MJADALA kuhusu muundo wa Muungano ndani na nje ya Bunge Maalumu la Katiba umeingia katika hatua ya ovyo na unaelekea kupoteza mwelekeo.
Mambo mawili makubwa yanaelekea kuharibu mjadala huu na pengine kuhatarisha kabisa mchakato mzima wa Katiba Mpya na hata nchi yenyewe.
Jambo la kwanza ni mgawanyiko kati ya washabiki wa Serikali mbili na washabiki wa Serikali tatu. Kutokana na ushabiki huo, uliogubikwa na misimamo ya vyama vya siasa, kumeibuka wimbi la zomeazomea na kejeli kati ya kundi moja dhidi ya jingine.
Kwamba ukiunga mkono pendekezo la Serikali tatu ndio unaonekana mzalendo, na ukiunga mkono Serikali mbili unaonekana umenunuliwa na CCM.
Hii ndilo lililompata Profesa Issa Shivji baada ya kutoa mhadhara ulioonekana kuunga mkono muundo wa Serikali mbili na kupinga muundo wa Serikali tatu.
Waliongoza mashambulizi dhidi ya Profesa Shivji ni mwandishi wa makala Joseph Mihangwa na Mbunge Tundu Lissu. Hawa wamediriki kumuita Profesa Shivji msaliti wa kitaaluma.
Kosa la Profesa Shivji ni kuwa na maoni tofauti na misimamo yao ya kutaka Serikali tatu. Profesa Shivji amejijengea heshima kwa uchambuzi wake huru na ubobezi wa kitaaluma Tanzania, Afrika na duniani kote.
Ameandika vitabu na makala nyingi katika majarida mbalimbali ya ndani na nje ya nchi. Ametoa mihadhara ya kitaaluma katika vyuo vingi duniani vinavyoheshimika.
Rika la Profesa Shivji kitaaluma ni akina Profesa Ali Marzurui, Mahmood Mamdan, Ngugi wa Thiongo, Chachage S. Chachage, Wole Soyinka, na wengine kadhaa.
Kimsingi Profesa Shivji ndiyo mfano wa namna ya kuwa msomi. Lakini watu wachache wanataka kumvunjia heshima hizi ambazo amejijengea kwa muda mrefu na kwa bidii kubwa. Kisa: haungi mkono pendekezo la Serikali tatu.
Kwamba katika nchi hii lazima kila msomi anatakiwa aunge mkono pendekezo la Tume la Serikali tatu. Ukipinga lazima umenunuliwa na CCM!
Huu ni upuuzi ambao hatuwezi kuuvumilia. Wanafunzi wake Shivji tuna wajibu wa kulinda heshima za kitaaluma pale ambapo anashambuliwa binafsi badala ya watu kushughulika na hoja yake.
Msingi wa mashambulizi dhidi ya Shivji umejengwa katika dhana kwamba ameyakana maandishi yake mwenyewe huko nyuma ambapo amekuwa akitetea muundo wa Serikali tatu, na hivyo amefanya usaliti wa kitaaluma.
Kuna matatizo mawili ya kiufundi katika hoja ya wakosoaji wa Shivji. Mosi, ni matumizi mabaya ya neno 'usaliti wa kitaaluma'. Pili, ni umbumbumbu kuhusu dhana nzima ya msomi. Nitafafanua.
Katika ulimwengu wa taaluma, usaliti wa kitaaluma una maana tatu kubwa. Maana ya kwanza ni kunakili kazi ya mwanataaluma mwingine na kujifanya kazi yako.
Maana ya pili ni kudanganya au kubadili taarifa (data) ili kukidhi matakwa fulani. Maana ya tatu ni kuiba mtihani kwa kupokea au kutoa majibu kwa mwingine wakati wa mtihani. Hizi ndizo maana za usaliti wa kitaaluma.
Sasa, Profesa Shivji kafanya lipi katika haya hata aitwe msaliti wa kitaaluma? Yeye anatuhumiwa kwa kubadili msimamo kuhusu Serikali tatu, jambo ambalo haliingii katika maana ya usaliti wa kitaaluma.
Jambo la pili la kuzingatia ni dhana nzima ya msomi. Msomi maana yake ni mtu ambaye kazi yake ni kusaka na kusambaza mawazo na maarifa yatokanayo na utafiti. Msomi hujenga hoja katika mambo mbalimbali katika taaluma yake.
Wasomi wamegawanyika katika makundi mawili. Kuna msomi wa taaluma ambaye kazi yake kubwa ni kufanya utafiti katika eneo lake la kitaaluma na kusambaza maarifa na ujuzi kwa njia mbalimbali ikiwemo machapisho ya vitabu na majarida ya kitaaluma.
Hii ni aina ya wasomi walio wengi katika vyuo vikuu duniani na kimsingi hawajulikani nje ya taaluma zao.
Kundi la pili la wasomi ni wale tunaowaita wasomi wa jamii. Msomi wa jamii ni yule ambaye, pamoja na eneo lake la kitaaluma, anafanya uchambuzi wa kisomi katika mambo yanayohusu jamii.
Wasomi wa aina hii ni wa chache sana katika jamii duniani kote kwa sababu kazi wanayoifanya inawaweka katika hatari kubwa.
Ni katika kundi hili wanaangukia akina Ali Marzurui, Issa Shivji, Ngugi wa Thiongo, Wole Soyinka, Mahmood Mamdani, Haroub Othman, Chachage S. Chachage, Richard Dawkins na wengine wengi.
Uchambuzi wa msomi unaongozwa na mambo mawili tu. Mosi, ushahidi wa kisayansi utokanao na matokeo ya utafiti. Pili, mantiki ya hoja (logical argument).
Msomi hafanyi uchambuzi kihisia. Ni katika mazingira haya msomi sio mtumwa wa msimamo. Hii maana yake ni kwamba msomi anaweza kubadilisha msimamo wakati wowote anapopata ushahidi wa kitafiti unaomwambia vinginevyo.
Kwa hivyo, hata kama Shivji angewahi kuwa na msimamo wa serikali tatu isingeshangaza hata kidogo kubadili msimamo huo kama angekuwa amepata ushahidi mpya wa kisayansi unaomwambia kwamba Serikali mbili ni bora zaidi kwa nchi yetu kuliko Serikali tatu.
Huo ndio ukweli mchungu kuhusu usomi. Tofauti na uanasiasa, ambapo huongozwa na misimamo ya kiitikadi, usomi sio ukasuku kwa sababu misimamo ya kisomi huendana na aina ya ushahidi wa kisayansi uliopo na mantiki ya hoja.
Bunge Maalumu la Katiba limekwama kwa sababu limejaa wanasiasa wanaoongozwa na misimamo ya vyama badala ya mantiki ya hoja na ushahidi wa kisayansi katika hoja zinazojadiliwa.
Kwa hiyo hatutarajii kwamba akina Tundu Lissu na akina Ole Sendeka watabadili misimamo bila kujali uzito wa hoja kwa sababu kinachowaongoza wao ni misimamo ya vyama vyao.
Lingekuwa Bunge la wasomi wangefikia mwafaka kirahisi na mapema kwa sababu hoja yenye mantiki na yenye ushahidi wa kitafiti ndiyo ambayo ingeshinda.
Sasa tuangalie kiini cha mashambulizi dhidi ya Profesa Shivji. Machi 30, 2014 Profesa Shivji alitoa mhadhara kwa vijana wa vyuo vikuu katika mada aliyoiita: Uchambuzi wa mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984: Je, sasa tuna nchi mbili?
Mhadhara huu ulilenga kujibu hoja za Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kueleza kwamba waliamua kupendekeza muundo wa Serikali tatu kutokana na, pamoja na sababu zingine, Katiba ya Zanzibar kuitambua Zanzibar kuwa nchi wakati nchi zilipoungana ziliunda nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya uchambuzi wa kina wa mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar na mazingira ya Muungano wa Serikali mbili, Profesa Shivji alihitimisha mambo matatu makubwa.
Mosi, mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar hayakuitangaza Zanzibar kama nchi kwa maana ya nchi bali yaliitangaza Zanzibar kama dola kama ilivyo katika msingi wa Muungano wa Serikali mbili. Kwa hivyo, kwa mujibu wa Shivji, hoja ya kuwa na nchi mbili haipo.
Hii haikuwa hoja nzuri kwa 'washabiki' wa Serikali tatu kwa sababu ilikuwa inaua hoja mama iliyotolewa na Jaji Warioba bungeni. Pili, na pengine hoja chungu zaidi, ni pale alipohitimisha kwamba muundo wa Serikali tatu utavunja Muungano na kwamba matatizo yaliyopo kuhusu Muungano yanaweza kutatuliwa bila kubadili muundo wa Muungano.
Hii nayo ilikuwa hoja chungu kwa 'wapenzi' wa Serikali tatu kwa sababu ndio kiini cha pendekezo hilo. Tatu, kama vile haitoshi, Profesa Shivji akaitimisha kwamba hoja ya Tume kuhusu Serikali tatu inahamasisha hisia za utaifa wa Tanganyika na Uzanzibar, kitu ambacho ni hatari kwa utaifa wa Tanzania uliojengwa kwa miaka 50.
Hizi ndizo hoja za Profesa Shivji ambazo hazishambuliwi kama hoja, na badala yake anashambuliwa yeye binafsi kwa kuambiwa amenunuliwa.
Binafsi sikubaliani na hoja zote hizi za Profesa Shivji, hasa hoja yake kwamba muundo wa Serikali tatu utavunja Muungano.
Pamoja na kutokukubaliana naye naheshimu mawazo yake kwa sababu ni ya kwake na mimi ninayo ya kwangu. Sina ugomvi naye na wala simuoni kwamba ni msaliti kwa kusema alichokisema.
Pamoja na kwamba kubadili msimamo si dhambi wala ajabu kwa msomi, ukweli ni kwamba Shivji hajawahi katika maandishi yake kushabikia aina yoyote ya muundo wa Muungano
Ambacho amefanya Shivji siku zote ni kuainisha udhaifu wa Muungano uliopo katika maeneo mawili. Eneo la kwanza ni uhalali wa Muungano huo kisheria.
Na aina ya pili ni uhalali wa Muungano huo kisiasa. Katika kongamano la kwanza la Katiba lililofanyika Nkrumah Hall, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Januari 15, mwaka 2011, walitoa mhadhara Profesa Shivji na Jenerali Ulimwengu.
Katika mhadhara wao wote wawili walijikita katika haja ya kuwa na Katiba Mpya. Shivji aliweka wazi kabisa kwamba hatuandiki Katiba Mpya kwa sababu Katiba ya sasa ni mbovu.
Tunaandika Katiba Mpya kwa sababu Katiba ya Tanzania haijawahi kuwa na uhalali wa kisiasa, kwa sababu wananchi hawakushiriki kuiandika.
Sasa akina Mihangwa wanasoma vitabu vya Shivji kama waumini wanavyosoma mistari ya Biblia na Quran. Mtu anasoma mstari mmoja na kuibuka na hitimisho.
Hata katika maeneo ambayo Mihangwa amemnukuu Shivji katika kitabu chake kimojawapo haonyeshi ni wapi Shivji amewahi kutamka kinagaubaga kwamba anaunga mkono Serikali tatu.
Lakini ajabu ni kwamba Mihangwa analazimisha kwamba 'Profesa Shivji ni muumini mkubwa wa Muungano wa Serikali tatu na Shirikisho' (Tazama makala yake katika Gazeti la Raia Tanzania, la Aprili 10, 2014, uk. 13).
Kimsingi Shivji haonekani kama ni muumini wa aina yoyote ya miundo inayopendekezwa. Hata katika mada aliyoitoa kwa vijana na ambayo imeibua mashambulizi kwake hakuunga mkono Serikali mbili wala tatu, bali alionyesha tu udhaifu wa miundo yote miwili.
Hivi ndivyo alivyohitimisha mada yake kwa vijana: "Pamoja na hayo, mimi sisemi kwamba muundo wa serikali au dola mbili tulionao hauna matatizo.
Unayo. Lakini tusiangalie Muungano kwa jicho la idadi ya serikali. Tuuangalie kwa mtazamo wa demokrasia. Na tukifanya hivyo tunaweza kubuni muundo ambao utakidhi mahitaji yetu bila kuhatarisha uhai wa Muungano".
Kwa maneno haya ni wazi kwamba Profesa Shivji haamini katika serikali mbili wala katika Serikali tatu.
Ukweli ni kwamba wasiwasi wa Profesa Shivji kwamba mapendekezo ya tume yataibua hisia za utaifa wa Tanganyika na Zanzibar umedhihirika.
Leo hii tunashuhudia wabunge wanavaa fulana za Tanganyika, na baadhi yao wamediriki kuiita nchi tuliyoijenga kwa miaka 50 kwamba ni haramu.
Eti nchi halali ni ile ya Tanganyika iliyoundwa na Waingereza na kudumu miaka mitatu tu baada ya uhuru. Kwamba kilichotengenezwa na wazungu wakoloni wetu ndio halali, lakini cha kwetu ni haramu.
Na bado watu wa namna hii wanatembea barabarani kujitangaza kwamba wao ni wazalendo. Huu ni ujinga ambao baadhi yetu hatutaufumbia macho.
Ajabu ni kwamba hawa akina Tundu Lissu wanaojifanya kutetea mapendekezo ya Tume ya Katiba leo ndio hawa hawa waliitangazia duniani nzima kwamba tume hiyo haikuwa na weledi wa kutosha kufanya kazi waliyopewa.
Akina Tundu Lissu walipeleka hadi hoja kwenye Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kutaka Profesa Mwesiga Baregu ajitoe katika tume kwa sababu haina maana.
Na Profesa Baregu alipokataa kujitoa, nusura afutwe uanachama. Lakini hawa leo ndio eti wamegeuka wazalendo wa kutetea mapendekezo ya Tume, na tena wanawaita wenzao wanaopinga pendekezo la tume kwamba ni wanafiki, mamluki.
Wosia wangu ni kwamba katika jambo gumu kama hili la Muungano haiwezekani tukafanana kimawazo na kimtazamo.
Muhimu ni kwamba tuwe wavumilivu wa hoja kinzani bila kupachikana majina. Ni usanii kuwaita wenzako mamluki kwa sababu tu hawaungi mkono hoja yako.
Kama wote wanaounga mkono Serikali mbili ni mamluki na wamenunuliwa na CCM, hao wanaounga mkono Serikali tatu wamenunuliwa na nani? Tutafakari.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/mashambulizi-dhidi-ya-shivji-ni-upuuzi-usiovumilika-kwa-kisomi#sthash.VYJ1UtQz.Flt4viCM.dpufSend Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments