[Mabadiliko] Al Shaabab Na Chimbuko La Ugaidi ( VI)

Friday, October 04, 2013


-        Sura mbili za Osama Bin Laden

"ANAYEOGELEA baharini haogopi mvua." Anasema Osama Bin Laden.

Tukio la ugaidi  la Westgate Nairobi linanuhusishwa pia na mtandao wa kigaidi wa Al qaida. Hata hivyo, wachunguzi wa masuala ya ugaidi wanapata tabu kuamini kama Al qaida inahusika moja kwa moja na tukio la Nairobi.

Ni kawaida ya Al qaida kutoa matamko ya kuhusika na ugaidi pale inapotokea.  Kwenye lililotokea Nairobi, bado hazijasikika sauti rasmi na za moja kwa moja kutoka Al qaida. Yawezekana kabisa, kuwa  Al Shaabab ina mahusiano ya kimtandao na Al qaida, lakini, Al Shaabab iliyopoteza nguvu nyingi yawezekana iko katika kutapatapa na kuonyesha dunia kuwa bado ni tishio.

Tukirudi kwa Al qaida na Osama Bin Laden, kuna wakati  akiwa mafichoni, Osama Bin Laden alijitokeza  na 'kuhutubia" ulimwengu kupitia kituo cha televisheni cha Al-Jazira. Ilikuwa mwezi Januari, 2006. Sauti ya Osama ilikuwa imenaswa kwenye mkanda na kuthibitishwa na wataalam wa sauti katika nchi za Kiarabu  na hata CIA, Shirika la ujasusi la Marekani.

Kauli  ya Osama kuulezea msimamo wa Al-Qaida na labda wake mwenyewe
ilitoa tafsiri nyingi. Kwa kiasi fulani ulimwengu ulishangazwa kwa Osama
kuamua kutumia kipindi cha mwanzo wa mwaka kuutangazia ulimwengu kuwa bado
yu hai na ana dhamira ya kuendeleza harakati zake.

Itakumbukwa, kuwa  mara ya mwisho kwa ulimwengu kumsikia Osama Bin laden
akiongea ilikuwa mwezi Desemba mwaka 2004. Mara ile Osama alitamka kumuunga
mkono aliyemwiita shujaa Abu Musab Zarqawi wa Iraq na kuwahamasisha kugomea
majaribio yenye kupelekea chaguzi za kidemokrasia katika Iraq.
 

Lakini, Januari ile ya 2006, Osama Bin Laden alijitokeza na sura nyingine
kabisa. Si Osama yule aliyezoeleka na sura yake ya kwanza ya Osama gaidi
anayepambana na dola yenye nguvu kuliko zote duniani, yaani Marekani na
washirika wake. Badala yake, mara ile ulimwengu  ulimwona Osama bin Laden aliyesikika
zaidi kama mwanasiasa, mpatanishi wa amani na pengine kiongozi wa nchi.

Hata hivyo, katika maelezo yake yale, Osama, na kama ilivyotarajiwa, alitishia kuishambulia Marekani ndani ya ardhi yake. Alisikika akitamka;
"Matayarisho yetu yako mbioni, nanyi (Wamarekani) mtashuhudia hayo mara
yatakapokamilika" .

Ulimwengu ulipokuwa ukiyafikiria  ya Septemba 11, 2001, haukujua kama safari ile  Al Qaida wangeweza  kufikiri kusababisha maafa makubwa ya kiasi gani na kwa kutumia
mbinu gani.

 Pamoja na Osama kutoa tishio hilo kwa Marekani, katika hali isiyo
ya kawaida kwa kiongozi wa kikundi cha kigaidi, Osama alikaribisha
upatanisho kwa maana ya pande mbili kufanya mazungumzo ya kusimamisha
mapambano.

Katika hilo, Osama alitoa masharti ya kufikiwa makubaliano hayo
ya kusimamisha mapambano. "Ondokeni Iraq na Afghanstan, ndipo hapo
wapiganaji wetu wa Mungu watapoiacha miji yenu katika amani. Kwa namna hiyo
pande zote mbili zitanufaika na hali ya  amani na utulivu. Hivyo basi
tunaweza kuijenga Iraq na Afghanstan. Na hivyo, lililo mbele zaidi, nyinyi
Marekani mtaacha kupoteza mabilioni ya dola bila faida yeyote." Alisema Osama Bin
Laden.

Bila shaka, Osama Bin Laden kwa kuyasema yale hakuwa na matarajio
kuwa utawala wa Rais George Bush ungeyakubali kirahisi mapendekezo yake.
Vivyo hivyo, kwa nchi za Kimagharibi ambazo mwaka 2004 alipata kuzitupia
nyavu zikubaliane na Al Qaida kusitisha mapambano kwa miezi mitatu ,lakini,
nchi hizo zilikataa. Na hata safari ile, utawala wa Bush ulitoa jibu la
haraka juu ya mapendekezo ya Osama Bin Laden. "Hatujadiliani na magaidi".
Ilisema Marekani.

Lakini, Bin Laden alifahamu fika, kuwa waliomsikiliza kwa kila alichosema si Marekani na nchi za Magharibi tu, bali alikuwa na  wasikilizaji wengi na zaidi katika mitaa ya nchi za Kiarabu. Bin Laden alijenga hoja zilizoathiri maoni ya mtu wa kawaida katika mitaa ya nchi za Kiarabu.

Hatua ile  pia huenda iliathiri mitazamo ya vyombo vya habari katika nchi za
Kiarabu ambavyo  vimekuwa na mwelekeo wa kupunguza kasi ya kuandika habari zenye kuhusu Al Qaida na harakati zao na hususan katika Iraq chini ya uongozi wa Zarqawi kwa wakati huo.

Kilichojitokeza ni kwa vyombo vya habari vya nchi za Kiarabu kuuweka upinzani dhidi ya Marekani katika Iraq katika makundi mawili. Kundi  la kwanza ni lile "lililokubalika". Ni kundi la upinzani unaondeshwa na  jumuiya za kisiasa ikiwemo vyama vu kisiasa. Na kundi la pili ni lile  "lisilokubalika". Hili ni kundi la upinzani linaloendesha harakati zake  dhidi ya Marekani  kijeshi na kwa mbinu za kigaidi.

Chochote kinachonukia Al Qaida kinaingizwa katika kundi la pili.
Hali hiyo ilipelekea nyota ya Osama Bin laden kufifia katika ulimwengu wa
Waislamu katika hali yenye kufafanana na kutoweka kwa imani ya Wamarekani
kwa Rais wao Bush kuhusiana na kuikalia Iraq kwa wakati huo.

Kupitia maelezo yale ya  Osama Bin Laden, tafsiri ya  kwanza na ya muhimu ilionyesha kuwa Osama alitaka kumwonyesha mtu wa kawaida  katika mtaa wa nchi ya Kiarabu,  kuwa yeye, Osama Bin Laden, ni mwanasiasa  mwenye kuwajibika na ambaye yuko tayari kufikia makubaliano na mahasimu wake. Kwamba alikuwa tayari kumaliza uhasama na umwagaji damu na kuanza  harakati za kuzijenga upya nchi zilizoathirika. Kwamba wote wawili, Osama na  Bush wangefaidika na kusitishwa kwa mapambano hayo.

Inaendelea...

Maggid.

0754 678 252

http://mjengwablog.com

 

--
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda; mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com
Utapokea Email ya kudhibitisha kujiondoa kwako.
 
TEMBELEA Facebook yetu:
http://www.facebook.com/MabadilikoForums?ref=hl
 
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

0 Comments