[wanabidii] MWALIMU NYERERE ANAJIGEUZA KABURINI KWAKE!

Wednesday, August 13, 2014

MWALIMU NYERERE ANAJIGEUZA KABURINI KWAKE!


Na Daniel Mbega

BABA wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere atakuwa anajigeuza kaburini kwake. Ndivyo tunavyoweza kusema katika kipindi hiki cha miaka 15 ya kifo chake wakati tunaposhuhudia wanasiasa wanavyobishana namna ya 'kuua' Muungano – mwanawe pekee aliyesalia – huku tayari wakiwa wameigeuza Ikulu mahali pa biashara na ufisadi ukitamalaki.
Tangu tuliposhuhudia Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Ben Mkapa na mkewe wakianzisha ujasiriamali wakiwa Ikulu na kujiuzia mashirika ya umma huku mengi yakiuzwa ama kubinafsishwa, hali imekuwa mbaya kila sekta na watendaji wengi wameamua 'kuchukua vyao mapema', hivyo kuifanya Tanzania inuke rushwa na ufisadi.
Ni mageuzi, lakini vikumbo hivi havikuwa na kasi namna hii, na hata kama ilikuwepo, basi ilikuwa na staha. Kinashuhudiwa hivi sasa ni ubabe, jeuri na mambo mengine kama hayo katika kuidai Tanganyika ndani ya Muungano na wakati huo huo wengine wakipinga muundo wa serikali tatu.
Wapo wenye nia ya dhati kulizungumzia suala hili: Wale wanaotaka muundo wa serikali tatu (ikiwemo ya Tanganyika) wana mambo yao - wengine wanataka ziwepo serikali nyingi ili waweze kupata vyeo vya kisiasa. Wananchi wanatumiwa kama daraja tu la 'kuhalalisha' hoja zao, hakuna kingine!
Wanaong'ang'ana na serikali mbili - hasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) - nao wanahofia kuwepo kwa serikali tatu kwa vile nguvu ya kulishika dola itapungua. Tena yawezekana wasirudi madarakani katika mfumo mpya.
Kikubwa zaidi ni kwamba, hofu ya kuvunjika kwa Muungano iko dhahiri kwa sababu hata Wazanzibari wenyewe - ambao kimsingi waliukataa Muungano tangu mwaka 1992 - wamesimama kidete wakiidai Tanganyika na wanapinga mbinja kweli kweli kuhakikisha serikali ya Tanganyika inarejea - halafu waingie kwenye Muungano wa Mkataba!
Lakini tunapoelekea kuazimisha miaka 15 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, ni dhahiri makundi mengi yamejitokeza na maono tofauti katika suala zima la Muungano – ambao yeye aliamua kuingilia kati na kuizima hoja ya Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano iliyotolewa na Njelula Mulugale Kasaka mwaka 1993.
Tuliokuwepo tunakumbuka mambo yaliyotokea, na kwa vijana wa sasa ni vyema kuwakumbusha tu kwamba Mwalimu alilipinga wazo hilo kwa nguvu zake zote na kusema Serikali Tatu siyo sera za chama.
Hata alipowauliza viongozi waliokuwa wakidai serikali tatu, walishindwa kujibu. Yeye akasema katika utenzi wake:

Ati kuuliza watu
"Serikali ziwe tatu?"
Ni swali gumu ajabu,
Wanashindwa kulijibu

Tena ati wanasema
Walihofia gharama
Ila serikali tatu
Gharama zake si kitu



--
"Kama hawatuwekei mgombea mzuri, kwanini watutawale?" ~ Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Dar es Salaam, 1995

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments