UJUMBE WANGU KWA VIONGOZI WA DINI MINTARAFU SIASA ZA CHUKI, FITINA , HILA, MANYANYASO NA ZA KIBABE NCHINI TANZANIA.
Na padre Baptiste Regina Mapunda (M.afr)
frmapunda91@gmail.com
Ni ukweli usiopingika kwamba viongozi wa dini ni viongozi wa imani katika madhehebu yao lakini pia ni viongozi wa jamii pana pia, tena ni viongozi wenye mamlaka ya Kimungu. Viongozi hao kwa kawaida wanaaminika sana katika jamii hata ya Watanzania. Biblia takatifu inamwonyesha nabii Jeremiya kama mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu na kukabidhiwa mamalaka ya kubomoa na kujenga.
Nabii huyu pia alipewa mamlaka ya kukemea hata watawala wabovu wa jamii kama ilivyo jamii ya Watanzania ambayo inatafunwa na maovu ya watawala kila kukicha utasikia mara EPA, ESCROW, mafuta machafu, umeme umepand kiholela nakadhalika.
Wito wa nabii Jeremiya ilihusu hasa kuwakemea Waisraeli waliojikita katika kutenda maovu baada ya kuacha njia ya Bwana, njia ya amani, upendo,njia haki na uhai. Hii pia ni kazi ya viongozi wa dini wa Tanzania katika nyakati hizi za sasa.
Mahali tulipofikia sasa jamii ya Watanzania inahitaji manabii wa kuonyesha njia, kuonyesha mwanga, na hasa kuwakosoa watawala ambao wanaonekana kujifanya wapo juu ya sheria na kuonekana kama ni 'miungu watu" wakati wao pia ni wanadamu.
Katika makala hii nitaongelea kwa kifupi tu juu ya matatizo yanayowakabili viongozi wa dini nchini Tanzania hasa katika kipindi hiki cha migogoro ya ardhi, mauaji, ukandamizaji, wizi wa mali ya umma, utapeli na mvurugano wa katiba mpya uliosababishwa na Rais pamoja na chama chake cha CCM.
Mambo ninayoyaandika ni tafakari na uchambuzi wangu mimi mwenyewe hata kama mambo mengine yanaweza yakawa yamesemwa na baadhi ya watu hii haijalishi mathalani kama alivyosema Tundu Lisu kwamba baadhi ya viongozi wa dini wanakula rushwa ili kupotosha mambo mimi sioni kama hayo ni matusi inawezekana kuwa ni hali halisi kama navyofahamu. Shida ninayoiona nchini mwetu sasa ni hii ya watu kuhruza ukweli kuwa uwongo, na ukweli ni matusi na chuki kitu ambacho hakitasaidia maendeleo na mstakabhali wan chi yetu bali nu migongano katika jamii yetu.
Kwwanza je, kuna kiongozi yeyote wa dini aliyesimama na kusema tumetukanwa? Sivyo, bali ni chuki za kisiasa ndizo zinapelekea watu kupandikiza maneno kama hayo. Je, kusema kamba padre mapunda ni mwongo ni kumtukana labada ndivyo anavyoonekana na wala hawezi kukasirika hata siku moja.Tabia ya mtu haitegemei watu wanasema mimi, bali yeye mwenyewe yukoje.
Hili ni tatizo katika jamii yetu watu kupenda kugombanisha watu. Naamini viongozi wa dini wanabusara ya kutosadiki maneno kama hayo wakijua kwamba kazi ya kitume inachangamoto nyingi na mojawapo ni kutukanwa, kudharau na kutungiwa uwongo. Pia viongozi wa dini lazima watambue kwamba siasa za Tanzania ni za majitaka na pia za kuchafuana na hivi ugonjwa huu upo katika jamii nzima zikiwamo taasisi za dini pia.
Kwa upande wa viongozi wa dini wenyewe mimi naona kama kuna ndoa na serikali iliyopo madarakani yaani ya kuwa watiifu hata pale serikali inapoboronga wanashindwa kuiambia wazi wazi. Kumbuka viongozi wakuu wa dini (Maaskofu, Wachungaji, mashekhe enz za Mwalimu walikuwa na heshima kubwa hata katika mambo ya kisiasa na walisikilizwa.
Inawezekana viongozi hao walikuwa wamejitenga na kujishirikisha sana na mambo ya kisiasa. Mfano leo unamwalika waziri anakuwa mgeni rasmi katika harambee yako ya kuchangia ujenzi wa kanisa yeye anakuletea million mia tatu pmaoja na rafiki zake, je hapo hujahongwa?
Mambo kama hayo yanawafunga midomo na hivi kushindwa kuwakemea viongozi hao wanapoboronga au serikali inapokiuka sheria. Askofu ni mtu mkubwa na jimbo lina watu wengi sana maskini na matajiri, je kweli inashindikana kuongoza harambee bila wanasiasa? Hili ni doa mojawapo kwa upande wa viongozi wa dini na wanasiasa wanatumia kama njia mojawapo ya kuwaziba midogo yenu. Je,bado hatujapoteza nafasi yetu katika masuala ya jamii hasa siasa?
Pia naona kuna unafiki kwa serikali na hivi kutoa taswira ya kushirikiana na mafisadi na hili nimeshalisema mara nyingi hata likanijengea chuki hata hivi napenda tena kulirudia leo kwa manufaa yetu sote kama viongozi wa dini. Je, kwa mantiki hii wananchi wakisema sisi tumepoteza nafasi yetu katika siasa nchini Tanzania tutawajibu vipi?
Viongozi wa dini wanaonekana kuamini kinachosemwa na viongozi wa serikali ya CCM na kukifuata hata kama pengine kina madhara kwa taifa. Mfano halisi ni propaganda ya CCM kwamba waliopotosha mchakato wa katiba mpya ni UKAWA, hivi warudi bungeni. Lakini wakati wakipigia kelele UKAWA mbona hawajaisema kisawasawa serikali ya CCM kulikoni, wananchi wengi wanahoji kwanini kuegemea upande mmoja. Kama wamefanya vikao na viongozi wa CCM kwa nini basi hawajakutana na viongozi wa UKAWA?
Pia wananchi wanawasiwasi kwamba viongozi wa dini ni waoga, na wana hofu kwa CCM, na hili wengi wanalisemea wazi wazi. Je, viongozi wa dini tunategemewa kuwa na ujasiri wa kusema ukweli pale ambapo watu wote wanakaa kimya ili uwongo usitamalaki na hivi kumwinua shetani. Ni vema viongozi wa dini wakajitathimini upya kuhusu suala la hofu kwa CCM. Au viongozi hao hawajiamini katika utendaji wao kwamba wanasauti ya Mungu ambayo inapashwa kusikika hasa katika kipindi kama hiki.
Je, wanahofia kutekwa , au wanahofia kushambuliwa na waandishi wa habari pamoja na kujenga uadui na serikali ya CCM? Sisemi kwamba viongozi wa dini tuanzishe mapambano sivyo. Hata hivi mapambano tayari yapo katika jamii, sasa tunafanya nini kama viongozi wa dini? Waingereza wanasema " if you cant beat them, then join them" (Usipoweza kupambana nao , basi ungana nao). Sisi tumechagua upane upi?
Wananchi wanaona tatizo jingine la baadhi ya viongozi wa dini katika nyakati hizi ni kushiriki unafiki na pengine hata uwongo wa serikali ya CCM kama tunavyoshuhudia siku hizi juu ya upotoshwaji wa nani kavuruga Bunge tukufu la Kutunga katiba nchini. Rais na wanaCCM wanajua walichofanya kwa kung'ang'ania sera zao na kuacha kujadili Rasimu ya maomi ya wananchi na hicho ndicho chanzo halisi cha mkwamo wa katiba hii.
Propaganda za CCM zimegeuza kibao na kuwabambikiza UKAWA ndiyo wanaokwamisha upatikanaji wa katiba eti kwa sababu wamesusia bunge hilo. Na kwa hiyo UKAWA wanamapepo (sijui ni mangapi) wanapaswa kuombewa, sijasikia kama viongozi wa dini wamewaombea UKAWA au la. Lakini imesikika miito mingi kutoka kwaa viongozi wa dini kuwasihi UKAWA warudi bungeni tena bila mashariti kujadili katiba mpya kupitia rasimu ya Warioba.
Viongozi wa dini kuwasihi tu UKAWA kurejea na kujadili rasimu ya Warioba bila kuwakemea CCM kuacha kuchakachua moani ya wananchi haitoshi na si sahihi. Hapa inaonekana wazi kwamba shida mojawapo ya viongozi wa dini ni kutotambua kwamba katika uwanja wa siasa kuna shida kubwa sana ya kubadilisha uwongo kuwa ukweli na kutaka na hata kulazimisha wananchi waamini hivyo.
Mkwamo wa katiba mpya ni mfano mzuri ambao kila mtu anajua nani kaharibu, yaani inakuwa kama baba anamlazimisha mtoto wake wa miaka mitano kwenda kulala akimwaminisha saa tano asubuhi ni usiku, wakati mtoto naye anajua ni bado mchana. Je hili linawezekana? Mtoto atakwenda kulala kama haelewi maana ya mchana na usiku, au atakwenda sababu ni mwoga anaogopa kupigwa, namna nyingine watoto wa siku hizi basi utaishia kuchekwa kwa sababu umebugi men.
Viongozi wa dini ni muhimu mujielimishe juu ya mkwamo wa mchakato wa katiba nchini Tanzania na wajibu wenu katika kusaidi kukwamua kwa kusimamia ukweli na siyo kuwa upande mmoja au kukaa kimya kabisai. Viongozi wa dini lazima wajue kwamba Bunge la Katiba linaendeleza mchakato na siyo kuanzisha upya kwa kutoa maoni tena bungeni. Hii hatua ya kutoa maoni imepita na tume imeshapendekeza muundo ambao ni waserikali tatu ambayo ni maoni ya wananchi.
Sasa uchakachuaji huu wa maoni ya wananchi na Serikali ya CCM ni alama wazi ya kulewa madaraka. Mara moja niliandika katika makala zangu kwamba ulevi ni ugonjwa unaomfumba mtu asijitambue ni nani na anafanya nini. Naomba kwa manufaa ya kutoa elimu nirudie tena kwamba katika dunia ya leo hakuna ugonjwa au ulevi mbaya kama wa "MADARAKA" katika jamii yeyote ile hata kama ni taasisi ya madhehebu ya dini. Hayo tunayashuhudia kila kukicha dunia nzima.
Inaonekana wazi kwamba CCM haitaki katiba mpya wala haitaki tume huru ya uchaguzi, bali inataka maigizo tu ya katiba mpya na tume huru ya kisanii.
Hayo tuyakatae wote kwa nguvu, akili na moyo mmoja na ndiyo wanayoyakataa UKAWA. Je, viongozi wa dini hawaoni hoja hizo? Sisi wengine kwa kuandika ukweli na kuonekana kama tunashabikia UKAWA tunatukanwa sana lakini kwa sababu ya ukweli tutaendelea kusimamia ukweli hata kama watu hawaupendi. Yesu alitufundisha kwamba " Ukweli utatuweka huru."
Jamii ya Watanzania ilitegemea viongozi wa dini iwaokoe na maovu, fitina, chuki,manyanyaso na ubabe wa serikali ya CCM, lakini sasa viongozi hao nao wanaonekana wamezama katika matope ya serikali hiyo hiyo. Wananchi waelewa hawaelewi maana yake ni nini na wanaoana kama viongozi wa dini wanajikosha (Kujikomba,kujipendekeza) kwa serikali ya mafisadi na kuonekana kama nao kunufaika na ufisadi huo.
Kinachotakiwa viongozi wa dini lazima tujitenganishe na maovu kama hayo.Na wale viongozi wa dini walioko katika Bunge la Katiba wasimamie ukweli na kuacha kuungana na wale wanaotaka kuchakachua rasimu ya maoni ya wananchi kiubabe. Wananchi sasa wanajiuliza dawa ni nini kama viongozi wao wanaona hawawasaidii kutetea katiba na mfumo wa haki, upendo, na usawa katika jamii? Je, hii siyo alama ya kupoteza nafasi zenu katika medani za siasa nchini Tanzania?
Wananchi wanaona sasa dawa ni moja tu yaani kuelimishana na kujisimamia wenyewehasa huko vijijini na kuiambia ukweli serikali ya CCM pamoja na viongozi wa dini kwamba tunaelekea pabaya. Na zaidi ya hapo wanaona kamba umaskini, maovu, mauaji, utesaji, utapeli, wizi wa mali ya umma, mikataba mibovu inayotesa wananchi ikiwamo ya gesi kule Mtwara inasababishwa na watawala wa serikali ya CCM.
Wananchi wengi wamechoka na ahadi hewa na kilichobaki ni ubinafsi na kulindana. Ajira ni shida kwa vijana isipokuwa kama wewe ni mtoto wa kigogo au unamjua yeyote ngazi ya juu au uhonge. Wananchi wanaona sasa ni muda mwafaka kuachana na CCM kwani imeshindwa kuwakwamua katika uamaskini wao pamoja na kwamba nchi imejaa rasilmali kibao nchini nzima.
Mtazamo huu ni wa wananchi wengi ingawaje hawana pa kusemea. Mimi binafsi naona ni changamoto kubwa sana kwetu sisi viongozi wa dini hasa katika kipindi hiki cha kueelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2015. Je sisi viongozi wa dini bado tuna nafasi yetu katika kusaidia kuendesha siasa safi na zenye sera nzuri nchini Tanzania hasa kwa ushairi, kukemea maovu,na kwa uwepo wetu.?
Kazi mojawapo ya viongozi je siyo kuwajengea viongozi wetu wa kisiasa hasa watawala roho ya uchamungu na kuongoza kwa kufuata misngi ya haki, usawa, demokrasia na utawala bora kwa wote bila kujali vyama vilivyopo. Wahenga hunena kwamba ' utavuna ulichopanda' kama ulipanda chuki utavuna chuki, na kama ulipanda 'upendo haki na amani basi wewe utavuna upendo,haki na amani' Mungu ibariki Tanzania na viongozi wote wa dini.
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments