MALAWI WAMEANZA KUONESHA NJIA, NI TAIFA LINALOELEKEA KATIKA DEMOKRASIA YA KWELI (USIKOSE KUSOMA NUKUU HIZI NILIZOZITAFSIRI)
HOTUBA YA RAIS PETER MUTHARIKA – BAADA YA KUAPISHWA KUWA RAIS WA TANO WA MALAWI – 02 Juni 2014.
1. VYOMBO VYA DOLA KUTOTUMIWA VIBAYA NA WATAWALA;
"Kuanzia leo jeshi la polisi, taasisi ya kuzuia rushwa, ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali na vyombo vingine vya ulinzi na vinavyolinda sheria vitafanya kazi zake kwa uhuru lakini kwa weledi. Tutaizatiti Taasisi ya kupambana na rushwa kwa rasilimali watu na uwezo wa kifedha ifanye kazi yake bila kuingiliwa na serikali"
2. MAWAZIRI NA WATUMISHI WA UMMA WEZI NA WABADHIRIFU;
"Katika utumishi wa umma, sitaongeza hata siku moja ya kumvumilia waziri wangu au mfanyakazi wa serikali ambaye anachukua mali za umma au mali isiyo yake. Mtakapoona waziri wa serikali yangu amekwamatwa msishangae. Baraza langu la mawaziri litaishi na msingi huu wa kuwatumikia wananchi.
Nataka ujumbe huu ueleweke kwa uwazi kabla sijateua baraza la mawaziri. Kama matakwa yako ni kuwa tajiri badala ya kuwatumikia wananchi wa Malawi, usijihangaishe kuja kwenye baraza langu. Nitakapokuteua jiambie moyoni kuwa leo ninachora mstari mwekundu dhidi ya rushwa, wizi wa mali za umma na najiandaa kuchora mstari huo kwa damu yangu"
3. VYOMBO VYA HABARI NA MAWASILIANO YA UMMA;
Uongozi wetu utahakikisha kuna upatikanaji wa habari wa kutosha na katika hili tutawasiliana na washika dau wote pamoja na vyombo vya habari ili kupitisha na kutekeleza muswada wa haki ya mawasiliano kuwa sheria.
Tutaruhusu Shirika la Utangazaji la Malawi (Hapa Tanzania TBC) kufanya kazi kwa uwazi, uhuru na utaratibu unaotenda haki, kufanya maamuzi ya uhariri kwa uhuru na sitaki waziri wangu wa mawasiliano kuingilia kazi yao. Hii ni ahadi nayoitoa kwa wananchi wa Malawi. Enzi za kutumia mashirika ya utangazaji ya UMMA kwa ajili ya kupendelea utawala zimepitwa na wakati. Enzi za kufanya makeke ya watawala kupitia vyombo vya habari vya umma zimepitwa na wakati"
4. KUBANA MATUMIZI YA SERIKALI;
"Tutatekeleza utaratibu wa kubana matumizi. Hii itajumuisha Rais kufanya kazi Ofisini kuliko barabarani. Ndiyo, nitakuja kuwatembelea katika shughuli za kijamii na kitaifa. Lakini msiniulize kuja kuwatembelea bila sababu za msingi huku nikitumia gharama kubwa za taifa. Nitawawezesha maafisa wote wanaohusika katika utumishi wa umma wafanye kazi zao karibu yenu kama wanavyotakiwa".
5. KASHFA YA "CASHGATE"
Wana- Malawi wenzangu, katika miezi kumi na mbili iliyopita, kulikuwa na jinai kadhaa zilizofanywa dhidi ya nchi yetu, kwa mfano KASHFA YA "CASHGATE". Ninapenda kuwaeleza kwamba uchunguzi wa kashfa hii ambao ulianzishwa na Rais Joyce Banda utaeendelezwa na kukamilishwa kwa haki. Wana wa Malawi wanasubiri kujua nani alifanya nini. Wana wa Malawi wanataka rasilimali zao zilizoibiwa zirudishwe. Wana wa Malawi wanataka haki itendeke na hakuna atakayeidanganya serikali kuwa eti inawawinda watu bila sababu.
6. UTANGAMANO WA KITAIFA;
"Ndugu zangu wana wa Malawi, nimeapishwa kuilinda katiba ya Malawi na kusimamia utawala wa sheria. Hili nitalitekeleza. Lakini naomba niweke jambo moja wazi. Sheria lazima iachwe ifanye kazi peke yake inapotokea makosa yametendwa. Lazima tukomeshe utaratibu wa kukamata mtu halafu tunatafuta kosa lake baadaye. Lazima tukomeshe tabia ya kuwaadhibu wale tusiowapenda kwa sababu wanafuata itikadi iliyo tofauti na ya kwetu. Nyakati za kutumia vyombo vya dola na vya haki kwa ajili ya KUWASHUGHULIKIA wapinzani wetu kisiasa zimeshapitwa na wakati. Tusichanganye utendaji na utafutaji wa haki na visasi vya kisiasa"
MAONI YANGU!
Kwa vyovyote vile, Tanzania tuna kila jambo la kujifunza kutoka kwa taifa hili masikini, Uvumilivu wa Kisiasa, Kauli za viongozi zenye kuonesha matumaini na Dira sahihi na Nia njema inayotoka katika kauli za viongozi. Hapa kwetu kauli za viongozi ni "JESHI LITACHUKUA NCHI", "TUTAINGIA MSTUNI", "KULENI NYASI" "WANANCHI HAWANA AKILI" n.k. Hata kashfa zetu kubwa za mabilioni ya fedha yaliyochotwa zimeishia hewani kwa sababu wakubwa wanalindana na wanalindana huku taifa LINAKWISHA. Tuendelee kutafakari.
J. Mtatiro,
Dar Es Salaam,
+255 717 536 759.
0 Comments