FIKIRIA wasomi wote wenye asili ya Mkoa wa Kagera unaowafahamu, waliopo na waliokwisha kutangulia mbele ya haki, wengi wao watakuwa wamesomeshwa na kahawa.
Huwezi kuzungumzia maendeleo yoyote ya kiuchumi na ya kijamii yaliyowahi kupatikana katika Mkoa wa Kagera bila kutaja kahawa. Umaarufu wa maendeleo ya Ushirika katika Mkoa wa Kagera tangu zama za ukoloni ulitokana na kahawa na hasa Mfuko wa Kahawa ambao ndio uliowasomesha wasomi wengi wa Kagera.
Kwa hiyo matukio yoyote yanayoathiri uzalishaji wa kahawa mkoani Kagera ni ya kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi wanaotegemea zao hili. Kadhalika, hatua zozote zinazoweza kuchukuliwa ili kuwezesha kufufua na kuongeza uzalishaji wa kahawa mkoani ni hatua za kuwakomboa wananchi wa mkoa huu. Kwa kufanya hivyo, uchumi wa wananchi utaimarika na kwa hiyo kuwawezesha kuingia katika awamu ya pili ya maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii.
Ukiweka hayo kando, leo baada ya mafanikio yote hayo ya kahawa, kuanzia wakati wa ukoloni na baadaye katika miaka kama 20 baada ya uhuru, zao hilo si maarufu tena, kati ya mambo mengi, wakulima wanalalamikia bei ndogo, na wapatapo nafasi huuza kwa magendo nchi jirani ambako bei ni nzuri.
Raia Mwema imezungmza na wadau mbalimbali wa kahawa juu ya matatizo yaliyoikumba na ambayo yanaendelea kuikumba, akiwamo Askofu Dk. Benson Bagonza, mzaliwa wa Mkoa wa Kagera na sasa Askofu wa Jimbo la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Karagwe.
Anasema Askofu Dk. Bagonza kuhusu kahawa: "Mkoa wa Kagera una bahati moja kubwa ambayo baadaye hugeuka kuwa balaa la mkoa huo. Mkoa huo una zao la kudumu la biashara na zao la kudumu la chakula.
"Kahawa ni zao la biashara na ndizi ni zao la chakula. Mazao yote mawili kwa vile ni ya kudumu, yanaweza kuendelea kutoa matunda hata kama mkulima hayatunzi vizuri. Kwa hiyo, mkulima wa kahawa na migomba ana uhakika fulani wa kipato bila kutegemea ubora wa zao lenyewe, na hii huua kabisa ubunifu na kuchochea uvivu katika jamii."
Anaongeza: " Kahawa katika Mkoa wa Kagera imekuwa na baraka nyingi lakini pia kahawa imeleta balaa za kutosha. Kabla na miongo miwili baada ya uhuru, zao la kahawa mkoani lilikuwa ni msingi wa kila kitu. Lilisimika mfumo wa kijamii na kuathiri kwa namna nzuri nyanja za elimu, siasa, utamaduni, dini na uchumi.
" Kielimu zao la kahawa lilikuwa na mfuko maalumu wa kusomesha watoto wote wa Mkoa wa Kagera, kuanzia shule za kati mpaka vyuo vikuu. Chama cha Ushirika cha Kahawa kilianzisha na kuendesha shule za mwanzo za sekondari na watoto wote wa wakulima wa kahawa walipata ama punguzo maalumu katika karo au walisoma bure.
" Si jambo la kutia chumvi, nikisema wasomi wa kwanza wa Mkoa wa Kagera ama walisomeshwa na mfuko wa elimu wa zao la kahawa, au wazazi wao waliwasomesha kutokana na fedha zilizotokana na zao la kahawa.
" Kisiasa, zao la kahawa ndilo lililokuwa agenda kuu ya wanasiasa wa Mkoa wa Kagera. Mwanasiasa alihukumiwa na kupimwa uwezo wake kutokana na maono yake katika kuendeleza kahawa. Kwa hiyo, haishangazi sana kuona kuwa viongozi wengi wa kijamii wa wakati ule walikuwa ama ni wale waliokuwa na mashamba mazuri ya kahawa au waliozaliwa na kukulia katika mashamba yale na kwa hiyo walikuwa na uwezo wa kueleza shida na baraka wazipatazo wakulima wa kahawa.
" Kiutamaduni, kahawa ni zao pekee lililokuwa na hadhi ya kutumika kama alama ya urafiki na hata kuunganisha koo mbili zilizoamua kuungana na kuwa na uhusiano wa damu. Kwa hiyo, mpaka leo ukiingia nyumba ya Mhaya ukakosa kupewa kahawa, ujue hutakiwi katika nyumba hiyo, au utandawazi umemomonyoa mila katika nyumba hiyo. Kahawa ni alama ya utu, urafiki, undugu na uzawa. Wazazi huwarithisha watoto wao miti ya kahawa na mche wa kahawa ni alama ya rutuba (fertility) katika uzazi.
" Kiuchumi, zao hili ndilo lililotawala medani hii. Ukubwa wa shamba la kahawa na ubora wake viliamua nani zaidi kati ya wawili washindanao. Na kwa sababu zao hili lilikuwa na uzalishaji na mapato karibu mwaka mzima, lilibadili hali za watu katika familia mwaka hata mwaka.
" Mathalani, baada ya mauzo halisi, bado mkulima alitarajia malipo ya nyuma (amalipo), yaani tofauti ya bei kati ya soko la hapa nchini na soko la dunia. Baadaye wakulima walilipwa fedha maalumu kulingana na idadi ya miche ya kahawa aliyokuwa nayo mkulima. Kutokana na hali ya hewa nzuri, mibuni ilikuwa inapamba tena matunda ya kahawa lakini yasiyokuwa rasmi (enjagashe), hii ilivunwa na kupikwa kwa ajili ya kutafuna. Hiki nacho kikawa chanzo maalumu cha mapato katika familia.
" Kwa hiyo mzunguko wa fedha katika familia ulikuwapo karibu mwaka mzima, kahawa ikawa ni chanzo cha ustawi kiuchumi katika familia nyingi. Kwa baadhi kahawa ikawa ni "sarafu-mbadala" katika mbadilishano na mauziano. Mathalani, mkulima angekwenda sokoni akanunua nyama kwa kubadilishana na kahawa. Mlevi angekwenda baa na kununua pombe kwa kutumia kahawa. Mfanyabiashara wa pombe ya kienyeji angeweza kuuza "rubisi" kwa kulipwa kahawa.
" Kahawa ilikuwa ni dhamana yenye thamani sawa na fedha au dhahabu katika mabenki. Mpaka miaka ya mwanzo ya 1980, hapakuwa na uhakika wa nani zaidi kati ya msomi mwenye kalamu na mkulima mwenye kahawa.''
Lakini ni nini kimetokea mpaka kahawa imeshuka hivyo ilivyoshuka na pamoja nayo Mkoa wote wa Kagera?
Anajibu Askofu Dk. Bagonza: " Majibu yako mengi, na wanasiasa ni mafundi wa kueleza ni nini kilitokea lakini bila kukidhi kiu ya wengi. Kudorora na hatimaye kuanguka kwa hadhi ya zao la kahawa mkoani Kagera kumechangiwa na sababu nyingi, lakini zilizo wazi na kuu ni mbili.
" Ya kwanza, ni kuibuka na hatimaye kukubalika kwa ufisadi kama njia ya kuongoza vyombo vya kiuchumi nchini. Kwa miaka mingi, watumishi wa vyama vya msingi vya kahawa mkoani Kagera walifanya kazi kwa kuaminiwa na wakulima wenyewe, na sifa njema katika jamii ilikuwa ni msingi mkuu wa mtu kuajiriwa katika chama cha msingi cha kahawa. Polepole utaratibu huu ulibadilika na ujanja ujanja ukawa sifa ya muhimu, ukawafanya makarani wa kahawa wabadhirifu na wezi wakubwa wa jasho la wakulima.
" Hata hivi leo ukitembea vijijini unaweza kuona tofauti ya maisha kati ya makarani hao na wakulima wa kahawa. Makarani wengi na wajumbe wa halmashauri zao wanaishi katika ukwasi mkubwa wa mali wakati wazalishaji wanaishi katika umasikini mkubwa. Hali hiyo inaonekana pia katika ngazi ya chama cha ushirika ambako watendaji wanaogelea katika utajiri usioelezeka huku wakulima wa kahawa wakiwa hawawezi kununua hata chupa moja ya maji kwa kutumia kilo moja ya kahawa.
" Hali hii haiwezi kujibiwa na maelezo ya wanasiasa kuwa bei ya kahawa imeshuka katika soko la dunia au kuwa ubora wa kahawa ya wana Kagera ni wa chini. Mbona makarani na watendaji wanatajirika kwa kutumia hiyo kahawa mbovu na bei hiyo hiyo duni ya soko la dunia? Kwa msingi huu, rushwa iliyozaa ufisadi ni chimbuko la kahawa ya Kagera iliyokuwa baraka ya mkoa huo, kugeuka kuwa balaa na laana kwa wana Kagera.
" Sababu ya pili ni wanasiasa kugeuka wafanyabiashara ya kahawa. "Enzi ya Mwalimu" wanasiasa wa Kagera walichaguliwa kutokana na msimamo wao katika kutetea bei nzuri ya zao la kahawa. Hivi sasa wanasiasa wanachaguliwa kwa kuangalia utajiri wao walioupata kwa kufanya biashara ya kahawa au kwa kuwalinda walanguzi na makuadi wa zao la kahawa. Wanasiasa wa sasa mkoani Kagera hawawezi kusimama na kutetea bei nzuri ya kahawa kwa sababu wao ndio walanguzi na wanunuzi wa zao hilo katika utaratibu wa sasa wa soko huria linaloangaliwa na walio wengi kuwa ni "soko holela".
Mmoja wa wanunuzi binafsi wilayani Karagwe, aliyezungumza na Raia Mwema kwa masharti ya kutotajwa jina, anasema pamoja na mambo mengine, kwamba ni vyema yanayoendelea sasa katika kilimo cha kahawa cha Kagera yaanikwe hadharani.
" Nakushukuru sana kwa Raia Mwema kutenga muda wa kuandika juu ya kahawa. Enzi za KDCU (Karagwe Development Co-operative Union) kununua kahawa peke yake kulikuwa na kero nyingi ambazo nyingine mpaka leo hazikupatiwa ufumbuzi.
" Kero hizo ni pamoja na chache ninazoweza kutaja; hakukuwa na uwazi, wakulima walikuwa hawapati pesa zao kwa wakati, viongozi wa KDCU walikuwa wanatumia pesa ya chama/wakulima wanavyotaka, karani wa vyama vya msingi walikuwa miungu wadogo, na mengine mengi.
" Kwa kuruhusu wanunuzi binafsi, kuna faida nyingi kama ifuatavyo; wanunuzi binafsi wote wanalipa wakulima bei ya juu kuliko KDCU na kwa wakati kuliko KDCU. Hawana ukiritimba, vituo vyao vya ununuzi viko karibu na wananchi, mfumo wao wa ununuzi ni wa moja kwa moja. Watu wanafurahia sana mfumo wa biashara huria kuliko mfumo uliokuwapo zamani kwa sababu kama hizi nilizoeleza na nyingine nyingi." Anaongeza mnunuzi huyo binafsi: " Maoni ya wanunuzi binafsi ni mengi. Wengi wao sasa wanapanga kupanua wigo wao kufanya biashara na wakulima kwa sababu, pamoja na kununua kwa bei iliyojuu ya ile ya KDCU, bado wanapata faida kubwa. Wanyambo wanafurahi kuwa na wanunuzi binafsi kwa sababu wanaweza kulinganisha kati ya mnunuzi na mnunuzi na pia inawasaidia kujiuliza maswali mengi kama kwa nini bei zinatofautiana kati ya mnunuzi na mnunuzi!
" Wengine sasa wanaendelea kutafiti na kuanza kufikiria namna ya wao kujiunga katika makundi na kuanza kuuza kahawa yao aidha nje ya nchi au kwenye mnada bila kupitia makampuni binafsi na hata KADCU, maana wamekwisha kujua kuwa sheria inawapa kipaumbele cha kuuza kahawa yao kwa utaratibu huo. Mfano mzuri ni Chama cha msingi cha Nkwenda kuamua kujitoa KDCU na kuuza kahawa yao moja kwa moja kuanzia msimu huu. Kuhusu kupanda na kushuka kwa kahawa Mkoa wa Kagera, ni kweli bei huwa zinapanda na kushuka, lakini kikubwa ni kwamba mfumo tuliokuwa nao hasa hasa kwa mkoa wetu ni kufanya biashara "as usual" (kwa mazoea). Kahawa ilivyokuwa inauzwa tangu miaka ya mababu zetu ndiyo hivyo inauzwa mpaka sasa (isiyosafishwa).
" Kuhusu Mfuko wa Elimu uliokuwa unatokana na mauzo ya kahawa umeharibika hasa kutokana na kuingia kwa siasa. Kwa Karagwe hiyo ilitokana na Serikali kuamua kuanzisha Mfuko wa Elimu Karagwe (KDEF). Fedha yote ikawa inakusanywa na kupelekwa KDEF ambayo kimsingi sasa wanasiasa wameifuta na kuifanya mfuko wa elimu chini ya halmashauri hatua ambayo kila mmoja wetu anasubiri kuona nini kitakachoendelea.
" Pamoja na Serikali kuwa na utaratibu wa kutoza kwenye kahawa, nadhani isingelizua vyama vya ushirika kuendeleza mfuko wao. Lakini kwa kuwa mfumo wa uongozi na utendaji katika sehemu nyingi umebadilika kutoka kuwa kwa ajili ya Mungu na nchi yetu kwenda kuwa kwa Mungu na matumbo/familia zetu, ndiyo maana hatuoni yale matunda ya BCU tunayoyasoma kwenye vitabu.
" Na kosa kubwa kuliko yote ni pale BCU ilipofutwa na kuwa WERECU mwaka 1974 na baadaye kuwa CAT. Walioingia baada ya hatua hizo wakaja na falsafa ya Mungu na matumbo yao."
Mnunuzi mwingine, Zimbehya Kachebonaho, anasema biashara yao inakwenda vizuri na kwa kuzingatia hilo yeye na kundi lake la KPD (Kaderes Peasants Development Ltd.), wanakusudia kuanzisha akaunti ya masomo kutokana na mazao wanayokusanya kutoka kwa wakulima hasa wanachama wa vikundi vya kuweka na kukopa (saccos).
Anasema Kachebonaho: " Tunataraji mfuko huo utawasaidia wakulima kuweza kusomesha watoto wao zaidi hata ilivyokuwa BCU kwa wakati ujao. Fikra zetu ni kwamba mfuko huo ujengwe kwa asilimia 10 ya faida itakayokuwa inapatikana."
Lakini zaidi ya kusaidia kuamsha tena mpango wa kusomesha na kuvisaidia vyama vya wakulima vya kuweka na kukopa, KPD ina mawazo gani zaidi hasa kuhusu uuzaji wa kahawa kwa magendo nchi jirani?
Anaeleza Kachebonaho: " Kuna mambo muhimu ya kuanzia, haya ni pamoja na ushirikiano wa pande zote tatu katika kuhakikisha kahawa yote (ya Karagwe) inakusanywa na kununuliwa na kampuni binafsi na vyama vya ushirika. Pande hizi ni Serikali, wanunuzi wa kahawa na benki.
" Utafiti tuliofanya unaonyesha kuwa makampuni na vyama vya ushirika vinakuwa na malengo maalumu ya kununua kahawa, hivyo huomba mkopo kutoka benki kulingana na uwezo walionao. Mara nyingi kampuni na vyama hivyo huwa vinapunguza kasi ya kununua kahawa kabla ya Novemba na Desemba kila mwaka.
" Pamoja na kwamba wakati wa ununuzi wa kawaida kati ya Julai na Desemba uvushaji wa kahawa kwa njia ya magendo hufanyika kwa kiwango cha chini, tofauti inakuwapo ukilinganisha na kipindi cha Desemba na Juni mwaka unaofuata. Kipindi cha Desemba makampuni yaliyo mengi yanaacha kununua kahawa, aidha kwa kufikia malengo yao kwa msimu huo, au kwa kuishiwa fedha walizokopa kutoka benki. Wakulima hubaki na kahawa nyingi bila kuuzwa.
" Ni wakati huo kampuni na vyama vya ushirika huwa pia na kahawa iliyojaa katika maghala ambayo inakuwa haikuuzwa na hiyo huzifanya zisiwe na fedha ya kununua mzigo mwingine. Ununuzi unaposimama ndipo wananchi wanapotafuta masoko mengine na hivyo huangukia kwenye mikono ya walanguzi wanaovusha kahawa nje ya nchi."
Kwa mujibu wa Kachebonaho suluhisho la hali hii ni mikutano ya pamoja kati ya wataalamu wa Serikali na wanunuzi wa kahawa.
Anasema katika mikutano hiyo wanunuzi na Serikali wajipange kununua kahawa kulingana na uzalishaji, si uwezo wa wanunuzi husika. Hiyo itawawezesha wanunuzi kuendelea na ununuzi kwa msimu mzima au mpaka kahawa itakapokuwa imekwisha kwa wakulima, kwa kuwa watakuwa na mikopo yenye dhamana ya Serikali katika benki. Hiyo itapunguza sana mianya ya wafanya magendo kuendelea kununua kahawa kwa uhuru na kwa jinsi wanavyotaka.
Anashauri pia Serikali ianzishe ghala maalumu la kuhifadhi kahawa wakati na kabla ya kahawa kuuzwa au inaposhuka bei, ili kusubiri bei itakapopanda tena. Anasema kama hilo linakuwa haliwezekani ndani ya muda mfupi, basi Serikali ifanye mpango wa kusafirisha na kuhifadhi kahawa kwenye maghala mahali pengine ndani ya nchi kama zinavyofanya nchi nyingine.
Anapendekeza pia kwamba Serikali kwa kushirikiana na wakulima waboreshe mfumo wa uzalishaji na soko. Mfumo unaopendekezwa ni wa kuwaelimisha wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika vya msingi, vikundi vya wakulima wadogo wadogo kujisajiri na soko la Fair Trade kupitia mtandao wa FLO – CERT ili kuwawezesha wakulima kupata bei nzuri ya mazao yao hata pale mazao hayo yanaposhuka bei.
Anasema mpango huo unawezesha wakulima kupata fidia ya bei kutoka kwa makampuni ya ununuzi hivyo kuwafanya kuwa wajasiriamali zaidi na kuipunguzia Serikali mzigo wa kufidia hasara zinazotokana na mazao kama pamba na kahawa.
Anasema mpango huo ukipita, ukafanyiwa kazi vizuri, utanufaisha sehemu tatu muhimu: Wakulima kupata bei nzuri, Serikali za Mitaa kupata ushuru mzuri wa mazao na Serikali Kuu kupata pesa za kigeni na kuepukana na fidia ya mara kwa mara isiyokuwa ya lazima.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/kahawa-baraka-na-balaa-la-kagera?fb_action_ids=577830972327742&fb_action_types=og.likes#sthash.aP8EKyiD.dpufSend Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments