[wanabidii] KATIBA MPYA - MUUNDO WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO

Monday, August 25, 2014

Ukiharibu Muundo wa Jamhuri kwenye Bunge utavuruga kabisa

Wakati Bunge Maalumu la Katiba likiendelea na vikao vya kamati zake, sintofahamu juu ya nini hatima ya mawazo ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea kuibuka.

Katika siku za hivi karibuni, mijadala ya Kamati za Bunge maalumu inaonyesha kugawanyika kimtAzamo. Baada ya kumaliza muundo wa Muungano, ambao kwa bahati mbaya mjadala wake haukujikita kwa kiasi kikubwa katika hoja na sababu zenye mashiko bali umamuzi wa wengi dhidi ya wachache, tatizo kubwa ambalo naliona kwenye mchakato huu ni pale tunapoamua kupuuza ukweli, uhalisia na kukumbatia uhalisia usiokuwepo.

Tunapaswa kuanza na Muundo wa Jamhuri

Randama ya Rasimu ya Katiba Mpya inaeleza bayana kwamba kwa kawaida, nchi ambazo zimeingia katika muungano, zinaweza kuchukua moja kati ya sura hizi tatu zifuatazo:

1. Muungano wa Serikali Moja (Unitary State);

2. Muungano wa Shirikisho (Federation); na

3. Muungano wa Mkataba (Confederation)

Kwa vyovyote vile, mfumo wa shirikisho unakuwepo pale ambapo nchi mbili au zaidi zimeungana na hazikuunda Serikali moja. Kwa maana hiyo, shirikisho (Federation) linamaanisha mfumo wa utawala wa nchi ulio na sifa zifuatazo:

1. Kunakuwa na ngazi mbili za Serikali zinazotawala eneo moja la nchi na raia wale wake; moja ikisimamia mambo ya Muungano (shirikisho) na nyingine mambo yasiyo ya Muungano (yasiyo ya shirikisho);

2. Kila ngazi ya Serikali, yaani ile ya shirikisho na ile ya nchi washirika inakuwa na mamlaka kamili na maeneo ya utendaji na uhakikisho wa kikatiba wa uhuru wa kutoingiliana baina ya Serikali hizo katika maeneo waliyo na madaraka nayo bila ya kushauriana. Mfumo huu ni tofauti na ule wa dola moja lenye Serikali moja (unitary state), ambapo Serikali kuu inaweza kuamua kuzinyang'anya madaraka Serikali za chini yake kadiri inavyoona inafaa;

3. Katika muundo huu, Serikali ya Muungano ndiyo yenye mamlaka juu ya masuala yote yaliyokubaliwa kuwa ya Muungano (shirikisho). Serikali za nchi washirika zinakuwa na mamlaka ya kikatiba ya kushughulikia mambo yasiyo ya Muungano katika maeneo yao ya utawala; na

4. Katika Muungano wa shirikisho, mamlaka kuu ya kidola (sovereign powers and functions) yapo chini ya Serikali ya Shirikisho (Muungano).

Ingawa katika mfumo huu wa Muungano wa Shirikisho kunakuwa na Serikali zaidi ya moja kwa mujibu wa Ibara ya 2 ya Mkataba wa Montevideo wa Haki na Majukumu ya Nchi (Montevideo Convention on Rights and Duties of States) katika sheria za kimataifa na uhusiano wa kimataifa, nchi inayofuata mfumo wa Muungano wa Shirikisho, huchukuliwa na kuhesabiwa kuwa nchi moja.

Sura ya Shirikisho la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni nchi yenye mamlaka tatu na Serikali tatu, inajidhihirisha katika masharti yaliyomo katika Ibara za 61, 63, 64, 65, 66, 67, 70, 71, 72, 110, 111,117, 119, 156 na 235. Ili kuleta mantiki ya Muundo wa Muungano na mjadala wake ni sharti vifungu vyote hivyo visomwe kwa pamoja.

Muundo wa Bunge la Jamhuri

Muundo tulionao una shida kubwa, sote tumeshuhudia malalamiko kutoka kwa watu wa Tanzania Bara ambao wamekuwa wakihoji iweje wabunge kutoka Zanzibar washiriki katika kuamua mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara?

Malalamiko haya yanaongezeka pale ambapo kuna watu kutoka Bara wanaoshiriki uamuzi kwa mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar. Ili kuondoa utata huu, Rasimu ya Katiba Mpya inapendekeza Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo wabunge wake watachaguliwa moja kwa moja kutoka katika ngazi za mikoa kama majimbo kwa Tanzania Bara na Wilaya kama majimbo kwa upande wa Tanzania Zanzibar.

Katika Muundo wa Shirikisho, kunakuwa na Bunge la Shirikisho (Muungano), ambalo linapewa dhamana ya kuisimamia Serikali ya Muungano, kutunga sheria kwa mambo ya Muungano na kuwa chombo cha uwakilishi katika ngazi ya Muungano. Kimsingi, Bunge la Jamhuri ya Muungano ndicho chombo kinachopokea taarifa ya utekelezaji wa Malengo Makuu na Misingi ya Mwelekeo wa Shughuli za Kiserikali na Sera za Kitaifa. Bunge hili ndilo litakuwa likilitazama taifa kwa mambo ya Muungano, lakini pia lina dhamana ya kupokea taarifa kutoka Serikali ya Muungano juu ya usimamizi na uratibu wa sera na sheria kwa mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika na Zanzibar.

Tukifika hapo, yale malalamiko ya upande mmoja kwenda kuamua mambo ya upande mwingine litakuwa limetatuliwa. Kila upande utakuwa na chombo chake cha kusimamia Serikali ya upande husika na ndicho kitakuwa chombo cha kutunga sheria na uwakilishi kwa mambo yasiyo ya Muungano kwa Zanzibar na kwa Tanganyika.

Muundo huu wa Bunge unabainisha mamlaka na madaraka ya Bunge la Muungano, linaleta taifa pamoja na linaongeza ufanisi ukizingatia ni Bunge dogo, wabunge wa majimbo 70 wanawake 35 na wanaume 35, pamoja na wabunge watano kuwakilisha watu wenye ulemavu.

Mapendekezo yatakayovuruga Bunge la Jamhuri

Wako wasomi nguli, ambao wakati wa kukusanya maoni walipata fursa ya kutoa maoni yao. Tena wengine hawakupewa nafasi ya kutoa maoni uwanjani, hawa walipewa nafasi maalumu, kuja kuwasilisha maoni yao mbele ya Tume nzima ya Mabadiliko ya Katiba. Baadhi ya maoni yao nitapenda kuyatolea ufafanuzi hapa. Maoni haya nitakayofafanua ni yale ambayo yamejikita katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Mmoja wa wasomi nguli ambaye alifika mbele ya tume na kupendekeza muundo ambao ulikuwa unafanya Jamhuri ya Muungano kuwa na dola mbili, kwa maana ya Dola ya Muungano na Dola ya Zanzibar ndani ya nchi moja, inaitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika muundo huu, msomi nguli anaeleza kwamba, kila dola litakuwa na Serikali, Bunge na Mahakama kwa maana ya Dola ya Zanzibar na Dola ya Muungano. Kwa namna ambavyo maelezo ya msomi nguli yalivyo, kinachoitwa Dola ya Muungano, ukiacha Serikali na Mahakama, Bunge lake litakuwa na sehemu mbili kwa maana ya Baraza la Nchi na Baraza la Wananchi. Kwa mujibu wa maelezo, Baraza la Wananchi pamoja na Baraza la Wawakilishi ndiyo watakaokuwa na jukumu ya kutupatia wajumbe wa Baraza la Nchi.

Muundo huu kwa hakika siyo tu unajichanganya wenyewe, lakini unachanganya dhana zisizochanganyika. Msomi nguli huyo anazungumzia uwepo wa dola mbili, dola kwa tafsiri ya Mkataba wa Montevideo (1933) ndiyo nchi yenyewe. Kwa maneno mengine, huwezi kusema una nchi mbili ndani ya nchi moja.

Nikija katika muundo wa Bunge, msomi huyo nguli, anabainisha muundo ambao yeye anahisi utaimarisha Muungano wetu na kutupa fursa ya kuzitatua 'kero' za Muungano. Pendekezo lake la kuwa na sehemu mbili kwa Bunge la Muungano (Baraza la Nchi na lile la Wananchi) ni boresho baya zaidi, ambalo litaongeza manung'uniko hasa kutoka upande wa Tanzania Bara.

Sote tunafahamu kuwa tuna mamlaka tatu za nchi na kila mamlaka inapaswa kuwa na Mahakama, Bunge na Serikali. Changamoto ya sasa ni kwamba Tanzania Bara wanatumia Bunge Moja na Tanzania Zanzibar kwa mambo ya Muungano na mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar na Bara.

Huwezi kupata majibu mazuri zaidi ya kubadilisha muundo na mfumo, kama ambavyo Rasimu inapendekeza, kitendo cha kuendelea kuififisha Mamlaka ya Tanganyia na kuiinua zaidi Jamhuri ya Muungano, kimsingi ndiyo kuibatiza au kuiweka maji Jamhuri ya Muungano na Bunge lake kuwa ni kwa Watanganyika pekee.

Tunapofika katika mazingira hayo, Wazanzibari wanakuwa wamepachikwa katika Jamhuri ya Muungano, tena kiongozi mwingine kwa mbali akasema; 'unajua Zanzibar ni koloni letu?' Haya ni makosa makubwa yanayotakiwa tuyakemee na tufafanue kwa nguvu ili umma wa Watanzania usikie, maana nasikia hivi karibuni msomi nguli ataitwa katika Bunge Maalumu.

Kwa ufupi, unapokuwa na dola mbili au nchi mbili kama ambavyo msomi nguli anasema, kwa lugha ya unyenyekevu, huwa ndiyo Muundo wa Mkataba rasmi. Lakini tukirudi katika muundo wa Bunge ni dhambi kuwapa Watanganyika au Watanzania Bara chombo cha kutunga sheria kwa mambo ya Tanganyika, bila kuwapa Serikali ambayo chombo hicho kitakuwa kinaisimamia.

Kitendo chochote cha kuipa Zanzibar mamlaka zaidi kwa mambo yake yasiyo ya Muungano, kinachukuliwa kama kitendo cha hila kwa huyu Tanganyika, ambaye anasemekana haonekani. Ile dhana ya Tanganyika kuvaa koti la Muungano ndiyo hasa kwa kutumia muundo wa msomi nguli inakaa sawasawa. Sina hakika kama msomi nguli alikuwa anatafiti mawazo yake au haya ndiyo hasa yake ya moyoni.

Imeandaliwa na Humphrey Polepole.
Chanzo: Mwananchi Newspaper.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments