[Mabadiliko] Al Shaabab Na Chimbuko La Ugaidi ( V)

Thursday, October 03, 2013

Al Shaabab Na Chimbuko La Ugaidi ( V)

WAKATI Afrika Mashariki, kwa kupitia shambulizi la kigaidi la Al Shabaab  pale Westgate, Nairobi, inaweza kusemwa, kuwa imefikwa na ' Septemba 11' yake yenyewe, leo tuliangazie kwa karibu  shambulio pekee kubwa la kigaidi kupata kufanywa   hapa duniani. Ni shambulizi lilofanywa na kikundi cha  Al-qaida. Na hilo linabaki kuwa ni shambulizi lao kubwa la kigaidi  tangu kuanzishwa kwa kikundi hicho cha kigaidi.

Naam, tunazungumzia  shambulizi la kigaidi la Septemba 11,2001. Ni shambulizi  dhidi ya Marekani katika ardhi  ya Marekani.  Na baada ya kuliona hilo, tutaangalia pia kihistoria,  vitendo vya kigaidi vilivyofanywa na Wamarekani ndani ya Marekani yenyewe.
     

Itakumbukwa, kuwa siku ya Jumanne ya Septemba 11,  2001, dakika chache kabla  haijatimu saa tatu asubuhi kwa saa za New-York, ndege kubwa iliyojaa abiria iligonga moja ya majengo pacha ya World Trade Centre. Majengo yale, marefu kushinda yote katika New York,  yalikuwa na ghorofa 110 kwenda juu.

Hata kabla  hazijatimu dakika ishirini baadae,  ndege nyingine kubwa iligonga jengo  lingine la World Trade Centre. Ni hapo, ndipo ulimwengu ulipoanza kuona picha ya tukio lile na kufahamu, kuwa kilichotokea ni moja ya matukio makubwa ya kigaidi kupata kutokea ulimwenguni.

Kama hilo halikutosha, mara ulimwengu ulioneshwa kupitia televisheni, jinsi ndege ya tatu ilivyofanya  shambulizi la kigaidi katika jengo la Idara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon. Na baada ya hapo, ikabainika pia,kuwa ndege ya nne ilikuwa imetekwa na magaidi na  ilianguka ikiwa njiani. Inasemekana,  kuwa ndege ile ya nne ilikuwa inaelekea  aidha kwenye Jengo la Bunge la Marekani (Congress)  au Ikulu ya Rais (White House).

Magaidi walioshiriki ugaidi ule jumla yao ni 20. Baadhi yao walipata mafunzo ya kuendesha ndege katika vyuo binafsi ndani ya Marekani. Ajabu  ni kwamba, baadhi yao walijifunza jinsi ya kurusha ndege angani tu,  na si kutua na ndege ardhini! Zaidi ya watu  elfu tatu waliuawa katika mashambulizi yale ya kigaidi katika WTC na Pentagon.

Bila shaka yeyote,  matukio yale ya kigaidi  yalichangia kubadilisha sura ya ulimwengu.  Hivyo, kuamsha maswali mengi juu ya mustakabali wake. Hata hivyo, katika hili la ugaidi,  tukumbuke kuwa, Marekani kama taifa, ilishapata kuathiriwa na vitendo vya ugaidi hata kabla ya Septemba 11, 2001.

Mengi ya matukio ya kigaidi yaliyotokea Marekani kabla ya Septemba 11 yamefanywa, aidha na mtu mmoja mmoja,  au vikundi vidogo sana vya kigaidi ndani ya Marekani.  Itakumbukuwa,  mwishoni mwa miaka ya 1960, Marekani iliathirika na vitendo vya kigaidi vilivyofanywa  na vikundi vidogo vilivyokuwa vikipinga Vita vya Vietnam, ambapo Marekani ilikuwa ni mhusika mkuu katika vita hivyo. Moja ya tukio la kigaidi kwa wakati ule ilikuwa ni kutekwa nyara kwa mjukuu wa mmiliki wa moja ya makampuni ya magazeti makubwa katika Marekani, mmiliki huyo aliitwa Bw. Patty Hearst.

Itakumbukuwa pia, kuwa shambulizi la kigaidi liliofanywa dhidi ya jengo la
Shirikisho katika jiji la Oklahoma  mwezi April, mwaka 1995. Tukio lile la kigaidi lilisababisha vifo vya watu 168. Mara moja, vikundi vya kigaidi vya Kiislamu ndivyo vilivyoshukiwa kuhusika na shambulizi lile. Hata hivyo, ikaja kubainika kuwa, aliyehusika na shambulizi lile alikuwa ni Raia wa Marekani (Mweupe) ambaye pia alikuwa ni veterani wa Vita vya Ghuba vya mwaka
1991. Raia yule wa Marekani aliitwa Mc Veigh.

Ajabu ya tukio lile la Oklahoma ni ile hali ya harakati za vikundi vidogo vidogo vya Wamarekani wenye msimamo makali na wa kibaguzi kushiriki katika kazi ya upelelezi wa kuwapata wahusika wa shambulizi lile. Vikundi hivi vilikuwa ni sawa na vikundi vya watu waliochanganyikiwa, waliona na walihofia kuangamia kwa taifa la Marekani.

 Katika hisia zao na  kuchanganyikiwa kwao, waliwaona maadui wa Marekani kila mahali.  Wakaja hata  na nadharia ya kwamba, ni Rais Bill Clinton aliyeamrisha shambulizi dhidi ya  jengo lile pale Oklahoma!! Kwamba yule Mmarekani Mc Veigh aliwekwa kidubwasha matakoni kilichomfanya aongozwe kwa "Kiongoza-mbali" (Remote-control)!

Itakumbukwa pia , katika Marekani  na hususan katika miaka ya 1970, kulikuwepo na matukio ya kigaidi yaliyoelekezwa kwenye kliniki za kutolea mimba. Wahusika wa matukio yale ya kigaidi kwa vyovyote walikuwa ni wafuasi wa jumuiya iliyojulikana kama  "Pro life" iliyokuwa ikitetea uhai wa viumbe hai na hususan mwanadamu hata akiwa katika hatua za mwanzo kabisa tumboni.
 

Tukija katika ugaidi tunaoshuhudia sasa, tunaona hali yenye kuzidisha hofu. Kilicho dhahiri ni kuwa,  vita dhidi ya ugaidi inakuwa ngumu sana kupiganwa kwa vile, mara nyingi, adui anaweza kujipenyeza bila kuonekana kirahisi.  

Na tunashuhudia pia, katika sehemu mbali mbali, kuongezeka kwa vitendo vya kigaidi  kwenye maeneo ya  mijini (Urban terrorism).  Aina hii ya ugaidi ni ngumu sana kudhibitika hata kama nchi  ina jeshi kubwa na lenye vifaa vya kisasa.  Inahitaji umakini mkubwa na ushiriki wa raia wema katika kupambana na ugaidi

Na kama tulivyoona kwenye makala ya kwanza kabisa, kuwa   moja ya sababu kadhaa ambazo Marekani ilidai ndizo  zilizopelekea uamuzi wa kuishambulia Iraq, ilikuwa ni kupambana na utawala  wenye kufadhili ugaidi duniani.

 Marekani iliwahi hata kumwusisha Dikteta  Saadam Hussein na Osama Bin Laden. Hata hivyo,  Marekani iliondoa dai hilo  kwa kukubali ukweli kuwa, Saadam na Osama walikuwa ni watu wawili wenye  itikadi , malengo na mitazamo tofauti.  Itaendelea...

Maggid.

0754 678 252

 

--
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda; mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com
Utapokea Email ya kudhibitisha kujiondoa kwako.
 
TEMBELEA Facebook yetu:
http://www.facebook.com/MabadilikoForums?ref=hl
 
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

0 Comments