[wanabidii] MKONO WA TANZIA KUTOKANA NA KIFO CHA MHE. SENGODO MVUNGI KUTOKA CUF

Wednesday, November 13, 2013
THE CIVIC UNITED FRONT CUF,

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
13-11-2013

MKONO WA TANZIA KUTOKANA NA KIFO CHA
MHE. SENGODO MVUNGI

Chama cha Wananchi – CUF kimepokea kwa mshituko na majonzi makubwa taarifa ya kifo cha Dr. Sengodo Mvungi, Kiongozi mwandamizi wa NCCR – Mageuzi, Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo.

Kifo cha Dr. Mvungi kimeishtua Tanzania nzima hasa kwa vile tulitazamia kuwa angeishi kwa muda mrefu zaidi. Kifo hicho kinazidi kusikitisha kwa vile kimetokana na kushambuliwa kikatili na watu wasiojulikana wanaodaiwa kuwa ni majambazi.

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi CUF, mimi mwenyewe na viongozi waandamizi wa CUF walimjua vizuri sana Marehemu Dr. Mvungi kwani tukifanya kazi naye kwa karibu.
Dr. Mvungi alikuwa mpambanaji jasiri asiyeyumba katika mapambano ya kuiletea Tanzania mfumo wa kidemokrasia halisi unaolenga kulinda haki za kila Mtanzania bila ya ubaguzi wa aina yoyote ile. Dr. Mvungi alichukia uonevu, manyanyaso, ukandamizaji na dhulma dhidi ya binadamu yoyote. 

Dr. Mvungi tulishirikiana naye kwa karibu katika mchakato wa kudai Katiba mpya ya Tanzania na pale vyama vya siasa vilipounda kamati ya kufanya rasimu ya Katiba mpya Marehemu Dr. Mvungi ndiye aliyekuwa Mwanasheria wa Kamati hio. Alitoa mchango mkubwa katika kuandaa na kukamilisha rasimu hio.

Wengi tulifarijika pale alipoteuliwa kuwa miongoni mwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Tanzania. Tulijua uwezo wake, umahiri wake, utendahi kazi makini wake na dhamira yake ya kuona Tanzania inapata Katiba nzuri kwa masilahi ya wananchi wote bila kujali itikadi za vyama.

Dr. Mvungi alikuwa ni Wakili mahiri, msomi makini na kiongozi shupavu. Alikuwa jasiri hasa katika kuwatetea wanyonge na katika kutoa mawazo yake. Alikuwa ni mchambuzi hodari wa mambo ya kisheria, hasa sheria inayoambatana na masuala ya Katiba. Halikadhalika alikuwa mchambuzi aliyebobea katika masuala ya kijamii na ya kisiasa na aliguswa sana na umuhimu wa kuendeleza elimu bora nchini Tanzania.

Kifo chake ni pigo zito kwa familia yake, Chama cha NCCR – Mageuzi, Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Tume ya mabadiliko ya Katiba na kwa jamii nzima ya Watanzania.

Kwa niaba ya Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, Wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF na Wanachama wote wa CUF, na kwa niaba yangu mwenyewe, tunatoa mkono wa tanzia kwa familia ya Marehemu, Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR – Mageuzi, Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na wafiwa wote.

Tunamuomba Mwenyeezi Mungu aipumzishe roho ya Marehemu Dr. Mvungi pema peponi, AMIN.


Seif Sharif Hamad
KATIBU MKUU
CHAMA CHA WANANCHI – CUF
ZANZIBAR

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments