[wanabidii] KAZI YA WABUNGE ILIKUWA NDOGO KWA NINI WAPOTEZE MUDA KIASI HIKI?

Tuesday, March 11, 2014
Watanzania tulio wengi tumekerwa sana na matumizi mabaya ya muda kwa wabunge wa Bunge la katiba. Kinachosikitisha sana ni kuwa wametumia muda mwingi sana katika kukubaliana mfumo gani wa kura utumike katika kupitisha rasimu ya katiba, kura ya wazi au kura ya siri. Kwa watu wenye hekima, kama wabunge wote wangeacha hekima zao binafsi zifanye kazi, kweli jambo hili lingekuwa la kubishaniwa kiasi hiki?

Tujiulize, 'Ni kwa nini huwa tunafanya kura ya siri au kura ya wazi?' Nini faida ya kura ya wazi na kura ya siri?

Kura ya siri hufanyika kwa nia ya kumpa uhuru mpigaji kura ili asishawishike kwa kuangalia wengine wamepiga namna gani. Lakini sababu nyingine ni kulinda uhuru wa mpigaji kura hasa pale kunapokuwepo na mashaka kuwa mpigaji kura anaweza kutishiwa au kufanyiwa kuadhibiwa kama upigaji kura wake haukuwafurahisha watu fulani, na hasa wakubwa wake.

Upigaji wa kura wa wazi, mara nyingi hufanyika pale mpigaji kura anapowakilisha kundi fulani, na hivyo kundi linalowakilishwa linapenda lishuhudie kama mwakilishi wao amepiga kama walivyokubaliana kabla ya kwenda kupiga kura. Upigaji kura huu unakuwa na maana tu pale ambapo kundi linalowakilishwa lilikwishakubaliana juu ya jambo linaloenda kupigiwa kura. Kwa hiyo, hapa upigaji kura hauangalii utashi wa mwakilishi bali unazingatia makubaliano ya kundi husika.

Tunachotakiwa kujiuliza, kwa wale wanaotaka kura za wazi, makundi yanayowakilishwa yalikwishakubaliana na wawakilishi wao juu ya mambo yote yaliyomo kwenye rasimu ya katiba? Nijuavyo jambo hili halijafanyika. Sijasikia wabunge au wawakilishi wa makundi wamekaa na watu/wapiga kura wa majimbo yao na kukubaliana na wawakilishi na wabunge wao juu ya vipengere vyote kwenye rasimu ya katiba. Na kwa vile jambo hilo halikufanyika, kwa vyovyote kura itakayofanywa na wabunge wa Bunge la Katiba, ni kura itakayotegemea utashi wa mbunge binafsi na wala siyo kikundi au wapiga kura waliompeleka bungeni. Ni kwa kuzingatia ukweli huu, ndiyo maana baada ya mchakato huu wa kibunge wananchi watapewa nafasi ya kupiga kura, na watakuwa na uwezo wa kutokubaliana au kukubaliana na wawakilishi wao.

Kwa mtazamo na ukweli huu si haki, na ni haramu kabisa kwa kipimo chochote cha kidemokrasia, mtu anayepiga kura kwa kutegemea utashi wake binafsi, ukataka apige kura ya wazi.

Kila mwananchi anafahamu kuwa wabunge wa CCM na CCM wanalazimisha kura ziwe za wazi. CCM kama chama kikongwe chenye serikali, na Rais aliyeanzisha mchakato wa katiba ametoka kwenye chama hiki, wanatakiwa waoneshe mfano mzuri wa kuheshimu demokrasia ya maamuzi ya utashi wa mtu binafsi. Wabunge wa wananchi kupitia CCM, CUF, CHADEMA, TLP au NCCR watambue kuwa hawapo kwenye Bunge hili kuwakilisha vyama vyao na wao siyo wawakilishi wa kupitia taasisi za vyama vya siasa, bali wanawakilisha wapiga kura wao. Wabunge hawa kama walivyo wabunge wengine wa kuchaguliwa wanatakiwa kuzingatia kwa umakini mkubwa juu ya wapiga kura wao. Kuna wabunge wa Bunge la Katiba ambao wameteuliwa na Rais kutoka kwenye vyama vya siasa, hawa wana haki ya kuangalia maslahi ya vyama vyao maana uwakilishi wao kimsingi umetokana na vyama wanavyoviwakilisha.

Vyama vya siasa kutoa maelekezo kwa wabunge wa wananchi waliopata ubunge kupitia vyama vyao, ni kosa maana wanataka kupokonya haki ya wananchi kuwakilishwa. Wabunge wa Bunge la Mwungano wameingia kwenye Bunge la Katiba kutokana na nafasi yao muhimu ya kuwawakilisha wananchi na wala siyo kwa sababu ya kukiwakilisha chama walichopitia katika kuupata ubunge. Wabunge hawa kabla ya kufanya maamuzi yoyote yale katika Bunge hili la katiba, jambo la kwanza inabidi wawakumbuke wananchi wao, na wajiulize wananchi wao wanataka nini, na maamuzi wanayoyafanya yatawasaidia vipi wananchi wanaowawakilisha. Ni aibu kubwa na kwa kweli upungufu wa uwezo wa kiuongozi kama mwakilishi huwezi kutambua matakwa ya unaowawakilisha.

Wabunge wa Bunge la Katiba inawapasa kufahamu kuwa vyama vya siasa, vikundi wanavyoviwakilisha, madhehebu ya dini wanayoyawakilisha ni jumuia tu walizopitia kufika mahali walipo. Na wala hakuna uhakika siku zote watapitia taasisi hizo. Tumeona wanachama wa vyama vya siasa, viongozi wa vyama, viongozi wa vikundi mbalimbali na hata viongozi wa kidini, wakifukuzwa au kusimamishwa uanachama/uongozi. Hata unapofukuzwa unachokitegemea kikulinde na kukuhakikishia ustawi na haki zako zote ni katiba. Kwa hiyo mbunge yeyote atakayefanya maamuzi yake kwenye uundwaji wa katiba kwa kuangalia maslahi na maelekezo ya chama chake yanayokinzana na maslahi ya kitaifa kwa vyovyote hakustahili kuwepo huko. Hatambui kuwa hata hicho chama anachotaka kukiwekea maslahi yake mbele kuliko maslahi ya Taifa, siku moja kinaweza kuwa adui yake, atakapokimbilia ni katiba ya nchi. Daima tunatakiwa kufahamu kuwa aliye rafiki yetu leo, kesho anaweza kuwa adui yetu, hivyo ni vema kufanya maamuzi ya msingi kwa kusimama katika ukweli na uhalisia maana ukweli ndiyo hulinda haki ya kila mtu.

Wananchi itabidi tumshangae na hata ikibidi tumlaani mbunge yeyote wa Bunge la Katiba, na hasa mbunge aliyeingia kwenye Bunge la Katiba kutokana na ubunge wake wa kuchaguliwa na wananchi, ambaye ataonesha au kutamka kuwa maamuzi yake yaliathiriwa na maamuzi ya chama chake. Tunataka maamuzi ya wabunge hawa yatokane na utashi wao wenyewe kwa kuangalia wapiga kura wao wanaowawakilisha wanataka nini, na nini maslahi ya kitaifa kwa kizazi cha sasa na vile vingi vijavyo.

Ni muhimu sana uundwaji wa Katiba Mpya uzingatie ulinzi wa misingi ya kidemokrasia, katiba iliyopatikana kwa kubana milango ya demokrasia haiwezi kujenga na kulinda demokrasia ya kweli.

Kwenye Management tunasema, 'Failure of the organization is failure of the Management', na kwenye hili la Katiba top Management inaundwa na Rais Jakaya Kikwete. Mchakato huu usipoenda vizuri, au ukaleta rabsha au ukazalisha katiba isiyokidhi matarajio ya Watanzania, itakuwa ni Failure ya Rais Jakaya Kikwete ambaye aliasisi na ndiye msimamizi mkuu. Hivyo ni ushauri wangu kwa Rais, pamoja na kuzingatia maoni ya viongozi wenzake ndani ya CCM na Serikali yake, atambue kuwa anayebeba jukumu zito ni yeye binafsi. Umahiri wa uongozi haupo katika kupokea ushauri wa kila mtu bali upo kwa kiongozi kutambua kipi kilichosahihi na kuwashawishi wenzake wamwunge mkono katika hilo jambo lililo sahihi na jema. Vivyo hivyo, kwa Rais Kikwete umahiri wake hautapimwa katika kusikiliza na kupokea ushauri wa kila mtu bali utategemea sana maamuzi yake sahihi na uwezo wake wa kuwashirikisha wenzake katika chama na serikali katika kumwunga mkono katika njia sahihi ya kufikia kupata katiba sahihi.

Bart Mkinga

Share this :

Related Posts

0 Comments