[wanabidii] JUMUIYA ya Kikristo Tanzania (CCT) yamkosoa Kikwete

Tuesday, July 15, 2014
JUMUIYA ya Kikristo Tanzania (CCT) imesema hotuba iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete, wakati wa uzinduzi wa Bunge Maalum la Katiba, ilionesha hali ya kutoafiki baadhi ya ibara au vifungu vilivyowasilishwa na Tume, kutokana na maono ya Watanzania kama ilivyoandikwa katika Rasimu ya Pili.


Tamko lililotolewa na CCT kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, lilieleza kwamba hotuba hiyo ilishusha hadhi ya kazi nzuri iliyofanywa na wajumbe wa Tume ya kukusanya maoni ya wananchi ambapo yeye mwenyewe aliwateua na kuwaapisha. Katika tamko lao la pamoja lililotokana na Mapatano ya Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 48 ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania iliyokutana mkoani Dodoma kati ya Julai 2 hadi 3, mwaka huu, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania waliafikiana kwamba;
"Hotuba ya kufungua Bunge hilo iliyotolewa na Rais ilionesha hali ya kutokuafiki baadhi ya Ibara au vifungu vilivyowasilishwa na Tume kutokana na maoni ya Watanzania kama yalivyoandikwa katika Rasimu ya Pili.


Jambo hili linaweza kufananishwa na mama anayeamua kubeba mimba, kuilea mimba hiyo kwa gharama na kujifungua kwa uchungu halafu mtoto akishazaliwa badala ya kufurahi na kushangilia anaamua mwenyewe kumbeza na kumtelekeza mtoto huy o."
Kutokana na hali hiyo CCT ilitoa tamko la kuwapa pole na kuwapongeza wajumbe wa Tume ya kukusanya maoni ya wananchi na inatambua kwamba walikuwa waaminifu kwa aliyewateua na kwa wananchi wa Tanzania bila kujali itikadi zao za kisiasa au kiimani.
"Tunawaomba wajumbe wote wa Tume hii wasijisikie vibaya kwa kile kilichotokea, kwani kazi yao imeweka historia hata kama itapata upinzani wa namna gani," lilieleza tamko hilo.


Wajumbe hao wa CCT walisema wanaamini kuwa Tume hiyo ilikuwa aminifu kwa aliyeiapisha, (Rais Kikwete) na hivyo kumshirikisha kila wakati katika kila hatua na katika kila jambo ambalo walihitaji ushauri wake na ya kwamba walifanya kwa pamoja kama walivyokubaliana.
"Tunaamini kuwa kile kilichoandikwa katika Rasimu ya Pili kilikubaliwa na mwenye kutoa hoja (Rais Kikwete) na hivyo aliagiza Rasimu hiyo itolewe kama ilivyo kwani aliamini kuwa hayo ndiyo maamuzi ya wananchi wengi kuhusu Katiba wanayoitarajia.
Pia tunaamini kuwa mwenye kutoa hoja alikuwa na uwezo wa kuzuia rasimu hiyo isitolewe endapo kuna Ibara ambayo inamwelekeo ambao ungekuwa hatari kwa mustakabali wa taifa letu."


Matumizi ya lugha
Katika hatua nyingine, CCT imeshangazwa na lugha za kudhalilisha zisizo za kiungwana zilizotolewa na baadhi ya wabunge wa Bunge Maalum la Katiba kwa wajumbe wa Tume ya Kukusanya maoni.
"Kwa maneno yao wenyewe, wabunge hawa wameonesha kutokumheshimu aliyeiteua Tume hiyo kana kwamba hakufanya vizuri katika uteuzi wake," lilieleza tamko hilo.
CCT imesema ilishangazwa sana jinsi ambavyo chama kimoja kimekuwa kikiwalazimisha hata wabunge wanachama wake kukubaliana na kile baadhi yao wanaona hakifai.


"Tuna waomba viongozi wa vyama vya siasa na Wabunge wa heshimu uhuru wa mawazo ya wanachama wao hata kama watatofautiana katika hoja moja au nyingine na wasitumie nafasi zao kulazimisha wanachama wote kukubaliana na mawazo yao.
Jambo hili linafanya wanachama wengine wasiwe huru na kuwafanya wakubaliane na kilea mbacho hawakipendi mioyoni mwao. Hii ni ishara ya kuwepo Udikteta kwa wananchama wa chama husika. Katika jambo hili, CCT inahimiza wabunge wote waangalie maslahi ya kitaifa kwa upana zaidi na si ya vyama vyao," alieleza taarifa hiyo.
Pia CCT iliwaomba wajumbe wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Wananchi kuwasamehe wale wabunge wote waliowadharau, kuwakejeli na hata kuwatukana.


Msimamo kuhusu rasimu
CCT imetoa tamko zito ikisema Rasimu ya Pili ya Katiba ndiyo mawazo ya Watanzania na kuhimiza wajumbe wote wa Bunge la Katiba waache kujadili maoni ya vyama vyao, bali wajadili na kuheshimu maoni ya Watanzania walio wengi.
"CCT inaendelea kusimamia kuwa muundo wa Muungano uwe wa Serikali moja, lakini pia inaheshimu na kukubaliana na wananchi wengi kuwa muundo wa Muungano uwe wa serikali tatu kama inavyoonekana katika Rasimu ya Pili ya Katiba.


Kwa mantiki hiyo, CCT inatamka kuwa Rasimu ya Pili ya Katiba ndiyo mawazo ya Watanzania," ilieleza CCT katika tamko lake.
Tamko hilo lilifafanua kwamba katika kuchambua maoni hayo, Tume ilijidhihirishia kwamba wananchi wengi wanapenda muundo wa Muungano wa Serikali tatu jambo ambalo Tume imeliwakilisha kama lilivyo katika Rasimu ya Pili inayojadiliwa.
"Katika kuchambua maoni hayo, Tume ilijidhihirishia kwamba Wananchi wengi wanapenda muundo wa Muungano wa Serikali tatu jambo ambalo Tume imeliwakilisha kama lilivyo katika Rasimu ya Pili inayojadiliwa," lilieleza tamko hilo na kuongeza;
"CCT inaendelea kusimamia kuwa muundo wa Muungano uwe wa serikali moja, lakini pia inaheshimu na kukubaliana na wananchi wengi kuwa muundo wa Muungano uwe wa serikali tatu kama inavyoonekana katika Rasimu ya Pili ya Katiba."


Kukosekana uvumilivu
Kuhusu kukosekana kwa uvumilivu wa kisiasa, CCT imewataka waumini wake wa dini na madhehebu mengine ambao ni wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa na wabunge wenye tabia ya kutukanana na kudharauliana waache tabia hiyo mbaya na wajenge utamaduni wa kuvumiliana na kujadiliana kwa hoja kwa kuweka maslahi ya nchi mbele na siya chama cha siasa.
Pia waliiomba serikali itumie vyombo vyake vya usalama wa raia bila upendeleo wa itikadi za vyama.


Vitisho, mateso
Katika tamko lake hilo, CCM imesema kumekuwa na matukio ya wananchi kutekwa, kuteswa vibaya, kujeruhiwa na hata wengine kuuawa bila watuhumiwa kugundulika, au wanaogundulika kutochukuliwa hatua.
Kutokana na hali hiyo, CCT inawaomba viongozi wake wote na hata wale wa dini na madhehebu mengine, waandishi wa habari na wananchi wote wanaoitakia nchi mema, kuendelea kutoa sauti ya unabii bila kuogopa vitisho na mateso hayo.

Wote kuwa ukimya utafanya nchi iendelee kutawaliwa kwa ukandamizaji na raia wema wengi ndio watakaoumia.

Chanzo;majira

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments