[wanabidii] KUBORESHA JESHI LA POLISI KATIKA KATIBA MPYA

Friday, February 21, 2014
Rasimu ya pili ibara 243(1) inasema kutakuwa na jeshi la polisi la jamhuri ya muungano. Mimi ninapinga kuwepo jeshi moja la polisi chini ya muungano kulingana na maelezo yafuatayo.

Moja ya zana muhimu ya polisi kufanikisha shughuli yao ni kutumia mamlaka waliyopewa kisheria kutumia maoni au mawazo yao binafsi kufanya uamuzi wenye usawa bila kubanwa kufanya maamuzi fulani na sheria moja kwa moja . Kwa kingereza inaitwa "discretion: the power of a judge, public official or a private party (under authority given by contract, trust or will) to make decisions on various matters based on his/her opinion within general legal guidelines"

MAMLAKA YA POLISI KUTUMIA NGUVU


Mamlaka haya yanajumuisha kutoa uhai wa mtu (kuua) na kunyima watu uhuru na haki zao pale wanapowakamata. Mamlaka haya yapo vichwani mwa watu hasa wale wanaoomba msaada wa polisi. Watu uita polisi ili polisi watatue migogoro au tatizo; wakamate mtu, kushusha munkari wa mtu au kumtoa mtu ndani ya nyumba. Hapa watu wanachotaka ni polisi kutumia mamlaka yao. Katika ili si raia tu hata viongozi utumia polisi wakijua mamlaka ya polisi ni vigumu kuyahoji pale tu wanapoyatumia.


NGAZI TATU ZA KUDHIBITI JAMII (SOCIAL CONTROL)


Mchambuzi wa masuala ya kijamii Stanley Cohen anatafsiri Udhibiti Jamii (Social Control ) kuwa njia mbalimbali ambazo jamii uchukulia juu ya tabia na watu inaowaona kwenda kinyume na maadili, wenye kuleta matatizo, wanaogofya, wanaohatarisha kwa njia tofauti, nk.

1. Ngazi ya Familia na Marafiki (private level) mamlaka ya kudhibiti watu ndani ya kundi hili kwa njia ya kuonya, kusifia na kupinga na hata kuadhibu. 
2. Ngazi ya Jumuiya (Parochial level). Inahusisha makundi kwenye jamii ambayo ndo yenye uwezo wa kudhibiti jamii kwa watu ambao ni sehemu ya jumuiya zao. Kundi hili linahusisha mashule, makanisa na misikiti, na jumuiya zinazoundwa kwenye jamii kama vyama vya siasa, jumuiya za kina mama. Pia makampuni ya biashara ambayo yanahusika na mtu au watu mfano makampuni yanayodhamini wasanii uwataka wasifanye maovu kuharibu sura ya kampuni. Mfano shuleni mwananfunzi anaweza kusimamishwa masomo, kijiji kinaweza kumwadhibu mwanakijiji, chama cha siasa kinaweza kumwadhibu mwanachama nk.
3. Ngazi ya Umma (public level). Katika ngazi hii mamlaka ya kudhibiti jamii yako chini ya taasisi za serikali kama polisi jamii, polisi maliasili na uhamiaji, na mamlaka nyingine za udhibiti wa shughuli mbalimbali kwa mujibu wa sheria kama sekta ya nishati. Mara nyingi ngazi hi ikifikiwa ni kwamba ngazi mbili za mwanzo zimeshindwa.


MAHUSIANO YA POLISI NA UDHIBITI JAMII

Polisi ni sehemu ya mfumo mpana wa kudhibiti jamii. Udhibiti jamii unaotumiwa na polisi hautakiwi kuwa ule unaolazimisha uwepo wa mawazo yanayofanana au ya aina moja katika jamii, au kwa makusudi ya kukandamiza mtu au watu kwa manufaa ya kisiasa. Kinachotautisha taifa la kidemokrasia na lisilo la kidemokrasia ni kuwepo na mfumo unaoruhusu mawazo kinzani na ubadilishanaji uongozi kwa amani. Uwepo wa uhakika wa uhuru na haki za raia kikatiba kulindwa kama uhuru wa kujieleza, uhuru wa habari na kujumuika ili kuwezesha mageuzi kwa amani kwa kuruhusu mawazo mapya, kinzani na yenye utata kusikika. Yote haya ni majukumu ya Polisi kuhakikisha raia wanatekeleza haki zao za kikatiba.


KWANINI POLISI HAWATIKIWI KUWA CHINI YA SHIRIKISHO NA AMIRI JESHI MKUU


Moja wapo ya wajibu wa polisi ni kulinda na kuhifadhi uhuru na haki za raia kikatiba. Tukaeleza pia mahusiano ya udhibiti jamii na polisi hasa katika taifa la kidemokrasia hapo juu. Kwenye mamlaka ya polisi kutumia nguvu tumeongelea kwamba watu wanapoita msaada wa polisi wanataka polisi itumie mamlaka yake ya kutumia nguvu. Lakini polisi wamepewa mamlaka ya kutumia maoni na mawazo yao (discretion) kufanya maamuzi yaliyo ndani ya sheria kutoa haki. 


Ntaita discretion, Utashi. Utashi waliopewa polisi kikatiba unaondolewa na mamlaka iliyopo juu yao ikiwa si umma. Mfano polisi wanapokuwa chini ya amiri jeshi mkuu hii inawaondolea kufanya maamuzi ambayo yanalinda haki na uhuru wa raia kwenye katiba kwa kutumia utashi wao kisheria. Mkuu wa polisi wa taifa, mkoa na wilaya wanawajibika kwa rais ambaye ni amiri jeshi mkuu, bila shaka hii inaondoa uhakika wa polisi kulinda na kuhifadhi haki za raia kikatiba. 


Rais anachaguliwa kupitia uchaguzi wenye wagombea wa itikadi tofauti kupitia vyama vyao ambavyo vitaendelea kueneza itikadi zao hata baada ya kushindwa uchaguzi, hivyo Rais anapokuwa amiri jeshi mkuu na polisi ikiwemo ni wazi anaweza kutumia mamlaka yake kutaka polisi watumie nguvu kwa mazingira ambayo polisi wangetumia mamlaka ya utashi (discretion) na uwezo wao wa kudhibiti jamii wasingetumia nguvu. Tumeshuhudia Arusha, Iringa na Morogoro ingawa si rais aliamrisha lakini kwa polisi kuwa chini ya mkuu wa nchi inawalazimu polisi kutumia nguvu badala ya utashi kulidhisha mkuu.


Polisi hawatakiwi kuwa chini ya shirikisho, badala yake polisi wawe chini ya serikali za washirika kwa maana Tanganyika watakuwa na jeshi lao la polisi na Zanzibar watakuwa na jeshi lao la polisi. Hii inatokana na ngazi za udhibiti jamii nilizoziongelea. Katika ngazi ya kwanza (familia na marafiki) tunaona mtu anaweza kuonywa, kusifiwa au kupingwa na akaridhika bila shari ndani ya familia na marafiki kuliko watu wa nje, isitoshe ndugu wanaguswa zaidi. Mfano mlevi ni rahisi kuzingatia ushauri wa ndugu na marafiki wanaoguswa kuliko watu wa nje. Katika ngazi ya pili ya jumuiya tunaona ilivyo wanajumuiya kumkanya mtu anayeenda kinyume na jumiya yao na akasikia na ukizingatia ndo watu wanaoguswa zaidi na maovu ya huyo mtu. Mfano mwanafunzi akizidi utoro walimu watamkanya kwani akifeli wataonekana hawafundishi (wanaguswa).


Ngazi mbili za kwanza ndo zinanifanya au zilifanya nchi nyingine polisi kuwa chini ya eneo moja la kimamlaka kama wilaya, mkoa, nk pia lisiwe chini ya amiri jeshi mkuu. Polisi watatoka maeneo hayo hivyo wanaguswa watu wanaoenda kinyume na jamii yao. 


Kati ya faida za shirikisho ni serikali za shirikisho kuwa na uwezo wa kubuni mifumo na sera za kujiletea maendeleo na watu wasiporidhika wanaweza kutumia haki zao kikatiba kupinga utawala wa serikali ya mshirika. Swali la kujiuliza: Ikiwa watanganyika wamechoka na utawala wa Tanganyika wakaandamana polisi kutoka Zanzibar ambaye kituo chake cha kazi ni Tanganyika hivi ataguswa kweli na kuilinda haki hiyo ya watanganyika kuandamana. Mawazo kinzani katika siasa za Tanganyika atayachukuliaje.


Rasimu ya katiba inasema watu watakuwa na uwezo wa kuwatoa wabunge mizigo, hivi ikiwa wapiga kura wa jimbo la Bagamoyo wamemchoka mbunge wao, Polisi toka Arusha mjini kituo chake cha kazi ni Bagamoyo atachukuliaje hali ya wapiga kura Bagamoyo kumsema, kuandamana kumpinga mbunge wao.


Uundwaji wa polisi katika mataifa ya kidemokrasia uyafikiria sana mambo haya wakati wa kubuni mfumo wa usalama wa raia. Polisi lazima wawe sehemu ya jamii wanayoitumikia ili kuongeza hali ya uwajibikaji. Uwajibikaji wa polisi haupo tu kwenye viapo bali na jamii inayowazunguka. Wanafikiri zaidi jinsi ya kuilinda jamii ambayo pia ndiko makazi yao ya kudumu yalipo. Uwezi kuniambia polisi toka Masaki atashughulikia tukio la dharula Manzese sawa na Masaki. Polisi ambaye familia yake iko Masaki akisikia tukio limetokea masaki atawashwa kujua nini kimetokea kwa njia yoyote kuliko ambavyo tukio lingetokea Manzese.


Shirikisho yani serikali ya Muungano itakuwa na kikosi kidogo ambacho kinaweza kuingilia pale ambapo polisi wa washirika wameshindwa kwa kuomba msaada lakini muda wote Shirikisho litajikita kwenye usalama wa taifa kwa maana ya mashushu na upelelezi wenye uwezo na utaalamu wa hali ya juu. Hii yote ili polisi wa washirika wakishindwa upelelezi wa uhalifu wanaomba msaada wa juu wa Shirikisho.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments