[Mabadiliko] KAULI YANGU KUHUSU HOJA ZA DK. KITILA DHIDI YA CHADEMA

Thursday, February 13, 2014
Wanamabadiliko,

Suala hili nililijadili jana katika mtandao wa wanabidii. Naomba nami niseme kidogo, nitoe maoni yangu kuhusu sakata hili na maoni ya Dk. Kitila Mkumbo anayoandika mtandaoni na gazetini.

Nimekuwa namsoma Dk. Kitila Mkumbo katika mtandao huu na safu yake katika Raia Mwema. Ni rafiki yangu. Nimemfahamu Dk. Mkumbo akiwa bado mwanafunzi, kiongozi wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 1998/9, wakati huo nikiwa mwandishi wa gazeti la The African. Nilishawishika tangu wakati huo kuamini kuwa Kitila ni kijana mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kujieleza. Sijabadili msimamo wangu katika hilo. Hata yeye analijua hilo.

Kwa hiyo, wengi wanaomjua au wanaomsoma Dk. Kitila wanaangukia katika kundi la mashabiki wa hoja zake, na mfumo wake wa kuziwasilisha. Naamini waathirika wa mfumo huu wapo wengi. Hata hapa nawaona.

Hata hivyo, katika siku za karibuni Dk. Kitila ninayemjua amebadilika sana. Tangu alipoingia matatani kuhusu waraka wake wa mabadiliko ndani ya Chadema, hoja zake zimekuwa na mwelekeo wa kishabiki zaidi ya kufikirisha. Ni hoja zenye kuwakilisha hisia zake zaidi badala ya uzito wa maoni mbadala.

Nitatumia makala yake haya ya sasa kujadili kidogo suala hili.

1. Anaposema Chadema si mbadala unaominika wa CCM, bila kutuletea chama mbadala anakuwa anafanya kazi moja tu - kujaribu kuchanganya wasomaji. Na wanapogoma kuchanganywa ndipo wanapoamua kusema "ametumwa," "anafanya kazi ya watu" na kadhalika. Hakuna jambo lisilo na mbadala. Kama si Chadema, basi aseme ni nani mbadala wa CCM. Na aeleze ni lini Chadema imeacha kuwa mbadala wa CCM, maana siku zote - kabla hajafukuzwa uanachama Chadema - amekuwa akiamini hivyo. Kwa hiyo, hapa tunaona hisia. Uchungu. Hasira. Chuki! 

2. Anapaswa kusema kwa majina na takwimu ufisadi wa viongozi wa chama chake cha zamani. Maana kwa jinsi tunavyojua, huo ufisadi anaoutaja kwa hao asiowataka upo pia kwa wale anaowashabikia tena kwa viwango vya juu sana. Kwa hiyo, kama angekuwa anachukia ufisadi kweli kweli, kuna watu asingewashabikia kabisa, wala singesubiri afukuzwe Chadema ndipo aseme ufisadi wa waliomfukuza.

Sitaki kumtetea mtu hapa. Lakini nataka kusisitiza kwamba hakuna popote ambapo Dk. Kitila amewahi kunukuliwa kwamba ndani ya vikao vya chama chake aliwahi kuibua hoja yoyote inayofanana na hii akakataliwa. Amekuwa kiongozi mkubwa ndani ya Chadema. Hakutaka kutumia kikao kusahihisha viongozi wenzake. Ameamua kutumia mitandao nje ya mfumo wa chama kushambulia wenzake. Ndiyo maana wakasema ni  "msaliti." 

Alipaswa kuyasema yale yaliyoandikwa kwenye waraka mbele yao akiwakazia macho kama msomi. Wakubali, wakatae. Lakini kusubiri waraka wao ukamatwe halafu ndipo wajifanye mashujaa, ni dalili kwamba hawakuwa na nia ya kusaidia chama chao, bali kutafuta utukufu wao, kuangusha viongozi kwa njia zisizo za kikatiba, au kuangusha chama kwa malengo wanayojua wao, wakitumia udhaifu fulani fulani wa ndani wanaoujua. Anachofanya hapa ni character assassination ambayo vile vile haitamjenga yeye binafsi wala kumrejeshea hadhi aliyokuwa nayo.

3. Chadema hawapendi kukosolewa? Tumewakosoa sana. Kama kiongozi, alipaswa kujua kuwa amepewa fursa adhimu ya kuwakosoa ndani ya vikao au katika mazingira yanayofanana na hadhi yake, nafasi yake na ya hao anaowakosoa. Kuwashambulia hadharani au kuwachimbachimba kisirisiri kama alivyofanya na waraka wake si kielelezo cha usomu, wala si njia mwafaka inayoweza kukubaliwa na chama chochote, au tasisi yoyote yenye uongozi.

Kama angetoa waraka huo kwenye kikao, akafanya uchambuzi yakinifu wa nguvu, udhaifu, fursa na vikwazo vya Chadema mbele ya wajumbe wake, akawaeleza ukweli anaoujua yeye wakaukataa, na bado wakamchukulia hatua, wengi tungekuwa nyuma yake. Kama msomi, fursa ya kuwa miongoni mwa viongozi wa Chadema, tena katika Kamati Kuu, ndiyo ilikuwa nguvu yake ya kutumia kurekebisha kasoro anazoziona. Hakuitumia. 

Au kama waraka huo ungeandikwa na mtu ambaye si kiongozi, hana fursa yoyote ya kukutana na viongozi wa chama kuwaeleza yaliyo moyoni mwake, awe mwanachama au la, tungeelewa kwamba alikuwa na nia njema, maana ndiyo fursa pekee iliyokuwa karibu naye. Dk. Kitila na wenzake walikuwa na fursa ya kukutana na viongozi nje na ndani ya vikao. Lakini busara zao ziliwaongoza kuwa uwanja mwafaka wa kuikosoa Chadema ni katika mitandao ya kijamii. 

Kwa kuwa watu hawa wameenda shule, tena zinazoeleweka; kwa kuwa wana uwezo mzuri tu wa kuelewa na kuchambua masuala mengi katika jamii; binafsi nashindwa kuelewa kwamba walishindwa kuelewa kwamba mtandao wa kijamii haukuwa uwanja mwafaka wa "kushauri" chama chao. Wao hawakuwa washauri huru. Walikuwa viongozi.

Kila mmoja wetu ana nguo ya ndani. Anajua anakoifulia na anakoianika. Kama demokrasia ni kufua nguo za ndani hadharani na kuzianika hadharani, hilo litakuwa ni somo jipya kwa baadhi yetu. Na kwa maana hiyo hatutakuwa na sababu ya kuwa na viongozi wala vikao. Tuache kila mmoja asemee anapotaka!

Na katika mazingira haya, si vigumu wenzako kukuona kama umetumwa, ni pandikizi au msaliti. Popote penye uongozi suala hili lingechukuliwa hatua. Nadhani wenzetu hawakuamini jambo lao lingegunduliwa au kama baada ya kugunduliwa wangechukuliwa hatua. 

Na kwa hulka hii wanayoonyesha hapa ni kwamba kama wao ndio wangekuwa viongozi wanaoshutumiwa na viongozi wenzao kwa staili hii wangekua wakali zaidi. Maana kama wamekuwa wakali kuhalalisha na kutetea kosa lao, ingekuwaje kama wangekuwa ndio wana wajibu wa kuadhibu wakosaji, kutetea na kulinda hadhi ya chama na vikao vya chama wanachoongoza?

4. Nahitaji muda kuelimishwa kuhusu mpasuko wanaozungumzia. Ni hivi, kila mtu ana rafiki, ndugu, mashabiki. Dk. Kitila, Zitto na wenzao wana watu hao. Lakini ushabiki huu hauitwi mpasuko wa chama. Sana sana ni msukosuko. 

Mpasuko unatokea pale taasisi inapogawanyika katika makundi makubwa mawili au matatu, kama ilivyokuwa kwa NCCR-Mageuzi. Mwenyekiti huku, katibu kule. Ofisi moja huku, nyingine kule. Lakini hasira na hamaniko la watu haliwi mpasuko. Kama kamati kuu ingekatika vipande vipande, kimoja kikiunga mkono uamuzi kingine kikikataa, huo ungekuwa mpasuko. Lakini wajumbe kadhaa kuunga mkono hoja na wengine wakapinga, halafu baadaye ukafanywa uamuzi wa kikao, katika misingi ya uwajibikaji wa pamoja, ni suala la kawaida, na uamuzi ukishafanywa ni wa kikao, ni wa taasisi. Hata wale waliokuwa hawautaki hulazimika kuukubali. Hakuna uamuzi uliowahi kukubaliwa na watu wote kwa asilimia 100.

Nadhani hii dhana ya mpasuko inakuzwa na wale wale waliokuwa wamedhamiria kupasuachama katika makundi mawili kwa nia ya kutengeneza chama mbadala. Yalitokea CUF na NCCR-Mageuzi mwaka juzi na mwaka jana. Haukuwa mpasuko bali msukosuko uliotokana na sakata husika. Mambo haya ni sehemu ya kukua kwa chama. Misukosuko inatokea, mnatikisana, mnatofautiana, baadaye chama kinakuwa kimoja mnaendelea na safari.

Wasioridhika kabisa hawalazimiki kuendelea kudumu katika taasisi isiyowaamini, na ambayo wao hawaiamini. Badala ya kulaani yaliyopita, huku wakijua kuwa hawana fursa ya kuaminika, kurejeshwa na kuheshimika kama zamani, ni bora kama bado wanataka siasa, waunde hicho kinachoitwa chama mbadala wakilee, wakikuze na waonyeshe wenzao umahiri wa kujenga chama mbadala.

Siasa za mezani na siasa za uwanjani ni vitu viwili tofauti. Chadema kimejengwa na makundi mengi ya watu. Wengine hata hawakumbukwi wala hawajulikani. Mnazungumzia mchango mliotoa? Wapo walioasisi chama; wapo waliofilisika kwa sababu ya Chadema; wapo walioachika kwa sababu ya Chadema; wapo waliopata vilema kwa ajili ya Chadema; wapo waliofukuzwa shule kwa ajili ya Chadema; wapo waliopoteza kazi kwa ajili ya Chadema; wapo waliokufa kwa ajili ya Chadema. 

Bora nyie mmepata hata fursa ya kuwa viongozi. Wapo waliopitia katika magumu mengi hayo na hawatapata hata fursa ya kuwa wajumbe wa nyumba kumi; na bado wanakipenda chama chao. Kila mtu ana mchango wake. Ni bora utambuliwe. Zitto na Kitila wamefanya yao. Lakini mchango wa mtu si tiketi wala kisingizio cha kuwageuka wenzako. 

Yuda Iskarioti alikuwa mtunza hazina wa wanafunzi wa Yesu. Alipomgeuka bosi wake akamuuza kwa vipande 30 vya fedha ameitwa msaliti hata leo. Hakuna anayekumbuka mchango wake wa miaka yote aliyoshikilia mfuko.Hata angeibuka mtaani leo, angeitwa Yuda Iskarioti Msaliti. Ndiyo anuani aliyochagua. 

Na akithubutu kushambulia Wakristo au mitume wenzake walioshikamana na Yesu, anajua majibu atakayopata kutoka kwao. Ndiyo haki yake.

Ni kweli, inawezekana usaliti wake umesababisha matokeo mengine mazuri katika mfumo husika, lakini hiyo ndiyo anuani yake - msaliti. Tayari yupo nje ya mfumo. Na kila anachosema kinatafsiriwa kulingana na mahali alipo na hadhi aliyo nayo sasa, si ile ya zamani.

Kwa hiyo, Dk. Kitila na wenzake wanapaswa kuyajua haya. Naamini wanayajua kwa sababu wameenda shule.


Ansbert Ngurumo
Existential Philosopher, Musician, Journalist & Media Manager
Vox Media Centre & Free Media
Tanzania

Share this :

Related Posts

0 Comments