku, hivyo pengine watakuwa wageni katika matukio. Hata hivyo haiwezekani uwe mwandishi wa habari halafu waandishi wengine wasikujue hata kama si wote. Bahati nzuri kazi ya habari haifanyikii chumbani kwa hiyo kama hatakujua huyu lazima atakujuwa yule.
Yako mengi yanayotokea katika tasnia ya habari japokuwa mengine hapa hatutayasema kwa sababu ya kulinda maslahi ya tasnia yenyewe. Hata hivyo lipo jukumu la msingi zaidi la Wanahabari wenyewe kulinda mustakabali wa tasnia yao na kutokubali ifanywe chaka la kufichia watu wenye dhamira tofauti na uandishi wa habari.
Imetokea mara nyingi katika mikutano ya waandishi wa habari kujiingiza watu ambao kabisa sio waandishi wa habari. Na mara nyingi inapotokea hivi waandishi wenyewe hubaki kimya kila mmoja akidhani si jukumu lake kumvua kilemba cha uandishi mtu asiye Mwandishi labda tu akijiingiza katika kudai posho.
Hata hivyo wakati mwingine hutokea pia kwamba katika utekelezaji wa dhamira zao, hao watu waliojichanganya katika kundi la waandishi wa habari wakasababisha mizozo ambayo inalikuta kundi zima kwa ujumla wake, huku waandishi wakiwemo ndani yake.
Matokeo yake waandishi na wadau wengine watapaza sauti juu ya kutotendewa haki kwa waandishi au kutoheshimiwa. Hata hivyo ukweli ni kwamba wao wenyewe hawakujitendea haki kwa kutoithamini fani yao na kukaribisha watu wasio waandishi kujiichanganya katika kundi lao bila kujua dhamira zao.
Kwa bahati mbaya wako pia waandishi ambao wameamua kuonyesha wazi misimamo na ushabiki wao wa kisiasa, kidini au katika michezo. Badala ya kusimamia taaluma zao na kuficha ushabiki wao, wako watu wanajivika uanaharakati badala ya taaluma yao ya uandishi wa habari. Hata kama mtu atajigamba kwamba hiyo ni haki yake ya msingi kama Mtanzania lakini ukweli haki hiyo inamuondolea uhalali wake wa kuheshimiwa kama mwanahabari. Na lolote linalowakuta wanaharakati wengine ni lazima litamkuta na yeye.
Yako mabaraza, vyama na taasisi nyingi zinazosimamia masuala ya waandishi katika nchi. Bila shaka vyombo hivi vingeweza kuwa watetezi wazuri zaidi wa waandishi wa habari kama vingeundwa na waandishi wenyewe waliomo katika utendaji. Kwa bahati mbaya wakati mwingine vyombo hivi vinavyojiita wadau wa habari vimekuwa vikiundwa na watu walioipa mgongo tasnia ya habari na kugeukia uanaharakati wa kisiasa.
Bila shaka hawa ni tatizo katika fani ya habari kwa vile hata kama wanajipa uhalali wa kutetea waandishi lakini ukweli wanazo dhamira nyingine tofauti na uandishi wa habari ambao ni taaluma yenye sheria na maadili yake.
Kwa kumalizia niseme tu kwamba pamoja na waandishi kuhitaji msaada mkubwa wa utetezi kutoka kwa wadau wake ambao ni jamii kwa ujumla lakini ni lazima na jamii ijifunze pia kujua nani ni mwandishi na nani ni mwanaharakati aliyejificha katika kundi la waandishi.
Tunajua na ni haki yetu kusema kwamba kama ambavyo baadhi ya Waandishi wameajiriwa na jeshi la polisi katika siku za karibuni wako pia waandishi ambao wamejiunga na makundi mbalimbali ya kiharakati, iwe kwa ajira au kwa ushabiki wao. Kwa vyovyote waandishi hawa wanafahamiana na pengine wanaviarifu vyombo waliojiunga navyo juu ya aina ya waandishi waliomo katika tasnia.
Kwa sababu hii, pamoja na kuendelea kuliasa jeshi la polisi kuwafunda askari wake juu ya ulazima wa kuheshimu wanahabari lakini lazima pia tujue kwamba na wao wako katika nafasi nzuri ya kujua nani ni mwandishi wa habari na nani siyo. Ni lazima sisi wenyewe tujisafishe kwanza na kujiweka mbali na wavamizi ili tuendelee kuheshimiwa na tusikutwe na udhalilishaji wa mara kwa mara.
Baada ya kusema haya narejea kuwapa pole waandishi wa habaro wote waliopatwa na msukosuko wa juzi na juu ya yote naendelea kuwakumbusha viongozi wa jeshi la polisi kuwaonya askari wao juu ya kudhalilisha waandishi. Hata hivyo ni lazima sasa waandishi wa habari watafute namna itakayowatambulisha kirahisi katika matukio yoyote.
0787013385/0655013385
0 Comments