Kote Duniani na hasa katika nchi zenye ustaarabu wa kuheshimu sheria,haki za binaadam,mila,silka,utamaduni wa
makabila/mataifa au taratibu za uandikishaji wa vyama vya siasa,haki za kuchagua na kuchaguliwa katika daraja
mbali-mbali za uongozi na hata taratibu za ufungaji na kuvunja ndoa .
Sheria za Ndoa na za Uandikishaji wa vyama vya siasa zipo nchini kote tokea Chanja-Njawiri,ya Zanzibar hadi kufikia
Matombo ya Tanganyika.Kwa kifupi sheria zipo katika kila pembe ya eneo lote la Tanzania .
Kwa upande wa barugumu za Itikadi,kwa kweli Watanzania wamefaidika kwa mazuri na baadhi ya mabaya ya hapa na pale
tokea kuanza wakati wa mfumo wa chama kimoja na hata huu mfumo wa vyama vingi na soko-huru la kumalizana .
Matajiri wamezidi utajiri na masikini wamezidi kubaki kwenye uduni wa walalahoi .Ufisadi na ujangiri umetia mizizi.
Ukosefu mambo ya nidhamu,uadilifu,uwajibikaji,miiko ya kulinda ethics na morals za taifa zimetetereka na hata kanuni za uwanachama au hata kufukuzana vyamani zimejaa telele kwa whims za viongozi wa vyote nchini.
Tatizo kubwa la kitaifa ni kujiuiza ; nini cha kufanya na jee sheria ,taratibu na kanuni za nchi zinafuatwa na kuheshimiwa ?
Niliyoyashuhudia baada Safari yangu ndogo hivi karibuni nchini Tanzania .
Siku chache zilizopita nilitembelea Bongo.Kimitaani huku niishio, sisi huiita Tanzania = Bongo. Sio Bingo !!
Ingekua Bingo , kwa kweli tungelikua tumepiga hatua ya mbali kimaendeleo.Hata hivyo ninaweza kwa shingo upande
nnaweza kusema tunshukuru kwa kiasi kwa kiasi cha hapa tulipofikia tukilinganisha na nchi za jirani .
Vituko,ukatili na Uimla uliopo Rwanda au hali ya kisiasa Zaire,Uganda,Sudan Kusini zinasikitisha .Tuombe M/Mungu nchi
yyetu isifikwe yaliyo wafika ndugu zetu wengine katika Afrika.
Kilicho nipeleka huko Bongo hasa ilikuwa ni kumtembelea Shangazi na Mjomba.Watu hawa wawili siku nyingi
nilikuwa sijawaona wala kuwasikia.Nilikuwa na hamu sana ya kuwaona,lakini sikutaka kuwaarifu mjoo wala siku ya mimi
kuwasili nchini. Nilitaka kuwapa "saplaiz" , lakini bila ya kujuwa kwamba kumbe ni mimi ndie nitakaye pigwa lile bonge la
"supa-saplaiz " ya jinsi mambo yalivyo kwa upande wa ndoa ya shangazi na ile hali halisi ya mambo ya vyama vya kisiasa
hasa kwa upande wa mjomba ambae ni shabiki sana na mambo kisiasa za upinzani nchini .
Nilifika Dsm usiku sana - nikaamua kuchukua Taxi moja kwa moja kwa shangazi.Kwa kweli nilipowasili nyumbani mimi
nilishanga jinsi nyumba ilivyojadidishwa ,milango na madirisha ilivyo jaa mavuma kama watu wamejitia kwenye jela "kwa hiari".
Lakini kumbe ile si kwa hiari yao,bali ni " ...khofu na hatari za ujangiri na majambazi walivyo tawala " Shangazi alinihakikishia .
Baada ya kusalimiana kwa vuzuri ,Shangazi kama kawaida yake akaingiya jikoni akanipashia moto chakula .
Ulikua ni mchuzi wa pweza wa nazi na wali wa nazi . Kwa vile Shangazi ,alikuwa anajuwa pendo langu la chakula hicho;
akaniambia " ... unaona mambo ya M/mungu hayo ,hujataka kunijulisha kama unakuja ,lakini mambo ya Mungu makubwa leo
hii wakati napika chakula hiki nilikuwa nakukumbuka na hii yote ni jinsi unavyokipenda chakula hiki tokea utotoni".
Nikamuambia Shangazi ,"..aloo wewe sasa nenda ukalale,usianze maneno yako ;wacha nimchape huyu pweza na wali wangu tuonane asubuhi. Akacheka kidogo akaenda zake kulala kwa tanganyika wa husema "..kaenda kurara "!!
Siku ya pili asubuhi tulipoamka nikaashitukia na meza iliyo jaa machopicho ya aina tofauti; chapati ,tambi ,samaki wa kukaanga,nyama ,mchuzi ,mbaazi za nazi ya kukata na shoka - almuradi shughuli kamili. Mimi nikasema mnaona :
"Mmambo haya makubwa ;sija kuageni kwamba nnakuja mambo ni kama hivi ; jee ninge kuarifuni kwamba nnakuja basi
mge- pasuwa watu matumbo na kutuvimbisha mashavu kwa sababu ya shida ya mitafuno ya machopicho kama haya.
Kibogoyo kama mimi si ange-n`golewa meno ".Mmoja kati ya watoto wa pale nyumbani na uchepe wake akarupukwa na
maneno na kusema "... babu mbona unasema wewe kibogoyo na meno hayo unayo ?"
Nikamuambia haya mengi ni ya Tembo. Bibi yake akamkemea "...wee Msankule acha jeuri kula wende zako shule,uchepe
wako kama nduguyo Sindano ".Kwa upande wangu mimi maneno ya kijana huyo niliyaona kama ni kawaida tu.
Wakati tunaanza kula naona mwenye nyumba hayuko mezani na kwa ushawishi wangu nikauliza " Je vipi Mze ameshaenda
kazini ?" Shangazi akafanya kama hakunisikia ,akawa anawaambia watoto wafanye haraka wendezao skuli na wengine
wadogo wende chuoni ,na huku akinikonyeza kunipa alama kwama nisiyaulize hayo ya baba watoto ,wakati watoto wapo
hapo ukumbini .Hapo hapo nikaelewaa kwamba kumbee........!!!!
Baada ya watoto kuondoka Shangazi ,akaaza kunieleza ya ndani baina yake na mumewe ."Mambo hapa nyumbani kwa
kweli si mazuri.Baba wa hapa nyumbani ana mambo mambo ambayo hayalingani na ule ujasiri wake wa kuubiri vitu na
mambo ya ustaarabu,lakini heshima na haki zangu za hapa nyumbani sizipati.
Kwa kweli leo ni kama siku ya 4 haonekani na mara nyingi huwa halali hapawala hatupitii kutujuwa hali .
Yupo kama hayupo.Yye ana lala-lala huko mitaani na wasichana wa huku na kule bila ya aibu .
Ninapo teta kwa mambo hayo huwa ananipigiya makelele na kunishangaza-shangaza kwamba atanipa talaka.
Makelele ya sijui nini na nini;almuradi mwanangu mambo ni mengi ,lakini sijachanganyikiwa na namshukuru mola wangu
kila wakati na kila dakika ".
Mimi nikamfanyia utani Shangazi , " ... sasa wewe wivu wivu huu wa nini na uzee huo ,watoto alhamdulahi unao ,nyumba
nzuri unayo, fedha zako za ustaafu unapata,watoto wakubwa wanakuangalia,sasa akilala asilale hapa; aibu ni yake usoni
mwa wanawe na majirani ?.
Shukuru Mungu umekuwa mchamungu na mtakatifu na wewe una pande la sijida hilo hata risasi haiwezi kupita.
Haki gani tena za unyumba unazozitaka ;huko kuliko halalishwa kindowa kote kwa umri wako huo basi hata shindano haiwezi
kupita.Si umuache tu huyo mumeo ajitafutiye "Vispringi Chikini anyoshe viungo ".
Shangazi akaniambia " Sasa ndugu yangu unaanza uchepe na mambo yako (na huku akicheka ),tatizo hapa sio kuwa na wivu
au kutokuwa na wivu na huyu mume wangu na nikiwa nawivu ni haki yangu au vipi?
Lakini khasa tatizo la msingi hapa ni suala la heshima yake ,utu na mila zetu,dini yetu na utamaduni wa silka zetu.
Kwa wewe unaeishi Ulaya pengine umeyasahau mambo haya au unanifanyika zihaka na uchepe chepe wako .
Walahi,bilahi talaahi kwa upande wangu mimi
hata siku moja sitapinga kwa hali yeyote ikiwa atafunga ndowa ya pili au hata ya tatu ila tu bora aachane na huu umalaya wake
wa kurukia vitoto vidogo-vidogo vya huku na kule .
Si unaujuwa ule ugonjwa uliojaa nchini na mahala ulipo? Hata yule Mzee "Rukhsa" rais wa zamani alisema kua
".. ugonjwa huu upo mahala pabaya,unawanasa wengi ".
Kwa upande wangu nataka tu ahalalishe vitendo vyake kwa ndoa ili ajikinge kwa mambo ya Dini na ya Dunia .
Na aowe hata ikiwa wake watatu ili tuwe 4 ;bora tu tusipatwe na aibu na yeye asiwe anasimangwa simagwa vichochoroni humo .
Kinyume ya hivyo ni aibu si kwake tu bali ni kwetu sote au vipi ?
Mimi nikamuambia kiutani kwa mara nyingine "-- hivi kweli Shangazi , hii ya hata muwe wake 4 , unasema kidhati ,mzaha au ndio
ile isemwayo eti.:" Utamu wa Mume , Raha yake Muwe Wane ?.
Shangazi akabwaga kicheko mpaka akawa anatokwa machozi na huku akisema ".... weee ...weee ... kumbe ...kichekoo !!!
weee ndugu yangu...kichekoo ... weeee ..mwanangu achana na mambo ya kunichekesha na kunipasuwa mapafu hapa .
Mimi nakuambia mambo ya nyumbani ,very serious ; wewe unakuja na mambo ya hizo nanihino za za muwe eti ni wa wake
4 na eti ndiyo raha ya mume .
" Raha gani ?? ".Kwani hata yeye huyo atawaweza kweli awe na wake 4 ,si anatafuta ajali ,ajifiye atubakishe duniani vizuka .
(Nikamchokoza tena " sasa hii ya kuniita "ndugu yangu " badala ya mwanangu kama kawaida unataka kujifanya mjanjaa ?")
Tukacheka weee yakaisha na akaniuliza fikira yangu kwa yale aliyoyasema kuhusu mumewe .
Mimi nikamuambia Shangazi, "... niwajuavyo hawa wanasiasa ;sio kwamba wanawaoa hawa dada zetu na mama zetu
kwa sababu ya kukutaabisheni,ikiwa wapo wanaofanya hivyo ,basi si wengi kama hivyo.Wanakuoweni kwa mapenzi.
Lakini wengi wa hawa wanasiasa ,wakati mwengine hua wanaolewa au wanaowana na vyama vyao vya kisiasa
kiasi ya kwamba hua hawana nafasi za kuwepo majumbani mwao kwa muda mwingi- ndoa zao hua shaghla baghla.
Sakata kama hizo zilinikuta hata mimi huko niishio hata ikahatarisha ndoa yangu.
Kwani hujamsikia yule Mpemba aliposema kuwa yeye aameolewa na siasa ?
Michakato ya jadili za Itikadi na shughuli zao mbali za mchana na usiku pamoja na ushabiki wa vyama vyao inakuwa kama
kumiliki au kumilikiwa na chama. Jinsi wafikiriavyo na kuamini kuwa ni sawa kama vile wanavyo wamiliki wake zao .
Wanafanya kama watakavyo ama kusudi au bila ya wao kutambua kwamba wanafanya kosa na makosa ya hapa na pale .
Kwani hujasikia yaliyo tokea CCM, CUF na haya yanayo endelea kwenye Chadema kuhusu yule kijana mshupavu wa siasa
kali za kulaaani ufisadi wa mali za taifa;ukwepaji wa malipo ya kodi ,uhamishwaji wa fedha za kigeni kwenda Uswisi,
kuharamisha posho za vikao bungeni,na hata yeye kudai pawepo uchunguzi wa kiserikali jinsi ya mahesabu na matumizi
ya fedha za wananchi?.
Shangazi akanijibu "Huyo kijana Zitto, kwa kweli ni jasiri ; anayoyasema mengi au yote ni ya ukweli usiopingika.Tatizo
ni kwamba ,anapodai mambo ya " uwajibiakaji na kuhojiwa viongozi kuhusu mambo ya uadilifu,nidhamu na utawala
bora inakuwa anajitia katika ajali za bure. Si umesikia yaliyo mfika amefukuzwa chamani.
Yeye na wenzake wanapachikwa majiana majiana mabaya kwamba wao ni wasaliti na ni wahaini.
Sisi akina mama zenu tukiteta kwa mabaya madogo na makubwa ya majumbani mwetu ,tunatishiwa vivyo hivo na hata
tunapewa talaka za kijinga jinga .Tukiteta waume zetu wanatuambia "..ama tu-zip-up au talaka ".
Wanatutishia hivyo kwa sababu vichwani mwao wanatufanya sisi kama vibuzi na ni milki zao".
Na hawa waasisi au viongozi wa vyama vya siasa nchini mtindo ndio huo huo " Ama uufwate,kama mbwa ; kama huufwati
basi watasema wewe "..uko dhidi ya chama na ni msaliti na haini aliyetumba mpaka .
Baadhi ya hawa viongozi hujifkiria kua "Wao ni chama,na chama ni wao ,wanajimilikisha Binafsi ".
Dola wanaifanya ni yao; na Dola ni wao "The state is me ,and I am the State - attitudes ".
Vivyo hivyo ndivyo wafanyavyo katika kujinasibisha na kumiliki vyama vyao vya kisiasa na kuamrisha nani wa kuchaguliwa
katika vyeo vya uongozi -kama ilivyo fanyika katika Mkutano Mkuu wa CUF -wa hivi majuzi .
Shangazi alikuwa mkali .
Mimi nikaongezea kwa kusema kwa hivyo :
Wakati umefika wa baadhi ya Wazee wetu hawa kuelewa kwamba dada na mama zetu "..si milki-zao-binfasi ";
bali wameingia ndoani kisheria na kidini ; na viongozi wa kisiasa wanapaswa kutambua kwamba demokrasia ni changamoto
tu ya taratibu za siasa za uwazi ,uhuru wa kufikiri na kujitamka ,kukosowa na kukosowana kwa shabaha za kurekibishana na kushindana katika ukuuzi na uendelezaji wa maendeleo katika taifa.Haya si mashinadano ya kunganganiya madaraka kwa
malengo ya ubinafsiya wa kupata au kuteka vyeo vya juu.
Uongozi ni dhamana sio Urithi wa shamba au Mali za Bibi , au Uchifu na Usultani .
Wakati nataka kuondoka kidogo Shangazi , nae akaleta uchokozi mwingine mpya kwa kuniuliza ",, Hivi kweli lile Azimio la
Arusha liko wapi ?.
Mimi nikamuambia "..... Shangazi hivi wewe kweli hujuwi kwamba Mwalimu alitangulia na original ya hcho kitu huko aliko
kwenda kwa sababu hakuwa na wa kumuamini huku duniani. Ila tu alichofanyana aliwaachilia kopi nyingi kwa wote.
Lakini ,inavyoonekana hata hizo kopi pengine zote zime fichwa fichwa na nyingine kuliwa na mapanya tokeya awamu ya
pili hadi hii leo ? Kule Zanzibar ,baada ya mapanya kuzila zile koipi za Azimio la Arusha ,wakanenepa wakageuka Mabuku
wakubwa wakubwa .Na nilipo wapigia simu wa Kijiweni kuwauliza kama wanazo kopi za Azimio ,mmoja wapo wa manguli
wa Front-Liners ambao ndio walio msaliti Jumbe kule Dodoma walinijibu kwamba "....lile Azimio la Arusha mwishowe chumbe".
Nikawauliza kina Ngombale na Jenerali Ulimwengu ikiwa wao hilo Azimio wanalo wakanijibu kipamoja " Hii ni herizi,inayo
tukinga na haya yanayotokea nchini ". Kwani huoni ,husikii au huyajui au hata huwaoni wale wote wanaozungumzia yale
yale ya 1967 ,yaliyomo kwenye hicho kitu ,bila ya hata ya kukitaka kijitabu hicho cha Azimio la Arusha na miiko yake ya
Uongozi ,hatari za ujipatiaji wa utajiri wa haraka haraka na silka za kusema uwongo - wanao taja mambo hayo hitimaye
unawakuta ama wamhutumiwa kesi za "Uhaini ,Usaliti na kutimuliwa kwenye vyama?
Ikiwa si hivyo, basi mara tu utasikia kua eti watu hao wameuliwa na majambazi?
Azimio la Arusha Oyeee !!!
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments