[wanabidii] Jinsi ya Kupata Mtaji kwa Bila Dhamana Kupitia DSE

Wednesday, November 27, 2013

Salaam sana

Tunaandaa vipindi vya TV na Radio vya DSE. Kwa niaba ya Soko la Hisa la DSM DSE, napenda kutoa mualiko kwa watu wachache hasa Wajasiliamali wadogo na wa kati (Small and Medium Enterprises - SME) katika mjadala wa kuhamasisha jinsi ya kupata mtaji kupitia DSE. Mjadala huu utaihusisha DSE na wataalamu wengine waliobobea katika mambo ya mitaji.

Mjadala huu utafanyika siku ya Ijumaa tarehe 06-December-2013 katika Private Studio: Tancot House, 2nd Floor along Sokoine Drive just opposite Luther House or Maendeleo Bank kuanzia saa 4.00 asubuhi hadi saa 6.00 Mchana.

Mjadala huu ni muhimu sana na utarekodiwa na baadaye kurushwa kwenye Luninga na Radio mbalimbali.

Kama utapenda kushiriki, tafadhali sana thibitisha kwa kutuma barua pepe kwenda: mtsimbe@micronet.co.tz na pia uandike namba yako ya simu.

Unaweza kupitia makala hapa chini kujiweka sawa:

KUORODHESHA MAKAMPUNI KWENYE SOKO LA KUKUZA UJASIRIAMALI NA MASHARTI YA KUDUMU BAADA YA KUORODHESHWA KWENYE MASOKO YA HISA


1. Utangulizi

Soko la Hisa la Dar es Salaam limeweka masharti nafuu na utaratibu uliorahisi zaidi ili kuwezesha makampuni machanga, madogo na ya kati kuorodhesha hisa katika Soko la Kukuza Ujasiriamali.

Soko la kukuza ujasiriamali ni soko jipya kwa ajili ya kuorodhesha hisa za makampuni ambayo ni mapya, madogo na ya kati. Soko hili limeanzishwa kuwezesha makampuni ambayo hayajafikia vigezo vya kuingia kwenye soko kuu kukusanya mitaji kwa ajili ya kuendeleza biashara zao. Soko hili pia ni kwa ajili ya makampuni mapya yasiyo na historia ya utendaji ambayo hutakiwa ili kuingia kwenye soko kuu.

2. Utaratibu wa Kuuza Hisa kwa Umma kwa Mara ya Kwanza (IPO)

Kampuni inayotaka kuorodhesha hisa inatakiwa kufuata utaratibu ufuatao:

(i) Kuwasilisha hoja kwenye board: Utaratibu wa IPO huanza kwa menejiment kuwasilisha hoja kwa bodi ya wakurugenzi – ikijumuisha mpango wa biashara na makadirio ya fedha – ikipendekeza kampuni kuingia katika soko la umma. Bodi ya wakurugenzi hutakiwa kufikiria pendekezo hili kwa makini.

(ii) Kupitishwa kwa pendekezo la kwenda sokoni: Kama bodi ya wakurugenzi ikiafikiana na wazo la kwenda sokoni, basi pendekezo hili lazima lipelekwe kwenye mkutano wa wanahisa wote wa kampuni kwa ajili ya kupitishwa. Baada ya kupitishwa na mkutano mkuu, vitabu vya mahesabu vya kampuni kwa miaka mitano iliyopita lazima vipitiwe upya na kuboreshwa, kama inalazimu, ili kwenda sawa na viwango vya kimataifa vya ripoti za fedha (IFRS) ili kuthibitishwa.

(iii) Kuteua timu ya washauri: Kampuni binafsi inaweza kuwa tayari ina baadhi ya washauri ambao huhitajika wakati wa IPO: wahasibu, wanasheria wakaguzi wa hesabu, na benki au washauri wa uwekezaji. Hata hivyo, kampuni inaweza kupitia mahusiano yake na washauri hawa upya au kuanzisha mahusiano mapya kwa ajili ya mchakato wa IPO. Kurasimisha uhusiano na washauri kupitia barua maalumu na kukubaliana kuhusu malipo hufuatia baada ya makubaliano. Baada ya kuteua timu ya washauri, ratiba ya IPO na matukio yatakayofuatia inabidi kuandaliwa.

(iv) Lazima ateue Mshauri Mteule ambaye atailea kampuni toka wakati ambapo wazo la kutafuta mtaji linaanzwa kutekelezwa; 

(v) Lazima kuwasilisha (kupitia Mshauri Mteule) kwa CMSA na DSE maombi ya kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa kwa idhini ya taasisi zote mbili; na

(vi) Lazima aandae waraka wa matarajio kwa ajili ya kuuza hisa na kuorodheshwa sokoni kama inavyotakiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, sheria na marekebisho ya mwaka 2010. Kupitishwa kwa waraka huu wa matarajio ndio kutatoa ruhusa na fursa ya kuuza hisa kwa umma.

3. Masharti ya kuorodheshwa kwenye Soko la Kukuza Ujasiriamali (EGM)

Yafuatayo ni masharti ambayo makampuni tarajiwa yanatakiwa kuyatimiza kabla ya kujiunga na EGM: 

S/NO

VIGEZO

SOKO LA KUKUZA UJASIRIAMALI (EGM)

1.

Historia ya biashara

Hakuna.Iwapo kampuni haina historia ya kufanya biashara, inatakiwa kuonesha kuwa ina mtaji wa kutosha kuanzisha mradi uliofanyiwa utafiti na gharama zake kujulikana

2.

Historia ya kupata faida

Hakuna

3.

Mtaji wa kampuni uliokwisha kulipiwa

Angalau TZS 200 million * (None as per CMSA Requirements)

4.

Kusajiliwa

Kampuni imesajiliwa Tanzania kama kampuni ya umma, au kama ni kampuni inayojisajili kutoka nje ya Tanzania, sheria ya makampuni iwe inafanana na ya Tanzania.

5.

Mali za kudumu

Kampuni iwe na angalau 50% ya mali za kudumu ndani ya Tanzania

6.

Aina ya kampuni itakayoorodheshwa

Makampuni yanayokua - kutoka sekta zote za uchumi

7.

Njia ya kutoa hisa kwa umma

Toleo kwa umma, toleo kwa wawekezaji wachache, kudhamini, au njia zote tatu

8.

Shughuli za biashara

Maelezo ya kina yanayohusu biashara husika ikiwa ni pamoja na mpango wa biashara wa miaka mitano na uchambuzi yakinifu kwa biashara zenye uzoefu wa chini ya mwaka mmoja.

9.

Umiliki wa umma

Angalau 20% ya hisa kumilikwa na umma.

10.

Idadi ya wanahisa baada ya kuorodheshwa na kutoa hisa kwa umma

Angalau wanahisa 100

11.

Kipindi cha kizuizi

Ikiwa kampuni haina historia ya miaka mitatu, waanzilishi hawaruhusiwi kuuza hisa zao kabla ya miaka mitatu

12.

Matumizi ya mtaji uliotolewa

Kutoa maelezo ya kiasi kitakachopokelewa (baada ya kutoa gharama) ikibainisha kwa kina matumizi ya mtaji huo. Endapo makusanyo hayatatosha kuanzisha mradi uliotarajiwa, kampuni inatakiwa kuonesha ni wapi itapata mtaji wa ziada. Endapo matumizi halisi hayafahamiki kwa kiwango chochote kilichokusanywa, kampuni itatakiwa kutoa maelezo ya ujumla ya matumizi ya mtaji utakaopatikana. Kampuni pia itatakiwa kutoa maelezo ni kiasi gani cha chini kitakachokubaliwa kama mtaji wa kuendeshea kampuni.

13.

Washauri Maalum

Kampuni lazima iwe na mshauri maalum kwa kipindi chote cha kuorodheshwa

14.

Wakarugenzi na viongozi waandamizi

Kuwepo na viongozi wenye uzoefu maalum wa angalau mwaka mmoja kabla ya kuorodheshwa

15.

Taarifa za Fedha

Lazima zitayarishwe kwa kufuata misingi ya kimataifa (IFRS) na kukaguliwa na mkaguzi wa mahesabu ya fedha

16.

Wakaguzi wa hesabu

Wawe wamesajiliwa na bodi ya usajili wa wahasibu (NBAA)

17.

Uongozi usiobadilika

Hakuna haja. Mkazo umewekwa kwenye uzoefu wa viongozi hawa.

18.

Kamati za ukaguzi

Lazima kuwe na kamati za ukaguzi kulingana na ushauri wa CMSA na misingi ya utawala bora

19.

Utoshelezi wa Mtaji wa kufanyia biashara

Wakurugenzi watoe maoni yao kuhusu utoshelezi wa mtaji kwa angalau kipindi cha miezi 12

20.

Barua ya kuridhika toka kwa wasimamizi wa kisheria

Kampuni itabidi kuleta barua hii toka kwa wasimamizi wake wa kisheria

21.

Katiba ya kampuni

Katiba kuwa na kipengele chenye kuonesha kuwa kampuni inaruhusiwa kutoa hisa kwa umma, inalinda maslahi ya wanahisa wadogo, kuhamisha umiliki wa hisa, majukumu ya wakurugenzi ya kukopa, misingi ya utawala bora wa kampuni

22.

Wajumbe wa bodi ya wakurugenzi

Kampuni iwe na angalau 1/3 ya wakurugenzi ambao sio watendaji

23.

Waraka wa matarajio kupitishwa na Mamlaka

Waraka wa matarajio lazima upitishwe na mamlaka

24.

Kutimiza masharti ya utawala bora wa kampuni

Kampuni iahidi kutekeleza masharti ya utawala bora wa makampuni kulingana na matakwa ya Mamlaka (CMSA)

25.

Sera ya gawiwo

Kampuni iwe na sera bayana ya gawiwo

26.

Kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari

Kampuni inatakiwa kutoa muhtasari wa waraka wa matarajio kwenye vyombo vya habari.


4. Taratibu za kuorodhesha kampuni DSE

Taratibu za kufuatwa na kampuni inayotaka kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) zimewekwa wazi kwenye Sheria za DSE. Taratibu hizo ni pamoja na; kupata idhini ya CMSA, kuteua Mshauri Mteule, udhamini wa Dalali wa DSE, maombi kufanya katika fomu maalumu, vigezo vya vielelezo (uthibitisho wa kusajiliwa kampuni toka kwa mwanasheria, uthibitisho wa utii wa sheria toka kwa mdhamini, kopi kumi za waraka wa matarajio, kopi 10 za taarifa ya ukaguzi wa hesabu za fedha, kopi 10 za fomu za maombi, maelezo ya ugawanywaji wa hisa za kampuni, na kadhalika.

5. Masharti ya kudumu ya kuorodheshwa kwenye masoko ya hisa
Masharti ya kudumu ya kuorodheshwa kwenye soko la hisa ni muhimu ili kuendeleza soko lenye kufuata taratibu na mfumo unaowezesha watumiaji wa soko kupata habari za soko kwa pamoja. Masharti hay hujumuisha:

1.      Masharti ya jumla na wajibu kutoa taarifa;

2.      Kutoa taarifa za fedha kwa vipind maalumu; na

3.      Vigezo vinginevyo.


Kila kampuni itatakiwa kufuata masharti haya kama yalivyobainishwa kwenye sheria za DSE and CMSA. Kampuni itatakiwa kwa haraka sana iwezekanavyo na si zaidi ya masaa 24, taarifa zinazohusiana na:

·        Mazingira au matukio yanayoweza kuwa na athari kwa kiwango kikubwa kwenye taarifa za fedha, msimamo wa fedha, au mtiririko wa fedha na/au taarifa zote muhimu zitakazowezesha wamiliki na wawekezaji kufanya maamuzi sahihi ya kuwekeza au kutokuwekeza kwenye kampuni husika.

·        Maendeleo yoyote mapya yenye athari kwenye utendaji wa biashara na mafanikio au matatizo ya utendaji na kifedha ya kampuni na habari yoyote ile ambayo yaweza kuathiri bei ya dhamana za kampuni iliyoorodheshwa

·        Mshauri Mteule wa Kampuni lazima aendelee kuwa na mahusiano na kampuni hiyo kwa muda wote ambao itakuwa imeorodheshwa kwenye EGM;


6. Hitimisho
Moduli hii ilikusudia kuwawezesha wajasiriamali kuzielewa taratibu za kuuza hisa na hatimaye kuorodheshwa kwenye kitengo cha kukuza ujarisiriamali (EGM) cha soko la hisa la Dar es Salaam (DSE). Imeelezea mchakato na vigezo muhimu vya kutimizwa na kampuni inayotaka kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa kwenye EGM ya DSE. Moja ya masharti ya kudumu ya kuorodheshwa ni ulazima wa kuwa na Mteule Maalumu kwa muda wote ambao kampuni itakuwa imeorodheshwa. Makampuni yaliyoorodheshwa yatahitajika pia kutangaza taarifa zote ambazo ni nyeti na zinazoweza kuathiri bei ya hisa zao sokoni. EGM ya DSE sio tu inatoa nafasi kwa makampuni ya kati kupata mitaji kwa njia rahisi na nafuu, inatoa pia urahisi wa kutimiza masharti ya kudumu ya kuorodheshwa sokoni.

 

Wasalaam

 

Sanctus Mtsimbe

CEO & Managing Director

 

ConsNet Group Limited

Eastern Africa Professionals & Business Network (EAPBN)

Tancot House, Sokoine Drive, 2nd Floor

Sokoine Drive /Pamba Rd.

P.O. Box 21605, Dar Es Salaam

T: +255 22 212 3545 | F : +255 22 212 3544

M : +255 782 820 820

E:mtsimbe@micronet.co.tz

Website: www.consnet.co.tz

 




This email is free from viruses and malware because avast! Antivirus protection is active.


Share this :

Related Posts

0 Comments