[wanabidii] ACT TAIFA KWANZA, TUVUTE SUBIRA KUITOA CCM IKULU?

Monday, March 03, 2014
Rafiki yangu Ibrahim Makbel aliniuliza uelewa wangu juu ya falsafa ya TAIFA KWANZA CHAMA BAADAE? Hivi ACT ni chama au ni SACCOSS kama ya CHADEMA? Nimeona ngoja leo nijaribu kufafanua kidogo.
 
Awali ya yote sikubaliani naye kuwa CHADEMA ni SACOSS, nafikiri hata yeye mwenyewe anajua kuwa CHADEMA ni chama cha siasa chenye usajili wa kudumu. Pia nafikiri anajua ACT ni chama siasa chenye usajili wa muda, na ni chama kilichoibuka katika kipindi ambacho kuna haja ya kupatikana kwa mbadala wa CCM na CHADEMA; Hapa naomba rejea makala za Dr Kitila Mkumbo zilizofafanua kwa kina hii dhana ya uhitaji wa mbadala wa vyama hivyo.
 
Huku nikizingatia hoja zilizoibuliwa na Dr. Kitila katika makala zake, tunahitaji mbadala wa CCM na CHADEMA kwasababu vyama hivyo vinakanyaga maana halisi ya neno "siasa" na kwa hivyo vinashindwa kukidhi matarajio ya umma kwa vitendo vyao ingawa kwa maneno yao wanakidhi hayo matarajio.
 
Siasa ni njia ya kufanya maamuzi ya umma kwa maslahi mapana ya umma husika. Wakati chama cha siasa ni mkusanyiko wa watu wenye malengo ya kisiasa yanayofanana, na malengo hayo sanjari na njia ya kuyafikia hayo malengo yanalindwa na katiba na kanuni za uendeshaji walizozitunga wenyewe.
 
Kwa kuzingatia tafsiri ya neno "siasa" kama nilivyofafanua hapo juu, Chama cha siasa katika shughuli zake za kila siku lazima kilenge katika kuathiri njia ya kufanya maamuzi ya umma, ulengaji huo ni lazima uzingatie maslahi mapana ya umma. Mwanachama wa chama siasa na kiongozi wa chama cha siasa, katika shughuli zake za kila siku za kichama lazima azingatie maslahi mapana ya umma, kwa kufanya hivyo chama chao kitaweza kuathiri maamuzi ya umma.
 
Kuna sababu kuu mbili za chama na wanachama kutakiwa kuzingatia maslahi mapana ya umma.
 
MOSI: MAANA YA "SIASA"
Kwa kuzingatia maana ya siasa kama nilivyo ifafanua hapo juu, chama siasa na wanachama wa vyama vya siasa hawana hiyari katika kuzingatia maslahi ya mapana ya umma. Huwezi kuathiri maamuzi ya umma kama ukifanya shughuli zako bila kuujali huo umma.
 
PILI: KURA YA MTU MUHIMU, KULIKO KADI YAKE.
Tangu huko juu nimekuwa nikizungumzia "maamuzi ya umma" lakini sijafafanua nini hasa maana ya maamuzi ya umma. Kwa kifupi (waweza kunikosoa) maamuzi ya umma ni makubaliano ya umma juu ya jambo fulani linalo wahusu, na makubaliano hayo yanaweza kufanywa kwa kila mmoja wao kushiriki au huo umma kuteua/kuchagua wachache miongoni mwao wafanye hayo makubaliano kwa niaba ya umma.
 
Katika nchi za kidemokrasia makubaliano ya kupata bunge na serikali mpya hufanywa na kila mwananchi kwa kuzingatia sheria za nchi husika. Nchini petu uanachama wa chama cha siasa ni hiyari, na kwa takwimu za sasa asilimia kubwa ya watanzania si wanachama wa vyama vya siasa.
 
Chama cha siasa chenye kuhitaji kupata wabunge wengi na kuunda serikali katu hakiwezi kutegemea kura za wanachama wake tu, lazima kitegemee zaidi kura toka kwa watu wasiokuwa wanachama wa vyama vya siasa na watu wa vyama vingine. Ili chama kipate kura hizo lazima kiathiri maamuzi ya umma(maamuzi ya kuingiza serikali na bunge jipya madarakani), kinyume chake ni ndoto kwa chama hicho kukabidhiwa dola na umma. Hapa ndipo utakapokuja kugundua umuhimu wa "kura" ya mtu kuliko hata kadi yake ya uanachama kama anayo.
 
Chama hakitakiwi kutumia propaganda tu katika kuathiri maamuzi ya umma, lakini pia kinatakiwa kifanye kazi zake zote kwa maslahi mapana ya umma na kifanye kila juhudi kuhakikisha huo umma unajua kuwa chama hicho kipo kwa maslahi ya umma.
 
CHADEMA, CCM NA MASLAHI YA UMMA.
Viongozi wa CHADEMA hawazingatii maslahi mapana ya chama. Ukiukwaji mkubwa wa katiba ya CHADEMA, matumizi mabaya ya madaraka, matumizi mabaya ya fedha za chama, ung'ang'anizi wa madaraka na ukiukwaji wa itifaki ni kiashiria tosha kuwa viongozi wakuu wa CHADEMA hawazingatii maslahi ya chama. Je, viongozi wasiozingatia maslahi ya chama wataweza kuthubutu kuzingatia maslahi ya taifa? Je, chama chenye uongozi usiozingatia maslahi ya taifa utasema chama hicho kinafanya shughuli zake kwa maslahi mapana ya taifa?
 
CHADEMA hakipo kwaajili ya maslahi ya umma na wala hakizingatii maslahi ya umma, ndio maana mwenyekiti wa PAC alipoinyooshea kidole CHADEMA alipata msukosuko ndani ya chama chake. CHADEMA ilitaka isiguswe, badala yake ilindwe na kutonywa kwasababu mwenyekiti wa PAC ni mwenzao. Yaani walitaka Zitto Kabwe awe kama Ndugai wa CCM ambaye kila uchao hukanyaga kanuni za bunge kwa lengo la kutoa tahafifu kwa CCM na serikali. Najiuliza hivi wabunge wa CHADEMA wataweza kuja kuikosoa serikali ya CHADEMA kama afanyavyo Deo Filukunjome kwa CCM sasa? Hawataweza, labda wakubali gharama za ukosoaji huo kama ilivyo kwa Zitto sasa.
 
CCM nayo ina tafauti ndogo sana na CHADEMA, na si nyingine, CHADEMA ni chama cha upinzani wakati CCM ni chama tawala. Vitendo vyao vinafanana kabisa. Chama cha siasa ndio mdhamini mkuu wa serikali, serikali ikiboronga mdhamini ndio mwenye kulaumiwa, na ili watu atakao wadhamini katika uchaguzi unaofuata wakubalike kwa umma ni lazima chama cha siasa kihakikishe serikali inawajibika kwa umma.
 
Mwenyekiti wa CCM ndio kiongozi mkuu wa serikali, kama ilivyo kwa CHADEMA; KUB ndio mwenyekiti wa CHADEMA. Ndio maana kelele za Nape za kusema kuna mawiziri mizigo zilikuwa hazina tafauti na kelele za mlango ambazo siku zote hazimfanyi mwenye nyumba kukosa usingizi. Hivi CCM inaweza kumwita Kikwete na kumuhoji kufeli kwake katika kutekeleza ilani ya CCM? Hicho kikao cha CCM kitaongozwa na nani? CHADEMA inaweza kumuita kiongozi wa upinzani bungeni na kumuhoji kufeli kwa kambi hiyo katika kufanya au kusimamia mambo kadha wa kadha ambayo chama kiliuahidi umma? Je, hicho kikao CHADEMA kitaongozwa na nani?
 
Mfano mdogo, Mbowe alitangaza hadharani kuwa hatochukua gari la serikali kwa lengo la kutekeleza maazimio ya chama ya kupunguza matumizi makubwa ya serikali kwa vitendo, yeye akifanya hivyo aliyekuwa naibu katibu mkuu wa CHADEMA alitangaza kutokuchukua posho na hadi sasa hachukui posho, lakini Mbowe huyo huyo alikwenda kulichukua gari kimyakimya bila kutoa ufafanuzi wowote kwa umma alioutangazia. Je, CHADEMA kama chama kilimwita na kumhoji Mbowe juu ya suala hili la kwenda kinyume na maazimio ya chama? Kama kilimwita hicho kikao cha kumuhoji kiliongozwa na nani?
 
Huku ndio kufanana kwa CHADEMA na CCM, na vitendo vyao vinavyo wafanya wafanane haviko kwaajili ya maslahi mapana ya umma. Watanzania wamechoshwa na CCM kwa kiasi fulani, lakini pia wameanza kuikubali CHADEMA kwa kiasi fulani. Kuikubali kwao CHADEMA hakutokani kwa uimara wa CHADEMA, bali kuikubali kwao kunatokana na kule kuichoka CCM na kazi za kibunge za Dr. Slaa na Zitto; kupitia kazi za hawa watu wawili ndipo maovu na ufisadi wa CCM ulipo tapakaa zaidi. Kinacho sikitisha, CHADEMA kimefanikiwa kuona maovu ya CCM lakini kimeshindwa kurekebisha maovu hayo kwa viongozi wa CHADEMA kuacha kuenenda kama viongozi wa CCM.
 
ACT, MBADALA NA MASLAHI YA UMMA.
Pamoja na kwamba hapakuwahi kuwa na chama cha upinzani chenye nguvu kama NCCR-MAGEUZI  lakini kwasasa hakuna chama cha upinzani chenye kuungwa mkono na watu wengi kama CHADEMA. CHADEMA imepoteza dira na haipo kwaajili ya maslahi ya umma, CCM ilipoteza dira tangu za enzi za Kolimba na sasa inatumia hila na ujinga wa watanzania kubaki madarakani.
 
ACT imekuja katika kipindi ambacho karibu viongizi wa vyama vyama vyote nchini vinajali maslahi ya makundi fulani ndani ya vyama hivyo badala ya maslahi ya chama na umma kwa ujumla wake, ACT imekuja katika kipindi ambacho tunahitaji mbadala wa chama kikuu cha upinzani kitachoweza kuwa mbadala wa chama tawala cha sasa. Kama ilikuwa sahihi kwa YEHOVA kuwasubirisha akina Joshua kwa miaka 40 katika Jangwa kabla kuingia Kaanani kwanini isiwe kwetu sahihi kusubiria kupata chama makini, imara, chenye kujali maslahi ya umma kabla ya kuitoa CCM madarakani? Rejea Hesabu 32:13
 
Hivi leo hii tunaitoa CCM madarakani, tunakiingiza chama gani? CHADEMA? CUF? Tuingize CHADEMA chama ambacho kila uchaguzi wake mkuu ndani lazima kuwe na mgogoro na ukiukwaji mkubwa wa katiba yake? Chama ambacho kina watu ambao wanaona hicho chama ni mali yao, na kwa kujua ni mali yao ndio maana walimzuia Zitto asigombee mwaka 2009 huku wakimuahidi atagombea uchaguzi unaofuata, uchaguzi unakaribia, watu hao wenye chama chao wakaanza kuratibu njama za kumchafua Zitto na wamefanikiwa kwani uanachama wa Zitto unalindwa na mahakama tu.
 
Tuingize CHADEMA inayotaka wanachama wake ambao ni viongozi wa umma wafanye kazi zao za umma kwa kuipendelea CHADEMA? Tuingize CHADEMA madarakani chama ambacho hakina mipango na maendeleo himilivu ya kiumchumi na kiuenezi? Hivi kitaweza kupaisha uchumi wetu wa nchi ikiwa chama chenyewe mambo yake ya kiuchumi yanaenda alijojo?  Tumepambana vya kutosha katika kuindoa CCM, lakini sasa ni vema hayo mapambano yaelekezwe katika kuleta mbadala wa CCM. Mapambano ya kuleta mbadala wa CCM yakifanikiwa yale ya kuiondoa CCM yatafanikiwa kabla hata ya jua la utosi.
 
Tunahitaji chama chenye mfumo usio ruhusu wanachama wake wenye nyadhifa za umma kuwa na nyadhifa pia kwenye vyama chao, chama kitakachokuwa tafauti na CCM na CHADEMA kimfumo. Mfano KUB, rais na wabunge kuwa viongozi wa chama ni kuleta mgongano wa kimaslahi.
 
HITIMISHO.
Kama ACT ndio wanatumbia kuwa TAIFA KWANZA CHAMA BAADAE, na kama wana maanisha kwa kusema hivyo, basi ACT ni mbadala wa CHADEMA utakaokidhi kuitwa na kuwa mbadala wa CCM. Kwa kuzingatia maudhui yote ya makala hii, hasa hasa kwenye hii "hitimisho" basi nami sina budi kusema na kukubali kuwa "TAIFA KWANZA CHAMA BAADAE"
 
Njano5.
 
0784845394.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

0 Comments