[wanabidii] Tunahitaji chama kitakachopigania Unyerere, kupinga ubwanyenye

Friday, January 31, 2014

NIMELAZIMIKA kuendelea na mada yangu leo kwa sababu ya msukumo wa wasomaji walionitumia maoni. Ninashukuru kwamba safari hii maoni yamekuwa chanya. Sio kwamba wasomaji wote walikubaliana na maudhui yangu. La hasha. Nasema ni maoni chanya kwa sababu, hata kama baadhi ya wasomaji walinipinga, walifanya hivyo kihoja na kwa hoja, badala ya kejeli, mipasho na matusi. Huu ndio utamaduni tunaotaka kuujenga katika siasa za nchi yetu. Utamaduni utakaojikita katika kupingana na/au kukubaliana kihoja.

Tunataka pia vyama vya siasa vipingane kwa hoja na katika maswala, badala ya kupinga sura za wanasiasa. Ndio maana mimi ni miongoni mwa wananchi walioshangazwa, kushtushwa na kukasirishwa na tukio la washabiki wa CHADEMA huko Mbeya cha kubeba jeneza wakiigiza kubeba mwili wa moja ya wanasiasa wasiompenda, Zitto Kabwe. Hiki kilikuwa ni kitendo cha kihuni na kijinga. Wanachama na washabiki wa vyama watapata mhemuko katika harakati za kisiasa na wanaweza wakajikuta wanafanya mambo ya hovyo na ya aibu, lakini ni jukumu la viongozi wao kuonyesha uongozi na kuhakikisha kuwa, sio tu wanakemea matukio kama hayo, lakini wanazuia yasitokee. Tunapoona viongozi wananyamazia, au kuyakemea kwa sauti isiyosikika au hata kushabikia matukio ya kijinga kama haya inatia shaka juu ya uwezo wao wa kiungozi.

Katika makala ya leo naeleza kidogo aina ya chama ambacho tungependa kichukue mbadala ya CCM na CHADEMA katika muktadha wa itikadi na falsafa. Itikadi na falsafa ndio mwongozo wa chama cha siasa ndani na nje ya serikali. Nje ya serikali itikadi na falsafa huongoza chama katika kuibua sera mbadala na kupinga na kukosoa sera za chama kilichopo madarakani. Chama cha siasa kinapopata fursa ya kuunda serikali, itikadi na falsafa ndio huwa dira ya kutengeneza sera za serikali na sheria mbalimbali katika nchi. Ndiyo kusema, chama kisicho na itikadi na falsafa ni sawa na debe tupu ambalo litapeperushwa kwenda upande wowote pale upepo utakapovuma.

Chama cha TANU na baadaye CCM kiliundwa katika msingi thabiti wa itikadi na falsafa. Ujamaa ndio ulikuwa msingi wa kiitikadi na Azimio la Arusha ilikuwa ni falsafa iliyobuniwa kutekeleza itikadi hiyo. Pamoja na matatizo yake kiutekelezaji, kama anavyoanisha mwandishi William Edgett Smith katika kitabu chake cha 'Nyerere of Tanzania: The first decade 1961-1971,  Azimio la Arusha lilikuwa ni dira muhimu ya kifalsafa katika nchi iliyotokana na viongozi wa kizalendo na ambalo halikusukumwa kutoka magharibi.

Baada ya kuachana na Azimio la Arusha, Chama cha Mapinduzi kimeshindwa hadi leo kuibuka na falsafa mbadala. Badala yake kimejikuta kikidandia sera za magharibina mashariki ya mbali. Kwa mfano, mwaka 2003 wakati wa awamu ya tatu ya utawala wa Rais Benjamin Mkapa serikali ya CCM iliibuka na mtaalamu wa kurasimisha biashara zisizo rasmi, Profesa Hernando de Soto. Mtaalamu huyu akaishawishi serikali ya Mkapa kwamba kurasimisha biashara zisizo rasmi kama vile mama ntilie, saluni za nywele, uchuuzi barabarani, n.k. ndio ilikuwa dawa ya umaskini. Ndio ulikuwa mwanzo wa sera ya MKURABITA. Hadi leo hatujui mafanikio yake yaliishia wapi. Hii ilikuja wakati serikali ikitekeleza mpango wa kukuza uchumi na kupungza umaskini (MKUKUTA) ambao nao ulinakiliwa kwa kiasi kikubwa kutoka magharibi.

Leo serikali ya CCM inatekeleza mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ulionakiliwa kutoka Malaysia na tunaambiwa mpango huu ndio kiboko ya umasikini na matatizo mengine hapa nchini. CCM haina tena uwezo wa kubuni falsafa za maendeleo na badala yake inadandia sera za mataifa ya nje ambayo mazingira ya utekelezaji ni tofauti kabisa na hapa kwetu na ni sababu mojawapo kwa nini sera hizi zinagonga mwamba kila mara. Kupoteza kwa mwelekeo kwa CCM ni jambo ambalo Katibu Mkuu wa zamani wa chama hicho, marehemu Horace Kolimba, aliliona mapema miaka ya tisini, pale alipotamka kinagaubaga kwamba CCM imepoteza dira.  Kwa kuwa wakati huo kukosoa CCM ilikuwa ni sawa na kumchungulia mama mkwe, Kolimba alisakamwa na kuzodolewa sana. Lakini leo tunaona bayana kile ambacho alikisema Kolimba zaidi ya miaka ishirini iliyopita.

Chama cha siasa bila itikadi na falsafa ya kueleweka kitaishia kupigania madaraka pekee na mara kipatapo madaraka kitakuwa hakijui kifanye nini na madaraka hayo, zaidi ya viongozi wake kujinufaisha nayo kibinafsi.

Nilipojiunga CHADEMA mwaka 2005 nilikuwa na matumaini makubwa ya kuchangia katika kujenga chama kitakachoibuka na itikadi na falsafa mbadala na kuziba ombwe lilioachwa na CCM. Nimewaambia marafiki zangu mara nyingi kwamba sikujiunga na CHADEMA kwa sababu ya imani kwamba kilikuwa chama bora na ambacho nilikubaliana na misingi yake mia kwa mia. La hasha. Nilijiunga CHADEMA kwa sababu niliamini kwamba kwa uchanga na uchangamfu wake wakati huo nilikuwa na fursa ya kutoa mchango wangu katika kukijenga chama hiki kiwe mbadala katika nyanja za kiitikadi, kifalsafa na kisera. Na nilitoka CCM baada ya kujiridhisha pasi shaka kwamba chama hiki kilikuwa hakiwezekani tena kubadilika kutokana na ukweli kwamba kimefikia hatua ya usuguna hakiwezi tena kubadilika kikiwa bado kina serikali.

Mara baada ya kujiunga, nilipata fursa ya kukarabati itikadi na falsafa ya CHADEMA katika hatua mbili. Kwanza, wakati wa marekebisho ya katiba ya chama hicho mwaka 2006 ambapo tulifanikiwa kuitoa CHADEMA kutoka mlengo wa kulia hadi mlengo wa kati. Kimsingi tulikihamisha chama angalau kidogo kutoka kwenye ubwanyenye na kukiweka katikati pasipo ubwanyenye wala ujamaa. Kwa lugha rahisi Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2006 ililazimisha CHADEMA kuachana na ubepari kwa kiasi fulani.

Lakini fursa muhimu zaidi niliyoipata ni mwaka 2009 kuelekea uchaguzi wa mwaka 2010 nilipoteuliwa kuratibu maandalizi ya ilani ya uchaguzi wa mwaka 2010. Kwa kutumia fursa hii mimi na wenzangu katika timu ya kutengeneza ilani tuliifanya ukarabati mkubwa sana kwenye msimamo wa CHADEMA kiitikadi na kifalsafa. Tulikihamisha chama rasmi kutoka mlengo wa kati hadi mlengo wa kati kushoto. Ni kwa sababu hii CHADEMA kwa mara ya kwanza ikaweza kuhubiri habari za kutoa elimu bure na serikali kujiingiza moja kwa moja katika kusimamia sekta muhimu kama vile kilimo. Kwa kifupi kupitia ilani ya mwaka 2010, CHADEMA kilichukua rasmi nafasi ya CCM ya Nyerere. Na hili liliwezekana kwa sababu CCM yenyewe ilishakimbilia kulia ikikumbatia ubwanyenye.

Mtu pekee aliyeshtukia ukarabati mkubwa wa kiitikadi na kifalsafa ndani ya chama ni Mzee Edwin Mtei. Ilikuwa ni katika Mkutano Mkuu wa Chama wa mwaka 2010 ambapo mzee Mtei aliniita pembeni na kwa ukali kidogo akaniambia kwa Kiingereza, ninanukuu: Kitila, you have put things in the manifesto which made me walk out of CCM (Kitila, umeweka mambo katika ilani ambayo yalinifanya mimi nitoke CCM). Nikamuulize yapi hayo mzee, akanieleza sera kama vile za elimu bure, serikali kusimamia kilimo, na akanionyesha sura kama mbili hivi katika ilani ambazo kwa maoni yake, na kweli ndivyo ilivyokuwa, zilikuwa haziendani na msimamo wa CHADEMA kiitikadi na kifalsafa. Nikacheka sana, na kisha nikamwambia Mzee umechelewa, hapa tupo kwenye Mkutano Mkuu. Ulipaswa kutoa maoni yako mapema ili turekebishe.

Nayaeleza haya ili wasomaji wapate kuelewa kwamba tulikuwa tumedhamiria kwa dhati kabisa kujenga chama chenye misingi ya kifalsafa na kisera inayoendana na matakwa ya jamii yetu. Kwa kifupi tulikuwa tumedhamiria kurudisha unyerere kupitia CHADEMA baada ya CCM kuutelekeza. Na kama ni usaliti huu ndio hasa ulikuwa usaliti na tulipaswa kufukuzwa kwenye chama kipindi hicho. Lakini tulipowakilisha katika vikao vya chama ilani ilipokelewa vizuri bila mjadala wowote mkali, na sisi tukaamini kwamba mapendekezo yetu ya kuihamisha CHADEMA kiitikadi na kifalsafa yalikuwa yamepokekewa vyema.

Hata hivyo juzi nimeshtuka baada ya kumuona Ali Mfuruki amekaribishwa kwenye mkutano mkakati wa CHADEMA uliofanyika huko Kilimanjaro na kupewa nafasi ya kutoa mada. Katika mada yake, pamoja na mambo mengine, Mufuruki alilishambulia sana Azimio la Arusha na kulaumu kwamba liliturudisha nyuma. Alishangiliwa vya kutosha. Viongozi wote wa juu wa chama, wabunge na wajumbe kadhaa wa Kamati Kuu walihudhuria mkutano huo na kumsikiliza vizuri. Ndio kusema sasa CHADEMA inarudi katika nafasi yake ya awali kiitikadi na kifalsafa, yaani mlengo wa kulia. Kwa lugha nyingine CHADEMA wanarudi katika asili yao ya ubwanyenye.

Sasa katika kipindi ambapo CCM hawana mwelekeo wowote kiitikadi na kifalsafa, na katika mazingira ambapo chama kikuu cha upinzani wanatamani ubwanyenye, tunahitaji, tena kama jambo la dharura, kujenga chama mbadala. Tunahitaji mbadala kwa sababu sera za ubwanyenyehaziwezi kamwe kufanya kazi katika mazingira ya kwetu zaidi ya kusimika unyonyaji. Sera za ubwanyenyehata hata huko magharibi zimeanza kupigwa vita. Sera za kibwanyenye lazima zipigwe vita kwa sababu zinagawa watu katika makundi ya wafanyakazi, wanaoendelea kumenyeka, na mabwana na mabibi wakubwa ambao kazi yao ni kulimbikiza mitaji na faida bila jasho. Mbaya zaidi wengi wa mabwana na mabibi wakubwa hawa ni wakala na makuhadi tu wa mabwanyenye wakubwa waliopo huko nje.

Tunahitaji chama ambacho kitakumbatia na kupigania unyerere bila aibu. Tunataka chama ambacho kitasimamia usawa, demokrasia na uzaleno kama misingi ya sera na matendo ya viongozi ndani na nje ya serikali. Tunahitaji chama ambacho viongozi wake watahubiri uzalendo wa kweli wa nchi na ambao watakuwa tayari kuifia nchi yao badala ya kuapa kufia vyama vyao vya siasa. Tunahitaji chama ambacho viongozi wake watatofautisha wakati wa kupanda na kuvuna. Tunahitaji chama ambacho kitaunda serikali ndogo lakini yenye nguvu na kuchukua nafasi yake katika nyanja muhimu katika kuendesha uchumi wa nchi na kuimarisha sekta binafsi inayotambua na kuchukua wajibu wake katika jamii.

Tunahitaji chama ambacho sera zake zitatoa fursa kwa sekta binafsi na asasi za kiraia kufanya kazi sio kwa hisani ya wanasiasa waliopo madarakani, bali kwa mujibu wa sheria. Tunahitaji chama ambacho sera zake zitawalenga moja kwa moja makundi maslahi katika jamii, wakiwemo wanawake, vijana, wazee, walimu, wakulima wa majembe ya mkono na pilao, wafanyakazi au wachuuzi.

Kwa kifupi, tunahitaji chama mbadala kitakachopigania usawa, demokrasia na uzalendo wa kweli katika nchi. Kama nilivyosema katika makala yangu ya wiki jana kujenga chama cha namna hii hatuhitaji mwongo mmoja kwa sababu kitajengwa na wananchi wenyewe kwa sababu kitakuwa ni chama chao!- 


See more at: http://www.raiamwema.co.tz/tunahitaji-chama-kitakachopigania-unyerere-kupinga-ubwanyenye#sthash.L9r35pWf.dpuf

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments