[wanabidii] PINDER LAZIMA ASHITAKIWE!!!

Friday, August 02, 2013

 
Mh Pinder kavunja Katiba ya Nchi kwa kuamuru watu WAPIGWE TU! Amekiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 100 kifungu kidogo cha pili (2). Lakini kabla ya kuwaonyesha ni jinsi gani Pinder alivyovunja katiba, ngoja niweke ibara yote ya 100 ili tuende sawa:
………………………………………………………………………………………………………
100 (1). Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika Mahakama au mahali pengine nje ya Bunge.
 
(2). Bila ya kuathiri Katiba hii au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika, Mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya Bunge au alilolileta bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au vinginevyo.
……………………………………………………………………………………………………....
 
UFAFANUZI WA KISHERIA:-
Mtaona kwamba kifungu cha kwanza (1) kinampa mbunge uhuru wa kuongea chochote bungeni bila kushtakiwa. Lakini kifungu cha pili (2) kimemuwekea mipaka, KWAMBA anaweza asishtakiwe pale tu jambo atakalokuwa amelitenda au kusema ndani ya bunge halitaathiri katiba au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika.
******************************************************************************
Je, pinder kaathiri (kavunja) Katiba hii au hajaiathiri? Ndio ameiathiri. Kivipi? Tazama vifungu vifuatavyo kwenye sheria mama (Katiba):
 
KIFUNGU CHA KATIBA KILICHOATHIRIWA NA PINDER:-
Mh Pinder kavunja (kaathiri) Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 13 kifungu cha sita (6), kifungu kidogo (e) ambacho kinasomeka kama ifuatavyo:-
 
13 (6) (e). Ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.
………………………………………………………………………………………………………
HITIMISHO:-
Pinder anashitakika na hakika hapa hachomoki hata kidogo. Wale mnaotetea kwamba analindwa na Katiba mmeona jinsi ambavyo katiba hiyo hiyo inatoa mwanya kwake kushtakiwa? Mkisoma Katiba msiwe mnasoma nusu nusu, someni kwa ukamuilifu wake na bila jazba. Haya tuonyesheni basi ni kifungu gani cha sheria kinachompa uhuru usio na mipaka kutamka au kutenda jambo lolote bungeni halafu asishtakiwe. Haya ni mambo rahisi kutambuliwa na mtu yeyote anayejua kusoma na kuandika. Sio lazima uwe na shahada ya sheria ili ufahamu jinsi Pinder alivyosigina Katiba ya Nchi. Tafakari, chukua hatua!

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments