Na: Albert Sanga, Iringa.
Kumekuwa na changamoto kubwa kwa waliojiajiri na walioajiriwa kuhusu dhana ya mikopo na madeni. Licha ya kwamba wakati mmoja hadi mwingine, wengi wetu tumepata kuwa na mikopo au madeni; ni wachache wanaotambua maana halisi ya mikopo na madeni na namna mambo haya mawili yanavyotakiwa kwenda nayo katika maisha ya kiuchumi.
Tuchukulie mfano wa wafanyakazi. Wafanyakazi wengi huwa wanajikuta wakiishiwa mishahara yao kabla hata ya tarehe ya kupokea mshahara mwingine. Wakishamaliza mishahara yao huwa wanajikuta hawana namna ya kumudu bejeti zao, ikiwemo chakula na usafiri; hivyo wanapata mbinyo wa kuazima fedha, huduma au bidhaa kutoka kwa wenzao, katika maduka na kutoka kwa watu binafsi.
Wakishaazima hizo fedha, huduma au bidhaa; mioyo yao inasuuzika, wanamalizia siku zilizobaki kabla ya mshahara. Mshahara unapotoka wanajikuta wanatakiwa kulipa madeni yao, hivyo wengi wao huwa wanaanza kulipa yale madeni kisha inayobaki ndio wanaanza kutumia matumizi mengine. Mtindo unakuwa ni ule ule wa kuishiwa kabla ya mwisho wa mwezi. Kwa kadri mfanyakazi huyu anavyoendelea kukopa madeni kwa mtindo wa namna hii; anaendelea kuzalisha mfumo wa utegemezi unaokua. Ukifuatilia utabaini kuwa kama mwezi huu mshahara ulikuwa unaisha tarehe 20, basi mwezi ujao utaisha tarehe 15, na unaofuata utakuwa unaisha tarehe 10!Mwisho wa siku mshahara wa mfanyakazi huyu usishangae kuona unaisha tarehe 2 ya mwezi! Kwa nini wafanyakazi na watu wengine waendelee kuishi maisha ya aina hii wakati fedha inapita mikononi mwao? Natambua wengi watasema tatizo ni kuwa mishahara wanayolipwa haitoshi, lakini ukweli ni kwamba tatizo kubwa ni kwamba, wengi hawaelewi namna ya kutumia fedha na jinsi ya kumudu madeni na mikopo.
Kanuni inasema kwamba kila fedha inayopita mkononi mwako unatakiwa kuichukulia kama mbegu. Ikipita shilingi kumi ni lazima itoke mikononi mwako ikiwa zaidi ya shilingi kumi. Hapo ndipo ilipo akili ya matumizi ya fedha. Kwa namna maisha yalivyo na halihalisi ya mishahara mingi ilivyo ni vigumu kukwepa suala la kukopa (na hata madeni).
Kwa ujumla hakuna ubaya wa kukopa, lakini kuna tofauti kati ya mkopo na deni. Mkopo ni fedha ama mali inayoazimwa kutoka kwa mtu ama kutoka kwa taasisi; kwa makubaliano ya kurejeshwa katika kipindi fulani; kwa madhumuni ya matumizi ya kuzalisha fedha zaidi ama mali zaidi. Wakati deni ni a) Fedha ama mali iliyoazimwa kwa ajili ya matumizi yasiyozalisha fedha ama mali zaidi b) deni ni mkopo uliopita muda wa makubaliano ya kulipwa.
Ndio maana mtu akienda kukopa fedha benki (kwa madhumuni ya kufanyia biashara) utasikia yule bwana ana mkopo, lakini akishindwa kurejesha mkopo ule kwa wakati uliopo kwenye makubaliano; utasikia yule bwana ana deni! Bahati mbaya ni kwamba kuna watu wengi sana ambao huwa wanachanganya kati ya deni na mkopo.
Wengi wana madeni lakini utasikia wanasema wana mikopo. Mtu anachukua fedha benki kwa dhamana ya mshahara wake kisha fedha hiyo anakwenda kununulia seti ya runinga, sofa na kununulia viwalo, halafu anajifariji kuwa ana mkopo, la hasha! Hilo ni deni. Wengine huchukua fedha benki na kununulia magari ya kutembelea nao hujifariji kwamba wana mikopo; sio kweli hawa ni kwamba wana madeni. Tena hawa wenye kuchukua fedha na kununulia magari ya kutembelea ambayo hayawaingizii chochote zaidi ya kuwalamba fedha zao; wanatakiwa kuyaita "madeni ya kutembelea" na sio magari ya kutembelea.
Katika nukta hii, namna nzuri ya kutumia fedha ni pamoja na kutambua vema nafasi ya mkopo na deni kwako. Unaamini nini kuhusu mikopo na madeni? Una uthubutu na tabia gani linapokuja suala la kudaiwa? Unahimili vipi madeni yako? Haya ni mambo ya kuyajua na kuyarekebisha yakae katika uelekeo sahihi kwa sababu yanaamua sana namna unavyoweza kutumia fedha zako.
Kukopa ni suala zuri sana. Biashara zote duniani zilianzishwa, haunzishwa na zitaendelea kuanzishwa kwa kutumia mikopo. Iwe umechukua hela mfukoni mwako na kuanzisha biashara huo ni mkopo, iwe umepewa fedha, huo ni mkopo kwa biashara yako.
Hata kama mkopo huo hauna riba wala hauhitaji kurudishwa hilo haliondoi uhalisia wa kwamba ni mkopo na katika mizania ya kihasibu mtaji wa kila biashara unatakiwa kuonesha kuwa mtaji wa mwanzo ni mkopo. Hata watu binafsi, iwe ni walioajiriwa ama laa, wenye cha kufanya ama wasio na cha kufanya; ukweli ni kwamba kuna wakati kwenye maisha utapungukiwa na utahitaji kukopa.
Unaweza kukopa benki, kwenye taasisi nyingine ama kwa mtu binafsi, kote huko ni kukopa. Imani yako kuhusu mikopo itaamua sana namna unavyotumia fedha zako katika kulipa ama kutokulipa. Bahati mbaya ni kwamba tunao watanzania wengi ambao hawataki hata kidogo kusikia habari za mikopo.
Hawa utawasikia wakisema, "Mikopo haina maana", "Kukopa ni umasikini", "Ukitaka kufilisika jaribu kukopa". Kama muhusika anaamini hivi uwe na uhakika kwamba ufahamu wake utapeleka taarifa katika ubongo inayoonesha kwamba mkopo ni utumwa!
Sheria ya uvutano wa kimaumbile (Law of attraction) inasema kwamba chochote anachokiogopa mtu hutokea na chochote anachokiogopa mtu hukiabudu na chochote mtu anachokiabudu hudhihirika. Mtu anaeamini kuwa mikopo haifai ikitokea amekopa atakachojitahidi ni kuhakikisha kuwa anahangaika kuulipa mkopo huo ama deni hilo haraka haraka.
Ikiwa mtu huyu ni mfanyakazi ndio atarudi kule mwanzo ambapo kila akipata mshahara atakuwa anakimbilia kurejesha deni analodaiwa. Kinachotokea? Ni kwamba ataendelea kukopa tena na tena na kuendelea kuwa katika utumwa wa madeni na mwisho wa siku akishalemewa atajidhihirishia yeye mwenyewe imani yake ya kwamba kukopa ni utuwa na mateso.
Bahati mbaya wapo wazazi ambao huwaaminisha watoto wao tangu wakingali wadogo ama wakiwa makazini ya kwamba mikopo ni mibaya. Hata wale wanaokopa kupitia makato ya mishahara yao hawawi salama ikiwa wana imani mfu kuhusu mikopo na madeni. Kwa sababu aliyechukua mkopo na kwenda kununua gari ama kununua fenicha za ndani, siku mshahara unapoanza kukatwa na kujikuta haumtoshelezi atageuka na kuanza kunung'unikia madeni kwa ukali wa makato anayoyapata.
Nini maana yake mambo hayo ya madeni na mikopo? Kumbuka kwamba tunaangalia namna ya kuwa na matumizi mazuri ya fedha. Na nimesema kwamba matumizi mzuri ya fedha ni kutumia fedha katika mtiririko unaokuimarishia uchumi wako na sio kukudidimza.
Sasa, kuna wakati katika maisha unaweza kupitia katika changamoto ya madeni. Huenda ulichukua fedha eidha kwa mtu ama katika taasisi kwa lengo zuri la kuzalisha, lakini mambo yakaenda mrama na ukajikuta mkopo umegeuka kuwa deni na huna namna ya kulipa kwa wakati husika. Lakini pia huenda ulichukua fedha na kuielekeza katika matumizi ya 'kimadeni-madeni' na unatakiwa kulipa. Walisema waswahili ya kwamba dawa ya deni ni kulipa; hilo ni kweli lakini unatakiwa kulipa deni lako na wakati huo huo uchumi wako uimarike.
Kama ulichukua mkopo benki kwa dhamana ya mali zako; hilo nitalileta kwa kina zaidi katika makala yenye kichwa, "Wajasiriamali na jinamizi la mikopo". Lakini kote kote, iwe ni kutoka benki, iwe umekopa kwa mtu ama iwe umekopa dukani (na ukajikuta una deni) ni lazima sana uhakikishe unalipa kwa akili.
Kuchukua mshahara wote na kulipa madeni hakutakusaidia zaidi ya kukuangamiza. Kuchukua faida yote na kuipeleka kwa wadeni nako kutakuachia umasikini. Ukiwa katika hali hii ni lazima uzikumbuke tabia za kitajiri; kuhakikisha unatenga kwanza akiba kisha mengine yanafuatia.
Hata kama kuna mbinyo mkali kiasi gani ili ujikwamue na madeni ni lazima uhakikishe unatenga sehemu ya mshahara ama faida yako kwa ajili ya akiba (nap engine uwekezaji) na inayobaki ndipo iende kwa kulipa madeni na matumizi ya kawaida (yale matumizi yasiyozalisha). Kujua namna nzuri ya kutumia fedha ni pamoja na kuwa imara na mwenye msimamo dhidi ya wanaokudai.
Wanaokudai wanaweza kuwa na vishondo vikubwa kweli kweli, wanaweza kuwa na matisho makali kweli kweli, lakini muda wote jitahidi kuvumilia vishondo na matisho yao na kamwe matisho na vishindo vyao visikutoe kwenye kanuni hii, "Madeni yote yalipwe baada ya kutenga akiba".
Kwa wale waamini wanaozingatia masuala ya sadaka, kanuni hii inanyumbuka na kuwa "Madeni yote yalipwe baada ya kutenga sadaka na akiba". Madeni ni changamoto na ni kitu ambacho kinatakiwa kuchukuliwa kama kipindi cha mpito kwa mtu yeyote anaepambana kuimarisha uchumi wake.
Kwenye kitabu cha The Richest Man In Babylon; tunapewa maarifa kwamba haijalishi upo kwenye madeni makubwa na magumu kiasi gani, njia rahisi ya kujikomboa kiuchumi ni kuhakikisha unatenga si chini ya asilimia kumi ya kila fedha unayoipata; na kisha kuanza kuitumia ile fedha uliyotenga kwa ajili ya kuwekeza na kuzalisha.
Sote tunastahili ushindi wa kifedha na kiuchumi.
stepwiseexpert@gmail.com 0719 127 901
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments