[wanabidii] NJAMA ZA KUTAKA KUVURUGA AMANI YA NCHI

Saturday, May 24, 2014
JUMAZA/GF/VO.2/014 19/05/2014

MHESHIMIWA,
Dr. ALI MOHAMED SHEIN,
RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI,
IKULU,

Assalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh.

KUH: NJAMA ZA KUTAKA KUVURUGA AMANI YA NCHI.


Mheshimiwa Rais, kwa heshima kubwa nakuomba uhusike na mada ya hapo juu.

Awali ya yote tunamshukuru Mwenyezi Mungu (S.W) aliyetujaalia kuwa Waislamu kwani bila ya hidaya yake kamwe tusingeweza kuongoka. Sala na salamu zimshukie Mtume wetu na kipenzi chetu Muhammad (S.A.W), jamaa zake, maswahaba zake na wote wanaowafuata kwa wema hadi siku ya malipo.

Mheshimiwa Rais,

Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) ni Taasisi ya Kiislamu isiyo ya kiserikali iliyosajiliwa mwezi
wa Juni / 2003 na kupatiwa nambari ya Usajili 199. Lengo la kuanzishwa JUMAZA ni kuwaunganisha Waislamu wote wa Zanzibar ili kuweza kuwa wamoja na kufanya kazi ya kuutumikia Uislamu ili kufikia mustakbali mzuri wa jamii yetu, kama inavyoelezwa katika ibara ya 3 ya Katiba ya JUMAZA:

"Lengu kuu ni kuleta Umoja na mshikamanao wa Waislamu na Wazanzibari katika kupiga hatua za Maendeleo"

Mheshimiwa Rais,

Kwa heshima kubwa tunachukua fursa hii kuwasilisha nasaha zetu kwako kuhusiana na mustakabali wa nchi yetu Zanzibar tunayoipenda. JUMAZA ikiwa ni Taasisi ya Kiislamu inaamini kuwa ina wajibu wa kutoa nasaha kwa viongozi wetu na hasa kwa vile wao ni ndugu zetu katika Uislamu.

Tumechukua hatua hii baada ya kuona katika siku hizi za karibuni wamejitokeza hadharani baadhi ya wanasiasa wanaotishia mustakbali, ustawi, amani, utulivu na mshikamano wa Waislamu na Wazanzibari kwa ujumla kwa kutoa kauli za uchochezi wa wazi wazi, ubaguzi na matusi ya hadharani na kuhisi wao kuwa huo ndio ustaraabu na utamaduni muafaka wa Wanzanzibari. Hili linastua na kutisha, zaidi kutokana na kufanywa na viongozi ambao walipaswa wawe kigezo cha kufuatwa na isiwe vinginevyo.

Mheshimiwa Rais,

Historia ya karibuni tu inatukumbusha kuwa Zanzibar ilianza kuingia katika msukosuko mkubwa wa kisiasa mara tu baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi nchini. Utaratibu huu mpya kinyume na matarajio ya Wazanzibari wengi kuwa ungechochea kasi ya maendeleo ya nchi yetu kinyume chake ulileta machungu na maafa makubwa kwa raia wa nchi yetu. Siasa za chuki, uadui na uhasama zilizojitokeza kati ya vyama vikuu viwili hapa nchini yaani Chama tawala CCM na Chama Kikuu cha upinzani CUF zilileta maafa na maangamizi kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi (10) kuanzia mwaka 1995 hadi 2009.

Mheshimiwa Rais,

Siasa hizi za uhasama zilizopaliliwa na wanasiasa zilipelekea raia kutengana, kuvunja udugu wao wa kiimani, kuuana, kuvunjiana heshima, kuvunja ndoa zao, kugomeana katika shughuli za kijamii na kiibada kufikia hadi kususiana katika mazishi. Maafa ya siasa za uhasama yalifikia kilele chake mwaka 2001 kwa kutokea umwagaji mkubwa wa damu kwa mamia ya Wazanzibari wasio na hatia waliopigwa risasi za moto katika maandamano ya amani kule Pemba na hapa Unguja. Aidha umwagaji huo wa damu ulifuatiwa na vitendo viovu na vya kinyama katika historia ya nchi yetu vikiwemo uporaji wa mali, kubakwa wasichana mbele ya wazazi wao na wake za watu mbele ya waume zao dhulma nyenginezo.

Mheshimiwa Rais,

Juhudi mbali mbali za ndani na nje ya nchi zilifanyika kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya kisiasa Zanzibar. Hata hivyo juhudi hizo hazikufanikiwa pamoja na kutumia fedha nyingi katika mazingira haya, Waislamu walijitokeza pamoja kutoa msimamo wao kuwa wanasiasa wameshindwa kuleta ufumbuzi na maeleweano hivyo njia pekee ni kurudi katika Dini yetu. Mheshimiwa Amani Abeid Karume aliyekuwa Rais wa Zanzibar wakati huo aliukubali wito huo na kuitisha kikao cha viongozi wa Dini kilichofanyika Ikulu. Mheshimiwa Amani aliwaeleza Masheikh na viongozi wa Dini azma yake ya kutaka kuleta maelewano ya Wazanzibari na kuondosha siasa za uhasama. Masheikh na viongozi wa Dini kwa kauli moja waliunga mkono azma hiyo na kuahidi kushirikiana naye kufikia lengo.

Mheshimiwa Rais,

JUMAZA kwa upande wake ilichukua jukumu la kuwaita Masheikh na Maimamu katika vikao mbalimbali ili kufanikisha maelewano ya Wazanzibari. Azimio muhimu lililofikiwa katika vikao hivyo ni kuitisha Dua ya Kitaifa ili kumuelekea Mwenyezi Mungu (S.W) kwa kutubu na kumuomba nusra yake. Kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, Dua hiyo ilifanyika mwishoni mwa mwezi wa Januari 2010 katika viwanja vya Maisara Suleiman ambapo maelfu ya Waislamu wa madhehebu zote, rika zote, jinsi zote, na wa vyama vyote waliinua mikono yao na kumuomba Mwenyezi Mungu (S.W) atie taufiki maelewano yetu.

Mheshimiwa Rais,

Shukrani zote anastahiki Mwenyezi Mungu (S.W) aliyeitikia dua yetu kwa kutia taufiki katika azma yetu. Aidha, Mwenyezi Mungu (S.W) aliziunganisha nyoyo za viongozi wetu, Aliyekuwa Makamo Mwenyekiti wa C,C.M Zanzibar Mheshimiwa Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa C.U.F Maalim Seif Sharif Hamad ambao walitumia nguvu zao zote kusimamia maelewano.

Mheshimiwa Rais,

Tukio hili halikutofautiana na kisa cha makabila ya Aus na Khazraj ambao walikuwa ni maadui wa kupigana vita kama ilivyokuwa Waislam wa Zanzibar. Kisa hiki kinaelezwa kwa ufupi katika aya zifuatazo:-

" Na shikamaneni kwa kamba ( Dini ) ya Mwenyezi Mungu (S.W) nyote, wala msiachane na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu (S.W) iliyo juu yenu. ( zamani ) mlikuwa maadui, naye akaziunganisha nyoyo zenu, hivyo kwa neema yake, mkawa ndugu…………………….." (AALI – IMRAN 103)

Mheshimiwa Rais,

Waislam na Wazanzibarii walikubali kwa yakini suluhu na maelewano ndio maana asilimia sitini na sita nukta tisa iliunga mkono kuanzishwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Mheshimiwa Rais, sote ni mashahidi wa mafanikio ya SUK, ikiwemo kudumisha amani, utulivu, maelewano, mashirikiano na umoja miongoni mwa Wazanzibari. Aidha SUK imejenga mazingira mazuri ambapo nchi yetu imepiga hatua kubwa za kimaendeleo chini ya uongozi wako, Allah azidi kukupa ilhamu ya kujua kheri na haki na kuzisimamia.

Mheshimiwa Rais,

JUMAZA imeshangazwa, kushtushwa na kusikitishwa sana na baadhi ya wanasiasa wanaopiga vita SUK na kutoa kauli za wazi wazi na azma yao ya kupeleka hoja binafsi katika Baraza la Wawakilishi kuondoa SUK na eti kukuomba wewe binafsi uwaunge mkono katika mpango wao huo ambao utaielekeza Zanzubar katika mtafuku unaepukika.

Mheshimiwa Rais,

Wanasiasa hawa wanaojali maslahi yao binafsi na kujikita mioyo yao katika siasa za chuki na hasadi wanakusudia kuturejesha tulikotoka katika siasa za uhasama, chuki na uadui.

JUMAZA inatamka wazi kuwa hawa ni maadui wa Zanzibar na Wazanzibari na wanastahiki kupigwa vita. Aidha, Mheshimiwa Rais, tunakuhakikishia kuwa Waislamu na Wazanzibarii hawako tayari kurejeshwa huko kwa vyovyote vile.

Mheshimiwa Rais,

Kwa heshima JUMAZA inawakumbusha viongozi wetu wa juu kukumbuka kuwa walichukua ahadi mbele ya Mwenyezi Mungu (S.W) kulinda maelewano ya Wazanzibarii, utulivu na amani ya nchi. Kwa hivyo tunaomba wanasiasa hao wadhibitiwe kwa maslahi ya Zanzibar. Aidha, viongozi wetu na wanasiasa wanapaswa kukumbuka kuwa wao watakuwa " Masuuli" mbele ya Mwenyezi Mungu (S.W) kwa maafa yoyote yatakayotokea chini ya uongozi wao na waelewe kuwa Zanzibar sio mali ya chama chochote cha siasa bali ni ya Wanzibari wote popote walipo.

Mheshimiwa Rais, mwisho JUMAZA inatoa ahadi kushirikiana nanyi viongozi wetu kudumisha amani ya nchi, maelewano na umoja. Aidha tunawaomba viongozi wetu wa Kitaifa, Waislam na Wazanzibari kuweka mbele maslahi ya nchi yetu tunayoipenda Zanzibar.

Mola wetu Mtukufu tunakuomba uilinde Zanzibar na Wazanzibari dhidi ya maadui wa ndani na nje wasiotutakia mema.

Natanguliza shukurani za dhati.

Ndugu yako katika Uislamu.

………………………………………..

Muhiddin Zubeir Muhiddin

Katibu Mtendaji – JUMAZA

Zanzibar


Nakala:

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
MAKAMO WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR,
MAKAMO WA PILI WA RAIS ZANZIBAR,
RAIS MSTAAFU WA ZANZIBAR DK. AMANI ABEID AMANI
MUFTI WA ZANZIBAR,
KADHI MKUU WA ZANZIBAR,
KATIBU MTENDAJI WAKF NA MALI YA AMANA,
SPIKA WA BARAZA LA WAWAKILISHI,
JAJI MKUU ZANZIBAR,
MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR,
AMIR WA BARAZA LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU ZANZIBAR,
WAJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI,
MABALOZI WA NCHI ZA NJE TANZANIA,
MWENYEKITI WA KAMATI YA MARIDHIANO,
KATIBU MKUU WA CUF
KATIBU MKUU WA CCM
MASHEIKH NA MAIMAMU WA ZANZIBAR,
WAISLAMU NA WAZANZIBARI WOTE,

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments