[wanabidii] Kwanini mtu achukiwe kiuongozi?

Saturday, March 23, 2013
Nakumbuka mwaka 1995 niliingia katika kinyang'anyiro cha ubunge,
lakini katu sitataja jimbo husika kwa sababu za kiusalama, na nimeamua
kugombea tena mwaka 2015 insha'allah Mwenyezi Mungu akinipa uhai na
afya njema.

Nilibwagwa vibaya sana kwa sababu kubwa mbili za kisiasa - sababu
ambazo hazitambuliwi mahala popote katika ulimwengu wa siasa, zaidi ya
jimboni kwangu ambako nilikuwa nagombea.

Sababu ya kwanza ilikuwa sina fedha za kuwagawia wajumbe ambao ndiyo
wanaopendekeza jina langu ili liende katika orodha ya wagombea ili
niingie katika mchakato. Sababu ya pili nilivishwa madhambi mengi
ambayo sikuweza kuyakataa kwa sababu walionivisha walitumia nguåvu ya
fedha katika kuiaminisha jamii inayonizunguka.

Mwaka wa uchaguzi ujao nimejiandaa ipasavyo kutokana na uzoefu
nilioupata mwaka 1995. Nimejiandaa kwa fedha kidogo za kuwaachia
wajumbe baada ya kuuza shamba langu hapa Kipatimo kwa mwekezaji ambaye
sijui ametoka wapi na anataka kufanya nini, na nimejiandaa kwa mambo
mawili; la kwanza kujisafisha kwa fedha na la pili kuwachafua ipasavyo
wagombea wenzangu.

Nimefikia hatua hii baada ya kuona huku kunakoitwa Tanzania sasa
kunatosha kwa shida zake, nataka niende Tanzania nyingine ya pepo,
maana kugaagaa na upwa kumefikia tamati sipati hata dagaa, ni afadhali
nitende dhambi kwa kuwaongopea wapiga kura kwa wananchi ili nipate
fursa ya kubadilisha maisha yangu kwa sasa ninapoelekea katika kifo
changu, maana sina hakika na pepo nyingine.



Leo nimeliangalia hili baada ya kusikiliza midahalo mingi ya kujiandaa
na kuingia katika uchaguzi ujao wa awamu nyingine, na jinsi
wanaotarajia kuwania nafasi hizo wanavyovutana katika vyombo vya
habari, mikutano ya hadhara na pengine kuwauma watu masikio ya unafiki
na uchochezi. Si muumini sana wa dini yoyote lakini pia si mpagani
kwamba nashindwa kutambua dhambi yoyote. Utambuzi wa dhambi upo moyoni
mwangu hasa ninapoona jambo ambalo nahisi haliswihi kwa mtu mwingine,
kwa maana ya kumtesa - iwe kwa mawazo au moyoni mwake.



Hivi sasa yapo makundi ambayo yanajua kuwa nitagombea ubunge,
yanafanya kila linalowezekana usiku na mchana kunichafua kuwa ni
mlarushwa, nimejilimbikizia mali, mimi tajiri wa kupindukia, mchawi,
natumia majukwaa ya kanisa na misikiti kujinadi, sifai kwa sababu
mwaka 1995 nilikataliwa na wajumbe, sina mvuto kwa chama change, na
kadhalika.



Hizo ni hoja ambazo naziona hazina mashiko na ni hoja za kunichafua na
unafiki, pengine zinafanywa hivyo ili wao waonekane wasafi na wapate
fursa nyingine ya kuendelea kuongoza hata kama matatizo yao na
migogoro yao iko hadharani; na inajulikana isipokuwa inafichwa kwa
vigezo vyao vya kujiona watakatifu.



Napenda sana msemo wa zamani wa wazee wetu kwamba mke mzuri usimtafute
siku ya sikukuu, kwani kila mmoja atajitahidi kuwa msafi na kuongeza
manukato, Mtafute siku ya kawaida na ikiwezekana mtafute akiwa
shambani akifanya kazi uone umahiri wake, lakini pia ni bora zaidi
akiwa hajui kuwa anachunguzwa kwa ajili ya kuposwa. Hilo litamfanya
ashindwe kuficha uvivu wake na umbeyaumbeya wake.



Naandika barua hii kwenu, ili kwa kina mfanye tafakari bainifu ya
kujua mkweli ni yupi. Yupo anayesimama kila siku jimboni kwangu
akinichafua kwa hoja zake ambazo katu sizijibu nanyamaza kimya ili
wananchi wachambue pumba na mchele, waangalie uwajibikaji wangu wa
moja kwa moja katika jamii na hoja zao za kuitwa tajiri, wathibitishe
uchawi wangu na yote waliyosema kabla ya uchaguzi kufanyika.



Najua yatasemwa mengi, lakini mkweli siku zote atachukiwa mbele ya
wanafiki. Mimi sijatangaza nia ya kugombea ubunge lakini sielewi
kwanini wananchi wanaambiwa maovu yangu kana kwamba wametumwa
wakanisemee. Hakuna aliyethibitisha maovu yangu na kama yupo kuna kila
njia ya kunitakasa ama nipelekwe mahakamani nikashitakiwe nifungwe,
ama kwa mganga mkubwa nikatolewe uchawi wangu.


Swali langu la msingi ni kwanini mtu achukiwe kiuongozi na wachukiaji
wawe viongozi wenyewe? Tujiulize sisi wapiga kura kabla ya kuwakubali
hao wanaonadi sera zao huku tukijua hawana jipya lolote walilofanya
katika kipindi ambacho wameweza kutuongoza katika jimbo letu.

Mtu mwenye akili nzuri na malengo mazuri hazungumzii mambo ya watu.
Atazungumzia mambo yanayowakabili watu, hatatafuta sababu za kupendwa
kwa kumchafua mwenzake, hatazungumzia majina atazungumzia matatizo ya
jimbo letu, hatazungumzia mambo yanayofanywa na mwenzake atazungumzia
anayofanya yeye ili tuyaone na mwisho ataingia katika kinyang'anyiro
bila hofu ya mtu kwa kuwa tayari amefanya jambo zuri.



Nawasihi wanajimbo wajiulize hao wanatafuta nini jimboni wakati
uchaguzi bado? Kwanini wasinichukulie hatua za kinidhamu wakati wapo
madarakani? Wana wasiwasi gani nikichukua fomu? Lakini bila hofu
natangaza rasmi kuwa fomu ya ubunge nitachukua na nitaingia madarakani
kwa kazi yangu nzuri, ambayo wanajimbo mnapaswa kujiuliza maswali
machache nitakayoyasema kabla ya uchaguzi.


Kidumu chama chetu,

TANU oyeeee!

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

Chanzo :
http://www.jamhurimedia.co.tz/index.php?option=com_content&view=article&id=747:yah-kwanini-mtu-achukiwe-kiuongozi&catid=22:siasa&Itemid=9

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

0 Comments