[Mabadiliko] Neno La Leo; Jua Linapozama Afrika...

Sunday, August 11, 2013


Ndugu zangu,

Kwa mwanadamu, mila yake ndio dini yake ya kwanza. Kwa Mwarabu na Mzungu sawia, Uislamu na Ukristo uliingia katika jamii hizo na kuzikuta jamii hizo zikiwa na mila zao.

Na sisi Waafrika vivyo hivyo, tuna mila zetu. Uislamu na Ukristo ni imani za kimapokeo. Hakuna dhambi kwa mwanadamu kupokea imani mpya. Hata hivyo, ni vema kwa anayeipokea akawa pia amejitambua, kuwa naye pia ana mila zake. Na mwanadamu anayeikana asili yake ni mtumwa.

Uafrika ni imani. Uafrika umejijenga katika upendo na ujamaa. Ndio maana Mwalimu aliijenga TANU na nchi yetu katika misingi ya Ujamaa wa Kiafrika, hivyo basi itikadi. Ni tofauti kabisa na Ukomunisti.

Mathalan, Afrika unapokuwa safarini na jua likazama, basi, Mwafrika hutafuta yalipo makazi ya watu. Afrika safari zetu nyingi ni za miguu, na kwa kawaida hatutembei usiku.

Na jua likizama na ukakutana na Mwafrika mwenzako kwenye mji wake, husemi kuwa unataka kusaidiwa pa kulala na mengineyo. Kwa mila zetu, utasema; " Mwenzenu niko safarini na jua limezama nikiwa hapa".

Kwa Mwafrika, hapo umehitaji msaada. Mwenyeji ataandaa pa wewe kulala. Utaandaliwa chakula na hata maji ya moto ya kuoga. Atakayefanya ukarimu huo hatajali kama wewe ni Mkristo, Muislamu, au wa kabila tofauti na yeye.

Na asubuhi kukipambazuka, utapewa kijana wa kukusindikiza kilomita zipatazo mbili. Uendelee na safari yako. Ndio, Uafrika ni imani iliyojengeka katika misingi ya upendo, umoja na kusaidiana bila kubaguana.

Na katika hili la misuguano ya kiimani kwenye jamii. Misuguano inayotokana na dini hizi za kimapokeo; Uislamu na Ukristo. Imefika mahali, kwa makusudi kabisa, tuandae mitaala ya kufundisha mashuleni maarifa ya imani tofauti za humu duniani.

Huko mashuleni watu wote wafundishwe, na waalimu mahiri, juu ya masuala ya imani za humu duniani, ikiwamo dhana ya Uafrika kama imani pia.

Maana, mingi ya misuguano hii inatokana na watu kukosa maarifa, au kuwa na maarifa haba sana.

Naam, Afrika jua linapozama unamtafuta Mwafrika mwenzio, bila kujali dini au kabila lake.

Ni Neno La Leo.

Maggid,
Iringa.
http://mjengwablog.com

--
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda; mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com
Utapokea Email ya kudhibitisha kujiondoa kwako.
 
TEMBELEA Facebook yetu:
http://www.facebook.com/MabadilikoForums?ref=hl
 
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
 
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forums" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments