[wanabidii] January Makamba na kiu ya Urais!

Sunday, July 06, 2014
January Makamba, mtoto wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba, ametangaza nia ya kuwania Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiwa jijini London, Uingereza, Makamba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, amesema katika ziara zake maeneo kadhaa ya nchi, 'watu wengi' wamemtaka agombee nafasi hiyo.

Ni jambo jema kwa 'kijana' kama Makamba kuwania fursa hiyo. Ni haki yake kuwania Urais. Ni uthubutu mkuu hata wa kufungua kinywa peke yake, iwe kwa kudhamiria ama kwa utani, akasema anautaka Urais!  

Si kama Makamba peke yake, hata watu wengine wanaokidhi vigezo na sifa zinazotambuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi, wanaweza kutangaza nia hiyo.

Lakini Januari Makamba, anapojitokeza hadharani na kujinadi kwa uhakika wa asilimia 90, kwamba anaielekea njia ya kuingia Ikulu kupitia CCM, kuna mambo mengi ya kujadili. 

Kwanza, inawezekana katika hali isiyopaswa kupuuzwa, kwamba Makamba ameiibua hoja hiyo si kwa dhamira ya dhati kwa alichokieleza, bali kutaka kuifikia jamii.

Aandikwe na kutangazwa kwenye vyombo vya habari ili jamii imtambue, jamii imjadili kama ninavyofanya sasa. Awe katikati ya fikra za watu.

Hilo linawezekana kwa maana ni hulka ama 'janja' inayotumiwa na wanasiasa wengi duniani. 

kuibua jambo ambalo watu wanajikuta wakikutaja, wakikujadili. Unaendelea kuwa katikati ya watu.

Kwa upande mwingine, inawezekana Makamba akawa katika mtandao wenye mwelekeo wa kutaka mtu mmoja miongoni mwa Watanzania walio zaidi ya milioni 45, agombee nafasi hiyo.

Hivyo, kwa kuwa kwake miongoni mwa 'wana-mtandao', akajitokeza na kutamka, ili kufikia lengo la kupata mwitikio wa umma. Inawezekana kwa maana inatumika katika siasa za mataifa mengi duniani.

Inawezekana katika hali hiyo, Makamba, akawa amezisoma ishara za nyakati na dalili za kwamba, mlengwa katika 'mtandao' aliomo, yule anayepewa nafasi kubwa ya kuwania Urais, anaweza asigombee.

Anaweza asigombee kutokana na kukataliwa na chama chake, ama kutokana na sababu nyingine za binafsi ama kitaasisi. 

Lakini kwa vile, mtandao umeimarika na kujiwekea mazingira bora ya ushindi, itakapotokea hivyo, basi chaguo la pili liwe jina la Januari Makamba.

Jambo hilo linatokea sana kwa makundi ya watu wanaojiunga na kuunda 'mtandao' wenye lengo la kutwaa madaraka. Inawezekana hata kwa Makamba ikawa hivyo.

Pia, inawezekana ikawa kwamba, Makamba ana dhamira ya kweli, akijiona kwamba anafaa kuwa Rais wa nchi. 

Kwamba atakapowania na kushinda Uchaguzi Mkuu wa 2015, aitwe Rais Januari Yusuph Makamba!

Hilo limefanyika kwa wanasiasa wengi duniani na wakashinda, kisha wakaitwa majina yao kwa kutanguliziwa cheo cha Rais xxxx.

Vile vile inawezekana katika hayo, lisiwemo hata moja lililomsukuma Makamba kuutangazia ulimwengu kwamba, anahitaji kuwa Rais wa nchi.

Inawezekana kwa maana wapo wanasiasa ambao wakiulizwa maswali, hawaruhusu akili zao zifanye kazi, zifikiri na kuutambua ukweli, badala yake 'wanaropoka'. 

Lisilostahili wanaliona kuwa linastahili. Wapo katika nchi duniani.
Sasa katikati ya hali hiyo, Makamba kwa maana ya Januari Yusuph Makamba, anafaa kwa ukweli usiotiliwa shaka, kwamba agombee na kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Pasipo kumhusisha Makamba, niweke wazi kwamba Urais si kama kuongoza kikao cha kumbukumbu ya mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja. Sivyo.

Urais si kama kuongoza vikao vya 'kitchen party' ama harusi. Urais ni jukumu ambalo kiongozi mwadilifu na mwenye uwezo anaweza kuthubutu kusimama kandoni mwa barabara, akapaza sauti akiualika umma umsikilize, kwamba 'anataka kuwa Rais'.

Inawezekana ikawa hivyo, kama Urais unaotajwa ni ule wa bendi ya muziki kama `Ngwasuma', `Twanga-pepeta', `Pekecha-pekecha' na vinginevyo, lakini si Urais wa nchi.

Urais unaohusu uongozi wa Taifa, ule ambao mhusika wake anakuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,  si jambo dogo kwa kufikirika, kwa maana linaihusu nchi.

Ukiacha matumizi makubwa ya rushwa na hujuma zinazofanywa na baadhi ya wanasiasa hasa barani Afrika, mgombea Urais wa ukweli hawezi kujitangaza.
 
Urais unamfaa mtu ambaye jamii imemfuatilia, imemuandaa, imempika na hatimaye kusimama naye, kwamba anafaa kushika wadhifa huo mkuu kwa nchi.

Mgombea Urais wa namna hiyo si kwamba anaandaliwa kama inavyofanyika kwa waliopo madarakani, kuwapenyeza watoto na ndugu zao kushika nafasi za uongozi na uwakilishi wa umma.

Mgombea Urais wa namna hiyo si kwamba anapikwa kupitia uwezo wake binafsi, bali kwa vile tu ni 'mtoto wa mwenzetu'. 

Hivyo, mgombea Urais anapoibuliwa katikati ya jumuiya za watu, anakuwa yule ambaye kwa uwezo wake, ameonyesha kuwa anaweza. Anasimama mwenyewe, anabuni mwenyewe, anakabiliana na changamoto mwenyewe, anaziona fursa na kuzichangamkia mwenyewe.

Inaweza ikatokea 'bahati nzuri' kwamba Rais anayetokana na 'kubebwa' akawa mzuri. 
Hilo linawezekana ingawa kwa nadra. 

Kwa maana kama 'waliombeba' watakuwa wazalendo, budi utumishi wake utakuwa wa kizalendo.

Lakini kama 'wanayembeba' mgombea wa aina hiyo watakuwa wabadhirifu, wala rushwa na aina nyingine za ufisadi, ni dhahiri kwamba nchi itakuwa imepotea, itaangamia kwa ubadhirifu, rushwa na aina nyingine za ufisadi.

Kwa namna nyingine, haifai kabisa hata kwa dakika moja, raia mwenye utimamu na kujiona anafaa kuwa Rais, atumie vigezo kama jinsia, rika, ukabila ama udini.

Mathalani, inaweza kufikia hatua raia akajiona kwamba anafaa kuwa Rais wa nchi kwa sababu tu ni kijana. Hiyo ni dhana potofu inayopaswa kupingwa na kupigwa vita katika majira yote ya mwaka mzima.

Inawezekana kijana mmojawapo ndani ya jamii akaiweza kazi ya kuwa Rais, lakini awe ni kijana anayeibuliwa kwa historia na  uwezo wake. 

Hivyo, mambo hayo yanakuwa kigezo cha kuchaguliwa na si ujana wake.
Wakati hali ikiwa hivyo, January Makamba anapaswa kujitafakari, je! anaegemea katika upande gani, pale anapojitokeza na kuutangazia ulimwengu kwamba anautaka Urais?
 
Mashaka Mgeta ni Mhariri wa Habari za Uchunguzi na mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana kupitia simu namba +255 754691540, 0716635612 ama barua pepe: mgeta2000@yahoo.com au mashaka.mgeta@guardian.co.tz.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments