[wanabidii] Shirikisho la Serikali 3 litatokomeza kero kuelekea 1

Tuesday, April 22, 2014
Shirikisho la Serikali 3 litatokomeza kero kuelekea Muungano wa serikali 1 Tanzania uliolengwa na waasisi

Kutokuiheshimu Tume ya Jaji Warioba ni kutokumheshimu Mh. Raisi Tanzania aliyeunda Tume hiyo, wateule walioingia kwenye tume hiyo, watanzania wote waliojitokeza kuchangia maoni kupitia Tume hiyo, watanzania waliochangia gharama zote husika na kazi nzuri iliyofanywa na Tume hiyo. 

Mheshimiwa Raisi kuikubali Rasimu ya katiba na kuiundia Bunge la maboresho ni kiashirio cha kuridhika na utimilivu wake, vinginevyo Bunge la maboresho lingeahirishwa hadi hapo Rasimu itakapokuwa imetimilika na hivyo kuwa tayari kuingizwa kwenye hatua ya pili ya maboresho. 

Raisi atakuwa amekiuka taratibu iwapo hataridhika na utimilivu wa Rasimu ya katiba mpya lakini akaipokea
shingo upande kwa tegemeo kwamba Bunge la Katiba alilounda na lililosheheni wengi kutoka Chama chake cha siasa linao uwezo wa kuandaa Katiba mbadala anayoitaka kwa kipindi kifupi kwa njia ya vikao Bungeni pasipo haja ya kuhusisha Tume ya kukusanya maoni na maoni ya wananchi.

Ni kukiuka taratibu kwa sababu Rasimu hutungwa na Tume teule ya wataalamu kutokana na maoni ya wananchi, maboresho yake hufanywa na Bunge maalumu la Katiba na Rasimu iliyoboreshwa hupigiwa na wananchi kura ya kuikubali au kuikataa. 

Mh. Raisi ndiye atakayelaumiwa iwapo Tume aliyoiteua mwenyewe haitafanikisha utunzi wa Rasimu ya katiba mpya iliyo timilifu na inayokubalika kama msingi wa upatikanaji katiba mpya ndani ya Bunge la katiba kutokana taratibu zilizokubalika kwenye mkataba wa utunzi wake kutokuzingatiwa. Ndiye pia atakaeyekuwa wa kulaumiwa iwapo Bunge maalumu la Katiba halitaheshimu Rasimu iliyowasilishwa mbele yake na badala yake likaandaa ingine, na hiyo ikakataliwa na watanzania kwenye kura ya maoni.

Njia pekee ya kukwepa lawama ni Bunge la Katiba kuheshimu Rasimu iliyo mbele yake na kuiboresha badala ya kutunga nyingine mbadala itakayokataliwa na wananchi kwa kura ya maoni. Kwa nini tupoteze muda mwingi na fedha nyingi kwenye awamu ya kwanza inayohusisha Tume ya utunzi wa Rasimu ya katiba mpya na maoni ya wananchi badala ya kwenda moja kwa moja kwenye awamu ya pili ya utunzi wa Katiba mpya ndani ya Bunge la Katiba kama hili linao uwezo mkubwa zaidi wa kutunga hiyo Rasimu kuliko Tume ya wataalamu inayohusisha maoni ya wananchi!?

Rasimu iliyoko mbele yetu iheshimiwe na iboreshwe badala ya kutunga mbadala ndani ya Bunge la Katiba kwa sababu Shirikisho la serikali 3 ndio pekee litakalowezesha watanzania waondokane na kero za uliopo wa serikali 2 kushindwa kutoa fursa sawa kwa watanzania ndani ya pande mbili za muungano, mshirika mdogo kujisikia amemezwa na mshirika mkubwa, mshirika mkubwa kujikuta akiingiliwa na mdogo kwenye yale yasiyokuwa ya muungano, na kasi toshelezi kuelekea Muungano wa serikali 1 uliolengwa na waasisi.

Madai Serikali 2 ni bora kuliko 3 kwa kuzingatia gharama hayana mashiko.

Madai kwamba kwa kuzingatia gharama Shirikisho la serikali 2 lililopo ni bora kuliko la serikali 3 lililopendekezwa kwenye rasimu iliyoko mbele yetu hayana mashiko kutokana na kutokuwa na kiambatanisho cha matokeo ya uchambuzi wa kitaalamu yanayoonyesha kwamba makadirio ya gharama ni madogo na manufaa ni makubwa kwenye serikali 2 kuliko kwenye serikali 3. 

Ingawa gharama ya serikali 3 inaweza inaweza kuzidi kidogo gharama ya serikali 1 au 2, manufaa ya serikali 3 ni makubwa kuliko ya serikali 1 au 2 na tofauti ya gharama ni ndogo mno inapolinganishwa na tofauti ya manufaa kati ya serikali 1 au 2, na ndiyo sababu iliyopelekea waasisi wa Muungano Tanzania kuchagua serikali 2 yenye gharama kubwa kuliko serikali 1 lakini yenye manufaa makubwa kuliko serikali 1. 

Huenda hata gharama ya serikali 3 ikawa ndogo kuliko ya serikali 2 kutokana na ya 3 kuondokana na gharama kubwa ya kukabiliana na milipuko ya mara kwa mara ya kero za serikali 2 kunakofananishwa na matumizi ya aspirin dhidi ya maumivu kutokana na gonjwa la malaria, yaani kuzima viashirio vya gonjwa la malaria (kero za shirikisho la serikali 2) badala ya kutibu gonjwa lenyewe (chaguo la shirikisho la serikali 3).

Faida ya serikali 3 ni kubwa kuliko ya serikali 2 au 1 kwa sababu hii hutoa haki sawa na uhuru mkubwa zaidi kwa nchi washirika wa kujiamulia mambo yake zenyewe kuliko serikali 2 au 1 na hivyo kuwezesha kasi kubwa ya kujitafutia maendeleo ndani ya nchi washirika. 

Kutushauri tuachane na serikali 3 kwa sababu ni gharama kuliko serikali 2 ni sawa kutushauri tuachane na kilimo kinachotegemea zana za kisasa kama matrekta kwa sababu ni cha gharama kuliko kilimo cha kutegemea jembe la mkono. Mara nyingi maendeleo makubwa hupatikana kutokana na ile miradi iliyo ya gharama kubwa. 

Kuna umuhimu wa kuhusisha wataalamu waliobobea kwenye kubaini makadirio ya gharama na manufaa ya miundo ya serikali 2 au 3 yatakayopelekea maamuzi sahihi ya chaguo la muundo wa serikali 3 wenye manufaa makubwa zaidi ya gharama husika. Majibu rahisi rahisi na ya haraka haraka yatatugharimu sana huko tuendako. 

Maendeleo hutokana na mapambano dhidi ya vikwazo na sio kukwepa vikwazo, na uongozi bora ni ule unaowezesha wafuasi kukabiliana na vikwazo na sio kuvikwepa kwenye harakati za kujitafutia maendeleo yao wenyewe. 

Madai udhaifu wa serikali 3 utavunja Shirikisho hayana mashiko 

Madai kwamba Shirikisho la serikali 3 litavunja Muungano kutokana na uwezekano wa nchi washirika kukataa kuchangia migawo yake ya gharama za Shirikisho hayana mashiko hata kidogo kwa hili letu laTanzania. Ni kwa sababu chini ya muundo wowote wa serikali ya Shirikisho Tanzania, Tanganyika ndio itakayokuwa na uzito mkubwa zaidi ndani ya Shirikisho na itakayochangia karibu sehemu yote ya gharama na kunufaika na karibu sehemu yote ya huduma za Shirikisho, na hivyo kutokutarajiwa igome kuchangia gharama za Shrikisho kwani ikifanya hivyo itakuwa ni ikijihujumu yenyewe.

Nchi washirika zitachangia bajeti za Shirikisho kwa kuzingatia idadi zake za watu (ambazo huendana sambamba na ukubwa wa nchi) na ukweli kwamba uzito wa nchi washirika na mgawo wao wa gharama na huduma za serikali ya Shirikisho unapashwa uzingatie idadi zake za watu. 

Kwa mfano kuendana na idadi za watu kwa mwaka wa 2012 (Tanganyika: 43,625, 354 na Zanzibar 1,303,569). Mgawo wa bajeti za serikali ya shirikisho ni kama ifuatavyo: Tanganyika: 43,625,354/ (43,625.354+1,303,569)100 %=97%; Zanzibar=3%. Kwa mwaka wa 2012 viwango vya uzito wa Tanganyika na Zanzibar kwenye serikali ya shirikisho ni 97 % na 3 % na havitarajiwi vibadilike sana kuendana na wakati kwa sababu ongezeko la watu Zanzibar na Tanganyika karibu ni sawa. 

Kwa hiyo, hata kama Zanzibar itakuja iamue kusitisha kuchangia 3% zake kwenye maswala ya Shirikisho, Tanganyika bado itaendelea kuwa na uwezo wa kuendelea kujihudumia mgawo wake kwenye hayo ya Shirikisho kutokana na mchango wake wa 93% kwenye ya Shirikisho. 

Kwa mfano, pamoja ni kwamba Zanzibar haikuwa ikichangia sehemu kubwa ya mgawo wake wa gharama kwenye maswala ya Shirikisho, bado Shirikisho liliendelea kutoa huduma zake kwa wazanzibari na watanganyika kwenye maswala ya Shirikisho lilioendelea kuwepo kwa kutegemea 93 % na zaidi iliyochangiwa na watanganyika (ingawa maendeleo kwenye maswala ya Shirikisho yangekuwa mazuri zaidi kama Zanzibar ingekuwa ikichangia mgawo wake wa gharama kikamilifu). 

Labda tuseme muundo wa serikali tatu utavunja Shirikisho kwa sababu utatokomeza fursa nyingi za upendeleo (zinazojumuisha Zanzibar kuweza kuendelea kuwepo na kufaidi huduma za Shirikisho pasipo kuchangia mgawo wake wa gharama za Shirikisho kikamilifu) kwa gharama ya watanganyika chini ya kivuli cha Shirikisho la serikali 2 lililopo. 

Hata hivyo, Tanganyika haitaathirika hata kidogo iwapo Zanzibar itakuja iamue kusitisha kuchangia mgawo wake wa gharama ya Shirikisho na hivyo kupelekea Shirikisho livunjike kwa sababu uzito wa Zanzibar kwenye shirikisho ni kidogo sana (3 % ≈ 0%) wakati wa Tanganyika ni mkubwa sana (97 %≈ 100%). Ukweli ni kwamba Zanzibar haitakaa ikatae kuchangia mgawo wake kidogo sana wa 3 % za gharama ya Shirikisho ambao ni mdogo sana unapolinganishwa na mgawo wake wa uwepo kwenye Shirikisho. 

Hata hivyo, maboresho ya Shirikisho la serikali 3 lililopendekezwa kwenye Rasimu ya katiba mpya iliyo mbele yetu yawe ongezeko la maswala ya Shirikisho lenye lengo la kuipa Serikali yake uwezo toshelezi wa kutekeleza jukumu lake la kuimarsha na kudumisha Shirikisho. 

Kulikubali Shirikisho la serikali 3 na kuliongezea maswala ya shirikisho ni zuri na toshelezi lengo kwa sababu hakutaathiri utoaji fursa sawa kwa watanzania ndani ya pande mbili za Shirikisho na ni wezeshi wa maendeleo ya Shirikisho kuelekea Muungano wa Serikali 1 uliolengwa na waasisi na unaofikika kwa nji moja pekee ya ongezeko la maswala ya shirikisho hatua kwa hatua hadi hapo yote yasiyokuwa ya Shirikisho yatakapokuwa yamekwisha. 

Kitakachoharakisha kutufikisha kwenye lengo la Muungano wa serikali 1 ni utendaji mzuri wa Serikali ya Shirikisho, wenye tija na unaochangia bila upendeleo kasi kubwa ya maendeleo kwa nchi washirika na kuzipa ushawishi wa kuharakisha kuingiza yasiyo ya Shrikisho kwenye Shirikisho.

Chagua la Shirikisho la Serikali 3 kuelekea kwenye Muungano wa Serikali 1 hatua kwa hatua ni zuri kwa sababu linatoa kwa nchi zote washirika fursa ya kutafakari athari za Shirikiso watakazokumbana nazo na kuwasilisha mbele ya Serikali ya Shirikisho (kupitia serikali za nchi washirika) kwa utatuzi hatua kwa hatua hadi hapo kero zote za Shirikisho la Serikali 3 zitakapokuwa zimegunduliwa na kutatuliwa ili kutengeneza mazingara mazuri ya Muungano wa serikali 1.

Muundo wa Shirikisho la serikali 3 uliopendekezwa kwenye Rasimu ya katiba mpya iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Warioba kwa kuhusisha maoni ya watanzania na makundi kutoka pande zote mbili za Shirikisho Tanzania uzingatiwe kama msingi kwenye maboresho ya Rasimu hiyo yanayoendelea ndani ya Bunge la Katiba. Ni kwa sababu madai kwamba muundo wa serikali 3 utavunja Shirikisho kutokana na gharama kubwa na udhaifu wa seikali yake hayana mashiko na Shirikisho la serikali 3 ndio pekee litakalopelekea kuondokana na kero za Shirikisho la serikali 2 kushindwa kutoa fursa sawa kwa watanzania ndani ya pande mbili za muungano, mshirika mdogo kujisikia amemezwa na mshirika mkubwa, mshirika mkubwa kujikuta akiingiliwa na mdogo kwenye yale yasiyokuwa ya muungano, na kasi toshelezi kuelekea Muungano wa serikali 1 uliolengwa na waasisi.

Imeandikwa na: 
Dk A. Massawe,
Mhandisi Migodi,
Dar es Salaam.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments