[wanabidii] Serikali isipolipa madeni nchi yetu itauzwa

Thursday, June 19, 2014
Tunalazimika leo kuihadharisha Serikali kuhusu madhara yatakayotokea kwa nchi yetu kutokana na kutolipa madeni, iwe ya nchini mwetu au ya nje. Dunia sasa inajua kwamba Serikali yetu imelimbikiza madeni na kujikuta ikidaiwa kila kona, huku watendaji wake wengi wakiishi kwa matanuzi na kufuja fedha mithili ya mabaharia walevi. Wakati huohuo, kasi ya kukopa inazidi kuongezeka na kutishia mustakabali wa nchi yetu kutokana na Deni la Taifa ambalo wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema haliwezi kulipika iwapo Serikali haitaelekeza mapato yake kwenye miradi ya kukuza uchumi badala ya anasa na matumizi yasiyo na maana.

Wananchi wasiwe na matumaini yoyote kwamba huko tuendako Serikali huenda ikaacha utamaduni wake wa kufanya matanuzi kuwa kipaumbele chake. Hebu angalia mlolongo wa bajeti zake za kila mwaka. Matumizi yake ya kawaida yanapewa zaidi ya asilimia 60, huku miradi na shughuli za maendeleo zikipewa chini ya asilimia 40. Bajeti ya mwaka wa fedha ujao, kwa mfano inaonyesha kwamba fedha za miradi na shughuli za maendeleo ni Sh6,445 trilioni sawa na asilimia 32.4 ya bajeti nzima ya Sh19.9 trilioni, huku matumizi ya kawaida yakitengewa Sh13.408 trilioni sawa na asilimia 67.4 ya bajeti hiyo.

Bajeti hiyo kwa kiasi kikubwa inategemea mikopo na fedha za wafadhili ambazo siyo tegemeo la uhakika kwa sababu hazipatikani kwa wakati au kinapatikana kiasi kidogo tu cha fedha hizo. Hivyo bajeti nzima inakuwa haitekelezeki, kwani inatayarishwa kwa kutumia vigezo vya kutunga na kufikirika pasipo kuangalia vyanzo vya uhakika vya mapato. Matokeo yake ni kushindwa kulipa madeni na kulisababishia Taifa hasara kubwa kutokana na riba itokanayo na ulimbikizaji wa madeni kwa muda mrefu.

Ipo mifano mingi ya hali hiyo. Kwa mfano, hebu tuangalie hasara itakayosababishwa na Serikali itakapolazimika kulipa riba ya Sh5 bilioni kutokana na malimbikizo ya miezi sita kwa kampuni ya Jacobsen Elekron AS inayotekeleza awamu ya kwanza ya mradi wa umeme wa Kinyerezi, jijini Dar es Salaam. Kampuni hiyo ya Norway inaidai Serikali Sh80.52 bilioni ikiwa ni malimbikizo ya malipo kuanzia Novemba mwaka jana na Mei mwaka huu.

Hivyo, inailalamikia Serikali kwa kuchelewesha malipo yake mara kwa mara kinyume cha mkataba na imetishia kusitisha kazi ya kutekeleza mradi huo muhimu utakaozalisha megawati 150 za umeme baada ya kukamilika.

Upo ushahidi kwamba kampuni nyingi za kigeni zimeamua kuweka vipengele vya ulipaji wa riba katika mikataba yake na Serikali, baada ya kugundua kwamba Serikali ya Tanzania hailipi madeni yake na kwa wakati. Madeni ya wazawa kama watumishi wa Serikali, makandarasi, wazabuni na wakulima waliokopwa mazao yao au waliochukuliwa ardhi yao pasipo fidia yanabaki pasipo kulipwa kwa miaka mingi, kwani Serikali inajua kwamba hawana uwezo wa kuipeleka mahakamani. Hadhari yetu kwa Serikali ni kwamba inaipeleka nchi yetu kubaya kwa kulimbikiza madeni, huku ikiendeleza kasi ya kukopa. Ni makosa makubwa kutumia ubabe kuchukua ardhi ya wananchi pasipo fidia au kukopa mazao yao bila kulipa. Kwa utamaduni huu wa Serikali kuendekeza madeni na mikopo, nchi yetu huko tuendako haiwezi kuepuka janga la kufilisiwa na hatimaye kuuzwa.

http://www.mwananchi.co.tz/uchambuzi/Serikali-isipolipa-madeni-nchi-yetu-itauzwa/-/1597604/2353966/-/e4ve8u/-/index.html

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments